Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Hati kwa wananchi Loliondo ilitolewa kimakosa-Kagasheki

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamisi Kagasheki (pichani) ameibuka na kusema eneo lenye mgogoro wa ardhi huko Loliondo, mali ya Serikali na kwamba hatua ya wananchi kupewa hati, ilifanywa kimakosa.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba kumshauri Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuingilia kati huo kwa kuzingatia kuwa unahusu maisha ya wananchi.

Mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa, ulishika kasi Machi 26, mwaka huu baada ya Serikali kutangaza kuchukua eneo la kilometa za mraba 1,500 na kuwaachia wananchi kilometa za mraba 2,500. Hatua hiyo iliambatana na maelezo kuwa uamuzi huo ni kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji, mazalia na mapito ya wanyamapori.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Balozi Kagasheki alisema mmoja wa mawaziri waliopita (hakumtaja jina), alitoa hati za vijiji kimakosa na kwamba mgogoro huo unachochewa na wanasiasa na mashirika 37 yasiyo ya kiserikali kwa faida zao binafsi.

“Penye ukweli nitasema, lakini kamwe Serikali haiwezi kuendeshwa na wanasiasa wala na NGOs, hao waliopinga barabara kujengwa katika mbuga ya wanyama ya Serengeti leo hii ndiyo wanalilia pori tengefu la Serikali, ajabu sana,” alisema Balozi Kagasheki.

Mbali na Nchemba kuiomba Serikali kushughulikia suala hilo, baadhi ya wakazi wa Loliondo ambao waliambatana na madiwani wawili, waliibukia Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) juzi na kudai kuwa wapo tayari kuuawa na kuzikwa katika kaburi moja, lakini si kuhama katika eneo hilo.

Katika ufafanuzi wake Balozi Kagasheki alisema eneo la Loliondo ni mali ya Serikali ambayo mwaka 1974 ilitenga kilometa za mraba 4,000 katika eneo hilo kuwa pori tengefu.
“Tangu wakati wa utawala wa Mwingereza, Mjerumani na baadaye chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere hadi sasa wakati wa Rais Jakaya Kikwete, eneo la Loliondo ni mali ya Serikali,” alisema na kuongeza;

“Mimi waziri mwenye dhamana nilifikia uamuzi wa kumega eneo la pori tengefu la Loliondo na kuwapatia wananchi kwa mujibu wa sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, nilizingatia ushauri na mgogoro wa eneo husika, hivyo kusema Serikali imepora ardhi kwa wananchi si sahihi,” alisisitiza. Alisema baadhi ya watu wanazungumza uongo kuhusu mgogoro huo lengo likiwa ni kujinufaisha kisiasa.

“Kama kiongozi lazima uwe na uamuzi, kila mtu anasema lake lakini tuangalie sheria zinasemaje, bora useme ukweli watu wachukie kuliko kusema uongo kwa ajili ya kujinufaisha kisiasa,” alisema.

Alisema Serikali ilichukua uamuzi wa kutenga eneo hilo kwa kuelewa kwamba mazingira ya uhifadhi ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha mfumo ekolojia kwa maendeleo ya jamii.
“Ipo sheria ya kulinda vyanzo vya maji, tumefanya vile kwa kuwa eneo lile likiachwa hakutakuwa na utunzaji, tutapoteza wanyamapori kama ilivyotokea Nigeria, Ghana na Ivory Coast.”

Imeandikwa na Mwananchi

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO