Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Wanafunzi waliotaka kuandamana Chuo Cha Uhasibu Arusha: Badala ya kupatiwa majibu wapewa mkong’oto wa nguvu na askari Polisi; Chuo kimefungwa kwa muda usiojulikana.

Maelfu ya wanafunzi wa Chuo Cha Uhasibu kilichopo Njiro Jijini Arusha wamejikuta wakimaliza siku vibaya baada ya kupewa kichapo cha nguvu na askari wa Jeshi la Polisi waliokuwapo chuoni hapo kufuatia azma ya wananfunzi hao kutaka kuandamana kwenda kwa Mkuu wa Mkoa kupeleka kilio chao kuhusu kile walichoeleza kuwa ni hali ya hatari kwa maisha yao chuoni hapo. Azma hiyo ya kuandamana ilichagizwa na tukio la mwananfunzi mwenzao wa mwaka wa pili kuuwawa usiku wa kuamkia jana kwa kuchomwa kisu na watu wasiojulikana wakati akielekea hostelini kwake.

Blog hii haikuweza kufahamu hasa sababu iliyopelekea Polisi hao kuanza kupiga mabomu mfululizo na kuwakimbiza wananfunzi hao huku wengine wakianguka na kuumia na wengine kupasuka vichwa kwa virungu vya askari hao.

Mabomu ya kutoa machozi yalianza kupigwa mfululizo mara tu baada ya Mkuu wa Mkoa aliyefika kuwasikiliza kushindwa kuongea nao kutokana na kitendo cha wananfunzi hao kumzomea muda wote aliotaka kuongea wakidai alikuwa amewadharau.

Taarifa nyingine kutoka chuoni hapo zinasema kuna tetesi kuwa Chuo hicho kimefungwa kwa muda usiojulikana.

Hali ilivyokuwa
Awali, mapema asubuhi kulikuwa na taarifa kwamba wananfunzi hao walikuwa wamejipanga kuandamana kutoka chuoni kwao Njiro hadi ofisi ya mkuu wa mkuoa kupeleka kilio chao cha matukio mfululizo ya kuuwawa wanafunzi wa chuo hiko.

Taarifa hizo zilimlazimu Mkuu wa Polisi Wilaya, OCD Muroto akiambatana na maofisa wengine wa Jeshi la Polisi kufika chuoni hapo mapema asubuhi na kuwasihi wanafunzi hao kutoandamana, jambo ambalo lilishindikana na kuonekana kuamsha hasira zaidi kwa wanafunzi hao.

Jitihada nyingine zilifanywa na Mlezi wa Wanafunzi (Dean of Student) aliyetambulika kwa jina moja la Nanyaro lakini hazikufua dafu.

Baadae mida ya saa nne asubuhi, Mbunge wa Arusha Mjini, Mh Godbless Lema ambae anaishi Njiro pia, alipata taarifa za kadhia hiyo na kupita chuoni hapo ambapo alisaidiana na OCD Muroto na Dean of Student kuendelea kuwatuliza munkari vijana hao. Jitihada za Lema zilionekana kuzaa matunda na wanafunzi wakawa wasikivu na akatumia mwanya huo kuwaomba wawe watulivu na wenye nidhamu ili waweze kupata ufumbuzi wa kile walichokuwa wanakitaka, na hivyo wazo la kuandamana likawa limekwisha.

Pamoja na kumsikiliza Lema na kutii maelezo yake, bado wanafunzi hao waliendelea kudai tena aje Mkuu wa Chuo (Joanas Monyo)  na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mh Magesa Mulongo waongee nao. Maofisa wa Chuo walijaribu kumtafuta mwakilishi wa Chuo aweze kuwasaidia lakini wanafunzi walikataa kumsikiliza mtu aliyeelezwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo. Bw Kasidi.

Hatua hiyo ilimlazimu Mbunge wa Arusha Mjini, Mh Lema kumpigia simu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mh Magesa Mulongo na kumsihi afike Chuoni hapo kutatua mgogoro uliokuwepo. Lema aliwatangazia wananfunzi hivyo na akaeleza kuwa Bw Mulongo amemuhakikishia kuwa atafika eneo lile…

Baada ya muda usiozidi dk 45 Mkuu wa Mkoa akafika eneo la Chuo na kupewa maelezo ya utangulizi na maofisa wa Chuo na Polisi na kisha akaelekea eneo maalumu wanapozungumzia wanafunzi matatizo yao.

Kinyume na matarajio ya wanafunzi, Mkuu wa Mkoa hakutaka kupanda juu (ghorofani kwenye ngazi) walipokuwa viongozi wengine akiwemo OCD Muroto, Mh Lema, Mlezi wa Wanafunzi na maofisa wengine wa Chuo na usalama wa Taifa, na badala yake akamuomba Mh Lema ashuke chini ampe maelekezo fulani.

Kitendo hicho cha Mkuu wa Mkoa kumuita Lema ashuke chini hakikuafikiwa na wanafunzi hao, baadhi yao wakapaza sauti kumtaka Lema asishuke.

Mh Lema alitii maagizo ya Mkuu wa Mkoa, akashuka chini kumsikiliza. Mkuu wa Mkoa akiwa amezingirwa na wanafunzi hao, ambae alisema asingeweza kuongea bila kipaza sauti na pia asingeweza kuongea na wanafunzi hao wasio na nidhamu..labda kwa vile walikuwa wanapiga makelele muda huo. Blog hii haikushuhudia jaribio lolote la mh Mulongo kuongea na wanfunzi hao akakataliwa kusikilizwa hadi muda huo.

Baada ya kusema na Lema kuwa hawezi kuongea pale (wandishi wa habari walikuwa wakishuhudia) Mkuu wa Mkoa huyo na msafara wake wakaondoka bila kuzungumza chochote na wanafunzi hao na kuelekea yalipo magari yao, kitu ambacho wanafunzi hao walikitafsiri kama ni dharau kwao na hivyo kuonekana kama kimeamsha hasira zaidi.

Hali hiyo ilimlazimu Mh Lema kupanda tena juu kuwatuliza na kuwaaga kuwa anaelekea msibani ambako alikatiza na kwenda Chuoni hapo kuona hali halisi. Lema kasema kama Serikali waliyokuwa wanaisubiri imefika na haijaweza kuzungumza nao yeye hana kingine cha kufanya zaidi ya kuondoka na kuendelea na ratiba zake za siku.

Wanafunzi hawakukubali Lema aondoke, walimzonga sana kiasi cha kuhatarisha usalama wake na wengine wakaishindwa kujizuia na kuangua kilio wakidai akiondoka hakuwataweza kusikilizwa tena.

Kabali ya wanafunzi hao ilimlazimu Lema kurudi na kukaa mahali wakisubiri hatua nyingine ya kupata suluhu. Uamuzi huu pia ulikuwa faraja kwa wanafunzi hao kiasi cha kuweza kutoa nafasi kwa msemaji wa Chuo (mama mmoja jina lake halikupatikana) sambamba na Rais wa Serikali ya Wananfunzi Bw Benja Simkoko kuweza kuzungumza na wanfunzi hao.

Mulongo ataka kuongea na wanafunzi eneo jingine..
Rais huyo wa Wanafunzi na msemaji wa chuo walipata wakati mgumu sana kuwashawishi wanafunzi ambao walishajawa na hasira zaidi kukubali tena kuhamia eneo la cafteria ambako walielezwa kuwa Mkuu wa mkoa amekubali kuongea nao kwa kutumia microfone. Mwishowe wanafunzi walitii na kukubali kuelekea mahali hapo kwa msaada wa Mh Lema tena aliyeamua kwenda hapo nao wakamfuata.

Wanafunzi wakiwa wamejikusanya eneo la Cafteria ya Chuo, Lema alikuja kuitwa na maofisa wa Polisi kwenda kuonana na Mkuu wa Mkoa aliyemuita tena, akaondoka lakini njiani akakutana na msafara wake.

Gari ya Mkuu wa Mkoa ikasimama na Lema akazungumza na nae pamoja na Mkuu wa Polisi (cheo chake hakikujulikana haraka). Maongezi yao hayakuwa na maelewano lakini wakahafikiana wacha waende kuongea nao wanafunzi hapo Cafteria.

Wote wakaelekea hapo kwa minajili ya Mkuu wa Mkoa kuweza sasa kuongea nao kwasababu spika zilikuwa tayari zimefungwa.

Hata hivyo wakati wa maandalizi ya eneo hilo, kulitokea vurumai nyingine wakatai viti vinapangwa na wanfunzi hao wakakataa visipangwe kwa madai kwamba wao wamesimama muda mrefu na hawajasikilizwa.

Baadae zikasikika tetesi kwa wanfunzi kuwa kuna taarifa kuwa Lema atakamatwa baada ya Mkuu wa mkoa kuhutubia.

Mabomu mvululu
Mkuu wa Mkoa Bw magesa Mulongo alifika eneo la cafteria lililoandaliwa maalumu kwa ajili ya kuzungumza na wanfunzi hao… Bw Mulongo kabla ya kuongea, wakati akiwasili alipokelewa na makelele mengi.

Baada ya kukaribishwa kuongea alisalimu na kuwaeleza wanafunzi hao kuwa kwa lugha ya picha aliyoiona kwa wanafunzi hao (munkari waliyokuwa nayo) alidai kuwa matokeo yake hayatatua mgogoro wao na hayatamnufaisha yeyote yule. Wanafunzi wakazidi kupiga kelele huku baadhi wakizomea na kuhoji kwanini aliwadharau mwanzoni alipokataa kuongea nao.

Ni kama vile makelele yalizidi kiasi cha Mkuu huyo wa Mkoa kushindwa kuongea tena. Ghafla askari kama nane wakajitokeza na kumzingira wakaondoka nae hadi kwenye gari yake, kitendo kilichofuatia na mfululizo wa mabomu ya machozi.

Mabomu yalipigwa kwa kushtukiza maana hata baadhi ya wanafunzi waliohojiwa na Blog hii wanadai hawakufikiria hali hilo ingetokea. Wanafunzi walianza kukimbia hovyo huku wengine wakianguka na kuumia na kupoteza simu, mabegi na vitu vingine.

Hali sasa ilikuwa si salama tena ama kwa wanfunzi, wageni chuoni na watumishi wa chuo kwasbabu ilikuwa vigumu kuwatofautisha na kama ni amabomu, marungu na mitama ilitembea kwa yeyote aliyezagaa, huku baadhi ya wanafunzi wakirushiana mawe na askari na mawe mengine kuelekea kwenye majengo yaliyojirani.

Kuna baadhi ya watu walijificha chini uvunguni mwa magari na wengine ndani kuepuka kipigo. Blog hii iliweza kushuhudia kijana mmoja aliyepasuliwa kichwa akivuja damu nyingi eneo la Utawala na kuwahishwa hospitali na gari ya chuo iliyokuwa imepaki eneo hilo.

Mageti yote ya kuingia na kutoka chuoni hapo yalifungwa kwa muda hadi hali ilipotengamaa lakini kila gari iliyokuwa inapita ilikaguliwa vya kutosha.

Kuna wanfunzi wengi wamekamatwa na kupelekwa kituoni

Lema anatafutwa
Baade wadau wetu wa Blog wakiwa wameshatoka eno la tukio wakapata taarifa kuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Mh Godbless Lema anatafutwa na jeshi la Polisi na kwamba walitaka kumkamata kama tetesi zilivozagaa chuoni kwa sababu ambazo hatujaweza kuzithibitisha bado.

Arusha255 Blog ilifanya jitihada kuwasiliana na Mh Lema kupata taarifa zaidi lakini hatukufanikiwa. Taarifa za nyumbani kwake zilimnukuu mke wake kutojua mume wake alipo na kudai kuwa hata yeye amesikia kuwa mumewe amejeruhiwa kwenye vurugu hizo ila hana uhakika.

Tukiwa tunamalizia kuandika taarifa hii ya jinsi hali halisi ilivyokuwa Chuoni hapo, tukapata taarifa za uhakika kuwa gari ya mh Lema imechukuliwa na Jeshi la Polisi kwa kuburutwa matairi yakiwa yametolewa upepo na magari ya kampuni ya Majembe Auction Mart hadi Polisi Makao Makuu jijini hapa.

DSC06267Mh Lema akizungumza kuwatuliza wanfunzi hao mapema leo asubuhi. Picchani kuna Dean of Student wa Chuo Cha Uhasibu Arusha, Bw Nanyaro, OCD Muroto pamoja na maofisa wengine wa chuo. TUNAOMBA RADHI KWAMBA PICHA NA MATUKIO YOTE UTAZIPATA HAPA BAADAE KIDOGO!
DSC06264

Picha ya Mwanfunzi wa mwaka wa pili BA Economics and Finance, Henry Koga enzi za uhai wake.

DSC06274Picha yenye ubora hafifu iliyopigwa kwenye simu ya mmoja wa wanafunzi ikionesha mwili wa mwanafunzi Henry baada ya kuchomwa kisu shingoni.

PICHA ZOTE ZA HALI HALISI ILIVYOKUWA ZITAKUJIA HAPA HAPA BAADAE KIDOGO

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO