Mataifa yanayoendelea kupiga hatua za haraka za Kiuchumi Ulimwenguni ya G. 20 yameshauriwa kuwekeza ndani ya Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kuunga mkono harakati za Kiuchumi za Mataifa hayo.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda katika Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Jumuiya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya Ngurdoto iliyopo Mkoani Arusha Tanzania.
Rais Museveni amesema Mataifa hayo yenye muelekeo mzuri wa Kiuchumi yanaweza kuongeza nguvu zao katika kusaidia miradi ya Miundo mbinu ya Barabara ,Mawasiliano na hata Sekta binafsi.
Amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki imelenga kunyanyua maisha ya Wananchi wake kwa kuimarisha Sekta zisizo rasmi kwa vile uwezo wa Serikali hizo katika kutoa ajira hasa kwa Vijana bado ni mdogo.
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ametolea mfano Taifa lake la Uganda ambalo limejizatiti katika kuimarisha nguvu za sekta binafsi ili kupunguza wimbi la vijana wengi wanaomaliza masomo yao ambao hubaki wakizurura bila ya utaratibu wa kufanya kazi.
Akiwahutubia Viongozi hao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, Waziri Mkuu wa Rwanda Bw. Pierre Damien, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar pamoja na Watendaji wao Rais Museveni amempongeza Rais wa Kenya Uhuru Kenyata kwa kujumuika pamoja katika mkutano huo baada ya kuchaguliwa kuiongoza Kenya
Viongozi wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wakiimba Wimbo wa Mataifa hayo kabla ya kuanza kwa Mkutano wao wa 11 kwenye Hoteli ya Ngurdoto Mkoani Arusha. Kutoka Kushoto kuelekea kulia ni Waziri Mkuu wa Rwanda Bw. Pierre Damien Habumuryemi, Rais wa Burundi Bw. Pierre Nkurunziza, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Uhuru Kenyata wa Kenya na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyemuwakilisha Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Sheni.
Rais Uhuru Kenyata wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya akihutubia Mkutano wa Wakuu wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza baada ya Kuchaguliwa kuwa rais wa Kenya hivi Karibuni.
Baadhi ya Mawaziri wa SMT na SMZ walioshiriki Mkutano wa Wakuu wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye Hoteli ya Ngurdogo Mkoani Arusha Tanzania. Kutoka kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais MBM Dkt. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Fatma Abdullhabib Fejeji, Waziri wa Afrika Mashariki Mh. Samuel Sita na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Tanzania Mh. Mahadhi Juma.
Mwenyekiti wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Yoweri Kaguta Museveni aliyeshika Kofia akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wenzake wa jumuiya hiyo mara baada ya kumaliza Mkutano wao wa 11 wa Jumuiya hiyo uliofanyika Ngurdoto Mkoani Arusha. Kushoto kwa Rais Museveni ni Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Uhuru Kenyata wa Kenya na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyemuwakilisha Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Sheni. Kulia kwa Rais Museveni ni Waziri Mkuu wa Rwanda Bw. Pierre Damien Habumuryemi pamoja na Rais wa Burundi Bw. Pierre Nkurunziza.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwaongoza Wajumbe wenzake kutoka nje ya Ukumbi wa Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mshariki mara baada wa kumaliza Mkutano wao kwenye Hoteli ya Kimataifa ya Ngurdoto Mkoani Arusha.(Picha na Hassan Issa OMPR – ZNZ).
.
credit: Audiface Jackson
0 maoni:
Post a Comment