HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHESHIMIWA MCHUNGAJI PETER SIMON MSIGWA, (MB) WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, KUHUSU MAKADIRIO YA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
A: UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii ilianzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 21 cha Nyongeza ya Waraka wa Rais uliochapishwa kama Tangazo la Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010. Majukumu ya Ofisi hii yameainishwa katika Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2010) lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17 Desemba 2010. Kwa mujibu wa TS Na. 494A, majukumu hayo ni pamoja na ufugaji nyuki, wanyamapori, malikale, makumbusho na sera za utalii na utekelezaji wake. Katika utekelezaji wa majukumu haya, Ofisi hii ina idara mbali mbali kama vile wanyama pori, utalii, mambo ya kale, usimamizi wa rasilmali watu, sera na mipango. Aidha, Ofisi ina taasisi zinazojitegemea kama vile Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Uhifadhi wa Eneo la Ngonrongoro (NCAA). Vile vile, Ofisi ina wakala na mifuko ya uhifadhi kama vile Wakala wa Misitu Tanzania (Tanzania Forestry Agency) na Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Conservation Trust Fund) na Mfuko wa Hifadhi ya Misitu ya Milima ya Tao la Mashariki (The Eastern Arc Mountains Forests Conservation Trust Fund). Na mwisho, Ofisi ina vyuo mbali mbali kama vile Chuo cha Misitu Olmotonyi, Vyuo vya Wanyamapori Mweka na Pasiansi.
Mheshimiwa Spika,
Ni hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba Ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii imeshindwa kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Tangazo la Serikali tajwa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba sababu kubwa ya kushindwa huko kutekeleza majukumu ya kisheria ya Ofisi hii ni ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka ambao umetapakaa katika kila sehemu ya Ofisi hiyo ukiwahusisha watendaji wake wakuu pamoja na watendaji wa ngazi za juu za Chama cha Mapinduzi (CCM) na wafanya biashara makada wa chama hicho. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba kushindwa kwa Ofisi hii kutekeleza majukumu yake hayo kumehatarisha utajiri mkubwa wa maliasili za nchi yetu kama vile wanyamapori, misitu na malikale, na kulitia aibu kubwa taifa letu kwamba ndio chanzo kikubwa cha ujangili wa kimataifa na biashara haramu ya wanyamapori. Maliasili kama wamanyapori hai na nyara nyingine za serikali zimeporwa na kusafirishwa nje ya nchi yetu kwa kupitia viwanja vyetu vya ndege vya kimataifa pamoja na bandari zetu bila hatua stahiki kuchukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Bunge lako tukufu limepitisha maazimio mengi kuhusu kashfa mbali mbali zilizogubika utendaji wa Ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii na utekelezaji wa majukumu yake kisheria. Aidha, Bunge lako limeunda Kamati za Uchunguzi ili kuchunguza tuhuma za ukiukaji sheria na matumizi mabaya ya mamlaka katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitika kuliambia Bunge lako tukufu, maazimio ya Bunge yamepuuzwa na taarifa za Kamati zake za Uchunguzi kuzimwa. Na katika hili, Mheshimiwa Spika, lawama za kwanza lazima zitupiwe katika Ofisi yako mwenyewe kwa kuwa ndio imekuwa kaburi kubwa la kuzikia taarifa za Kamati za Bunge ambazo pengine Ofisi yako inaona zitaonyesha udhaifu katika utendaji wa Serikali hii ya CCM!
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 27 Aprili mwaka 2006 aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Anthony Diallo aliunda Kamati ya Maalum ya Uchunguzi Kuhusu Uboreshaji wa Tasnia ya Uwindaji wa Kitalii Tanzania. Lengo la kuundwa kwa Kamati hiyo lilikuwa ni “… kuchambua na kubaini matatizo yanayoikabili tasnia ya uwindaji wa kitalii na … namna ya kuyatatua matatizo hayo na kuboresha tasnia hiyo.” Kamati ya Diallo iliwasilisha Taarifa Kuhusu Uboreshaji wa Tasnia ya Uwindaji wa Kitalii Tanzania mwezi Juni 2006. Pamoja na mengine, Kamati hiyo iligundua kwamba licha ya biashara ya uwindaji wa kitalii kutakiwa kuwa “… ni chanzo kikubwa cha mapato ya fedha za kigeni, (biashara hiyo) inaingiza fedha kidogo, wastani wa dola za Kimarekani milioni tisa tu kwa mwaka wakati wenzetu wa Zimbabwe, (biashara) hii inawaingizia dola milioni thelathini kwa mwaka.”
Aidha, Kamati iligundua kwamba “… makampuni mengi ya uwindaji hayaajiri wataalam wa ndani ila huwatumia wananchi kwa kazi ndogo ndogo wakati wa msimu wa uwindaji. Makampuni haya pia yanawatumia wawindishaji kutoka nje ya nchi badala ya kutumia wawindishaji bingwa wa Kitanzania.” Vile vile, Kamati ilibaini kwamba licha ya kuwepo makampuni mengi yanayomilikiwa na raia wa Tanzania, makampuni machache ya kigeni yanamiliki idadi kubwa ya vitalu vya uwindaji ambavyo vina “… wanyama wengi ukilinganisha na vitalu vya makampuni ya wananchi ambavyo viko kwenye maeneo ambayo hayana wanyama wengi.”
Na mwisho, Kamati ilibaini kwamba “Idara ya Wanyamapori haisimamii kikamilifu tasnia hii kwa maana haina taarifa muhimu kuhusu vitalu na thamani halisi ya vitalu hivi.” Kwa kadri ya taarifa za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Taarifa hii ya Kamati ya Diallo haijawahi kutolewa hadharani na wala kuwasilishwa kwenye Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Inaelekea Kamati ya Diallo ilitokana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2005-2010, iliyokuwa imewaahidi Watanzania kwamba Serikali ya CCM itaendelea “… kuelekeza nguvu zake katika kuhifadhi, kulinda, kuendeleza, kudumisha na kuvuna maliasili kwa manufaa ya Taifa letu.” Ahadi hiyo ilirudiwa kwa karibu maneno hayo hayo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2010-2015. Aidha, tuliambiwa na CCM katika Ilani yake ya 2005 kwamba Serikali yake itahimiza “… miji ianzishe bustani za ufugaji wa wanyamapori (zoos) kwa maonyesho.” Hakuna bustani ya wanyamapori hata moja iliyoanzishwa katika kipindi hicho na ndio maana ahadi hiyo ilipotea kabisa katika Ilani ya CCM ya 2010!
Na kama tutakavyothibitisha, Serikali ya CCM imeshindwa kabisa kutekeleza mapendekezo ya Kamati ya Diallo. Badala yake, Serikali hii imeelekeza nguvu zake katika kudidimiza na kudhoofisha uhifadhi, ulinzi na uendelezaji wa maliasili za nchi yetu. Aidha, Serikali ya CCM sio tu imeelekeza nguvu kubwa katika uvunaji haramu wa maliasili za nchi yetu, bali pia imefanya hivyo kwa manufaa ya wafanya biashara wa kigeni wakishirikiana na wafanya biashara wachache ndani ya nchi na viongozi waandamizi wa CCM na makada waandamizi wa chama hicho.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2009 Bunge lako tukufu liliunda Kamati ya Uchunguzi ili kuchunguza matukio ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu za wananchi wa Liliondo katika Wilaya ya Ngorongoro ambapo wananchi walidaiwa kuchomewa nyumba zao na wanawake kudhalilishwa na Jeshi la Polisi. Taarifa ya Kamati hiyo, iliyoongozwa na Naibu Spika wa sasa wa Bunge lako tukufu, Mhe. Job Ndugai, haikuwasilishwa Bungeni na, kwa kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imezikwa kwenye kaburi la Ofisi ya Spika. Matokeo yake, mgogoro kati ya wananchi wa Loliondo kwa upande mmoja, na Serikali ya CCM na Kampuni ya Orthello Business Corporation (OBC) inayomilikiwa na mfanyabiashara kutoka Oman kwa upande mwingine, umezidi kuwa mkubwa kama inavyothibitishwa na maasi ya wananchi wa Loliondo dhidi ya CCM yaliyoshuhudiwa mwezi uliopita na viongozi na makada wa CCM waliopo ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka jana Kamati Ndogo ya Kamati ya Kudumu ya Maliasili, Utalii na Mazingira iliwasilisha taarifa ndani ya Bunge lako tukufu kuhusu utoroshwaji wa wanyamapori hai. Kufuatia kuwasilishwa kwa taarifa hiyo, Bunge lilipitisha azimio, pamoja na mengine, kwamba Serikali itengeneze kanuni za uwindaji ili “… iweze kubana mianya ya rushwa inayoikosesha mapato (na kanuni hizo) ziwe tayari ndani ya mwaka mmoja kuanzia sasa.” Bunge lako liliazimia pia kwamba wale wote waliohusika na utoaji wa kibali cha kutorosha wanyama hai wachukuliwe hatua za kinidhamu. Aidha, Bunge liliitaka “… Serikali kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya watumishi waliohusika kutoa kibali hicho.” Mwisho, Bunge lako lilirudia mapendekezo ya Kamati ya Diallo ya kuunda mamlaka maalumu kwa ajili kushughulikia masuala ya biashara ya wanyamapori na uwindaji wa kitalii. Bunge lako liliipa Serikali kipindi cha mwaka mmoja kutekeleza maazimio hayo. Hadi wakati wa kuwasilisha Maoni haya Serikali imepuuza utekelezaji wa maazimio ya Bunge lako tukufu kuhusu jambo hili. Aidha, licha ya Mheshimiwa Waziri kutoa ahadi kwa Bunge lako tukufu kuwa wanyamapori hai waliotoroshwa nje ya nchi watarudishwa nchini, hadi leo ahadi hiyo haijatekelezwa na Bunge hili halielekei kutaka kuchukua hatua stahiki kwa Mheshimiwa Waziri kwa kupuuza kutekeleza ahadi ya Serikali ya CCM kwa Bunge.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka jana Mheshimiwa Waziri alichukua vielelezo kutoka kwa Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu masuala ya ardhi Mh. Halima Mdee juu ya kampuni ya uwindaji ya Game Frontiers kukodisha kitalu chake cha uwindaji kwa ajili ya utafutaji wa madini ya urani katika eneo la Mbarang’andu katika Wilaya ya Namtumbo. Mh. Waziri aliahidi kwamba atachukua hatua stahiki kuhusiana na suala hilo. Hadi ninapowasilisha Maoni haya, Serikali haijaeleza hatua zozote, kama zipo, ilizochukua kumnyang’anya mmiliki wa kampuni hiyo ya uwindaji leseni ya uwindaji katika eneo hilo kwa kukiuka masharti ya leseni hiyo. Aidha, hadi sasa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni bado inasubiri majibu ya Serikali kuhusiana na ujangili wa tembo unaohusisha watendaji wa Serikali kwa kushirikiana na makada wa CCM.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 28 Julai, 2007, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Prof. Jumanne Maghembe alipatiwa taarifa ya kitafiti juu ya Uwindaji Haramu Katika Pori Tengefu la Selous na Maeneo Yanayolizunguka iliyoandaliwa na Bw. Baruani Mshale wa Shule ya Masomo ya Misitu na Mazingira ya Chuo Kikuu cha Yale cha Marekani. Pamoja na mengine, taarifa ya Bw. Mshale ilidai kwamba kumekuwa na ‘maslahi haramu’ (vested interests) kati ya Serikali na wafanya biashara wa uwindaji wa kitalii wa nje ambayo yamesababisha Serikali kufanya maamuzi yasiyofaa yanayowanyima wananchi vijijini faida zitokanazo na utajiri wao wa maliasili. Mtafiti huyo anataja viashiria vya maslahi hayo haramu kuwa ni pamoja na mvutano kati ya Mkurugenzi wa Wanyamapori na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na uamuzi wa Rais kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii aliondolewa kwenye Wizara hiyo. Katika kile kinachoonekana kwamba ‘maslahi haya haramu ya kisiasa kwa faida ya kiuchumi ya watu wachache’ yanajulikana serikalini, Mtafiti Mshale alimwambia Waziri kwamba “inawezekana nakukumbusha kitu ambacho tayari unakifahamu”!
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba ‘maslahi haramu ya kisiasa kwa faida ya kiuchumi ya watu wachache’ katika sekta ya uwindaji wa kitalii imekithiri ndani ya CCM na Serikali yake na inawahusisha viongozi na watendaji waandamizi wa chama hicho na Serikali yake. Kwa mfano, mwaka 2009 shehena ya pembe za ndovu zenye uzito wa tani 4 kutoka nchini Tanzania na Kenya zilizoripotiwa kukamatwa na vyombo vya usalama vya Vietnam ilisafirishwa na kampuni ya wakala wa meli iitwayo Sharaf Shipping Co. Ltd. Taarifa za Wakala wa Usajili wa Biashara na Makampuni (BRELA) zinaonyesha kwamba Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana anamiliki robo tatu ya hisa za Sharaf Shipping Co. Ltd., wakati robo iliyobaki ya hisa hizo inamilikiwa na mtu aitwaye Rahma Hussein. Kwa mujibu wa taarifa ilizonazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Rahma Hussein ni mkewe Abdulrahman Kinana!
Sio tu kwamba kampuni ya Katibu Mkuu wa CCM na mkewe imehusishwa na usafirishaji haramu wa pembe za ndovu kutoka Tanzania, kampuni hiyo inaelekea kutoa ajira haramu kwa wageni. Wakati shehena ya meno hayo tembo inakamatwa nchini Vietnam, nyaraka zilizoambatana na shehena hiyo zilionyesha kwamba kibali cha kusafirisha shehena hiyo kilisainiwa na raia wa India anayeitwa Samir Hemani mnamo tarehe 13 Novemba 2008. Hemani alikuwa Meneja wa Fedha na Utawala wa Sharaf Shipping Co. Ltd. Hata hivyo, nyaraka za Idara ya Uhamiaji ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imezipata zinaonyesha kwamba wakati Hemani anasaini kibali cha kusafirisha shehena ya meno ya tembo kwa niaba ya wateja wa Kinana na mkewe, kibali chake cha kuishi Tanzania kilikuwa kimeisha tangu tarehe 7 Mei, 2008!
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kuhusu kushiriki kwa Katibu Mkuu wa CCM katika kusafirisha kiharamu nyara za serikali ambazo kwa vyovyote vile zinathibitisha kuwepo kwa ujangili wa kutisha unaohusu maliasili wanyamapori wa nchi yetu. Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli mbele ya Bunge lako tukufu juu ya kuhusika kwa Katibu Mkuu wa CCM katika kuajiri wafanyakazi wageni ambao walikuwa wanaishi nchini kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya Tume ya Rais ya Kuchunguza kero ya Rushwa Nchini ya mwaka 1996 iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu Joseph Sinde Warioba ililalamikia kile ilichokiita ‘ukaribu wa wafanyabiashara na viongozi wa kisiasa’ ulioanza kujitokeza mwanzoni mwa kipindi cha pili cha serikali ya awamu pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi. Taarifa hiyo ilitoa mfano wa makampuni ya Kigoma Hill Top Hotel, Shenis Commercial Ltd., Tile and Tube Ltd., Royal Frontier (T) Ltd., Game Frontier (T) Ltd. nee MNM Hunting Safaris Ltd., ambayo yalikuwa yanamilikiwa na mfanyabiashara Mohsin Abdallah, mkewe Nargis Abdallah na washirika wao wengine wa kibiashara.
Mohsin Abdallah ni kada maarufu wa CCM na mjumbe wa zamani wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho. Inaelekea kuwa mfanya biashara na kada huyu maarufu wa CCM ameendelea kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya Serikali ya CCM na hasa hasa katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Zaidi ya hayo, inaelekea kwamba, kama ilivyokuwa kwa Tume ya Warioba miaka kumi na saba iliyopita, ushawishi mkubwa alionao kada huyu wa CCM unatoa uvundo na harufu mbaya ya ufisadi.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati Ndogo ya Kamati ya Kudumu ya Maliasili na Mazingira iliyotolewa ndani ya Bunge hili tukufu, “Kampuni tatu zenye majina yanayoelekea kufanana na zina Ofisi katika jengo moja, Royal Frontiers of Tanzania Ltd., Game Frontiers of Tanzania Ltd., Western Frontiers of Tanzania Ltd., … zinaonyesha kuwa wanahisa wa Kampuni hizo wana nasaba za kifamilia hivyo kuleta hisia kuwa lengo la Sheria na Kanuni kuzuia mtu mmoja kumiliki vitalu zaidi ya vitano linapuuzwa kwa ujanja wa kusajili Kampuni mpya kwa malengo fulani…. Kamati ilipata ushahidi wa Maelezo ya Kampuni zinazofanya biashara ya uwindaji wa kitalii kuwa mmiliki wake ni mmoja, na hata maelezo ya baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kumshauri Waziri kuhusu Ugawaji wa Vitalu yanaashiria kuwa kampuni zote hizo zinamilikiwa na mtu mmoja, hali inayoweza kusababisha mtu huyo kupata vitalu vingi kinyume cha Sheria.”
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli mbele ya Bunge hili tukufu juu ya mahusiano yake na mfanya biashara na kada huyu wa CCM ambayo yamepigiwa kelele kwa karibu miaka ishirini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua kama huu sio mfano wa wazi wa ‘maslahi haramu ya kisiasa kwa faida ya kiuchumi ya watu wachache’, basi Serikali iliambie Bunge lako tukufu kuna maslahi gani ya umma katika mahusiano haya.
Mheshimiwa Spika,
Mohsin Abdallah sio mfanya biashara na kada pekee wa CCM mwenye maslahi yenye mashaka katika sekta ya uwindaji wa kitalii. Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya Diallo, makada waandamizi wa CCM wenye maslahi ya aina hii ni wengi na baadhi yao wako humu ndani ya Bunge lako tukufu. Taarifa hiyo inayataja makampuni ya Coastal Wilderness (Tz) Ltd., ambayo wakurugenzi wake wanatajwa kuwa Napono Edward Moringe Sokoine na Namelok Edward Moringe Sokoine; Enzagi Safaris (Tz) Ltd., yenye wakurugenzi Makongoro Nyerere na Mh. Muhamed Seif Khatib; Said Kawawa Hunting Safaris yenye wakurugenzi Chande Kawawa na Hassan Kawawa; na M.S.K. Tours & Hunting Safari Co. ya Mh. Muhamed Seif Khatib.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati Ndogo ya Kamati ya Maliasili na Mazingira, mengi ya makampuni haya yalipewa vitalu vya uwindaji wakati hayana uzoefu wala mtaji wa kuendesha biashara ya uwindaji wa kitalii katika vitalu hivyo. Matokeo yake ni kwamba makampuni hayo yalishindwa kusimamia uhifadhi wa wanyamapori katika vitalu vyao na kusababisha tatizo la ujangili kushamiri katika vitalu hivyo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli mbele ya Bunge lako tukufu ni kwa nini Serikali hii ya CCM imekuwa ikitoa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa makada waandamizi wa CCM ambao wanajulikana kuwa hawana weledi wala uwezo wa kibiashara wa kuendesha biashara ya uwindaji wa kitalii na hivyo kusababisha tatizo la ujangili kuwa kubwa zaidi na kuleta hasara kwa taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
Nchi yetu imeanza kufedheheshwa katika mikutano ya kimataifa ya uhifadhi kwa sababu ya Serikali hii ya CCM kukumbatia makada waandamizi wa CCM wanaojihusisha na ujangili. Kwa mfano katika Mkutano wa 16 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya Wanyama Walio Hatarini Kutoweka (CITES) uliofanyika Bangkok, nchini Thailand mwezi uliopita, Mohsin Abdallah alitajwa na Shirika la Upelelezi wa Masuala ya Mazingira (Environmental Investigations Agency, EIA) kuwa ni mmoja wa majangili wakubwa wanaojihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo lakini Serikali ya Tanzania imeshindwa kumchukulia hatua za kisheria kwa sababu ya ushawishi wake mkubwa katika siasa za ndani ya chama tawala na Serikali hii ya CCM. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni fedheha ya aina gani kimataifa itakayoiamsha Serikali hii ya CCM katika usingizi wake wa pono ili iweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya makada wa CCM wa aina hii?
UKIUKWAJI WA HAKI ZA WAMAASAI
HIFADHI YA ENEO LA NGORONGORO
Mheshimiwa Spika,
Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Loliondo ni moja ya maeneo ya asili ya jamii za Wamaasai. Kwa mujibu wa taarifa za kitafiti za ekolojia ya maeneo haya, Wamaasai wameishi katika maeneo hayo tangu karne ya kumi na nane. Kabla ya mwaka 1959 eneo hili lilikuwa ni sehemu ya maeneo ya Serengeti-Ngorongoro ambayo yalikuwa yakikaliwa na wafugaji wa Kimaasai. Mwaka 1959 Serikali ya kikoloni iliigawanya Serengeti-Ngorongoro baada ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti upande wa magharibi, na Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro upande wa milima ya mashariki ya eneo la ekolojia la Serengeti-Ngorongoro.
Wafugaji wa Kimaasai waliokuwa wakiishi katika maeneo ya Seronera, Moru na Sironet katika upande wa magharibi waliondolewa katika maeneo hayo na kuhamishiwa Hifadhi ya Eneo la Ngoroongoro na Loliondo. Hata hivyo, Serikali ya kikoloni iliahidi kwamba haki za Wamaasai juu ya ardhi za maeneo walikohamishiwa zitapewa kipaumbele na kulindwa na Serikali. Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya kikao cha Baraza la Kutunga la Sheria (LEGCO) cha siku ya Jumatatu ya tarehe 17, Novemba 1953, Gavana wa Tanganyika wa wakati huo alisema yafuatayo: “Wakati eneo hili lilipotangazwa kuwa hifadhi ya taifa, ilitambuliwa kwamba kulikuwa na watu waliokuwa na haki za asili za machungio ya mifugo na maji ndani ya mipaka yake na kwamba haitawezekana kuwaondoa watu hawa kwa nguvu.”
Kauli hii ya Serikali ilitiliwa nguvu na Waraka wa Serikali Na. 1 wa 1956 (Government Sessional Paper No. 1 of 1956) uliochapishwa kufuatia kuongezeka kwa shinikizo la mashirika ya uhifadhi ya kimataifa yaliyokuwa yanataka Wamaasai wafukuzwe katika maeneo ya Serengeti-Ngorongoro: “Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti chini ya Sheria ya Wanyamapori na baadaye kuundwa kwake upya chini ya Sheria ya Hifadhi za Taifa hakukuathiri kwa namna yoyote haki zilizokuwepo za mtu yeyote ndani au juu ya ardhi za Hifadhi. Badala yake, haki hizo sio tu kwamba zililindwa wazi wazi, bali pia Wamaasai waliokuwa tayari wanaishi ndani ya eneo la Hifadhi walipewa ahadi chanya na Serikali kwamba haki zao hazitavurugwa bila ridhaa yao.”
Kufuatia kuchapishwa kwa Taarifa ya Tume ya Uchunguzi juu ya Ngorongoro iliyoongozwa na Sir Barclay Nihill aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, iliyopendekeza Wamaasai wafukuzwe Serengeti na pia katika maeneo ya Kreta za Ngorongoro na Empakaai, Serikali ya kikoloni ilirudia msimamo wake kuhusu haki za Wamaasai wa Serengeti-Ngorongoro katika Waraka wa Serikali Na. 6 wa 1956 (Government Sessional Paper No. 6 of 1956): “Mapendekezo ya kuwa na maeneo tengefu katika Kreta hizo mbili hayakukubalika. Yanaashiria kuondolewa kwa Wamaasai kutoka kwenye maeneo haya mawili. Haikuonekana sawa sawa kuomba ridhaa ya Wamaasai kuachia haki zao ndani ya Kreta hizo mbili wakati huo huo wakiwa wanaachia haki zao ndani ya Hifadhi yenyewe.”
Mheshimiwa Spika,
Ahadi za kulinda haki za ardhi za Wamaasai wa Serengeti-Ngorongoro ziliendelea kutolewa kwa nyakati tofauti na viongozi wa ngazi za juu wa Serikali ya kikoloni ya Tanganyika. Hivyo basi, katika kikao cha Baraza la Kutunga Sheria cha tarehe 25 Aprili 1956, Gavana Sir Richard Turnbull aliliambia Baraza hilo kwamba: “Wakati Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ilipoanzishwa mwaka 1940, ahadi rasmi zilitolewa na Serikali hii kwa Wamaasai. Hii haimaanishi kwa kabila lote la Wamaasai bali wale waliokuwa na haki za kisheria au za asili katika eneo hilo. Nina uhakika kabisa kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kutegemea Serikali hii, au Serikali yoyote ya Kiingereza kuvunja ahadi zake rasmi. Imekuwa ni lazima, kwa hiyo, kupata ridhaa ya Wamaasai kwa ajili ya mabadiliko yanayopendekezwa.”
Miaka miwili baadae Gavana Turnbull alirejea kauli yake hiyo wakati akifungua Mkutano wa 34 wa Baraza la Kutunga Sheria tarehe 14 Oktoba, 1958: “Nadhani ni lazima nichukue fursa hii kusisitiza kwamba kwa misingi yote ya haki na nia njema hakuna Serikali itakayofikiria kuwaondoa Wamasai kutoka maeneo yote ya hifadhi za wanyama za Serengeti na Nyanda za juu za Kreta.” Kama inavyojulikana, baadae Serikali ya kikoloni iliingia mkataba na Wamaasai ambapo Wamaasai walikubali kuhama kutoka maeneo yao ya Sironet, Moru na Seronera ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuhamia kwa eneo jipya la Hifadhi ya Ngorongoro. Kwa maneno ya Gavana Turnbull, “… uhifadhi wa eneo la Ngorongoro utajengwa kuzunguka nguzo ya maslahi ya wenyeji wa eneo hilo.”
Na katika mwaka ambao Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ilianzishwa, yaani 1959, Gavana Turnbull alisisitiza msimamo wa Serikali yake juu uhifadhi wa Ngorongoro kujengwa kwa kuzingatia maslahi ya wakazi wake katika hotuba aliyoitoa mbele ya Halmashauri ya Wilaya ya Maasai mwezi Agosti 1959: “Nataka kuweka wazi kwenu wote kwamba ni nia ya Serikali kuendeleza Crater kwa maslahi ya watu na matumizi yake, wakati huo huo Serikali inakusudia kulinda hifadhi ya wanyama katika eneo hilo, pamoja na kuwepo kwa mgongano wa jamii na serikali bado serikali inathamini na kuheshimu shughuli za jamii na haitaingilia shughuli za wafugaji wa Kimaasai.”
Mheshimiwa Spika,
Makubaliano kati ya Serikali ya kikoloni na Wamaasai wa Serengeti-Ngorongoro yalikuwa ndio msingi wa kutungwa kwa Sheria ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ya 1959. Sheria hiyo iliweka msingi kwamba eneo hilo litakuwa ni eneo la matumizi mseto wa rasilmali ambako Wamaasai wataruhusiwa kuishi na kutumia maeneo ya Ngorongoro kwa ajili ya malisho ya mifugo yao. Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NGorongoro Conservation Area Authority, NCAA) ilipewa majukumu ya kisheria ya kuhifadhi maliasili za eneo hilo na pia kuwaendeleza Wamaasai kiuchumi.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kwa mingi Serikali ya Tanzania imeshiriki katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu za Wamaasai wa Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Loliondo katika Wilaya ya Ngorongoro. Serikali pia imekiuka wajibu wake wa kuwaendeleza Wamaasai wa Ngorongoro kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 1995 na Shirika la Misaada la Denmark (DANIDA), licha ya NCAA kupokea mamilioni ya fedha za kigeni kutokana na utalii unaoendeshwa katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, umaskini katika familia za Kimaasai ulifikia hatua ambayo 50% ya kaya zao zilikuwa na chini ya mifugo saba kwa kaya – ambacho kinachukuliwa kuwa chini ya kiwango cha kujikimu kiuchumi – wakati 40% ya kaya hizo zilichukuliwa kuwa ni fukara kwa maana ya kuwa na chini ya mifugo miwili kwa kaya.
Miaka karibu ishirini baadaye, hali ya kiuchumi na kijamii ya Wamaasai wa Ngorongoro imekuwa ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa wakati wa utafiti huo wa DANIDA. Ushahidi wa suala hili ni Taarifa ya Tume ya Uchunguzi ya CCM iliyoundwa na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana na kuongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Tanzania Bara, Mh. Mwigulu Nchemba iliyosambazwa jana tarehe 29 Aprili 2013. Wajumbe wengine wa Tume hiyo ni pamoja na Mbunge wa Longido Mh. Lekule Laizer, Mbunge wa Simanjiro Mh. Christopher ole Sendeka na Mbunge wa Viti Maalum na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha Mh. Mary Chatanda. Ukimwacha Mh. Chatanda, wajumbe wengine wa Tume hiyo ni wajumbe wa NEC ya CCM. Kwa vyovyote vile, taarifa ya Tume hiyo ya uchunguzi inahitaji kupewa uzito na umuhimu wa kipekee kutokana na uzito kichama wa wajumbe walioiandaa.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba: “Kutokana na ukosefu wa ardhi ya kuendeshea shughuli za kiuchumi, umaskini umekithiri miongoni mwa wakazi wa Ngorongoro kiasi cha kupelekea wakuu wa familia kukimbia familia zao.” Ukosefu wa ardhi unaopelekea umaskini kukithiri ni wa kutengeneza na Serikali hii ya CCM kwani kati ya km2 14,036 ambazo ndio eneo lote la Wilaya ya Ngorongoro, km2 8281 au 59% zimechukuliwa na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wakati km2 870 au 6% zimechukuliwa na Hifadhi ya Misitu ya Nyanda za Juu Kaskazini. Maeneo ya wanyamapori na malisho ya mifugo ni km2 3916 au 30%, wakati maeneo ya kilimo ni km2 435 au 3% ya eneo lote la Wilaya hiyo.
Katika miaka ya mwanzo 2000, NCAA ilipiga marufuku kilimo cha mazao ya chakula katika maeneo ya Nainokanoka na Endulen ambayo yako ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Matokeo ya sera hizi za kuwanyang’anya wananchi wa Ngorongoro ardhi kwa ajili ya mifugo yao na kupiga marufuku kilimo yamekuwa, kwa mujibu wa Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba, ni “… tatizo … sugu la njaa isiyoisha katika Tarafa ya Ngorongoro.” Taarifa hiyo inafafanua zaidi: “Wananchi wa Ngorongoro wana njaa ya muda mrefu ambayo haijapatiwa ufumbuzi. Wananchi hawa hawaruhusiwi kulima ndani ya Hifadhi hivyo hutegemea mgawo wa chakula toka Mamlaka ya Hifadhi.” Ahadi ya Rais Dokta Kikwete kuwa Serikali ya CCM itashughulikia suala la kilimo cha kujikimu ambacho kingewasaidia Wamaasai kujipatia chakula, ahadi hiyo haijatekelezwa licha ya ukweli kwamba “… Mamlaka ya Hifadhi imeshindwa kuwapatia chakula.”
Hivyo, kama walivyosema Profesa Issa G. Shivji na Dr. Wilbert Kapinga katika kitabu chao The Maasai Rights in Ngorongoro, Tanzania, Serikali ya Tanzania, kwa kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, imekiuka sio tu haki za binadamu za Wamaasai wa Ngorongoro, bali pia imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwaendeleza Wamaasai hao kama inavyotakiwa na sheria. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, hiki ndio chanzo cha migogoro ya ardhi ya muda mrefu na isiyomalizika kati ya Wamaasai na Serikali ya CCM na mashirika yake ya uhifadhi wa wanyamapori. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba njia pekee ya kutatua matatizo ya kiuchumi na kijamii ya Wamaasai na migogoro juu ya haki zao za ardhi na rasilmali, ni sharti Serikali iweke utaratibu mpya utakaoruhusu Wamaasai kufaidika na rasilmali za wanyamapori katika maeneo yao kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Kama inavyosema Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba, kuwapatia wananchi wa Ngorongoro mgawo wa shilingi bilioni moja wakati mapato ya Mamlaka ya Hifadhi ni zaidi ya shilingi bilioni 51 kwa mwaka ni ‘dhihaka na kuwapuuza.’
Aidha, utaratibu wa uhifadhi unaosisitiza binadamu na mifugo yao kuondolewa katika maeneo ambayo wameishi pamoja na wanyamapori kwa karne nyingi hauna msingi wowote kisayansi na umepitwa na wakati. Kama walivyowahi kusema watafiti Homewood na Rodgers katika kitabu chao The Maasailand Ecology: Pastoralist Development and Wildlife Conservation in Ngorongoro, Tanzania, hakujawahi kuwa na sababu za msingi za kisayansi za kuwakataza wafugaji wa Kimaasai kutumia rasilmali asili za Serengeti-Ngorongoro kwa ajili ya mifugo yao. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama bado kuna sababu zozote za kuendelea kuwazuia wafugaji wa Kimaasai wa Ngorongoro na Loliondo kutumia maeneo ya malisho ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na maeneo ya Kreta za Ngorongoro, Olmoti na Empakaai na vile vile katika Hifadhi ya Msitu wa Nyanda za Juu za Kaskazini ili kukabiliana na matatizo ya ukosefu wa malisho na maji ya mifugo hasa hasa wakati wa kiangazi.
LOLIONDO, WAARABU NA CCM
Mheshimiwa Spika,
Mgogoro wa ardhi katika eneo la Loliondo ni taswira nyingine ya jinsi ambavyo Serikali ya CCM imekiuka haki za wafugaji wa Kimaasai kwa manufaa ya wawekezaji wa kigeni katika sekta ya uwindaji wa kitalii. Kama tulivyoeleza mwanzoni, kufuatia Wamaasai kuondolewa Serengeti mwaka 1959, baadhi yao walihamishiwa katika Tarafa za Loliondo na Sale na wengine walihamishiwa katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Licha ya ahadi za Serikali ya kikoloni kwamba haki za ardhi za Wamaasai zitaendelea kulindwa katika maeneo hayo, miaka ya uhuru ilishuhudia Serikali ya Tanzania ikianza kuhujumu haki hizo. Hivyo basi, mwaka 1975 Serikali iliwaondoa kwa nguvu wafugaji waliokuwa wakiishi ndani ya eneo la Kreta ya Ngorongoro. Miaka tisa baadaye, kati ya 1983/84, Serikali ilitwaa eneo la Sukenya lenye ukubwa wa ekari 10,716 na kuligawa kwa Kampuni ya Bia Tanzania (Tanzania Breweries Ltd.) Aidha, mwaka 1990 Serikali ilipima vijiji vyote vya Tarafa ya Loliondo na Sale na kuvipatia hati milki ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuvitambua kisheria. Hata hivyo, mwaka huo huo Serikali hiyo hiyo ilitwaa sehemu ya ardhi ya vijiji hivyo na kuimilikisha kwa Kampuni ya Orthello Business Corporation (OBC) inayomiliwa na Brigadia Mohamed Abdulrahim al-Ali anayesemekana kutoka katika familia ya kifalme ya Oman. Mwaka 1992 Serikali hii ya CCM ilipanua “… wigo wa umiliki wa ardhi wa kampuni ya OBC na kuiruhusu kampuni hiyo kuwinda katika vijiji vyote 19 vya Tarafa ya Sale na Loliondo.” Ilipofika mwaka 2003, “mkataba wa OBC na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa niaba ya vijiji ukaisha lakini OBC ikaendelea na uwindaji mpaka sasa.” Licha ya kampuni hiyo kutokuwa na mkataba halali na wananchi wa Loliondo, mwaka 2009 “operation kubwa ilifanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwaondoa wafugaji katika maeneo ya Sale na Loliondo na kupelekea wananchi kuchomewa nyumba zao.” Na mwaka 2011 Serikali ya CCM “ikavitangazia vijiji vyote kurudisha hati miliki za ardhi na pia vijiji vyenye vyeti vya usajili vikaamriwa vivirudishe.” Inaelekea kwamba amri hii ilikuwa ni sehemu ya mwisho ya maandalizi ya kuwanyang’anya wananchi wa Loliondo na Sale ardhi zao kwani mnamo tarehe 26 Machi, 2013 Waziri wa Maliasili na Utalii aliitembelea Wilaya ya Ngornognoro na kuwatangazia wananchi na wakazi wa Loliondo kwamba “ameagizwa na Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, kugawa eneo la Loliondo Game Controlled Area ya zamani katika sehemu mbili: Yaani km2 2500 zimeachwa kwa ajili ya matumizi ya watu kwa kilimo, ufugaji, makazi, etc.; km2 zimechukuliwa na Serikali … ili eneo hilo liwe Game Control (sic!) mpya ya Loliondo.”
Mheshimiwa Spika,
Maelezo yote haya yanatoka katika Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba. Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, Serikali hii ya CCM “… imeamua kumega … eneo la Loliondo Game Control (sic!) Area ya zamani na kulifanya Game Control (sic!) Area mpya, na kwamba eneo hilo sasa litakuwa mali ya mwekezaji OBC kwani analimiliki kisheria.” Aidha, kwa mujibu wa Taarifa hiyo, endapo eneo hilo litamegwa kama ilivyotangazwa na Waziri Kagasheki, “… wakazi wa Tarafa (ya Loliondo) watakuwa wamebakiwa na eneo la km2 265 tu. Eneo hili ni dogo sana kwa wakazi 60,000 waTarafa hii.”
Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba inasema wazi kwamba kauli ya Waziri Kagasheki kuhusu unyang’anyi huu wa wazi wazi wa ardhi ya wananchi ndiyo ‘iliamsha hasira za wananchi.’ Hii ni kwa sababu, “… eneo … wanalonyang’anywa ndilo eneo pekee wanalolitegemea kwa maji ya mifugo na matumizi ya kibinadamu. Kuwaondoa ndani ya eneo hilo ni sawa na kuwauwa. Hivyo wako tayari kufa wakipiginia eneo hilo.” Aidha, “… eneo hilo … ndilo eneo pekee walilolitenga kwa ajili ya malisho ya mifugo hasa wakati wa kiangazi panapokuwa na uhaba wa malisho. Kuwaondoa hapa ni sawa na kuiuwa mifugo yao, jambo ambalo hawako tayari kulishuhudia, bora wafe.”
Mheshimiwa Spika,
Mgogoro kati ya wananchi wa Loliondo na Sale kwa upande mmoja na Serikali na OBC kwa upande mwingine umekuwa ukitokota kichini chini kwa zaidi ya miaka ishirini na tatu. Mgogoro huu ni mali binafsi ya CCM na Serikali zake za awamu ya pili, ya tatu nay a nne ya Dokta Kikwete. Ni mtoto wa ndoa haramu ya CCM na wawekezaji wa kigeni katika sekta ya uwindaji wa kitalii. Mtoto alizaliwa na Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi, akalelewa na baba wa kufikia Rais Benjamin Mkapa na sasa amefikisha umri wa mtu mzima chini ya baba wa kambo Dokta Jakaya Mrisho Kikwete!
Licha ya Serikali ya CCM kuwatukana wananchi wa Loliondo kwa kuwaita Wakenya, ni wazi – kama inavyothibitishwa na Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba – kwamba waathirika wa landgrab hii ni Watanzania wapatao 59,536 wanaoishi katika vijiji vya Ololosokwan, Soit Sambu, Oloipiri, Oloirien/Magaiduru, Arash, Losoito/Maaloni na Piyaya. Vijiji hivi vina shule za msingi na za sekondari zenye wanafunzi 2,302; zahanati nne na nyumba kadhaa za wahudumu wa afya; mashine za maji tatu; na mabwawa ya maji mawili. Maelfu ya wananchi hawa na miundo mbinu iliyojengwa kwa nguvu zao na kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania inatakiwa kutolewa kafara katika hekalu la urafiki wa Serikali ya CCM na mwekezaji huyu wa Kiarabu! Huu ndio uso halisi wa Serikali hii sikivu na inayotaka ‘maisha bora kwa kila Mtanzania’!
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na hoja na ushahidi ambao tumeueleza hapa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya mambo yafuatayo:
- Kama kampuni ya OBC ina haki zozote za ardhi katika maeneo ya Kata za Loliondo na Sale licha ya ukweli kwamba maeneo hayo yalikwishapimwa na wananchi kumilikishwa kihalali, na vijiji vyao kupatiwa usajili halali kwa mujibu wa sheria za nchi yetu;
- Kama ni halali kwa kampuni ya OBC kuendesha shughuli za uwindaji wa kitalii katika vijiji vyote 19 vya Tarafa ya Loliondo na Sale wakati eneo ililopewa kwa ajili mwaka 1990 lilihusu sehemu ndogo tu ya maeneo ya vijiji hivyo;
- Kama kampuni ya OBC inaendesha shughuli za uwindaji wa kitalii katika maeneo ya Loliondo kihalali licha ya ukweli kwamba mkataba wake na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa niaba ya wananchi wa Loliondo ulikwisha muda tangu mwaka 2003;
- Kama ilikuwa halali kwa Serikali kuwahamisha wananchi wa Loliondo kwa nguvu na kuwachomea nyumba zao moto mwaka 2009, na baadaye kudai wananchi hao ni raia wa Kenya. Kama Serikali hii ya CCM itakiri kwamba vitendo hivyo vya kinyama havikuwa halali, basi itoe kauli kama iko tayari kuwaomba radhi na kuwalipa fidia kwa mujibu wa sheria za nchi yetu wananchi wote wa Loliondo na Sale waliodhalilishwa kwa kuitwa raia wa Kenya na kuathirika na unyama huo;
- Kama Serikali hii ya CCM iko tayari kuwachukulia hatua za kisheria, au kiutendaji au kinidhamu wale wote walioamuru na au kushiriki katika vitendo vya kuwaondoa kwa nguvu wananchi wa Loliondo na Sale na kuwachomea nyumba zao moto pamoja na kuwatendea vitendo vya udhalilishaji au ukiukaji wa haki zao za kibinadamu;
- Kama ni kweli kwamba kitendo cha hivi karibuni cha Waziri Kagasheki kutoa amri ya wananchi wa Loliondo na Sale kunyang’anywa maeneo yao mengine na maeneo hayo kukabidhiwa kwa kampuni ya OBC kilitokana na maagizo au maelekezo ya Mh. Rais Dokta Jakaya Mrisho Kikwete au yalikuwa na Baraka zake kama inavyodaiwa na Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba;
- Kama huu sio wakati muafaka kwa Waziri Kagasheki kuwajibika kwa kujiuzulu kwa hiari yake au, kama atashindwa kufanya hivyo, kuwajibishwa kwa kufukuzwa kazi kwa kusababisha mgogoro wa sasa katika maeneo ya Loliondo na Sale;
- Kama, licha ya ushahidi wote ulioibuliwa na Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba na licha ya upinzani mkubwa wa wananchi, bado kuna sababu ya kuendelea kuiruhusu kampuni ya OBC kuendesha shughuli zake katika maeneo ya Loliondo na Sale;
- Kama, licha ya ushahidi wote ulioibuliwa na Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba kwamba chanzo cha migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro ni sera za Serikali hii ya CCM, ni halali kwa Serikali na CCM yenyewe kuendelea kuyalaumu mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ya kutetea haki za binadamu na za wafugaji wa Kimaasai kuwa yanachochea vurugu za wananchi wa Loliondo na Ngorongoro;
- Kama, baada ya mambo yote yaliyoeleza hapa, Serikali hii ya CCM iko tayari kusitisha uamuzi wake wa kuwanyang’anya wananchi wa Loliondo na Sale maeneo yao na kuyamilikisha kwa kampuni ya OBC au kampuni nyingine yoyote katika siku za mbeleni;
Kama alivyopata kusema Dalai Lama: “Lengo letu kuu katika maisha haya ni kuwasaidia watu wengine. Na kama hatuwezi kuwasaidia, basi angalau tusiwaumize.” Serikali hii ya CCM ilikuwa na bado ina wajibu kisheria kuwasaidia Wamaasai wa Wilaya ya Ngorongoro kwa kuwaendeleza kiuchumi na kijamii. Kama imeshindwa kufanya hivyo, kama ilivyoonyeshwa katika Maoni haya, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM angalau iache kuwaumiza wananchi hawa kwa kuwaachia ardhi zao!
UJANGILI
Mheshimiwa Spika,
Madhara makubwa ya ujangili inawezekana kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na mfumo wa kiuwajibikaji ambao hauko wazi, kwani mtu anayetoa vibali au anayejua ni mnyama gani anatakiwa kuwindwa ni Afisa wanyamapori wa Wilaya(DGO), ambaye kiuwajibikaji yupo chini ya Mkurugenzi wa halmashauri. Taasisi inayowajibika kwa wanyamapori ni Wizara ya Maliasili na Utalii, tunaweza kuona mfumo ulivyo na nani anatakiwa kuwajibika kwa nani na mazingira gani wanafanyiakazi na wawindaji wanauzito gani kifedha.
Mheshimiwa Spika,
Ujangili pia unazidishwa na kutokuwepo kwa askari wa kutosha. Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri hapa Bungeni, “… Idara ya Wanyamapori inasimamia Game Reserves 28, inasimamia Game Controlled Areas zaidi ya 40, kwa ujumla inasimamia maeneo yenye zaidi ya kilomita za mraba laki mbili. Vigezo vya Kimataifa kwa ajili ya ulinzi peke yake vinasema kwamba Askari mmoja wa wanyamapori anapaswa alinde eneo lisilozidi kilomita za mraba 25. Kwa hiyo, kwa kilomita za mraba laki mbili unajikuta kwamba Askari tuliopaswa kuwa nao karibia Askari 8,400. Hivi tunavyozungumza Askari tulionao hawafiki 1,700 kwa Tanzania nzima.”
Mheshimiwa Spika,
Kwa tafsiri ni kwamba ni rahisi kwa askari waliopo kukaa kwa muda mrefu katika eneo moja na matokeo yake ni kuwapa majangili ratiba nzima ya mfumo wa ulinzi na mienendo ya wanyama. Kwa mfano hifadhi nzima ya Katavi ina wafanyakazi 45 tu, eneo lake ni karibu ha.10,000. Eneo hilo halina mawasiliano ya aina yoyote na ratiba ya tembo kutoka eneo moja kwenda lingine inajulikana kwa majangili. Hapa ni dhahiri kuwa mauaji ya tembo yanayofanyika ushiriki wa watendaji hauwezi kuepukwa?
Ujangili na silaha za Kivita
Mheshimiwa Spika,
Kumekuwepo na malalamiko mengi toka kwa watendaji kuwa majangili wanatumia silaha za kivita katika kutimiza azma yao. Kambi Rasmi ya Upinzani inaliona hili kuwa ni jambo la kimtandao zaidi. Kwani tunaamini kuwa taasisi zenye uwezo wa umiliki wa silaha hizo ni jeshi la polisi na jeshi la wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Upatikanaji wa silaha hizo kwa majangili ni lazima kuwe na uhusiano wa moja kwa moja na baadhi ya watendaji katika majeshi hayo mawili. Hili linazidisha hofu kutokana na ukweli kwamba tembo wanazidi kuuawa na TANAPA hawana silaha za kukabiliana nazo, silaha zilizoagizwa zimezuiwa kwa ajili ya kulipiwa ushuru, na hilo linawezekana ni kosa la maksudi la kimtandao ili kukwamisha upatikanaji wa silaha za kukabiliana na ujangili. Utaratibu wa kuagiza silaha unajulikana kuwa jeshi ndilo lenye jukumu hilo.
Mheshimiwa Spika,
Mtandao wa ujangili ni mkubwa sana kwani upo katika uuaji, usafirishaji, masoko, polisi, TRA na mahakama. Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya mahakimu wa mahakama za wilaya katika mikoa ya Mara, Simiyu, Shinyanga,Katavi na Kigoma ni sehemu ya mtandao huo kwani watuhumiwa wengi wanaokamatwa na nyara zikiwemo silaha hupewa dhamana na hawarudi mahakamani. Mfano, mtuhumiwa aliyekamatwa kwa tuhuma za kuwinda faru, nyani na ngiri ndani ya hifadhi ya serengeti mwaka 2010, madubu Masunga Dusara (33) mkazi wa Ng’walali haonekani mahakamani baada ya hakimu mkazi wa mahakama ya shinyanga, Lydia Ilunda kumpa dhamana kwa masharti nafuu.
Kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali itoe taarifa kwanini wale waliotajwa katika ripoti ya ujangili wameweza kupewa nafasi kubwa ya uongozi wa nchi hii? Biashara ya pembe za ndovu inamilikiwa na nani? Usafirishaji wa pembe hizo na nyaraka nyingine unaratibiwa na magenge gani katika bandari na viwanja vya ndege? Ni kwa kiasi gani vyombo vya serikali kama jeshi la Polisi, usalama wa taifa na mamlaka ya mapato nchini (TRA) vinahusika?
Mheshimiwa Spika,
Mwezi Desemba shehena yenye tani 1.3 ya meno ya Tembo iliyofichwa kwenye magunia ya Alizeti ilikamatwa na Maafisa wa Forodha wa HongKong, Shehena hii ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni moja na nusu, pia wiki mbili kabla ya hapo takribani tani nne za meno ya Tembo zilikamatwa huko huko Hong Kong. Kwa matukio haya mawili, hawa ni sawa na Tembo 900 waliouwawa. Aidha, katika mwezi Desemba 2012 Polisi mkoani Arusha walikamata nyara nyingi za Serikali katika eneo la Kisongo, zikiwemo ngozi za Simba na wanyama wengine, pembe za ndovu na wanyama wengine na vichwa vya wanyama. Nyara hizi zilikuwa tayari kwa kuuzwa nje ya Nchi, vivyo hivyo mkoani Katavi walikamatwa majangili kadhaa na kuachiwa huru kwa amri kutoka juu kwa mujibu wa taarifa za maafisa wa wanyama pori.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika mjadala wa makadirio ya bajeti ya mwaka 2012/2013 ilizungumza sana juu ya hali tete iliyopo katika usalama wa wanyamapori kwa ushahidi wa kutosha ili kuweza kuisaidia serikali katika kulinda rasilimali asili ya wanyamapori kambi rasmi ya upinzani ilichoambulia kwa serikali ni kubezwa na kudhalilishwa na sio kupokea maoni yetu na kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika,
Wakati hivi karibuni nchini Kenya watetezi wa hifadhi waliishinikiza serikali kuanzisha sheria kali dhidi ya ujangili ili kuwepo na adhabu stahiki, pili idara ya wanyamapori ya kenya (KWS) na wahifadhi maliasili kutangaza teknolojia mpya ambayo itasaidia kupambana na ujangili kama ilivyotangazwa na Daily Nation ya tarehe 26 March 2013, na tatu serikali ya Kenya kuongeza askari zaidi ya 1,000 ili kukabiliana na ujangili, haya yote yakifanyika Kenya kukabiliana na ujangili, Serikali ya Tanzania inaendelea kulinda majangili ambao taarifa zao zimekuwa zikizifikia mamlaka zilizo chini ya serikali.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani bungeni inapenda kutoa rai kwa serikali, pamoja na kejeli na udhalilishaji kwa kambi yetu ya kuashiria kuwa na chuki ya wazi na CHADEMA, hili halina tija kwa wananchi waliowachagua, ni vema wakarejea kuwa na uzalendo kwa nchi yetu na kuona umuhimu wa kulinda rasilimali zetu na kuwafanya watanzania wanufaike na rasilimali hizo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa za kanzidata ya mfumo wa taarifa za biashara ya tembo, Elephant Trade Information System (ETIS) kwa kipindi cha mwaka 2002 hadi 2012, Tanzania katika matukio ya kukamatwa kwa shehena za pembe za ndovu kwa matukio 23 sawa na asilimia 28% ya shehena zote kubwa duniani, kwa takwimu hizo imethibitika kuwepo mauaji ya tembo 24,000 kwa shehena zilizokamatwa za pembe za ndovu, hivyo Tanzania kuwa ni nchi inayotoa pembe za ndovu kwa wingi duniani.
Mheshimkiwa Spika, kwa mwaka 2012 tu shehena zilizokamatwa nchini Hong Kong zenye uzito wa kilo 1,330 pia kwa mfululizo kuwepo kwa shehena zilizokamatwa kwa nyakati tofauti nchini Vietnam kilo 6,232 mwezi March 2009 na 2005. 6 mwezi August, pia nchini Ufilipino (Philippines) kilo 3,346, mwaka 2011, Malaysia, na nchi nyingine duniani, kwa matukio haya baadhi na kutokuwepo kwa hatua zozote zinazochukuliwa ni dhahiri Dola imekuwa ni mhusika mkubwa wa kulinda tatizo hili la ujangili na hivyo kuendelea kuwa na walakini na kutokuhusika kwa dola kuchochea tatizo la ujangili kuendelea kuwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio hasi kwa nchi kwa takribani miaka saba ijayo Tanzania itakuwa na historia ya kuwa na akiba ya tembo, ikiwa tafiti za mwenendo wa mauaji ya tembo kuonesha kukua na kuashiria mauaji kufikia 10,950 kwa mwaka huu wa 2013, ni dhahiri juhudi za kutokomeza ujangili zilizopo zitatufikisha mwaka 2020 tukiwa hatuna akiba ya tembo hata mmoja tena.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kutoa rai kwa serikali kama ilivyotoa katika hotuba ya bajeti ya mwaka jana, kwamba kuna haja ya kuangalia upya mfumo mzima wa ulinzi wa wanyamapori kama kweli serikali inayo nia ya dhati ya kukabiliana na taizo la ujangili nchini.
Kwanza Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kuchukua hatua dhidi ya tatizo la ujangili kwa nia ya kizalendo kwa nchi, ni vema sasa serikali ikaanza kujitathmini yenyewe na viongozi ndani ya serikali na chama cha mapinduzi juu ya tuhuma zilizopo kwa viongozi wake kuhusishwa na ujangili ili kuweza kutoka nje kwa ujasili kushughulikia tatizo hilo baada ya kuwajibisha viongozi wahusika na kuacha watendaji na viongozi safi ndani ya serikali na chama watakao shughulikia pasipo kuwa na haya.
Mheshimiwa Spika, pia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuona umuhimu wa kurejea sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 kifungu cha 103 kinachohusu adhabu kwa makosa ya yanayohusu umiliki wa silaha zinazotumiwa na shughuli za ujangili kuifanyia marekebisho ili adhabu kali zaidi zitolewe kuliko sheria inavyosema kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni pia inaitaka serikali kushirikisha wadau wa ulinzi hususani jeshi la Wananchi (JWTZ) kushiriki katika ulinzi wa wanyamapori kutokana na mamlaka za hifadhi na jeshi la polisi kuzidiwa nguvu na mitandao ya ujangili ambayo imekuwa ikitumia silaha kubwa za kivita katika shughuli za ujangili.
SEKTA NDOGO YA WANYAMAPORI
Mheshimiwa Spika,
Shoroba (corridor za wanyama –Mapitio ya Wanyama) zote za wanyama nilazima zilindwe kikamilifu, hii ni kutokana na ukweli kuwa wanyama huwa wanaendelea kupita njia ile ile wakati wote wa maisha yao na katika mapito hayo ndio pia hupata muda wa kuzaliana. Mbali na hilo ni pia katika shoroba hizo majangili ndipo hutumia mwanya huo kuwaua. Aidha, pamoja na umuhimu wa Shoroba hizi za wanyama serikali imekuwa ya kwanza kuziharibu na mfano ni ushoroba uliopo Mvomero ambako yalikuwa ni mapito ya Tembo serikali imejenga jengo la Mkuu wa Wilaya na Halmashauri kwenye eneo hilo, na ni hivi majuzi tu Tembo aliyekuwa anapita eneo hilo iliamriwa auwawe na maaskari wa wanyama pori baada ya kukwama njiani kutokana na kukosa njia eneo hilo, pia upo mfano wa shoroba iliyopo kati ya Tarangire na Manyara inayopitia njia ya Mijingu nayo imevamiwa na kaya za watu wasiozidi 22 na kufunga njia hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ambayo inasema kuwa inahifadhi uhalisia wa mazalia ya wanyamapori wetu, inakuwaje wataalam wetu na Serikali badala ya kulinda wanakuwa ndio waharibifu wakubwa? Hifadhi ya Taifa Rubondo ni hifadhi ambayo ni Kisiwa kinachoundwa na visiwa tisa vidogo vidogo ambapo kisiwa hiki cha Rubondo ni makazi na mazingira muafaka ya kuzaliana Samaki wakiwemo Sato na Sangara wenye ukubwa wa uzito wa kilo hadi 100. Wanyama wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni pamoja na Viboko,Pongo, Nzohe, Fisi maji, Mamba na Pimbi, wanabadilishana makazi na wanyama wengine waliohamishiwa katika hifadhi hii kama Sokwe, Tembo, Mbega weusi na weupe na Twiga.
Mheshimiwa Spika,
Kukosekana kwa shoroba za kuwafanya wanyama waweze kutoka na kurudi katika hifadhi ni tatizo kubwa kijenetik, kutokana na utafiti uliofanyika unaonyesha kuwa kitendo cha wanyama kukaa eneo moja kwa muda mrefu na kuzaliana wenyewe kwa wenyewe kunaweza kuadhiri wanyama hao. Hili linatokana na ukweli wa kibailojia kuwa uzaliano wa kindugu (In breeding) una madhara makubwa kwa jamii kwani kama kwenye familia ina magonjwa ni dhahiri kuwa familia nzima itakuwa na magonjwa hayo na vivyo hivyo, kwa hifadhi ambazo wanyama wake wametengwa na kufungiwa sehemu moja. Hii ni hatari kwa muendelezo mahiri wa hifadhi hiyo.
TAASISI YA UTAFITI WA WANYAMAPORI-TAWIRI
Mheshimiwa Spika,
Uwekezaji katika tafiti umeendelea kuwa ni vigumu kwa serikali yetu hususani katika sekta ya wanyamapori kutokana na kutokuwa moja ya vipaumbele vya serikali, na hii ni kutokana na dhana ya serikali kutotambua umuhimu wa rasilimali hizi kwa maendeleo ya uchumi wa nchi,taasisi ya utafiti wa wanyamapori ambayo ni TAWIRI na inafanyakazi zake lakini kutokana na kutokupatiwa fedha za kutosha za kufanya tafiti zake kwenye sekta ya wanyamapori kumepelekea taarifa muhimu na za maana kutokupatikana hapa kwetu kwa maendeleo ya sekta ya wanyamapori, badala yake tafiti muhimu kwenye sekta hii zinafanyika kwa ufadhili toka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa huu ni udhaifu kwa nchi ambayo inapata mapato mengi kupitia sekta hii na kutowekeza zaidi katika utafiti wa sekta hii, kwa mfano kwa mwaka wa fedha 2011/2012 makusanyo sekta wanyamapori yalikuwa kiasi cha shilingi 15,074,053,972.10 na kwa mwaka wa fedha 2012/2013 makisio yalikuwa shilingi 25,175,381,917.00 Hizi ni fedha nyingi kwa sekta ambayo uwekezaji katika sekta hiyo ni karibia na hakuna, kuna haja ya serikali kuona umuhimu wa kujitathmini zaidi na kuona ni muhimu zaidi kwa maendeleo ya sekta ya wanyamapori kuwa na fungu maalumu kwa ajili ya kuwezesha tafiti mbalimbali.
Mheshimiwa Spika,
Kuna taasisi ambayo imepewa dhamana ya kuratibu na kuwezesha tafiti mbalimbali hapa nchini ambayo ni COSTECH, lakini cha ajabu ni kwamba taasisi hii imekuwa haitoi kipaumbele kwa watafiti ambao wanafanya utafiti kwenye sekta hii ya wanyama na badala yake utafiti unaegemea sana fedha za mashirika ya nje ambayo yanakuwa na haki zote za tafiti husika. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka vipaumbele kwa kuangalia mchango wa sekta kwenye uchumi husika ambako tafiti zitafanyika.
MAHUSIANO KATI YA TANAPA NA JAMII ZINAZOZUNGUKA MBUGA
Mheshimiwa Spika,
Wananchi wanaozunguka Mbunga za hifadhi ndio wenye jukumu kubwa la kuhakikisha ulinzi wa wanyama. Hivyo basi, mahusiano kati ya Mbuga na wananchi ni muhimu sana. Mipaka ya hifadhi iliyowekwa miaka hiyo wakati idadi ya wananchi katika vijiji mbalimbali ilikuwa ni ndogo na hivyo mipaka ya hifadhi ilikuwa ndani ya vijiji na shughuli za vijiji hazikuwa na madhara katika hifadhi hizo. Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wananchi katika maeneo hayo na shughuli zao za kiuchumi kuwa kubwa na hivyo kupelekea maeneo ya hifadhi kutumiwa.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha uhifadhi wa wanyama wetu unaendelea vyema, ni lazima ushirikishwaji wa wananchi katika zoezi lolote la kuweka mipaka ya hifadhi au kuchukua mipaka iliyokuwepo miaka ya sitini ni muhimu, pia ni bora kuangalia kama nchi tuangalie jukumu letu la msingi ni nini kati ya kulinda raia wake au kulinda wanyama?
Mheshimiwa Spika, Mbuga ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha inapakana na jamii kubwa na kwa sasa kuna mgogoro wa ardhi baina ya TANAPA na wananchi wa Ruaha kwa kuwanyang’anya ardhi yao hasa kwenye kata ya Rwembe, na hivyo kuwafanya wananchi kushindwa kufanya shughuli za maendeleo kama vile kilimo na wakati hawana njia nyingine ya kupata kipato chao cha kijikimu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa kauli kuhusiana na madhira haya wanayopata wananchi wa kata ya Rwembe ambao vijiji vyake vinne wamezuiliwa wasifanye shughuli yoyote ya maendeleo na uongozi wa TANAPA.
I: USHIRIKISHWAJI WA JAMII KATIKA UHIFADHI WA WANYAMAPORI NA MALIASILI (WILDLIFE MANAGEMENT AREAS-WMA).
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa jamii zinashiriki na kunufaika na maliasili zetu hasa wanyamapori na kukuza uhifadhi wa wanyamapori nje na maeneo ya makazi yao hivyo kuanzisha Maeneo ya Jumuiya ya Usimamizi Wanyamapori (WMA). Kazi kuu za WMA ili kuwa ni kuhamishia usimamizi wa Maeneo ya Jumuiya ya Usimamizi Wanyamapori kwa wananchi vijijini na hivyo basi kuulinda ushoroba wa wanyama, njia za uhamaji, maeneo ya usalama wa wanyama, na kuhakikisha kwamba jamii zilizo katika maeneo hayo ya wanyama zinafaidika vilivyo kutokana na uhifadhi wanyamapori. Kuzuia matumizi haramu ya wanyamapori nchini kote kwa kuchukua hatua endelevu za usimamizi, ulinzi na kutekeleza sheria.
Mheshimiwa Spika, kitendo chochote kitakachofanyika cha kuzifanya hizi WMA kushindwa kufaidika na uwekezaji wa wananchi katika hilo ni hujuma kwa na wananchi na kinapelekea wananchi badala ya kuwa wasimamizi wanakuwa wahujumu.
Mheshimiwa Spika, MBOMIPA ni kifupi cha chenye maana ya – matumizi bora maliasili IDODI na PAWAGA ina undwa na vijiji 21 kama wanachama waanzilishi. Vijiji vyote vipo katika Tarafa za Idodi na Pawaga Wilaya ya Iringa. ilianzishwa mwaka 1998 iko Mashariki ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Asasi ya MBOMIPA inasimamia eneo lenye ukubwa wa km za mraba 773. Eneo hili lina aina na idadi kubwa ya wanyama wakubwa, wadogo, ndege na madhari nzuri ya kuvutia kandokando ya mto Ruaha ambao ndio Mpaka na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Mheshimiwa Spika, matatizo yanayoikumba asasi hii ya WMA yanaakisi asasi zingine za uhifadhi za wananchi. MBOMIPA ilipata mwekezaji tangu mwaka 2008 anayeitwa Kilombero North Safari (KNS) kwaajili ya ujenzi wa hoteli na lodges za kitalii. Mwekezaji huyu hajajenga hoteli yoyote hadi sasa na amekuwa akiwadanganya wananchi na Jumuiya juu ya ujenzi wa hoteli kulingana na makubaliano na MBOMIPA. Mwekezaji huyu pia amekuwa akilazimisha kufanya shughuli ya Uwindaji kwenye kanda hiyo na kukiuka sheria ya uwindaji na Resource Zone Management Plan (RZMP) ambayo imepitishwa na MBOMIPA kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, Ujangili ni mkubwa sana hasa wa tembo kwenye kanda ambayo inasimamiwa na Mwekezaji huyu, na hata tarehe 20 na 21 April 2013 wameuwawa tembo 4 wakubwa karibu kabisa na kambi ya mwekezaji (KNS) na meno yote kuchukuliwa na Majangili. Hili suala linajulikana kwa watendaji karibu wote wa Serikali, hii inatokana na maslahi na mahusiano binafsi kati ya wahusika na wamiliki wa Kilombero North Safari. Taarifa zilizopo ni kwamba, kampuni ya kilombero hunting ina wanahisa ambao baadhi yao ni wajumbe wa bodi ya asasi ya MBOMIPA ambao pia ni wafanyabiashara wawili maarufu iringa, mbunge mmoja na mfanya biashara maarufu nchini ambaye mdogo wake ACRAM AZIZ ni msimazi wa karibu kwa niaba ya kaka yake. Hii ndiyo siri ya ubabe wa kampuni ya kilombero North safari katika eneo la LUNDA ndani ya eneo la MBOMIPA.
Mheshimiwa Spika, Usimamizi wa eneo la Asasi ya MBOMIPA unakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na vitendo vya rushwa vinavyofanywa na kampuni zinazotaka kupata maeneo ya uwindaji hasa KAMPUNI YA KILOMBERO HUNTING SAFARI na nyingine ambayo inatoa rushwa kwa baadhi ya wajumbe wa bodi ya MBOMIPA, Afisa wanyamapori (W) Iringa, baadhi ya Viongozi wa Vijiji na Wajumbe wa Vijiji kwenye Asasi.
Mheshimiwa Spika, Kiini cha Mgogoro na migongano inayotokea kwenye eneo la asasi linasababishwa na maslahi ya Wawindaji na siyo suala la Uhifadhi endelevu wa eneo husika. Kwa kuwa lengo ni Uhifadhi wa Wanyama pori na mazingira yao, mgogoro huo utaisha pale tu ambapo jumuiya hii itaondokana na kuachana kabisa na shughuli za uwindaji katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa, eneo la MBOMIPA kuendelezwa kwa shughuli za Utalii wa Picha ambazo ni endelevu, na ipige marufuku shughuli zote za uwindaji. Aidha ifanye ukaguzi maalum kwa WMA hiyo ili kubaini mwenendo wa asasi hiyo kama unazungatia maslahi mapana na uanzishwaji wake hatua za haraka zichukuliwe ili kunusu raslimali za nchi kuishia kwenye mifuko ya wahujumu uchumi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa taarifa ni kwa kiasi gani makubaliano kati ya WMA na kampuni ya Kilombero North Safari yametekelezwa kwa kiwango gani?
UKUSANYAJI WA MADUHULI
Mheshimiwa Spika, katika ukusanyaji wa maduhuli ndani ya idara mbalimbali kumekuwepo na baadhi ya takwimu zinazoashiria ubadhirifu wa rasilimali za umma kwa kuzingatia viwango vinavyotajwa kwenye makadirio ya makusanyo,ukisoma katika randama ya wizara iliyowasilishwa ndani kamati, kifungu namba 1001-idara ya utawala na usimamizi wa rasilimali watu kinatoa kiasi cha fedha zinazotarajiwa kukusanywa kutokana na vyanzo vya mapato kwa mwaka 2013/2014.
Mheshimiwa Spika,kwa mfano taarifa inaonesha makusanyo katika mauzo ya vifaa chakavu ni shilingi 1,000 (Elfu moja)mapato yatokananyo na mauzo ya vifaa sh 1,000 (Elfu moja),Masurufu ambayo hayajarejeshwa sh 1,000 (Elfu moja) pia katika kifungu cha 2001 mapato mengine sh 1,000 (Elfu moja) kwa kutokuwa makini na watendaji wa wizara na kutumia mbinu chafu kuiba rasilimali za umma kwa kuweka viwango vidogo vya makadirio ya ukusanyaji huku takwimu hizi kutokuakisi uhalisia ni dhahiri taifa litaendelea kutafunwa na baadhi ya watendaji wasio waamininfu.
Mheshimiwa Spika, kwa akili ya kawaida wizara haiwezi kufanya kazi ya kukusanya shilingi elfu moja kwa mwaka mzima na huu ni mfano wa maeneo machache kwa kuonesha tabia hii kukithiri ndani ya serikali kwa wahujumu na kujificha katika mgongo wa serikali kutopata mapato ya kutosha huku mapato yakipatikana kwa kiwango kikubwa na bila taarifa zake kuwekwa wazi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutolea ufafanuzi hujuma hii inayofanywa na watendaji na ni kwa vipi wizara inadhibiti taarifa za makadirio ya maduhuli kwa kuhakiki ili ziwe na uhalisia zaidi kuliko hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2012 serikali imeendelea kutoa vibali vya kuendelea na uwindaji kwa kampuni zilizokuwa na malimbikizo ya madeni, mfano kampuni saba za uwindaji: M/S Malagarasi Hunting Safaris, Mwanahuta & Company Limited, Usangu Ltd, Rana Tours & Safaris Ltd,Coastal Wilderness (T) Ltd, Kilimanjaro Game Trails Ltd na Said Kawawa Hunting Company Ltd kampuni hizi kwa jumla zikidaiwa na wizara jumla ya dola za kimarekani 973,493.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa maelezo ya kina juu ya sababu za kutoa vibali pamoja na kampuni hizi kushindwa kulipa maduhuli kwa wakati na kuendelea kuruhusiwa kufanya shughuli za uwindaji.
Mheshimiwa Spika, pia wawindaji halali waliopewa leseni wamekuwa wakifanya shughuli za uwindaji na kufikia mwisho wa mwaka 2012 bado serikali haikukusanya maduhuli yenye jumla ya dola za kimarekani 216,000 na kuisababishia hasara serikali, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inachelea kulithibitishia bunge kuwa ni vitendo vya rushwa vinavyoifanya serikali ikose mapato na mapato hayo kuingia mifukoni mwa watumishi wasio waaminifu ndani ya wizara, hivyo basi Serikali itoe ufafanuzi wa kina nini tafsiri yake kama siyo ruhusa?.
SEKTA NDOGO YA UTALII
Mheshimiwa Spika, Taarifa za upotevu wa mapato ya serikali imeendelea kuonekana katika sekta ya utalii kupitia ada ya Utalii isiyokusanywa, Dola za Kimarekani 158,000 kwa mujibu wa Kanuni Na. 4 ya Kanuni za Utalii (ada na tozo) za mwaka 2009 inaeleza kuwa “ada ya leseni kwa kila daraja italipwa kila mwaka kwa kiasi ambacho kimeainishwa katika Jedwali la Pili la Kanuni hizo”. Mapitio ya makusanyo ya mapato yatokanayo na Leseni za Uendeshaji wa Huduma za Utalii katika Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2011/2012 yameonyesha kuwepo kwa Kampuni zilizojiingiza kwenye biashara ya kutoa huduma ya utalii lakini hawajalipa ada ya Leseni za Utalii yenye jumla ya Dola za Kimarekani 158,000.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano, malengo ya kiutendaji ni kuboresha mfumo wa makusanyo ya mapato yatokanayo na shughuli za utalii. Kambi ya Upinzani inauliza kama mambo yaliyowazi ya ukusanyaji yanashindikana, huo mfumo utaboreshwa vipi wakati hujuma inafanywa kwa ushirika na watendaji?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa maelezo ya kina ni kwa jinsi gani imehakiki ili kutorudiwa kwa matatizo haya ya kupoteza mapato. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri serikali kuchukua hatua kwa watendaji wasiozingatia sheria na kanuni katika kutimiza majukumu yao maana utaratibu huu ni hujuma inayofanywa na wafanyabiashara na watendaji wasio waaminifu kwa umma.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mpango wa maendeleo, unaonyesha kuwa kwa mwaka huu wa fedha uwekezaji kwenye sekta ya utalii ni shilingi bilioni 43.968 wakati kitabu cha bajeti fedha zilizotengwa za maendeleo katika sekta ya utalii inaonyesha shilingi bilioni 1 tu sawa na asilimia 2.2 tu ya fedha zilizotengwa kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza kwa nini hili limekuwa hivi? Na nini tafsiri ya kuwa na mapango wa maendeleo wa taifa kama hatuwezi kuutekeleza? ni kweli sekta hii itaweza kuwa shindani na wenzetu katika jumuiya ya Afrika ya Mashariki au tupo tukisubiri miujiza? Kama si dharau kwa ofisi ya rais idara ya mipango ni nini hiki?
L: SEKTA NDOGO YA MISITU NA NYUKI
Misitu
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kitabu cha Transforming the informal Sector, How to overcome the Challenges (ESAURP) kinaainisha takwimu za ukubwa wa eneo la misitu Tanzania ikiwa ni hekta million 33.5 za misitu ambayo ni sawa na asilimia 38% ya eneo la ardhi yote nchini,pia kinaainisha mchango mkubwa unaoweza tolewa na sekta ya misitu katika uchumi kwa kuirasimisha sekta hiyo kuweza kuweka mazingira bora ya ajira kwa wananchi ikizingatiwa shughuli za misitu ni moja ya chanzo kikubwa cha kipato kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Spika, na kwa mujibu wa taarifa za TRAFFIC 2007 zinaanisha kuwa ni asilimia 4 tu ya mazo ya misitu huvunwa kihalali na asilimia 96 huvunwa bila kupata vibali rasmi na serikali kukosa mapato kwa uvunaji mkubwa unaofanywa kutokana na kutorasimisha biashara ya mazao ya misitu na kuwa na utaratibu ulio rasmi wa kufuatailia uvunaji wa mazao haya ya misitu, Kambi rasmi ya Upinzani bungeni inaitakla serikali kuona umuhimu wa kuona aslimia kubwa ya wananchi wanaotegemea bidhaa za misitu kuendesha maisha yao kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, katika hizo asilimia 96 ambazo huvunwa bila ya kupata kibali, kuna miti ambayo inavunwa kwa ajili ya uchomaji wa mkaa, kwa mujibu wa tafiti zilizokwishafanyika, sekta ya mkaa huingiza zaidi ya dola milioni mia sita na hamsini sawa na zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwaka na kuajiri mamilioni ya watanzania hususani waishio vijijini. Ni wazi kuwa sekta hii imeachwa bila mikakati na sheria unganifu. Kama nilivyoeleza kwa kina katika hotuba yangu ya wizara ya mazingira, Tanzania tunapaswa kujifunza kutoka Brazil ambayo inazalisha mkaa asilimia 11% na Tanzania pekee inazalisha asilimia 3% ya mkaa wote unaozalishwa duniani. Sekta hii ikiwekewa mikakati mizuri ya makusudi itaweza kuzalisha mikaa kwa njia ya kisasa huku ikipunguza hewa ya ukaa na kuifanya sekta hii kuwa endelevu.
Mheshimiwa Spika, Brazil huzalisha asilimia 11% ya mkaa wote unaozalishwa duniani. Kwenye miaka ya 1990 asilimia 60.3% ya uzalishaji wa mkaa Brazil ulifanywa kutoka kwenye uvunwaji wa misitu ya asili baadaye mkakati wa makusudi ulifanywa ili mkaa uzalishwe kutoka katika misitu ya kupandwa. Ingawa matumizi ya mkaa nchini Brazil ni kwa ajili ya viwanda vya kufua chuma. Jambo la msingi ni kwamba uvunaji wa mkaa kwa misitu asili ilipungua kwa asilimia 82% kati ya mwaka 1989 hadi 1996. Makampuni makubwa yalipewa jukumu la kupanda miti, kuzalisha na kusambaza mkaa kwa ajili ya kuifanya iwe endelevu. Hapa nchini upo uwezekano kabisa wa kuboresha ubora wa mkaa kwa kuwajengea uwezo wazalishaji na kuifanya kuwa sekta rasmi huku tukiendelea kuboresha mazingira yetu. Hali hii ikiwezekana itasaidia sana katika kuboresha na kuhifadhi misitu katika Tanzania.
Ikiwa sekta ya mkaa itafanywa kuwa endelevu ni dhahiri kuwa athari zitokanazo na mkaa kama vile uharibifu wa mazingira, hewa ya ukaa iharibuyo tabia nchi na gesi ya ozone kupunguzwa kwa kiasi kikubwa.
Kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali kuanzisha mikakati ya makusudi ya kuweza kuifanya sekta ya mkaa iwe sekta rasmi na endelevu kwani ni nishati tegemewa na asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania. Pia, mchango wake wa zaidi ya shilingi trilioni moja katika ukuaji wa pato la Taifa ni mkubwa ukilinganisha na mazao mengine yatokanayo na misitu hivyo haiwezi kupuuzwa na kuachwa bila mkakati wowote.
Mheshimiwa Spika, na badala ya kuacha serikali iendelee kupoteza mapato kupitia watendaji katika halmashauri ambao wamekua wakitoza faini kwa bidhaa za misitu na mapatao yake kutoingizwa katika mfuko wa serikali, na ukweli ni kwamba hata tusipo rasimisha mkaa utaendelea kutumika na itaendelea kuwa ni biashara ya wakubwa tu, na kama taifa misitu itaendeleka kukatwa na mapato tutaendelea kuyakosa. Kwani ukweli ni kwamba hatuna chanzo mbadala cha nishati kwa watanzania wa kipato cha chini. Hivyo basi, ni wakati muafaka kwa serikali kurasimisha biashara za misitu na kuwafanya wananchi waendelee kufanya kwa utaratibu maalumu na kuweza kuipa serikali sehemu ya mapato hayo.
Mheshimiwa Spika, mwanamazingira mmoja duniani aliwahi kusema hivi, naomba kunukuu,”To be poor and be without trees, is to be the most starved human being in the world”, Hakuishia hapo na akasema tena “To be poor and have trees, is to be completely rich in ways that money can never buy” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, tatizo la uharibifu wa misitu bado limeendelea kuwepo nchini na kuathiri juhudi za utunzaji wa misitu nchini, itakumbukwa mnamo tarehe 19 April 2013, ilizungumzwa ndani ya bunge hili kuwa magogo yamekuwa yakisafirishwa nje ya nchi kupitia bandari ya Dar es Salaam katika maswali kwa mawaziri huku tatizo la madawati kwa wanafunzi likiwa halijapata suluhu. Swali linakuja je pamoja na majibu ya waziri kuwa serikali imekwisha piga maruku usafirishaji wa magogo nje ya nchi ni sahihi kuwa hali iliyopo sasa inathibitisha utekelezaji wa katazo hilo la serikali?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haihitaji kujua nani alitoa taarifa zilizo sahihi kati ya mbunge na waziri, lakini jambo kubwa hapa ni kusimamia sera na taratibu rasmi za serikali katika kulinda misitu nchini, itakumbukwa kuwa takwimu zinaonesha kuwa ni asilimia 4 tu ya misitu yetu ambayo huvunwa kwa vibali halali na asilimia 96 ni kwa njia isiyo halali, hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama cha waandishi wa habari za mazingira (JET)- “Biashara haramu ya mazao ya misitu yaisumbua Serikali”.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ubadhirifu huo katika sekta ya misitu serikali inakosa mapato yatokanayo na uvunaji wa misitu, pia wananchi wa pembezoni mwa misitu wanashindwa kujikwamua katika umaskini, kwa kurejea taarifa ya shirika la mazingira la TRAFFIC ya mwaka 2007 ilitoa takwimu zilizoonesha hasara inayoipata serikali kwa mwaka kutokana na biashara haramu ya misitu ikiwa ni shilingi bilioni 75, pamoja na kuonesha hasara hiyo ya mapato ya serikali pia ilieleza uhusikaji wa viongozi wa serikali katika ubadhirifu huo.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka serikali kuona umuhimu wa misitu katika kukuza uchumi na kuwaondoa wananchi katika wimbi la umaskini, hivyo kuweka kipaumbele katika swala la usimamizi wa misitu iliyopo.
Nyuki
Mheshimiwa Spika, Katika hotuba ya waziri mkuu aliainisha moja ya vipaumbele vya ofisi yake ikiwa ni pamoja na Ufugaji Nyuki, na kueleza mwenendo wa sekta ya nyuki nchini, pamoja na maelezo ya waziri mkuu bado sekta hii ipo nyuma ikilinganishwa na matamshi ya kuonesha kuwepo kwa juhudi kubwa katika kuiwezesha sekta hii kukua na kuwa na tija kwa uchumi wa nchi na jamii husika,Ufugaji wa Nyuki ni shughuli ya kiuchumi inayoweza kuwaongezea Wananchi wetu kipato na kuwaondolea umaskini. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita 2009 – 2012, uzalishaji wa Asali ulifikia Wastani wa Tani 8,747 na Nta Tani 583 kwa mujibu wa taarifa ya Waziri mkuu bungeni katika hotuba ya makadirio ya bajeti ya 2013/2014,
Mheshimiwa Spika, swala la kipaumbele chochote cha serikali si kufanya kwa malengo ya kutangaza nia kwa wananchi kwa maslahi ya kisiasa, kuna haja ya serikali kuhakiki inatekeleza vipaumbele kwa kuonesha utendaji halisi hasa kuifanya sekta ya nyuki kuwa na manufaa kwa wananchi wanaoingia katika biashara hiyo, takwimu zinazotolewa na taarifa za serikali juu ya kuiwezesha sekta ya ugfugaji nyuiki si za kuridhisha kutokana na rasilimali nyuki tulionayo nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inatoa rai kwa serikali juu ya uwekezaji katika sekta ya nyuki kwa kuendeleza sekta hiyo kuweza kuwafanya wananchi waweze kuuza bidhaa za nyuki na sio bidhaa ghafi.
Mheshimiwa Spika, taarifa za mauzo yatokanayo na bidhaa za misitu,licha ya ukweli kwamba bidhaa za misitu zimekuwa kianzio kikubwa cha mapato kwa Wizara ya Maliasili na Utalii,wizara inaendelea kukiri katika taarifa zake kwa uwazi kwamba hakuna udhibiti wa kutosha kwenye eneo la misitu,hivyo kusababisha makusanyo ya maduhuli sawa na asilimia 40 kutokusanywa kwa kutokana na changamoto mbalimbali hususani kuingiliwa na wanasiasa, maslahi madogo kwa watumishi wasimamizi wa misitu,ulegevu katika usimamizi wa sheria na Kutoeleweka vizuri kwa vianzio vya kodi na wakusanyaji mapato kama vilivyoainishwa kwenye kifungu 49 cha sheria ya misitu ya mwaka 2002 (Act No 14 of 2002).
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kuona umuhimu wa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma ili kuwapa motisha na kulinda rasilimali za taifa, pia kuzingatia sheria katika utekelezaji wa mipango ya serikali hivyo itaweza kudhibiti siasa kuingilia utendaji.
M: HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na nguvu hadi wakati huu. Napenda kushukuru viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo kwa msaada mkubwa ambao wamekuwa wakinipatia katika kutekeleza majukumu yangu ya kibunge na uwaziri kivuli wa maliasili na utalii. Napenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Iringa mjini kwa kunipa nguvu, msaada na ushirikiano tangu wanichague niwe Mbunge wao hadi wakati huu. Nawaambia kwamba nawapenda na nitaendelea kuwatumikia kadri ya uwezo wangu wote.
Mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa ni kwa familia yangu, kwa uvumilivu mkubwa kwa kipindi chote ninachokuwa sipo nyumbani.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.
_____________________________________
Mchungaji Peter Msigwa (Mb) Iringa Mjini
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani
Wizara ya maliasili na Utalii
29.04.2013
0 maoni:
Post a Comment