Kutangazwa kwa Esther Bulaya kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo la Bunda Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kumesababisha uongozi wa jimbo wa chama hicho ‘kubomoka’ na kutangaza kumuunga mkono mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wassira.
Mpusuko huo, ulidaiwa kusababishwa na uongozi wa ngazi za juu kumpitisha Bulaya kugombea jimbo hilo wakati alishindwa kwenye kura za maoni, hivyo kufanya mwenyekiti wa wilaya, Samwel Alfred, katibu wake, Rita Itandilo na katibu mwenezi wa chama kujiuzulu nafasi zao.
Baadhi ya viongozi na wanachama wa chama hicho walisema watamuunga mkono mgombea wa CCM, Stephen Wassira, kwa sababu viongozi wao wamejichanganya na kuwafanyia maamuzi yasiyo sahihi.
Walisema kwa mujibu wa Katiba ya chama chao, uteuzi wa mbunge unafanyika kamati kuu, lakini walishangazwa kuletewa jina la Bulaya bila kuushirikisha uongozi wa wilaya hiyo ambao umekuwa mstari wa mbele kukijenga chama.
Alfred alisema ameamua kujiuzulu wadhifa wake kwa sababu ya kukerwa na uongozi kuvunja Katiba ya chama.
“Cha kwanza tulipiga kura za maoni wakapatikana washindi watatu wakiwamo wawili ambao wamekitumikia chama, lakini cha ajabu wakarudisha jina la mshindi wa tatu (Bulaya)…hiyo ni kuvunja katiba, lakini cha ajabu aliyerudishwa hakuonyesha ushirikiano na viongozi waliokuwapo madarakani na kuingiwa na hofu ya kusababisha chama kishindwe,” alisema.
Naye Katibu mwenezi wa Chadema jimbo la Bunda, Malibwa alisema kama katibu mwenezi wa Chadema jimbo la Bunda aliamua kutangaza kujiuzulu pamoja viongozi wa kata 20 zilizopo jimboni humo, wakiwamo wenyeviti na makatibu wa kata.
Hata hivyo, akizungumza kwa niaba ya katibu wa wilaya Chadema, Kaunya Yohana, alisema viongozi wapatao 11 waliotangaza kujiuzulu ni wazushi, kwa kuwa chama kimewasimaisha uongozi kwa sababu mbalimbali zikiwamo za kupandikiza mamluki, rushwa na ukiukaji wa maadili.
CHANZO: NIPASHE
0 maoni:
Post a Comment