Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Kesi ya Lwakatare hatarini kufutwa tena • Polisi, ofisi ya DPP wanyosheana vidole

KESI ya ugaidi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph huenda ikafutwa tena na kufunguliwa upya, Tanzania Daima Jumapili limebaini.

Duru za kisheria kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na mahakama zililieleza gazeti hili kwa nyakati tofauti kuwa kesi hiyo huenda ikafutwa tena na kufunguliwa upya kutokana na utata na makosa ya kisheria.

Kosa kubwa linaloelezwa kuwapo katika mashitaka mapya ni kuyaingiza mashitaka yanayowakabili watuhumiwa katika makosa ya sheria ya ugaidi wakati hayana sifa kisheria ya kuwamo katika makosa ya ugaidi.

Endapo kesi hiyo itafutwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, itakuwa mara ya pili kufutwa na kufunguliwa upya.

Baadhi ya wanasheria waliobobea, waliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa ofisi ya DPP imerudia kosa lile lile ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya kufungua kesi ya ugaidi dhidi ya watuhumiwa huku wakijua fika kwamba makosa yao hayajafikia kiwango cha ugaidi.

Kwa mujibu wa magwiji hao wa sheria ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, makosa ya watuhumiwa hao yamo katika kanuni za adhabu kama makosa ya kawaida kwa mujibu wa sheria, kifungu cha 384, hivyo ni makosa yanayostaili dhamana na hayamo katika makosa ya ugaidi.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya polisi wanaochunguza kesi hiyo na ofisi ya DPP.

“Mashitaka yaliyofunguliwa ya ugaidi na DPP dhidi ya washtakiwa yametuweka katika wakati mgumu, maana tunahaha kupata ushahidi kuithibitishia mahakama kwamba hayo ni makosa ya ugaidi,” alisema mmoja wa viongozi wa polisi wanaoendelea na uchunguzi wa kesi hiyo.

Kosa jingine kisheria linalodaiwa kufanywa na DPP ni katika shtaka la nne linalomkabili Lwakatare peke yake.

Katika shtaka hilo, Lwakatare anadaiwa kuwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume na kifungu cha 23(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi.

Inadaiwa kuwa Desemba 28, mwaka jana, Lwakatare akiwa mmiliki wa nyumba anayoishi Kimara King’ong’o, kwa makusudi aliruhusu kufanyika kwa mkutano baina yake na Ludovick wa kutenda kosa la ugaidi, kutaka kumteka nyara Denis Msacky, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi.

“Shtaka hili nalo lina makosa kisheria. Kwa wanasheria mahiri kama Tundu Lissu, mawakili wa serikali lazima wajipange. Kwa sababu sheria ya mikusanyiko ya watu, au tuseme kikao au mkutano kama shtaka linavyosema unaanza na watu wangapi?

“Ule mkanda wa video nimeuona, anaonekana Lwakatare akiongea, na mtu mwingine anapitapita na kusikika akiitikia. Maana yake kulikuwa na watu wawili tu. Hicho ni kikao au mkutano?” alihoji mwanasheria huyo.

Habari zaidi zinasema kuwa ili kupata ushahidi wa kutosha kuthibitisha ugaidi unaodaiwa kufanywa na Lwakatare, polisi wanadaiwa kutumia kila mbinu zikiwamo chafu kujaribu kupata ushahidi.

Juzi Mkurugenzi wa Mambo ya Katiba na Sheria wa CHADEMA, Tundu Lissu, alifichua kile alichokiita moja ya mbinu chafu zinazofanywa na polisi.

Lissu ambaye ni mmoja wa wanasheria katika kesi ya Lwakatare, alidai kuwa polisi kwa kushirikiana na baadhi ya vyombo vingine vya usalama na ujasusi, vimekuwa vikitengeneza ushahidi wa uongo kwa ajili ya kuutumia mahakamani katika kesi ya ugaidi inayomkabili Lwakatare na mwenzake.

Alisema mbali na hayo, pia kuna baadhi ya vijana wa CHADEMA wa Idara ya Ulinzi na Usalama wanaopewa fedha na kuahidiwa kufundishwa namna ya kuzungumza katika kesi ya Lwakatare mahakamani.

Lissu alisema mpaka sasa vijana hao wameshapewa sh 400,000 ili wakubali kwenda kufundishwa jinsi ya kuzungumza mahakamani kuwa CHADEMA ni chama cha kigaidi na Lwakatare alipanga mikakati ya kigaidi.

“Awali walipewa sh 400,000, wakapewa tena sh 300,000, pia wakapewa sh 35,000 mara mbili. Na pesa zote hizo walikuwa wanapewa kwa njia ya M-Pesa,” alisema Lissu.

Hata hivyo, Lissu alikataa kuwataja vijana hao wa CHADEMA waliopewa fedha hizo. Lakini akamtaja mmoja wa wafanyakazi wa chama hicho aliyekuwa makao makuu (jina tunalihifadhi) na alikwishakufukuzwa kazi kwa kukosa uaminifu, kuwa alikuwa anawafuata na kuwapa fedha hizo.

Habari zinasema kuwa bila kutumia ujanja huu, kesi hiyo inaweza kufutwa na kufunguliwa upya kama ilivyofutwa awali.

Machi 20, mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam ilimfutia kesi ya makosa ya ugaidi Lwakatare na Ludovick kisha kuwakamata tena na kuwafungulia kesi mpya yenye mashtaka yaleyale ya ugaidi.

Ingawa kesi inapofutwa na DPP hakuna sababu zinazoainisha kufutwa kwake, lakini kesi ya awali ilifutwa kutokana na makosa ya kisheria.

Inaelezwa kuwa kwa vile makosa yake yanahusishwa na ugaidi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina uwezo wa kuisikiliza, lakini badala yake Hakimu Emilius Mchauru aliamua kuisikiliza kinyume na sheria.

Hata hivyo baada ya kesi ya awali kufutwa na watuhumiwa kuachiwa, Lwakatare na mwenzake walikamatwa tena na kufikishwa mahakamani hapo kisha kufunguliwa kesi mpya namba 6/2013, ambayo imepangiwa hakimu mpya, Aloyce Katemana badala ya Mchauru.

Mashtaka mapya yanayowakabili watuhumiwa wa kesi hiyo inayovuta hisia za wengi ni manne.

Shtaka la kwanza linaangukia kwenye sheria ya kanuni ya adhabu ya mwaka 2002 na makosa matatu yote yanaangukia kwenye sheria ya kuzuia ugaidi ya mwaka 2002.

Shtaka la kwanza ambalo linawakabili washitakiwa wote ni kula njama kwa nia ya kutenda kosa la jinai kinyume na kifungu cha 284 cha sheria ya kanuni ya adhabu ya mwaka 2002.

Chini ya shtaka hilo, inadaiwa kuwa Desemba 28, mwaka jana huko Kimara King’ong’o Stopover, washitakiwa kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kutaka kutumia sumu kwa lengo la kumdhuru Dennis Msacky, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi.

Kosa la pili ni la kula njama ambalo pia linawakabili washtakiwa wote.

Shtaka hili lipo chini ya kifungu cha 24(2) cha sheria ya kuzuia ugaidi Na. 21 ya mwaka 2002 ambapo wanadaiwa kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka nyara Msacky.

Shtaka la tatu ambalo pia linawakabili washitakiwa wote ni la kupanga kufanya makosa ya ugaidi kinyume na kifungu cha 59(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi.

Inadaiwa kuwa Desemba 28, mwaka jana, washtakiwa hao walishiriki katika mkutano wa kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyara Msacky.

Shtaka la nne linamkabili Lwakatare peke yake ambalo ni kuwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume na kifungu cha 23(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi.

Inadaiwa kuwa Desemba 28, mwaka jana, Lwakatale akiwa ni mmiliki wa nyumba hiyo iliyopo Kimara King’ong’o kwa makusudi aliruhusu kufanyika kwa kikao hicho baina yake na Ludovick cha kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka nyara Msacky.

Chanzo: Tanzania Daima, 07/04/2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO