Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Mungu amemtuma Lowassa kuangusha CCM – Mbowe

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewasihi Watanzania wasikubali kutiwa hofu na watu wanaomwogopa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyejiunga na chama hicho hivi majuzi, na kupewa fursa ya kugombea urais kuwakilisha vyama viulivyo katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Akifungua kikao cha Baraza Kuu la Chadema jana Jumatatu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema ujio wa Lowassa umetia hofu baadhi ya watu, hasa viongozi, katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema, na kwamba walio ndani ya chama tawala wanaogopa kuangushwa katika uchaguzi mkuu, wakati walio ndani ya Chadema wanaogopa kwamba ujio wa Lowassa unaweza kupoka fursa zao,, hasa kwa kuwa Lowassa amehama CCM akiwa na jeshi kubwa la wafuasi.
Hata hivyo, alisema tayari viongozi na wanachama wengi wa Chadema na UKAWA wameshagundua kwamba Chadema ni chama cha siasa, na ni chama cha watu, wala si cha viongozi, na kwamba baada ya miaka 25 ya ushindani wa vyama vingi, Mungu ameamua kumtumia Lowassa na Chadema kujeruhi na kuiangusha CCM.
Alisema Chadema kimekuwa chama tawala mbadala kinachojiandaa kuongoza serikali kwa kushirikiana na vyama vingine ndani ya UKAWA, baada ya uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu, na kwamba chama hicho kipo tayari kumpokea yeyote nje ya vyama vinavyounda UKAWA anaweza kusaidia kubomoa mfumo mkongwe wa CCM.
“Kipigo wanachopata CCM hawajawahi kukipata tangu tuanze siasa za mageuzi… hatuwezi kuwa chama cha kuendelea kuhubiri mabaya ya zamani tukashindwa kuhubiri mema ya sasa na matumaini ya kesho,” alisema.
UKAWA unaundwa na Chadema, NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na National League for Democracy (NLD). Katika makubaliano ya UKAWA, Chadema ndicho kimepewa fursa ya kuteua mgombea urais na mgombea mwenza kwa niaba ya vyama vyote.
Aliwaomba viongozi wa Chadema watumie chama chao kama kimbilio la wananchi wote, hata wale ambao wamekuwa wanasemwa kuwa wabaya, kwa maana ndiyo njia pekee ya kuunganisha na kupatanisha Watanzania wote kwa ajili ya maisha mema ya baadaye.
“Katika siasa kuna kitu kinaitwa “game change”…ndiyo dynamism ya kisiasa,” alisema Mbowe.
Chadema kinatarajia kuteua rasmi na kutangaza mgombea urais na mgombea mwenza katika Mkutano Mkuu wake utakaofanyika kesho Jumanne katika ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa, aliyejiunga na chama hicho baada ya kuhama kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) wiki iliyopita, ndiye mgombea pekee aliyechukua na kurejesha fomu ya kugombea urais. Jana Jumapili Kamati Kuu ya Chadema ilipitia na kujadili fomu ya mgombea urais.
Lowassa ndiye mgombea anayetarajiwa kuwakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kupambana na mgombea wa CCM John Magufuli.
Wakati huo huo, Baraza Kuu la Chadema, linalojumisha viongozi wakuu wa chama hicho kutoka kila wilaya, limeridhia ombi la Katibu Mkuu Dk. Slaa kupumzika kwa muda wakati mchakato wa uchaguzi mkuu unaendelea.
Akihutubia Baraza hilo leo Jumatatu, Agosti 3, 2015, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema, “tumekubaliana na Katibu Mkuu apumzike kwa muda, na kwamba mambo anayoshughulikia yatakapokuwa uameisha, atatukuta mbele ya safari.”
Baada ya kutoa taarifa hiyo, akauliza kama wajumbe wa Baraza Kuu wanaridhia; akasema wanaoridhia wasimame. Wajumbe wote ukumbini wakasimama kama ishara ya kukubaliana.
Akihitimisha taarifa hiyo, huku akisisitiza kuwa kauli ya wengi ni kauli ya Mungu, Mbowe alisema, “chama hiki hakiendeshwi kwa siri; kinaendeshwa kwa mikakati.”
Kauli hiyo ya Mbowe inahitimisha minong’ono iliyokuwa inaendelea kuhusu Dk kutoshiriki katika vikao vinavyoendelea hasa baada ya Lowassa kujiunga na Chadema, huku baadhi ya wanong’onaji wakidai kwamba amekasirishwa na chama chake kumpokea kiongozi huyo ambaye amekuwa akitambulishwa kama “fisadi” kwa miaka minane mfululizo,
Hata hivyo, Chadema kinajua kuwa Dk. Slaa amekuwa mmoja wa viongozi walioshiriki kuongoza mazugumzo ya chama chake na Lowassa, na kwamba kinachotokea sasa ni changamoto nyingine katika kukua kwa chama na demokrasia nchini, na kwamba changamoto hizo zitakapokuwa zimepungua, Dk. Slaa atarejea katika shughuli zake za kisiasa.
Kwa sasa, shughuli za kiofisi za Dk. Slaa zinakaimiwa na Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar, Salum Mwalimu. Baada ya kufungua kikao cha Baraza Kuu jana, Mbowe alimuomba Naibu Katibu Mkuu, John Mnyika, kuongoza kikao hicho wakati yeye na viongozi wengine wakishughulikia masuala mengine ya kichama kuhusu vikao vinavyoendelea.

Picha Zaidi za Kikao Cha Baraza Kuu Chadema


Mhe. Edward Lowassa akiongea na wajumbe katika Kikao cha Baraza Kuu katika ukumbi wa Kisange Conference Center leo

Naibu Katibu Mkuu Bara Mh John Mnyika akiwa na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Mh Salum Mwalim.

Mh Tundu Lissu (Kulia) na Mh Godbless Lema wakiwa katika mkutano wa baraza Kuu la Chadema.

Vigogo watatu wa CCM waliomsindikiza Lowassa kwenye mkutano wa Baraza kuu la Chadema. Kutoka kushoto ni Matson Chizii, Mh Ole Medeye na Mgana Msindai.

Wajumbe Kutoka kanda mbalimbali waliohudhuria mkutano wa Baraza kuu la Chadema, mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Kisange, Makumbusho Dar es salaam.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar Said Issa Mzee akisoma dua kwa dini ya kiislam wakati wa ufunguzi wa kikao cha baraza kuu la Chadema.

Mbunge wa Iringa Mjini Mchingaji Petermsigwa akisoma dua ya kikristo katika ufunguzi wa Mkutano wa Baraza Kuu

Aliyekuwa mbunge wa Arumeru magharibi ccm Ole Medeye akipungia mkono wajumbe walioshiriki kikao Cha Baraza Kuu la Chadema.

Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM Mh Mgana Msindai leo alikuwa ni mmoja wa watu waliohudhuria kikao cha Baraza la Chadema.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr TW

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO