Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

KARIPIO KALI LA M.M MWANAKIJIJI KWA CHADEMA! usiache kulisoma hapa

kamati Kuu CDM Dar3M. M. Mwanakijiji

KUNA vitu sielewi; nimejaribu kuvielewa lakini vimenishinda; na vipo vingine ambavyo japo kwa wengine vinaeleweka kirahisi, kwangu vimekuwa vigumu kweli kweli. Inawezekana nina lile tatizo maarufu la kutokuelewa. Pamoja na jitihada zangu zote za kujaribu kuelewa nimejikuta nikitoka kapa. Sielewi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinataka nini kutoka kwa watawala wetu walioshindwa.
Nitajaribu kujieleza na kama na wewe hutanielewa basi na wewe una tatizo lile lile linalonikabili mimi – la kutokuelewa.Kwa miezi sasa na labda niseme miaka karibu miwili na nusu sasa tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa katika hali ya kuishambulia CHADEMA kwa kila namna; kimechukua hoja zake kuzifanya za kwake (kama ile ya katiba) na kimetumia Bunge kuzima kila aina ya mashambulizi ya chama hicho.

Kwa kweli baada ya mwaka 2010; CCM iliamua kwa dhati kabisa kuwa haiwezi kwenda kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 ikiwa dhaifu kama ilivyokuwa kabla ya ule wa mwaka 2010. CCM walielewa ipasavyo tishio lililo mbele yao. Hofu yangu ni kuwa CHADEMA wanaishi kama wasioelewa kuwa CCM inaelewa! Kwa muda wa miaka hii miwili tumeshuhudia mengi yakitokea ndani ya CHADEMA ambayo wengine wameyaita ‘migongano’ na hata ‘hujma’ ndani ya chama. Tumeshuhudia CHADEMA ikijikuta kwenye wakati mgumu kwenye mambo mengi, na kati ya yote yaliyotokea hakuna ambalo limewashtukiza vibaya kama hili la Lwakatare na mashtaka ya ugaidi dhidi yake.

Ukifuatilia sana mwitikio wa CHADEMA katika masuala karibu yote ni kuwa inaibebesha lawama zote CCM na serikali. Hili ni kweli kwenye sakata la vijana waliotimuliwa na ni kweli pia kwenye masuala ya mameya kule Arusha na Mwanza. Matatizo yote yanayotokea CHADEMA – baina ya wanachama na viongozi au baina ya viongozi na viongozi yanasababishwa na CCM. Kama si CCM basi maajenti wa serikali wanaomtumikia Bwana Mkubwa CCM.

Ukifuatilia sana utaona kuwa CHADEMA haiamini kuwa ina tatizo lolote ndani yake na ukiwasikiliza viongozi wake na hata wanachama wa kawaida utaona wanakubaliana kuwa ni CCM ndiyo yenye kupandikiza matatizo kwenye upinzani na hususan CHADEMA. Naomba kwa ajili ya hoja yangu hii – ya karipio kali – tukubaliane kuwa ni kweli CCM na serikali yake ndio wanasababisha matatizo ndani ya CHADEMA, kwamba tukubaliane pia kuwa watu kama Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) Mwigulu Nchemba, na viongozi wengine wa CCM wanatumia kila njia kudhoofisha CHADEMA.

Naomba tukubaliane pia – kwa ajili ya hoja yangu ya karipio kali – kuwa CCM haitaki kuona upinzani unakomaa nchini na kwa kuwa haina nia ya dhati ya kukaribisha mageuzi ya kisiasa nchini.Wale wote mashabiki, wapenzi na wanachama wa CHADEMA tukubaliane kuwa CCM inapanga mbinu chafu za kuwachafua viongozi wa CHADEMA na hata kuwabambikizia kesi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015 CHADEMA iwe dhaifu, imegawanyika na kama alivyosema Stephen Wassira iwe imekufa ifikapo mwaka 2015. Tumekubaliana? Sawa.

Sasa swali langu liko wazi na la moja kwa moja – tunataka CCM wafanye nini? CCM kama chama tawala ambacho kimeonja utamu wa madaraka; kimezaliwa na kurithishwa madaraka; yalipokuja mageuzi ya kisiasa mwanzoni mwa miaka ya 1990 CCM ikapewa usajili bila kutafuta mwanachama hata mmoja; ikawa chama cha siasa bila kupimiwa kipimo walichopimiwa kina Mtei, Mapalala na wengine walioanzisha vyama wakati ule. CCM haikuhangaika kabisa kutafuta wanachama kwa sababu sheria ilisema kuwa baada ya tarehe fulani wakati vyama vinaruhusiwa basi CCM itakuwa ni ‘de facto’ chama cha siasa. Na kutoka hapo kikaingia kwenye chaguzi mbalimbali kikiwa na nguvu kuliko chama kingine chochote nchini.

CCM ikajijenga na kuonja utamu wa madaraka na utawala. Na sasa imefika mahali haina mpango wa kuachia. Sasa najiuliza CHADEMA wanataka CCM ifanye nini? CCM kama chama cha siasa na ambacho kimetishiwa kung’olewa madarakani mwaka 2010 na kikakataliwa na mamilioni ya wananchi kuliko wakati mwingine wowote wa historia yake, kinatambua kuwa inabidi kitumie njia zote (halali na zisizo halali sana) ili kujiimarisha na kujikita madarakani.Ni kama simba aliyekamata swala na kumshika kwenye shingo yake; halafu swala wengine waje na kuanza kulalamika kwanini simba amekamata swala na wanamtaka ili awe ‘fair’ basi aachie kidogo shingo ili swala apumue. Simba anaweza kuuliza tena kwa dharau; are you serious?!

Na inanikumbusha simulizi mojawapo la Hisopo ambapo nyoka alifika mtoni na akashindwa kuvuka mto. Alipoangalia huku na kule akatokea chura ambaye alikaa mbali naye akamuuliza ana shida gani. Nyoka akajieleza kuwa alikuwa anahitaji sana kuvuka mto.
Yule chura akamwambia: “Ungekuwa si nyoka kwa kweli ningekusaidia kuvuka.”
Nyoka akasema: “Ah nisaidie bwana kwa kweli nina shida.”
Chura akamuuliza: “Si utanigonga nikikusaidia?”
Nyoka huku macho yamemtoka na ulimi wake ukicheza cheza kwa shauku; akatoa ahadi:
“Naapa kabisa kwa kweli sitokugonga ukinivusha; yaani unisaidie halafu nikugonge tena, itakuwa sina shukrani.”
Chura akamuangalia nyoka machoni akaamini anasema kweli kabisa. Akajitolea kumbeba nyoka mgongoni. Hakuamini akili zake, kweli nyoka akatulia mgongoni mwa chura huku wakivuka mto hadi ng’ambo ya pili. Chura akamfikisha salama nchi kavu na nyoka kumshukuru sana kwa kumvusha salama.
Chura akaaga na kugeuka kuelekea majini. Lakini kabla hajachupa nyoka akamgonga mgongoni ‘ngoo!!!’ Chura akaruka pembeni akibiringita kwa maumivu na sumu ikiianza kufanya kazi taratibu.
Akajikuta anamuuliza nyoka: “Sasa ndiyo nini umenigonga?”
“Aah kwa kweli niliahidi kuwa sitokugonga ukinivusha lakini sikusema ukishanivusha sitokugonga.”
Nyoka akatumia ujanja wa maneno.
“Aaaah,” chura aliendelea kulia kwa maumivu na nyoka akasema: “Lakini zaidi ya yote mimi bado ni nyoka!”
Sasa chura wengine walipopata habari zile bila ya shaka walishangazwa na kitendo cha chura kukubali kumbeba nyoka mgongoni. Na wengine hawakumshangaa nyoka kumgonga chura!

CHADEMA wanataka CCM isiwe CCM? Wanataka CCM iache tamaa ya kuendelea kubakia madarakani? Wanataka CCM ifanye nini ili CHADEMA ifanikiwe? Kwamba CCM itengeneze sheria nzuri za uchaguzi; itengeneza sera zitakazoisaidia CHADEMA kuingia madarakani?Watu wa CHADEMA wanapoilalamikia CCM wanataka CCM iwe vipi? Inawezekana kweli waliamini kuwa CCM imejivua gamba? Lakini si wote tumeona kuwa CCM gamba limeshindwa kuvuka? Sasa kama gamba limeshindwa kutoka nyoka kageuka kipepeo?Hili ni karipio kali!

Ni karipio kali kwa uongozi wa CHADEMA kitaifa. Nimejipa wajibu wa kuwakaripia kwa sababu sidhani kama kuna chombo au mtu mwingine yeyote anayeweza kuwakaripia.Wanastahili kukaripiwa vikali kwa sababu katika kupendwa kwao wameanza kujisahau. Wameanza kujisahau kiasi kwamba wameanza kusahau kuwa wameanza kujisahau! Wamejisahau kuwa wanataka kuiondoa CCM madarakani.

Katika kutaka kuiondoa CCM madarakani ina maana wanataka kusababisha mamia ya watu kupoteza kazi zao! Na ukisababisha mamia (kama siyo maelfu) ya watu kupoteza kazi zao kuna familia nyingi zitakosa mahali pa kula na kupata ulaji wa kila siku. CHADEMA inajisahau kuwa katika kusababisha kuiondoa CCM madarakani wanataka hata kusababisha baadhi ya watu waishie jela; kwani ikiingia madarakani mojawapo ya majukumu ya kwanza kabisa ni kuanzisha kamatakamata ya mafisadi waliovumuliwa chini ya CCM.

Sasa CHADEMA inasahau hili kiasi kwamba inafikiria inataka kupokezana tu utawala na CCM bila matokeo yoyote. CHADEMA wanataka CCM ifanye nini ili ijipange vizuri kushinda chaguzi mbalimbali? Wanataka CCM ijikaange yenyewe kwa kutengeneza sheria na mifumo itakayosaidia kuiondoa madarakani?Kwani CCM hawakujifunza yaliyomkuta Kaunda? Au wanadhani CCM haikujifunza kutoka Kenya (Moi na baadaye Kibaki)? CHADEMA wanataka CCM ichukue kamba iitundike mtini halafi ijining’inize yenyewe?

Kati ya makosa makubwa kabisa ambayo CHADEMA inafanya sasa hivi, ni kutegemea CCM kuimarisha upinzani. Kutegemea kuwa CCM na serikali yake itafanya mambo ambayo yataisaidia CHADEMA kujijenga. Binafsi silaumu hata kidogo kwa CCM kuleta mikorogano ndani ya CHADEMA (tukiamini ni kweli hili). Siwalaumu wakitenga mamilioni ya fedha kutafuta wasaliti ndani ya CHADEMA na kuwatumia; siwalaumu na wala siwashangai wakitumia mbinu za kiintelijensia kuwabambikizia kesi watu wa CHADEMA.

Kwanini siwalaumu? Kwa sababu watawala wanaotaka kuondolewa wameamua kung’ang’ania madarakani na hawana mpango wa kuondoka hivi karibuni.Maneno aliyonukuliwa Mbowe kusema kuwa CCM itaondolewa kirahisi 2015 ni njozi ya Alinacha; CCM haina mpango wa kuondoka kesho wala keshokutwa; na haina mpango wa kuondoka mtondogoo. Ni ukweli huu unafanya CCM itumie mbinu zote – za vitabuni na zisizo vitabuni – kudhoofisha upinzani, kuwachanganya wapinzani, kutumia Bunge kudhoofisha makali ya hoja ya CHADEMA na kufanya kila liwezalo kuhakikisha kuwa inapata jina baya, inakimbiwa, na inakataliwa. Na hata kesi hii ya ugaidi ambayo tayari baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM (Mwigulu mmojawapo) wamekiri kushiriki, kwangu mimi hainishangazi wala kunishtua.

Kusema kuwa ati CCM inahusika na watu wanashtuka ni sawasawa na kuwakuta watu Jehanam halafu kutuambia ati shetani anahusika! Well, mlitaka nani ahusike?Kama CCM inapandikiza mashushushu; inawafuatilia viongozi wa CHADEMA au inajaribu kuwapa rushwa watumishi wa makao makuu ili kuivuruga CHADEMA mlitaka CCM ifanye nini? Kwamba itume mashada ya maua ofisi za CHADEMA na kuwatumia suti mpya wapiganaji wake? Ni kushindwa kuelewa vita iliyopo na kile tunachokigombania.Kuendelea kuilalamikia CCM ni kudeka kulikopitiliza kunakotokana na kupendwa.

CHADEMA inaanza kudeka sasa kwa sababu inaamini kuwa watu wanaipenda sana na matokeo yake ni kuwa hawaamini kuwa wapo watu wanataka kuiangamiza, kuivuruga. Ni sawasawa na kumuona Lionel Messi akisakata kabumbu halafu akawa anaamini kuwa kwa vile yeye ni mchezaji bora wa dunia basi hatakiwi kukabwa; wala kupigwa ngwala. Na kwamba Messi akiona wachezaji wanambana kweli kweli anyoshe mkono juu na kulia kwa refa: “Jamani mbona wananikaba sana?” Watu watamdharau.Messi anajua kuwa kwa vile ni mchezaji bora zaidi atakabwa zaidi na hivyo na yeye kujikuta akinoa mbinu zake vizuri zaidi na kusababisha madhara kwa wapinzani uwanjani!

CHADEMA ilisababisha madhara kwa CCM kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010; sasa hivi ni madhara kidogo sana (kama yapo) ambayo CHADEMA inawapa CCM. CCM hawashtuki sana na pale wanaposhtuliwa (kama bungeni) inajua jinsi ya kujipanga na kuharibu makombora ya CHADEMA. CCM haina mpango (hata wa ndotoni) wa kuona CHADEMA inajiandaa kushika madaraka.Hili ni karipio kali!

CHADEMA ni lazima ijiangalie yenyewe; ishike kioo na kukiweka mbele yake na kujiangalia. Ijitazame kwa karibu na kujiuliza kama kweli matatizo yanayotokea ndani ya chama – baina ya watu na watu na migongano yao na CCM au serikali inatokana na nini hasa?Je, ni kweli matatizo yote ya CHADEMA yanatokana na CCM? Kama hili ni kweli (Na kama nilivyosema hapo juu wapo wanaoamini kuwa ni kweli) basi jambo moja liko wazi. CHADEMA ina udhaifu mkubwa wa kutisha. Ina udhaifu mkubwa kiasi kwamba CCM inaweza kuwafanyia kila aina ya mchezo; ina udhaifu mkubwa kiasi kwamba viongozi wake wa juu wanatumiwa na CCM; walioaminiwa ndani ya chama tena makao makuu wanaweza kununuliwa na kuwa baadhi ya viongozi wa taasisi zake nao ni dhaifu kiasi cha kununuliwa kirahisi; CHADEMA itakuwa na udhaifu mkubwa zaidi kiasi kwamba ‘video’ iliyorekodiwa tangu Desemba imekaa mikononi mwa watu bila kujulikana kwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama na kuwa CHADEMA haina mifumo mizuri ya kiintelijensia kiasi kwamba hadi kinachodaiwa ni karatasi iliyotumika wakati wa kurekodi iko mikononi mwa watu wa CCM; hili linatisha zaidi.

Hata kama video iwe ni ya kufoji ukweli kwamba kufojika kulifanyika bila CHADEMA kujua au kujiandaa inatisha zaidi! Mwigulu aliposema ana ‘video inaonesha CHADEMA wanapanga mauaji’ viongozi wa CHADEMA walichukua hatua gani? Au hata hawataki kujua kama alikuwa anasema kweli, anapanga kitu kibaya au ni kweli kulikuwa na video ya aina fulani?Hili ni karipio kali!

CHADEMA isijisahau kuwa katika kupendwa kwake bado ina wajibu wa kujionesha kuwa ni bora kuliko CCM. Sasa hivi kwa wiki hizi kadhaa CHADEMA imekuwa ikijihami (on the defensive) na haiko tena katika kushambulia (offense). Inajaribu kupata huruma ya wananchi kuwa CCM inawaonea; tumeshuhudia bungeni kuwa CHADEMA inatishia kujitoa kwenye mchakato wa katiba mpya wakati walienda na kunywa soda na rais na wakaamini kuwa CCM itakubali mchakato huru! Sisi wengine tulipoukataa mchakato huu na kuubeza na kuwashangaa watu walidhani tunatania! Leo wanashtuka ati mchakato utapendelea CCM. Really? Aliyewaambia nyoka hatagonga nani? Ooh tuliamini rais ana nia nzuri!!

Leo hii CHADEMA imeanzisha mchakato wa kutengeneza ‘kanda’ kama baadhi yetu tulivyoshauri ili ioneshe kweli inaamini kupeleka madaraka kwa wananchi. Lakini kile ambacho wengine tulikuwa tunakihofia ndicho kimetokea tena; wale wale watu walioko makao makuu sehemu nyingine wamepewa madaraka ya kuongoza kanda na sehemu nyingine ambapo tayari watu walikuwa ni viongozi wamepewa tena uongozi.Kanda zinaongozwa kwa katiba gani, na utaratibu gani? Hayajafanyika mabadiliko ya Katiba ya CHADEMA kuonesha madaraka ya kanda.

Matatizo yatakapoanza kutokea kwenye kanda wale wale watu walioko kwenye taifa watarudi kwenye kanda kwenda kutatua!! Sasa CCM ikianza kuvuruga hizi kanda tutawalaumu tena? Ninachosema ni kuwa CHADEMA itambue kuwa kutaka kuondoa chama tawala madarakani si lele mama; si jambo la kutokea kwa kuombea. Wale wanaosema kuwa ati CHADEMA “ina Mungu” wanajidanganya tu; Mungu hana itikadi wala hana kadi. Mungu hajiungi na vyama vya siasa na hana upendeleo. Siasa zinafanywa na wanadamu; tukianza kumwingiza Mungu tutaanza kuvumilia ujinga kwa kuogopa kupingana na Mungu.CHADEMA kama chama cha siasa kinahitaji kujipima vizuri kama kimejiandaa vizuri na kama kweli kina nia ya kuitoa CCM madarakani au kuendelea kuwa wapinzani wa kudumu – maana kuna watu wanafikiria zaidi kugombea ubunge mwaka 2015 kuliko kuuondoa utawala ulioshindwa wa CCM na matokeo yake wanatumia muda mwingi kwenye majimbo yao au majimbo tarajiwa na kusahau kuwa kuirejesha Tanzania mikononi mwa wananchi ni lazima tuinyang’anye kutoka kwenye kucha za CCM.

Bahati mbaya CHADEMA haioneshi ule umakini unaotakiwa wa chama kinachotaka kuja kututawala. Kuna baadhi ya makosa yanafanywa ambayo mengine yanapakana na uzembe; hili linatisha.Linatisha kwa sababu Watanzania wanataka chama kinachotaka kuja kuwaongoza (siyo kuwatawala tu) kiwe ni bora zaidi ya CCM; kwa maili nyingi sana. CHADEMA isipoangalia itaishia kushangiliwa ‘People’s power’ huku CCM ikiendelea ‘ku-exercise power over the people.

Source; Tanzania Daima

MAJIBU YA DR. SLAA

Kwanza ni shukuru sana kwa onyo kali la Mzee wangu Mwanakijiji.

