Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

MAMA NKYA - NAMUUNGA MKONO LOWASSA KUGOMBEA URAIS

 

Mimi Ananilea Nkya tatizo langu kubwa kwa Lowassa lilikuwa ni ufisadi wa Richmond uliotafuna zaidi ya shilingi bilion 172 za wananchi. Baada ya kusikia kauli yake alipohojiwa na wanahabari siku alipojiunga na CHADEMA, na baada ya kujiridhisha kuwa kama alikuwa amehusika na ufisadi wa Richmond leo angelikuwa jela kama Yona na Mramba, namuunga mkono kugombea Urais. Naamini hata Dr Slaa amemkubali Lowassa kuwa mgombea Urais wa vyama vinanyounda UKAWA baada ya kujiridhisha kuwa mamlaka ya juu ilimbebesha Lowassa kashfa ya Richmond ili kunusuru serikali nzima kuanguka.

Lakini zaidi nimeongeza imani yangu kwa Lowassa baada ya kubaini kuwa hata Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere alimuona kama kijana makini mwenye maono na dhamira safi ya kuwatumikia Watanzania. Mwaka 1995 wakati Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi anamaliza muda wake mwandishi wa habari Mwita Matinyi alimuliza Mwalimu Nyerere alikuwa anafikiri ni nani angeweza kumrithi Mwinyi kuiongoza Tanzania. Mwalimu alijibu Matinyi hivi. Nanukuu:

Ni kweli Mzee Mwinyi anaondoka lakini ndani ya CCM kuna viongozi wengi wenye sifa za kuwaongoza Watanzania, kikubwa tu awe na dhamira kwa mfano wapo wakina Warioba, Mzee Msuya na Mark Bomani na wapo vijana hodari na wenye upeo mkubwa sana kama Mkapa, Kikwete na Lowassa ni jambo la heri sana CCM kuwa na watu kama hawa (Majira 26/5/1995) ukurasa wa 3; na Nipashe 26/5/95 ukurasa wa 3).

Pia nikiwa ripota Radio Tanzania Dar es Salaam niliwahi kufanya kazi na Lowassa katika miaka ya 90. Nilivyouona utendaji wake wa kazi zama hizo nashawishika kwamba anafaa kuwa kiongozi wa nchi yetu. Nilishuhudia akijituma kweli kweli kwenye kazi za umma zama hizo.

Kadhalika namuunga mkono Lowassa kwa sababu hagombei Urais kupitia chama cha CCM ambacho kinakumbatia mfumo wa kuwadharau na kuwafukarisha wananchi huku watawala wachache wakineemeka kwa kutumia rasilimali za nchi kama vile nchi hii ni mali ya watawala, familia zao na marafiki zao. Ninaamini kwa kugombea Urais kupitia UKAWA, CCM itapunguziwa dharau na jeuri yake dhidi ya wananchi ambao ndio wenye mamlaka ya mwisho kuhusu hatma ya nchi yetu. Mfano CCM mwaka jana 2014 ilionyesha dharau kubwa sana kwa wananchi kwa kuizika Rasimu ya Katiba iliyotengenezwa kwa kutumia maoni ya wananchi wakati fedha zaidi ya bilioni 130 zilitumika. Kwa kutumia mabilioni hayo bila Katiba Mpya kupatikana ni kufisadi mali za wananchi mchana kweupe. Haikubaliki.

Vile vile namuunga mkono Lowassa kwa kwa sababu anaukataa hadharani umaskini wa kuchongwa ambao watawala wanautumia kwa faida yao ili waendelee kuwanunua wananchi mafukara wakati wa uchaguzi na wakishapata madaraka waendelee kujineemesha na mali za nchi.

Nchi yetu siyo maskini bali watawala wanaendekeza matakwa ya wawekezaji (wakoloni wa zama hizi za utandawazi wizi) ambao wanaliibia taifa rasilimali nyingi na na hatimaye nchi za wawekezaji hao (donors)wanawapoza watawala kwa vijimisaadaa uchwara. Ni aibu sana kwa kiongozi wa Tanzania kijipitisha nchi moja hadi nyingine Marekani, Ulaya, China, India na Ausralia n.k kutembeza bakuli (omba omba kama matonya vile) huku nchi yetu ikiwa na rasilimali tele. Tena wakati watawala wanakwenda kuomba eti wanapanda ndege daraja la kwanza. Huu ni wenda wazimu. Ni kuiaibisha Tanzania na Afrika.

Sina chama cha siasa ninachofungamana nacho kwa sasa, lakini namuunga mkono Lowassa kugombea Urais kupitia UKAWA kwa sababu naamini akiwa Rais wa nchi yetu upuuzi huu wa kuendekeza umaskini kwa kuomba omba nchi za nje huku tukitoa mali za nchi honyo hovyo kwa wageni na kuamini kuwa maendeleo ya nchi yetu yataletwa kwa misaada kutoka nje, kutakomeshwa. Naamini hata hao wakoloni wa zama hizi za utandawazi wizi wanajua Lowassa hatachekacheka nao.

Lakini zaidi namuunga mkono Lowassa kwa sababu Watanzania wakiridhia kwenye sanduku huru la kura hapo Oktoba awe Rais wa Tanzania, vyama vinavyounda UKAWA vitasimamia kuhakikisha kuwa mamlaka ya wanannchi hayaporwi hovyo hovyo tena. Kwa hiyo Rasimu ya Katiba ya wananchi itaheshimiwa na nchi yetu itapata Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi. Kwa kufanya hivyo taifa hili litaanza kupiga hatua kubwa ya kuondoa ufukarishwaji wa wananchi walio wengi unaofanya na watawala wa CCM kwa kushirikiana na wakoloni wa zama hizi za utandawazi wizi.

Naridhia andiko langu hili lichapishwe na yeyote anayetaka

Ananilea Nkya

E-mail:ana...@yahoo.com

Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO