Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (pichani) ameiponda Serikali kwa kuwa na uchumi unaokua kwenye makaratasi wakati maisha ya wananchi yakiendelea kuwa magumu siku hadi siku.
Profesa Lipumba alisema hayo jana kwenye mkutano wa 18 wa mwaka wa Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa Umaskini Tanzania (Repoa).
Akizungumza mbele ya Makamu wa Rais, Dk Mohamed Bilal, Profesa Lipumba alisema uchumi wa Tanzania hivi sasa unakwenda kama mtoto anayetambaa akiwa na watu wazima wanaokimbia.
“Tulikuwa na mipango mingi lakini isiyotekelezeka, tulielezwa ni lazima tukimbie wakati wenzetu wanatembea, lakini badala ya kuongeza mbio, sasa tunatambaa wakati nchi za wenzetu zinakimbia kwa kasi kimaendeleo,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema ingawa uchumi unakua kwa asilimia saba kwa mwaka, lakini ukuaji huo haulingani na maisha ya wananchi ambayo yanazidi kuwa magumu siku hadi siku.
Profesa Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi, alisema sekta ya kilimo ambayo inaajiri asilimia 75 ya wananchi inakuwa kwa asilimia 25.
“Unategemea nini kama sekta ambayo inawahusisha wananchi wengi, lakini bado haijaboreshwa ili iwanufaishe,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema ingawa Serikali imekuwa na mipango mizuri, lakini imeshindwa kuitekeleza hatua ambayo inawafanya wananchi wakate tamaa ya maisha.
Akitoa mfano, alisema kitendo cha kuwa na vipaumbele vingi wakati uwezo wa fedha ni mdogo ni kikwazo cha kuleta maendeleo.
“Hata kwenye bajeti zetu tumekuwa na vipaumbele vingi kiasi kwamba hata kuvitekeleza inakuwa vigumu, tuchague vipaumbele vichache na tuvifanyie kazi,” alisema Profesa Lipumba.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Dk Bilal alisema kukua kwa uchumi unaowafikia wananchi ni mchakato ambao hauwezi kuja ghafla. Alisema kitendo cha Serikali kutengeneza miundombinu ikiwamo barabara ni moja ya juhudi zinazofanywa ili wananchi waweze kunufaika.
“ Ni kweli ukuaji wa uchumi haufanani na maisha ya wananchi wengi, lakini hatua zinazochukuliwa na Serikali kama kujenga barabara, maji ,huduma za afya na elimu zinasaidia kukuza uchumi kwa watu walio wengi,” alisema Dk Bilal.
Naye,Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Profesa Samwel Wangwe alisema mkutano huo wa watafiti unaangalia namna ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi walio wengi.
Kwa upande wake,Mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Malaysia, Datuk Chris Tan alisema uchumi utakuwa juu kama viongozi watakuwa na nia ya dhati ya kuleta mabadiliko.
Imeandikwa na Mwananchi, 04/04/2012
0 maoni:
Post a Comment