Mtazamo, kwa mtazamaji wa Real Madrid na Barcelona, anayekaa nje ya uwanja ni rahisi sana kuona na kuchambua makos a ya Timu iliyoko uwanjani. Ebu mruhusu mchambuzi mkubwa wa mchezo aingie uwanjani, mwachie mwenye nusu uwanja, kipa aondoke alafu uone ” yuko peke yake”halafu uone Kama hatashindwa kufunga boa.

Nimwombe ndugu yangu Mwanakijiji achukue likizo, hata ya nusu mwezi tu, tumpitishe kwenye mapito tunayopitia, Kama baada ya mud huo atatumia lugha anayotumia.

I) Chadema inajua fika kuwa CCM imeisha panick, hawataki na hawako tayari kung’oka na sababu inajulikana angalau kwetu. Hivyo hatutegemei kama watacheka tu wakati Chadema intake kuwaondoa kwenye “utamu”.

2) kwa wanaofuatilia, wakati ccm inapanga kila siku mikakati, mbinu ya uhujumu, kununua shahada, kuiba kura, kubambikiza kesi, Chadema kwanza hatuna uwezo wa kufanya hivyo au kufanya hayo yote kwa kuwa kuwa ni kinyume na Imani na maadili ya Chadema. Chadema inafanya na itaendelea kufanya siasa za kisayansi wao waendelee na hujuma, na watashindwa tu.

3) iwapo Chadema itafanya rafu Kama wao Watanzania hawatajua na wall hawataona tofauti Kati yetu na CCM. Kwa approach yake, kwa matendo yake, kwba mipango yake Chadema la zima iwe tofauti kabisa na CCM Kama mbingu na ardhi indigo maana tunataka kuwaondoa kwa kuwa wananchi wamechoka na hizo wao, ufisadi wao, umafia wao, manyanyaso Yao. Huwezi kupanga kuleta mabadiliko makubwa ya chi na bado ukafanana na wao.

4) rafiki na kaka yangu Mwanakijiji inaelekea hajui tulitoka wapi. Tumeanza kazi ya kuzunguka chi tangu 2004. Baada ya uchaguzi mkuu wa 2005 na 2010 tumezunguka sana. Ndiyo sasa watanzania wanaanza kutuelewa. Ndiyo maana militia repot kuwa katika kaki kubwa tuliyofanya, Maandamano yamefanikiwa kwa asilimia 99.99999. Hii haikuja tu kwa kuteremka mbinguni, ni mkakati wa kisayansi wa Chadema. Leo Serikali na CCM wamepanic kwa kuwa wanaona sasa wataondoka.

Utawala wowote, ukifikia hatua hiyo hautaogopa kuua raia wake. Uzoefu wa North Africa ni ushahidi tosha. Leo vijijini vinavyofanya uchaguzi wa marudio iwe ngome za ccm, au vijijini ambavyo Chadema haijakanyaga wananchi wamejiwekea wagombea kwa ticket ya Chadema waneshinda wenyewe. Hii haikutokea hivi hivi, ni kwa kuwa wananchi sasa wanaona Chadema ni Tumaini Lao pekee.Tungeenda njia ya mapambano na tabia umwagaji damu kama wanavyofanya Serikali wananchi wangelituona ni wale wale tu.

Leo wanajua Chadema si chama cha vurugu isipokuwa pale tu polisi wanapoingilia kutuzuia bila msingi na Mara nyingi kinyume na sheria. Hii ni credit kwa Chadema na ndiyo inayotuletea Leo mamilioni ya Watanzania. Mkakati hue hauwezi kubezwa. Umekuwa tested na umeonyesha matunda.5) sasa hive ninapoandika, tuko kwenye TOT ya viongozi wakufunzi watakaoenda kufundisha viongozi wa kanda wapatao 1,200, na wao watashuka kwenye majimbo na kufundisha viongozi wapatao 428 wa majimbo, na wao watashuka kwenye Kata kufundisha viongozi makundi yote takriban 30,000. Hii maana yake ni kuwa kuanzia Juni tuna uwezo wa kushika kwenye vijiji takriban 18,000 na vitongoji takriban 250,000, katika hatua hiyo sasa tutakuwa kweli Real Madrid na Barcelona, kwa kuwa tunaenda kuwakaba kule kule chini ambayo miaka yote walidhani hakuna chama chochote cha Upinzani kitafika huko.

Kama kuna mtu Ana mkakati bora zaidi wa kuwafikia wananchi, kuwaelimisha na kuwaelimisha katika masahibu Yao, kuunda matawi na misingi katika ngazi ya chini kabisa na kusimika uongozi had mabalozi katika kila kaya 10, yaani kila namba ya ccm ikabwe na namba inayofanana. Tofauti ni kuwa Chadema inaweka timu iliyopikwa na kufunzwa maadili, uongozi na namna ya kung’amua hila na hujuma za ccm. Hawana pa kupita tena.

Mbinu hii haikubuniwa tu, ni matokeo ya utafiti wa kisayansi, kutafakariwa athari na strengths and weaknesses zake kwa kina. Inatokana na uzoefu wa Arumeru Mashariki ambapo tulifanikiwa vituo hewa 55 vyenye jumla ya kura bandia 20,000. Jambo amble tusingeligundua mapema, Leo hued Nassari asingekuwepo Bungeni. Ni dhahiri Challenge ya Mwanakijiji tunazipokea, tutazifanyia kazi, lakini mazingira ya kila siku kukimbizana na polisi, kukataliwa mikutano ya hadhara wakati wananchi hawajahamasishwa ya kutosha ( wakati ule), kubambikiziwa kesi za kila aina ikiwemo ugaidi, wapenzi wetu kuwekwa rumande na kuwekewa masharti magumu kwa mfano Masasi walikamatwa watu 140 Kati Yao watu chini ya miaka 18 kwa sababu tu ya kukutwa na banner, kadi, tshirt, nembo za Chadema, na kila mdhamini kutakiwa aweke dhamana ya hatimiliki ya Mali isiyoondosheka ya T sh 70,000 kwa kila mmoja huo ni wenda wazimu ambao Mwanakijiji hajui.

Au kijijiji cha Ruaha Kilosa ambako Kinana alishindwa kuhutubia juzi ambako kiongozi, ambae wananchi wanamtaka awe Mwenyekiti wa Kijiji yuko rumande leo ni mwezi wa nne. Uwenda wazimu huu, au mpigane damu imwagike watu wadhurike, jambo amble Chadema tumesema hatutaki, wala hatutafanya pamoja na kupakaziwa kila siku ( wakati wa Kampeni niliwaahidi watanzania sitaki hata mtu mmoja apoteze maisha, au amwage damu kwa ajili ya Ikulu) ndivyo ilivyokuwa isipokuwa pale Polisi walipotumia nguvu bila sababu( tazama Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu- combo cha Serikali ambayo ilipingana wazi wazi na taarifa ya Kamati ya
Waziri Nchimbi).

Ustaarabu huu wa Chadema ndio umekifanya Chadema ipate mafanikio iliyoyapata, na hasa ya kukubalika na Watanzania. Watanzania wa Leo si wajinga, Kama mbunge wa ccm anatukana matusi makubwa akalindwa, mbunge wa Chadema anayesema The Government is impotent, ccm na hata Spika anaita ni kuwatukana kwa neno ——-… Umbumbu wa wazi wa wabunge wa ccm, kitu kinachotia mashaka wao wote na Spika wao. Impotent ni neno la kawaida la kiingereza ( lenye asili ya kilatini) .

Wameshindwa nini kuchukua dictionary, siku hizi hata kwenye simu kuna dictionary kujua maana halisi ya neno Hilo katika context iliyotumika. Hasara ya shule ndogo, au ushabiki usio na tija wakifikiri watapata umaarufu wa muda mfupi.

JAMII FORUMS

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO