Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Lwakatare asikilizwa mafichoni • Mawakili waumana, Jaji kuamua baadaye

lwakatareOMBI la Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, la kuiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuifuta kesi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana lilisikilizwa mafichoni, hivyo kuibua malalamiko makubwa kwa wafuatiliaji.

Kesi hiyo ambayo inafualitiliwa na wananchi wengi, iliendeshwa katika chemba ya Jaji Lawrence Kaduri, hatua iliyowafanya hata waandishi wa habari za mahakamani kuzuiwa na askari wa Jeshi la Magereza kuingia ndani ya chumba hicho kidogo.

Badala yake waandishi hao walilazimika kufanya juhudi za ziada kuwashawishi askari hao ili angalau wamruhusu mmoja wao, Faustine Kapama, aingie ndani asikilize halafu baadaye awasimulie, ombi ambalo hatimaye lilikubaliwa, hivyo wengine zaidi ya 15 kubaki nje.

Kadhia hiyo haikuwakuta waandishi pekee, bali hata wabunge wa CHADEMA na wafuasi wao zaidi ya 70 waliofika mahakamani hapo tangu saa moja asubuhi kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo, walijikuta wakiishia kwenye korido za mahakama hiyo.

“Tunajua Lwakatare ameshtakiwa na serikali. Serikali hiyo hiyo leo hii imeamua kesi hii iendeshewe kwenye chemba ili sisi wananchi na waandishi wa habari tusisikie na kuona yanayozungumzwa katika kesi hiyo.

“Mahakama inafahamu fika kesi hii hivi sasa imezua mjadala mkubwa sana, kwanini huyu Jaji Kaduri hakusoma alama za nyakati na akaamua kuipeleka katika mahakama ya wazi?” walihoji wananchi hao.

Kitendo hicho kiliwakera waandishi wa habari za mahakamani wakidai chemba iliyotumika ni chumba kidogo, hivyo wamenyimwa fursa ya kuisikiliza kesi hiyo na kisha kwenda kuiripoti kwa umma.

Mawakili waumana

Mvutano mkubwa wa kisheria ulijitokeza wakati mawakili wa pande zote mbili za serikali na Lwakatare wakichambua hoja zao mbele ya Jaji Kaduri.

Awali, upande wa Serikali ukiongozwa na mawakili Prudence Rweyongeza, Peter Mango na Ponsian Lukosi uliweka pingamizi mbili kuwa maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa utetezi, Mabere Marando, Peter Kibatala na Tundu Lissu, vifungu vyake vilikosewa.

Hata hivyo, upande wa utetezi nao uliweka pingamizi kuwa upande wa serikali ulikosea vifungu walivyonukuu katika kupeleka maombi yao Mahakama Kuu, hoja ambayo mawakili wa Serikali walilazimika kuifuta kabla haijaanza kujadiliwa.

Pingamizi la pili lilihusu hati ya kiapo ambapo mawakili wa serikali walihoji uhalali wake, lakini hoja za kisheria zilizojibiwa na Kibatala zilimaliza mjadala huo, hivyo kuanza kusikiliza kesi ya msingi.

Katika kesi hiyo, upande wa utetezi ulisema kitendo alichofanya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hakikuwa cha lazima. Kwamba licha ya mkurugenzi huyo kuwa na mamlaka ya kufuta kesi, lakini anapofanya hivyo lazima aoneshe amefuta kwa masilahi ya umma, kutafuta haki au pengine kuzuia mahakama isidhalilike na hukumu ambayo ingetolewa.

Mawakili hao walisema kuwa kesi iliyofutwa na kurejeshwa tena Kisutu ilikuwa ni matumizi mabaya ya mamlaka ya DPP, hivyo kuiomba Mahakama Kuu kupitia upya mwenendo wa kesi namba 37/2013 iliyofunguliwa Kisutu kwani ilifunguliwa kwa nia ya kumdhalilisha mtuhumiwa.

Walihoji iliwezekanaje kufuta kesi na kuifungua ndani ya muda mfupi, kwamba walipata wapi ushahidi mwingine mpya.

Mawakili hao wa utetezi wanaiomba Mahakama Kuu ifanye yafuatayo:

Kwanza, ipitie mwenendo wa kesi zote mbili, namba 37/2013 na 6/2013 ili kujua kama zina hoja ya msingi, halali au la.

Pili, wanaomba mahakama iamrishe kuwa mwenendo wa kesi namba 6 urudi katika kesi namba 37, ili Mahakama ya Kisutu iweze kutoa hukumu kutokana na mambo yaliyokuwa yanabishaniwa kisheria.

Tatu, wanaiomba Mahakama Kuu kuingilia mchakato wa ‘nole’ (hawana hatia) iliyotolewa na DPP kwa muda mfupi kisha kumtia mtuhumiwa hatiani, ambavyo ni kinyume kabisa cha madaraka ya DPP.

Mmoja wa mawakili hao, Lissu alisema kuwa mashtaka hayo ni ya kutunga na hayana uhai kisheria kwa kuwa Mahakama ya Kisutu tayari ilishaanza kuisikiliza.

Lissu aliongeza kuwa hakuna haja ya kuibebesha lawama Mahakama ya Kisutu kwa masuala hayo bali wanasheria wa serikali walioielekeza mahakama vibaya kwa kuingilia mchakato wake ili waweze kutekeleza azima yao.

Alidai kuwa kesi ilikuwa ni ya jinai inayosikilizwa wazi tena bila kificho, hivyo hakukuwa na ulazima wa mawakili wa serikali kumvizia Lwakatare kwa kuifuta na kuifungua upya.

Awali wakili Rweyongeza alipangua hoja za mawakili wa Lwakatare ambazo zilidai DPP alitumia madaraka yake vibaya kuifuta kesi Na. 37/2013 na akazitaja sababu zilizosababisha aifute kesi hiyo na kufungua kesi mpya Na. 6/2013 Machi 20 mwaka huu, kwa kuwa mashitaka ni yale yale.

Aliitaja sababu ya kwanza iliyofanya DPP aifute kesi Na. 37 /2013 iliyofunguliwa Machi 18 mwaka huu, kuwa ni uongozi wa Mahakama ya Kisutu kukosea na kuifungua kesi hiyo katika jalada la kesi zinazoendeshwa katika mahakama za chini (Subordinate Court) badala ya kuisajili kesi hiyo katika rejista ya kesi zinazopaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu.

Pili, ni kwamba hakimu aliyeisikiliza kesi hiyo, Emilius Mchauru, alikosea kuwaruhusu washtakiwa hao kujibu mashitaka wakati Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi hiyo ya ugaidi.

“Hivyo basi upande wa Jamhuri tunasisitiza kuwa uamuzi wa DPP wa kuifuta kesi ile ulikuwa wa haki ambao ulikidhi matakwa ya kifungu cha nane cha  Sheria ya Uendeshaji wa Mashitaka ya mwaka 2008,” alidai Rweyongeza.

Akipangua hoja ya mawakili wa utetezi iliyokuwa ikiiomba Mahakama Kuu iifute kesi ya msingi inayowakabili washitakiwa hao kwa sababu kosa la pili, tatu na nne hayaoneshi nia ya washitakiwa hao kutenda makosa ya ugaidi, alidai kuwa hoja hizo zimeletwa wakati usio sahihi kwani kesi ya msingi ipo katika hatua za uchunguzi, upelelezi bado haujakamilika.

Alidai kuwa huenda siku za usoni DPP akaamua kubadilisha hati ya mashtaka kwa hiyo ombi hilo halina msingi na kwamba hata hivyo Sheria ya Kuzuia Ugaidi  inasema kitendo cha kumteka nyara mtu ni kosa la ugaidi, kwa hiyo kinachotakiwa kuzingatiwa katika hilo ni suala la ushahidi tu.

Kwa upande wake, Jaji Kaduri alisema amesikiliza kwa makini hoja za mawakili wa pande zote mbili na kwamba tarehe ya kuja kutoa uamuzi wa malumbano hayo ya kisheria itatolewa kwa njia ya maandishi.

Chanzo: Tanzania Daima; na Happiness Katabazi

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO