Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

HOTUBA YA MGOMBEA URAIS KUPITIA CHAMA CHA CHADEMA NA UKAWA MH. EDWARD NGOYAI LOWASSA YA KUZINDUA ILANI NA KAMPENI YA UCHAGUZI MKUU 2015

 

Jangwani-Dar-es-Salaam, 29 AGOSTI 2015

Ndugu Wana Dar es salaam na Watanzania wenzangu

Leo ni siku ya kihistoria. Baada ya miaka ishirini na tano tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe, vyama vya upinzani wa CHADEMA, CUF, NCCR na NLD umeungana chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi kupigania uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kuwa na mgombea mmoja katika ngazi zote.

Miaka zaidi ya hamsini ya utawala wa serikali za CCM na waasisi wake, umekuwa utawala wa wachache walio hodhi madaraka na mali za nchi.

Leo tunaanza safari ya uhakika ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini.

Mabadiliko yaletayo neema na kujenga upya mfumo wa uchumi, haki na sheria nchini.

Mabadiliko ya kuimarisha huduma za jamii kama elimu, afya, maji na makazi.

Mabadiliko ya kuondoa umaskini.

Mabadiliko tunayatoahidi ni mabadiliko ya kurejesha matumaini kwa Watanzania kwa kubadili hali zao za maisha.

Kila mwaka hali na ubora wa maisha ya Watanzania imeshuka wakati tunaambiwa kuwa pato laTaifa linakuwa.

Lakini Watanzania wanachotaka siyo takwimu bali kuona kipato chao kinakua, shule, hospitali na barabara bora zinajengwa.

Wanataka kupata maji safi na salama ya kunywa. Wanataka makazi bora.

CHADEMA na UKAWA, tuna dhamira ya kuleta mabadiliko ya kweli ili kuona azma ya Watanzania tangu uhuru ya kuondoa umaskini, maradhi,na ujinga inahitimishwa.

Ili tufanye hivyo tuahitaji tufanye mabadiliko ya fikra, uongozi, sera na utendaji.

Leo Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi za ki-uchumi, kisiasa na kijamii. Changamoto hizi ni matokeo ya sera za utawala wa Chama kimoja wa miaka hamsini. Sote ni wahanga wa siasa na sera hizi.

Miaka Hamsini ya CCM imetosha. Tunataka mabadiliko na siyo ahadi zile zile kila mwaka

Tusidanganyike, CCM hawana jipya

Chagueni UKAWA wenye dira ya kubadili maisha ya wananchi.

Mimi ninauchukia umaskini na mimesimamia maendeleo kwa vitendo. Nilipokuwa Waziri Mkuu nilijaribu kubadili hali hii. Nilisimamia ujenzi wa shule za kata, Chuo Kikuu cha Dodoma. Nilihakikisha mikataba mibovu ya maji inavunjwa na sasa wananchi wa kanda ya ziwa wanapata maji safi.

Ndugu watanzania

CCM wanauliza tuna mpango gani wa kumaliza umaskini. Sisi hatuahidi tu. Tutatenda.

Ilani yetu ni dira ya kuondoa umaskini kwa mikakati sahihi na siyo nadharia.

Mkakati wa kuondoa umaskini si wa sekta kwa sekta bali wa sekta zote kwa pamoja. Ni ujumla wa utendaji na utekelezaji wa sera za kila sekta utakao leta maendeleo.

Mkakati wangu na UKAWA wa kuondoa umaskini utakuwa na nguzo tano:-

Kupunguza matumizi ya serikali na mashirika yake na kuimarisha utendaji na uwajibikaji.

Kukuza pato la serikali kwa kudhibiti ukwepaji na misamaha ya kodi holela na kuhakikisha nchi inawekeza katika sekta muhimu na inapata gawio halisia kutoka wawekezaji

Kukuza uchumi kwa sera na sheria endelevu ikiwa ni pamoja na kukuza biashara na uwekezaji hasa katika sekta za madini, kilimo, viwanda, ufugaji na uvuvi na kuondoa kodi kwa wanyonge.

Kuimarisha huduma za umma kama elimu, afya, maji na makazi, na mazingira

Kuimarisha utawala bora na mfumo wa haki na sheria chini ya Katiba ya Wananchi.

Chini ya misingi hii na ili kufanikisha mkakati wa kuondoa umaskini, serikali yangu itafanya yafuatayo:-

ELIMU BORA KWA KILA MTANZANIA

Nimelisema hili huko nyuma. Nalisema tena leo. Elimu kwanza, Elimu kwanza, Elimu kwanza.

Kwa hiyo mkakati wetu wa msingi utakuwa kutoa Elimu itatayogharamiwa na serikali kwa kila Mtanzania kutoka elimu ya msingi hadi Chuo Kikuu na pia:-

Kuimarisha elimu ya teknolojia, ustadi na ufundi inayojenga uwezo wa kujiajiri na ushindani katika soko la ajira.

Ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na shule za Kata.

Kusimamia ubora wa viwango vya elimu kote nchini.

Kuimarisha taaluma na mitaala katika mashule.

Kuondoa utoro darasani, na kuboresha afya za wanafunzi.

Kuboresha maslahi na vitendea kazi kwa walimu ikiwa ni pamoja na nyumba, posho ya kufundishia, usafiri na zana za teknolojia.

Kufuta michango ya maabara ya shule za kata

AFYA

Afya na tiba ya kila Mtanzania itagharamiwa kupitia bima za gharama nafuu na mifuko ya hifadhi ya jamii

Tutaimarisha afya ya msingi pamoja na kinga kupunguza gharama za tiba.

Serikali itahakikisha kuna uwiano na upatikanaji wa watumishi wa afya katika kada mbalimbali ili kuleta tija na huduma stahiki.

Itaimarisha miundombinu ya afya pamoja na kujenga hospitali za kisasa ili kusogeza huduma za afya karibu na jamii na pia kuepukana na tiba za nje ya nchi.

Tutarejea kwa lengo la kuboresha maslahi na vitendea kazi katika sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na nyumba na usafiri.

Tutathibiti ongezeko la gharama za huduma za afya bila kuathiri uendeshaji wa watoaji huduma za afya kama vile serikali na hospitali za sekta binafsi.

ARDHI, MAJI NA KILIMO

Tutaimarisha mfumo wa umiliki wa ardhi kwa Watanzania na kudhibiti migogoro ya ardhi hasa kati ya wakulima na wafugaji.

Tutapima ardhi yote ya Tanzania na kumilikisha vijiji na wakulima kwa hati za serikali ili kuipa thamani.

Tutaleta mapinduzi ya kilimo kwa kuimarisha elimu, ufundi na teknolojia ya kisasa na kumkomboa mkulima kutoka jembe la mkono.

Tutasimamia kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa na kuunganisha sekta hizo na ya viwanda.

Kuhakikisha kuwa wananchi wanatunza na kulinda vyanzo vya maji.

Tutakuza kilimo cha umwagiliaji kwa kuwapa wakulima elimu na mikopo ya riba nafuu ya kuvuna maji na kujenga miundombinu husika.

Tutaweka mazingira rafiki yatakayomhakikishia kwa kila Mtanzania kupata maji safi na salama. Kumaliza kero za maji nchini kutamkomboa mwanamke kutokana na adha ya kuchota maji kwa kichwa

Nitafuta kodi zote za mazao na mifugo kwa wakulima na wafugaji.

Tutasimamia kilimo cha biashara kinachozingatia maslahi ya nchi na ya Watanzania.

Tutaanzisha programu maalum ya kufufua mazao asilia ya Tanzania hususan mkonge.

Tutaanzisha Benki ya Maendelo ya Ufugaji na Uvuvi.

MIUNDOMBINU

Tutaboresha bandari zilizopo na kujenga mpya kama vitega uchumi vya Taifa ili kurejesha biashara tulizopoteza kwa bandari za nchi jirani.

Tutajenga barabara nchini kwa kuzingatia ubora hasa zile za vijijini.

Tutajenga reli ya kati kwa viwango vya kisasa

Tutajenga shirika la Ndege la Taifa linalojiendesha kwa misingi ya faida.

Tutajenga miundombinu ya kisasa na kuondosha misongamano ya magari hasa katika majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha

Tutaimarisha uzalishaji na usambazaji wa umeme vijijini ili kufikia zaidi ya asili mia sabini na tano ya Watanzania

VIWANDA

Tutaimarisha sekta ya viwanda kuwa mhimili wa uchumi kwa uzalishaji wa bidhaa na ajira endelevu

Tutajenga viwanda vipya vya kusindika mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji.

Tutahakikisha kuwa ndani ya miaka mitano mali ghafi zote za Tanzania zinasindikwa kabla ya kusafirishwa nje ili kuongeza mapato na ajira ya mamilioni ya vijana.

Tutaanzisha Benki ya Ukuzaji wa Viwanda

UCHUMI

Tutabadili mfumo wa Uchumi wa nchi ili kuhakikisha kuwa mfumo wa uchumi wa Tanzania unakuwa ni wa soko-kijamii ambapo nguvu za soko zitatumikia jamii kwa serikali kuweka uwiano wa mapato unaohakikisha huduma za kijamii zinapatikana kwa ufanisi.

Tutalinda sekta binafsi na bidhaa za ndani kwa kuwapa Watanzania upendeleo wa maksudi kwa kipindi cha mpito ili waimarike na waweze kuhimili ushindani. Tutawapa wafanyabiashara wetu upendeleo katika manunuzi ya serikali na kuwajengea mazingira mazuri ya biashara na kodi endelevu.

Tutawawezesha Watanzania kupata mitaji ya biashara kwa masharti nafuu kabisa.

Tutavutia uwekezaji na wawekezaji wenye tija. Kuweka udhibiti wa wahamiaji wasioleta tija wala maslahi kwa Taifa.

Tutaimarisha sera ya ubia baina ya Serikali na Sekta binafsi kwenye maeneo muhimu ya kiuchumi na kibiashara. Pia, kuwawezesha Watanzania kuwekeza kwa njia ya ubia na wawekezaji wenye mitaji mikubwa bila kujali wanapotoka.

Tutaimarisha usimamizi kwa kubadilisha mfumo wa Vyama vya Ushirika nchini ili utokane na uendeshwe na wakulima wenyewe ikiwa na pamoja na kuwawezesha kuboresha makazi kwa mpango wa kushirikiana kujenga nyumba bora

Tutaanzisha na kuwezesha uanzishaji wa viwanda vidogovidogo vinavyotoa ajira kwa wingi kwa kuvihusisha na vyuo vya ufundi na benki maalum kwa lengo hilo.

AJIRA

Tutasimamia swala la ajira hasa kwa vijana kwa kukuza elimu ya ufundi ili waweze kujiajiri

Tutazipa kipaumbele sekta zinazozalisha ajira kwa wingi hasa za viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi na utalii na kuzipa unafuu wa kodi ili zikue kwa haraka.

Tutawapa wawekezaji wakubwa katika sekta hizi upendeleo maalum na viwango vya kodi nafuu.

NISHATI NA MADINI

Serikali itashiriki kikamilifu katika uzalishaji wa nishati

Itatengeneza mazingara mazuri ya kisera yatakayovutia na kuwezesha ushiriki wa Watanzania na ubia kati yao na wageni.

Serikali yangu itaupa uzalishaji mkubwa wa umeme wa maji kipaumbele namba moja, umeme wa makaa ya mawe kipaumbele namba mbili, umeme wa gesi asilia kipaumbele namba tatu na umeme wa urana kipaumbele namba nne.

Serikali itatoa vipaumbele muhimu kwenye usambazaji wa huduma kubwa ya umeme sehemu za uzalishaji uliyolenga masoko ya ndani, ya nchi jirani na ya nchi za kigeni.

Itapitia upya mikataba yote mikubwa ya nishati na madini ili kubaini iliyo mibovu na kuifanyia maboresho.

Serikali yangu itatumia sehemu ya hisa zake kwenye raslimali kubwa ya gesi asilia iliyopatikana hapa nchini kama rehani kwenye kujichukulia mikopo kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya mabomba ya gesi.

Serikali itatoza kodi na ada ndogo zaidi kwa wazawa wenye ubia kati yao na wageni kuliko zitakazotozwa kwa wageni wasiowekeza kwa kushirikisha wazawa.

Serikali itasitisha utoaji wa misamaha ya kodi isiyo lazima kwenye sekta ya madini, na badala yake itawekeza kwenye kuongeza thamani ya raslimali zake za madini.

Tutakuza nishati mbadala kutamkomboa mwanamke kutokana na adha ya kukata kuni

MALIASILI NA UTALII

Tutasimamia uvunaji na matumizi ya rasilimali za Taifa kwa manufaa ya kila Mtanzania wa kizazi hiki na kijacho

Tutapiga vita ujangiri na kuimarisha utunzanji wa hifadhi za taifa na mazingira

Tutachochea ujenzi wa miundombinu ya utalii nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mahoteli na kuimarisha mafunzo

Tutaongeza idadi ya watalii kufikia milion mbili ifikapo 2020.

UTAWALA BORA, ULINZI WA NCHI NA USALAMA WA RAIA

Tutasimamia Katiba mpya inayolinda haki za msingi za wananchi na kuweka bayana mipaka ya madaraka ya serikali na viongozi, Bunge na Mahakama.

Tutasimamia haki za raia na kuangalia upya sheria kandamizi ili wananchi kama Masheik wa Zanzibar hawasoti jela kwa sababu za kisiasa.

Tutaimarisha mafunzo ya vyombo ya Polisi hasa wapelelezi na waongoza mashtaka ili wapate uwezo wa kusimamia utoaji wa haki.

Tutavipa vyombo vyote vya ulinzi na usalama nyenzo na kuboresha mazingira yao ya kazi na maslahi

UZALENDO, UTENDAJI NA UWAJIBIKAJI

Tutajenga uzalendo ili kila Mtanzania aweze kutathmini mchango wake kwa taifa kila siku

Tutaimarisha nidhamu, utendaji na uwajibikaji katika Sekta ya Umma

Tutaimarisha mchango wa Wataalam wetu, wanawake na vijana katika kusimamia uchumi na kuwajengea mazingira stahiki ya kazi pamoja na mafao.

Tutapiga vita rushwa na ubadhirifu katika sekta ya Umma na binafsi

Tutadhibiti na kupunguza matumizi ya serikali ikiwa ni pamoja na kufuta safari za watumishi serikalini zisizokuwa muhimu pamoja na zile za Rais na kupiga marufuku matumizi ya mashangingi serikalini.

Tutadhibiti deni la Taifa kwa kuanza na ukaguzi wa madeni ya serikali ili kuhakiki jinsi yalivyotumika

Tutaimarisha uwazi na kuondoa usiri katika shughuli za serikali na kuweka bayana mikataba yote ya nchi ikiwa ni pamoja na ile ya mafuta, madini na gesi asilia

KUKUZA PATO LA SERIKALI

Tutadhibiti mapato kutokana na raslimali kwa kupitia upya viwango vya mirabaha kutokana na madini na gesi asilia ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapata gawio stahiki.

Serikali itaanzisha Wizara maalum itakayosimamia nishati ya gesi na mafuta.

Tutaimarisha ofisi ya Msajili wa Hazina ili kusimamia vema uwekezaji wa Serikali katika mashirika na mapato yake.

Tutahakikisha kuwa mashirika ya umma yanaendeshwa kwa misingi ya faida na uadilifu.

Tutadhibiti ukwepaji kodi za ushuru wa forodha na kupiga marufuku misamaha ya kodi holela ili kuokoa mabilioni ya fedha yanayopotea kila wiki.

Sambamba na hilo tutarahisisha utaratibu wa kulipa kodi ili kuondoa kero na mazingira ya rushwa. Kwa kudhibiti makusanyo ya kodi tutakusanya fedha za kugharimia huduma za msingi kama afya na elimu kikamilifu.

KUIMARISHA MUUNGANO

Tutaimarisha umoja, usalama na udugu wa Watanzania na Muungano kwa misingi ya haki na usawa

WANAWAKE, WATOTO NA WAZEE

Wanawake watapewa fursa na haki sawa katika elimu na uchumi ili waweze bila kuwezeshwa.

Tutahakikisha wazazi wanapata fursa ya kuwa walezi na wafanyakazi kwa kuongeza urefu wa likizo ya uzazi

Tutaimarisha elimu ya watoto hasa wasichana na kukuza fursa zao na kukomesha ndoa za watoto wadogo.

Tutaongeza uwakilishi wa akina mama katika ngazi zote serikalini na mashirika yake kufikia asili mia hamsini ifikapo 2020.

Wazee na wasiojiweza watapewa posho ya kujikimu inayokidhi mahitaji ya msingi itakayowawezesha kuishi kwa heshima na kulinda utu wao ndani ya familia na jamii zao.

SANAA, UTAMADUNI NA MICHEZO

Tutaendeleza na kuwezesha vipaji vya sanaa na michezo

Tutarudisha viwanja vya michezo vilivyovamiwa

Tutafuta kodi zote za vifaa vya michezo.

Tutadhibiti viwango na maadili ya bidhaa za nje zinazoingizwa nchini na kuzitoza kodi halisia

Tutajenga taasisi na vyuo vya kukuza michezo ili kuhakikisha kuwa ndani ya miaka mitano Tanzania inashiriki kwa ushindi katika mashindano ya kimataifa ya soka na riadha

Tutalinda Hakimiliki za sanaa nchini

Tutafuta kodi za sanaa kwa wasanii chipukizi ili kuwapa muda kwa kujijenga.

SERA YA MAMBO YA NJE YENYE TIJA KWA TAIFA

Tutakuza ushirikiano wa Kimataifa wenye tija na Ujirani mwema.

Tutatetea haki za binadamu, usawa wa nchi na kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika diplomasia ya kimataifa.

Tutakuza umoja na ushirikiano wa Umoja wa Afrika, Jumuia ya Afrika Mashariki, SADC na Umoja wa Mataifa.

Tutaimarisha Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kudai mabadiliko ya mfumo ili kuleta usawa wa nchi shiriki.

Ndugu Watanzania

Naomba nimalizie kwa kusema yafuatayo

Natambua kuwa uongozi ni dhamana. Mkinichagua nitaienzi dhamana hiyo kwa utendaji uliotukuka.

Nawaahidi Watanzania kuwa kwa uwezo, akili, uzoefu na nguvu zangu zote nitawatumikia. Nawaomba nanyi mniahidi jasho lenu na uwezo wenu wote ili kwa pamoja tuvuke. Tutajikomboa toka utawala wa CCM unaodumaza uchumi na maendeleo. Tutaanza safari ya uhakika kuondoa umaskini.

Mabadiliko pia ni kuthamini utu na kukataa hadaa ya hongo ili kuuza haki yako ya kuchagua. Msikubali rubuni za uchaguzi kwa kupewa pesa au vitu. Rushwa ya uchaguzi ndiyo sera ya CCM. Ukikubali basi umeuza pia haki na sauti yako ya kuwalalamikia walio madarakani. Imetosha. Tukatae. Tulinde utu na haki zetu. Tuchague mabadiliko.

Mabadiliko ni fikra. Ni kufikiri na kutenda tofauti. Hatuwezi kuendelea kufikiri na kutenda kama kwamba hatuna dharura ya maendeleo. Kwanza tuanze kwa kufanya mabadiliko na tujiamini kuwa sisi kama Taifa tunaweza. Tunaweza kujitegemea na kuleta maendeleo yetu wenyewe bila kutegemea wafadhili. Hii si ndoto. Nchi nyingi zimefanikiwa kuondoa umaskini katika kizazi kimoja. Tujifunze kutoka kwao.

Tuwe taifa linalotumia raslimali zake kujiendeleza na siyo kuwanufaisha wageni na kuwafanya Watanzania watwana katika nchi yao. Inabidi tuache kuwa taifa ombaomba. Tuache kuukubali na kuvaa umaskini kama joho la fahari.

Mabadiliko ya kweli hayawezi kuletwa na CCM. Tusitegemee kuwa leo wana jipya. Ndiyo maana ahadi walizotoa miaka thelathini iliyopita ndizo wametoa juzi. Tukatae hadaa. Miaka hamsini ya CCM imetosha.

Tunaamani kwamba tutashinda kwa sababu Watanzania mpo nyuma yetu. Watanzania mmeamua kuleta mabadiliko. Kura yako ndiyo itakayokuwa mkombozi wako. Hakikisha unapiga na kuilinda kura yako. Wakati wa mabadiliko ni sasa.

Mungu ibariki Tanzania. Asanteni sana

Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO