“Kamanda” wa Chadema, James Millya akizungumza na waandishi wa habari jana nyumbani kwa Hayati Edward Moringe Sokoine katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 29 ya kifo chake, maadhimisho ambayo yalitanguliwa na mashindano mengine ya riadha mini marathoni, kurusha mishale na kuruka juu. Millya alihoji mhusika halisi wa kifo cha Sokoine na baadae Blog hii iliweza kupata waraka wake huu hapa chini. Picha na Said Sambala, Monduli Juu-Arusha.
***************************************
MIAKA 29 YA KUOMBOLEZA KIFO CHAKO EDWARD MORINGE SOKOINE
Nilikuwa takribani miaka 5 tu ulipotangazwa na RTD kuwa umetutoka kwa ajali ya gari tarehe 12/04/1984.
Kifo chako miongoni mwa watu wako, mimi nikiwa mmoja wao bado kinaibua maswali mazito na ambayo mpaka sasa tangu nilipojiunga na Darasa la Kwanza mwaka 1986 hadi namaliza Shahada ya Uzamili (LL.M-Masters in Human Rights and Democratization in Africa), sijapata majibu ya kuridhisha na ya kutosha. Siamini sana kama tunaweza kuwa na fursa ya kujua ukweli wa kifo chako lakini cha muhimu kwetu tunaokukumbuka Daima na kukuenzi na kutaka kuishi namna ulivyoishi kwa uongozi uliotukuka nchini mwetu, ni kumshukuru Mungu kwa kukuleta duniani ili watu wote tuendelee kushuhudia kwa mataifa ya kwamba, “…binadamu mwema, kiongozi mwema katika nchi masikini kama yetu ya Tanzania inawezeka…”. Tunakukumbuka sana na tungali tunakuhitaji mno.
Hata hivyo sisi kama jamii uliyotokea, imetuchukuwa muda mrefu sana na kwa masikitiko makubwa kwamba, neno ‘HAYATI’ ilikuwa ni heshima uliyotunukiwa na serikali kutokana na uhodari wako na uchapakazi wako. Mkanganyo huu, umetokana pamoja na mambo mengine mengi, na ukosefu wa elimu miongoni mwa watu wako. Tunakukumbuka sana na tungali tunakuhitaji mno.
Hayati Edward Moringe Sokoine, natamani Mungu Akurudishe hata kwa mwaka mmoja tu uone ni kwa jinsi gani watu wako, “…tumegeuzwa watumwa katika nchi uliyoshiriki kutafuta uhuru wake, Tanzania...”. Katika kumbukumbu ya maisha yako na kukumbuka kifo cha aibu kilichokukuta wewe kama Waziri Mkuu wa Tanzania, ninaomba niyaseme yafuatayo kwa Watanzania ili sisi sote kama jamii tutafute ufumbuzi wa pamoja na wa kudumu katika kuenzi utumishi wako uliotukuka nchini mwetu. Tunakukumbuka sana na tungali tunakuhitaji mno.
HAYATI EDWARD MORINGE SOKOINE;
Tangu ulipoondoka duniani, Ardhi yetu imekuwa ya kumegwa kila kukicha na serikali kuliko ambavyo ardhi ya jamii nyingine ya kitanzania inamegwa. Tunaadhibiwa kwasababu sisi kwa mila na desturi zetu hatufanyi kitowewo wanyama pori na kutokana na hilo, tumewahifadhi na kuwatunza tukiishi kwa amani wanyamapori hao na mifugo yetu. Kwa kutumia mabavu kila siku mbuga na hifadhi zinaongezwa kwa kuchukua ardhi ya wafugaji wenzako. Hata kwa kutumia Mahakama ya Rufani chini ya Jaji Mkuu Mstaafu Nyalali, Mbuga ya Wanyamapro ya Mkomazi imechukuliwa na wafugaji kufukuzwa na kupewa fidia ya shilingi 250’000/= tu kwa familia chache eti kama fidia ya usumbufu na garama za kuwahamisha kutoka kwenye eneo lao eti kwasababu sheria za nchi zinatoa mamlaka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutwaa eneo lolote atakalo kwa manufaa ya umma. Leo hii tunapokuenzi na kukumbuka kutoweka kwako wakina mama wa kifugaji kwa maelfu wanalia na kuandamana Loliondo kwa ardhi aliyoongezewa Raia wa Kiarabu. Wanalia watu wako Simanjiro kwa kuongezwa kwa hifadhi ya Tarangire(Eneo la Mkungunero). Kilio cha wafugaji ni kila mahali tena kwa uchungu mkubwa sana. Wafugaji wanalia Morogoro, wakihamishwa na kutii amri hufukuzwa kwenye maeneo yote hata kwa kutumia jeshi la Polisi kama walivyofanyiwa Ihefu na pengine pote. Tunakukumbuka sana na tungali tunakuhitaji mno.
Tangu ushirikiane na Mwl. Julius Kambarage Nyerere kuwasomesha kina Mhe. Vincent Ole Kone, Mhe. James Kisota Millya (Mkuu wa Wilaya ya Longido), Mzee Ole Kambaine, Mzee Kimesera, Mhe. Edward Ngoyai Lowassa, Mhe. Sodoweka, Mhe. Benedict Ole Nangoro, na wengine wachache kwa kutambua kuwa kihistoria waliachwa nyuma na jamii nyingine, serikali zilizofuata hazikutilia maanani mapungufu haya ya kihistoria hivyo basi, wengine kama sisi kama isingekuwa ni wazungu wachache waliotuonea huruma, tungekuwa miongoni mwa walinzi waliotapakaa mote nchini kama walinzi wa majumba na mali za matajiri katika mikoa mbalimbali ya nchi yetu. Hayati Baba yetu Sokoine, hata Zanzibar tumevuka pamoja na ukweli kwamba, maji tunayaogopa sana lakini shida humfanya binadamu yeyote apoteza utu wake na msimamo yake ya asili. Sasa tufanye nini? Tunakukumbuka sana na tungali tunakuhitaji mno.
Serikali ya wote, nchi yetu sote. Ni kwa namna gani mfugaji naye huweza kwa majivuno kabisa kusema, serikali hii ni yetu sote, nchi hii ni yetu sote na keki ya Taifa ni yetu sote?. Nani asiyefahamu ndani ya mipaka ya nchi yetu iliyobarikiwa ya kwamba, kihistoria wafugaji waliachwa nyuma kwa Nyanja mbalimbali na jamii nyingine nyingi baada ya uhuru wa Tanzania mwaka 1961? Nani hafahamu kuwa kutokana na ukosefu wa uadilifu, uzalendo kuisha, watu waovu, wabinafsi na wabaya toka makabila mbalimbali nchini mwetu huwatafuta ndugu zao ili kuwatafutia ajira, na fursa nyingine nyingi katika taasisi mbalimbali za nchi yetu? Leo vitengo fulani fulani vya serikali vimetawaliwa na jamii moja? Nani miongoni mwetu ambaye hafahamu walivyofanya waafrika ya kusini baada ya uhuru wa kweli mwaka 1994? Mzee Nelson Mandela (Madiba) baada ya kutawazwa Rais wan chi ya Afrika ya Kusini alitambua ukweli kwamba, watu weusi baada ya uchumi na nafasi nyingi kuhodhiwa na waafrika kusini weupe serikali ilikuja na SERA ya Utaifa ya “Black Economic Empowerement(BEE)”. Sera hii ililetwa mahususi ili kurekebishwa na kutatua makosa ya kihistoria miongoni mwa waafrika kusini?. Kwa lugha ya wageni wanasema, “positive discrimination”. Nani hafamu kuwa kuna ukweli usiopingika kuwa ukifanya tafti hata leo kuwa keki ya Taifa inaliwa na wachache na baadhi ya jamii nyingine ni wasindikizaji tu? Wachache wa vijana wa namna yangu waliofanikiwa kusomeshwa na wazungu hadi chuo kikuu miongoni mwa jamii yangu wamekimbilia Taasisi za Kirai (NGOs) kutokana na madhaifu makubwa niliyotaja hapo juu. Najua wengi wanajua ukweli ninaouongelea hapa lakini kutokana na uoga na kuambiwa Taifa letu halina ukabila watu wengi wanajua ukweli kwamba wafugaji ni kama wakimbizi kwenye nchi yao hivyo wazalendo wameamua kunyamazia ukweli huu na kusema, “Funika Kikombe Mwana Haramu Apite”. Tunakukumbuka sana na tungali tunakuhitaji mno.
Wachache miongoni mwetu ndani ya jamii yako, tunaotaka kuishi kwa mfano wako bila kuogopa na kusema ukweli ndani ya nchi yako, tunapingwa na kupigwa marungu yasiyostahili na mengine mazito sana ili mradi tunyamaze kimya na kulazimishwa pia tuseme, “funika kikombe mwanaharamu apite”. Tunakukumbuka sana na tungali tunakuhitaji mno.
Hayati Edward Moringe Sokoine, ulikuwa rika moja na Baba yangu mzazi na nakumbuka baada ya matangazo ya jioni ya kifo chako, kwa kuwa baba alikuwa ni mfanyabiashara wa ng’ombe alifanikiwa kuwa na radio ya mkulima, na kwa kuwa wakati fulani ulikuwa mbunge wake pia, alikufahamu na alilia sana. Mimi sikupata bahati ya kukuona kama baba yangu mzazi lakini historia na heshima uliotuachia miongoni mwa watanzania ni kubwa mno. Uliishi maisha ya kinabii, uliwapenda watu wote na ulitenda haki, ni kweli unakumbukwa kwa uongozi uliotukuka. Nami naahidi mbele ya kaburi lako, sitanyamazia maovu yote katika nchi hii ninayoijua kama nyumbani kwangu na ninaahidi kujaribu kuishi maisha yako hata kama nitakutana na pingamizi zozote za maisha ya uongozi katika uhai wa maisha yangu lakini nipo tayari pia kufa ili kutetea ukweli na kupinga kwa akili na nguvu zangu zote manyanyaso na ukiukwaji wa HAKI ndani ya Taifa langu la Tanzania, Afrika na Duniani. Tunakukumbuka sana na tungali tunakuhitaji mno. Watanzania wanakusalimia na Wanakukumbuka kwa wema ulionyesha katika uhai wa maisha yako.
Mungu Ailaze Roho Yako Baba Yetu, Kinara wetu Edward Moringe Sokoine Mahali Pema Peponi.
MUNGU ALITOA NA MUNGU ALITWAA JINA LA BWANA LIHIMIDIWE.
………………………….
James K. Millya
0 maoni:
Post a Comment