Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Shahidi: Mwigulu ndiye alikodi watu kufanya fujo na Jumbe Ismaily, Singida

SHAHIDI wa kwanza upande wa utetezi katika kesi inayowakabili watu 10 wanaodaiwa kufanya vurugu katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Shabani Limu, ameiambia mahakama kuwa Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba ndiye aliyekodi kikundi hicho ili kifanye fujo.

Mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida Tersophia Tesha, shahidi huyo alidai kuwa walipata taarifa kuwa Mwigulu ndiye aliyekodi kikundi hicho ambacho baadhi ya washtakiwa ni wakazi wa jijini Dar es Salaam ili kifanye fujo na mkutano wa CHADEMA usifanyike.

Limu ambaye pia ni Kaimu Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Singida, alifichua siri hiyo wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kufanya fujo na kupiga watu mawe kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ndago Jimbo la Iramba Magharibi.

Washtakiwa 10 wanakabiliwa na mashtaka ya kufanya vurugu na kupiga watu mawe kwenye mkutano wa hadhara wa CHADEMA.

Katika ushahidi wake, Limu alidai kuwa alikuwa mratibu wa mkutano huo na kwamba hata kabla ya kuanza walijua kuna kikundi cha watu waliokodiwa kwa ajili ya kuuvuruga.

Alidai kuwa baada ya Ofisa Sera na Utafiti wa CHADEMA Makao Makuu, Mwita Waitara kusema kuwa Mwigulu anatumia jina lisilo lake na kwamba ni mwogo ndipo vurugu zilianza kwa watu kupigwa mawe.

Aliongeza kuwa meza kuu walikoketi viongozi wa CHADEMA Taifa yaani Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, mshauri wa chama, Dk. Kitila Mkumbo pamoja na Waitara haikudhurika na fujo hizo wala hakuna mali iliyoharibiwa.

Baada ya maelezo hayo ya shahidi huyo, Mwendesha Mashtaka Mkaguzi wa Polisi, Shukran Magafu alimuuliza maswali kama ifuatavyo:

Swali: Je, ni hawa washtakiwa waliopo mahakamani ndio waliokuwa wanapiga watu mawe?

Jibu: Sina hakika kwa kuwa nilificha uso wangu kwa kiti ili nisipigwe mawe.

Swali: Je, washtakiwa uliishawaona kabla ya siku ya tukio au ni wakazi wa Mkoa wa Singida?

Jibu: Sijawahi kuwaona na kwa ujumla washtakiwa hawa sio wakazi wa Mkoa wa Singida.

Naye mshitakiwa Mohamed Abdala alipata fursa ya kumhoji shahidi huyo kama ndiye anatunza rekodi ya wakazi wa Singida hadi awafahamu wakazi wote wa mkoa huo.

Washtakiwa waliokuwepo mahakamani hapo ni Abdala Mbwana, Laizimu Njama, Ludovic Muganizi, Justin Sanga, Salum Ali na Mohamed Abdallah wote ni wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa tena Mei 6 mwaka huu na washtakiwa wote wako nje kwa dhamana.

Hata hivyo, Magafu aliieleza mahakama kuwa washtakiwa wengine, Shabani Hamisi na Daniel Wambura ambao ni wakazi wa Kijiji cha Ndago waliisharuka dhamana mapema kesi hiyo ilipoanza.

Washtakiwa hao wote kwa pamoja wanashtakiwa kwa kutenda kosa hilo Julai 14 mwaka jana, saa 8:30 mchana kwenye mkutano wa hadhara wa CHADEMA uliofanyika katika Kijiji cha Ndago na hivyo kusababisha kuvunjika amani na utulivu kwa muda.

Tanzania Daima, 13 Aprili 2013

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO