Mgombea Urais wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa, Mgombea Mweza wake, Dkt. Juma Haji Duni pamoja na viongozi wengine waliowasindikiza, wakitoka kwenye ofisi za Tume ya Uchaguzi baada ya kurudisha fomu leo Agosti 21, 2015.
Mgombea urais kupitia CCM Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damiani Lubuva, wakati alipowasili ofisi hizo. Picha na GPL
************************
Wakati mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli, akitarajiwa kuzindua kampeni zake kesho jijini Dar es Salaam, mgombea kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa amekwama kuzindua kampeni zake jana kama ilivyotangazwa awali.
Ukawa unaoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), National Convention for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-Mageuzi), Chama cha Wananchi (CUF) na National League for Democracy (NLD) umeahirisha uzinduzi kutokana na kukosa mahali patakapotosha ‘mafuriko’ ya watu watakaohudhuria.
Lowassa alitarajiwa kufungua pazia kwa kuzindua kampeni zake kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa jijini Dar es Salaam, lakini serikali imekataza uwanja huo kutumika kwa kampeni za vyama vya siasa.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene, akiongea na waandishi wa habari Jumatano wiki hii, alisema serikali imefikia hatua hiyo kwa vile kusudio la ujenzi wa uwanja huo ni shughuli za michezo pekee na si vinginevyo.
Kampeni zinazoanza kesho pia zitahusisha wagombea urais kupitia vyama vingine vya siasa vikiwamo ambavyo wagombe wake hawapewi nafasi kubwa ya kuibua ushindani kama itakavyokuwa ama kukaribia kwa CCM na Ukawa.
Pia kuanza kwa kampeni hizi kutawahusisha wagombea ubunge na udiwani watakaoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Afisa Habari wa Chadema iliyo mshirika katika Ukawa, Tumaini Makene, aliimbia Nipashe Jumamosi, jana kuwa, Lowassa anayewania Urais akiwa na mgombea mwenza Juma Duni Haji, ameahirisha kuzindua kampeni zake mpaka itakapotangazwa baadaye.
Alisema kuahirishwa kwa uzinduzi huo kunalenga la kutoa fursa kwa Ukawa kujiweka sawa hasa katika kupata uwanja wenye uwezo wa kuwajumuisha watu wengi na nafasi za kuegesha magari.
“Mgombea wetu hatazindua kampeni leo wala kesho, waache hao wengine waanze sisi tunajipanga kupata eneo zuri litakalotosha kwa idadi kubwa ya watu tunaowatarajia ikiwamo na maegesho ya magari,” alisema.
Makene alisema kutokana na uzeofu uliojionyesha wakati mgombea wao akitafuta wadhamini ama kutambulishwa mikoani, wanaamini kuwa mkutano wao utahudhuriwa na watu wengi, hivyo ni muhimu wakatafuta eneo kubwa la kutosha watu wengi na maegesho ya vyombo vya usafiri,” alisema.
Wakati ikitarajiwa kuzindua kampeni zake kesho, CCM imeshatangaza kamati ya watu 32 kwa ajili ya kutafuta ushindi, ikiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahaman Kinana.
Kamati hiyo ilitangazwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, Jumanne wiki hii ambaye alimuita Kinana kama mwanaharakati wa kivita anayefahamu medani za ushindi.
Uchaguzi wa mwaka huu ambao unatarajiwa kuwa na changamoto kubwa hasa kutokana na mgombea anayeungwa mkono na Ukawa (Lowassa) akitokea CCM, kuonyesha upinzani mkubwa dhidi ya CCM alichokuwa mwanachama wake tangu mwaka 1977.
Licha ya kuwa mwanachana, Lowassa ameshika nafasi tofauti ndani ya CCM na serikalini ikiwamo Uwaziri Mkuu aliojiuzulu mwaka 2008.
Lowassa alikuwa pia katika timu ya kampeni za mwaka 2005 ambapo Rais Jakaya Kikwete aliwania nafasi hiyo kwa mara ya kwanza na kupata ushindi wa kishindo.
Hata hivyo, Julai 29, mwaka huu, Lowassa aliamua kujiunga na Chadema ikiwa ni siku chache baada ya jina lake kukatwa katika hatua za awali za kuwachuja watia nia waliotaka kuwania Urais kupitia CCM.
Jumla ya makada 42 wa CCM walijitokeza kwenye kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais ambapo 38 walirejesha fomu na Magufuli aliibuka kuwa mshindi atakayegombea Urais katika ‘kumrithi’ Rais Kikwete.
Macho na masikio ya wapiga kura wengi kuanzia kesho yataelekezwa kwenye uzinduzi wa kampeni hizo kusikia sera za vyama hivyo vikubwa vinavyoshindana kumpata Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
CCM, Ukawa 'kutifuana' majimboni.
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu unaratajiwa kuwa na upinzani mkubwa katika ngazi za urais, ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na udiwani. Pamoja na mambo mengine, hali hiyo inatokana na kuimarika kwa upinzani nchini.
Ushindani halisi utakuwa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo vimeweka utaratibu wa kumsimamisha mgombea mmoja katika nafasi hizo ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetangaza idadi ya majimbo ya uchaguzi kuwa ni 265.
Hata hivyo sehemu ya ushindani mkubwa katika nafasi za ubunge kwa upande wa Tanzania Bara unatarajiwa kwenye majimbo yafuatayo:
UBUNGO
Jimbo hili lilikuwa likishikiliwa na Chadema kwa kipindi cha miaka mitano tangu uchaguzi wa mwaka 2010. Awali, Mbunge wake alikuwa Charles Keenja wa CCM. Tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, mbali na John Mnyika wa Chadema Ubungo imewahi kuwakilishwa na Masumbuko Lamwai (NCCR-Mageuzi).
Wagombea katika uchaguzi wa mwaka huu ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi (CCM) na Mhariri wa Mwanahalisi, Saed Kubenea (Chadema). Wote wanagombea kwa mara ya kwanza.
ILALA
Jimbo hili ni kitovu cha jiji la Dar es Salaam kutokana na ofisi nyingi za serikali ikiwamo Ikulu kuwa katika jimbo hili. Kwa sasa linashikiliwa na Mussa Azzan Zungu (CCM) ambaye anawania kwa mara nyingine baada ya kuongoza kwa vipindi viwili tangu mwaka 2005.
Zungu atashindana kwa karibu na mgombea aliyesimamishwa kupitia Ukawa, Muslim Haiderally Hassanali (Chadema) ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema. Hassanali anatajwa kuwa na wafuasi wengi maeneo mengi ya jimbo hilo.
KINONDONI
Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi 1992, jimbo hili limekuwa ngome ya CCM. Kwa sasa linawakilishwa na Idd Azzan. Mpaka sasa Ukawa inaendelea kutafakari mtu wa kumsimamisha kupambana na Azzan.
KAWE
Jimbo hili limeongozwa na Halima Mdee (Chadema) tangu 2010 baada ya kushikiliwa na CCM tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza. Uchaguzi huu CCM imemsimamisha Kippi Warioba.
UKONGA
Unaweza kuiita ngome ya CCM kutokana na wagombea wake kushinda kwa kipindi kirefu. Ni jimbo lililokuwa linaongozwa na marehemu Eugene Mwaiposa.
Ugumu wa jimbo hili unafuatia pale aliyekuwa Meya wa Ilala, Jerry Slaa kuwania nafasi ya kuliongoza kupitia CCM, huku Ukawa wakimsimamisha Mwita Waitara (Chadema).
KIBAMBA
Ni jimbo jipya ‘lililomegwa’ kutoka Ubungo ambapo kila chama kikiwania kuliongoza.
Ukawa imemsimamisha John Mnyika (Chadema) wakati CCM imemsimamisha Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenela Mkangala. Chama cha ACT-Wazalendo, kimemsimamisha Mwandishi wa habari, Dickson Amos Ng’illy.
SEGEREA
Lilikuwa likiwakilishwa na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga (CCM) ambaye kwa sasa amehamia Chadema baada ya ‘kukatwa’ katika kura za maoni.
Hivyo ni jimbo linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kati ya Bonna Kaluwa (CCM) na Julius Mtatiro wa CUF anayeungwa mkono na Ukawa.
IRINGA MJINI
Ushindani mwingine upo katika jimbo hili, baina ya Fredrick Mwakalebela (CCM) na Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Wagombea wote wana mvuto kwa wananchi wa Iringa Mjini hasa vijana. Mchuano katika jimbo hilo unatarajiwa kuwa mkali hasa ikizingatiwa kwamba Mwakalebela alishinda kura za maoni mwaka 2010 lakini vikao vya juu vya CCM ‘vikamkata’.
Mbunge wa sasa, Mchungaji Msigwa ameliwakilisha jimbo hilo kwa miaka mitano.
ARUSHA MJINI
Ushindani mkubwa unatarajiwa kuwapo jimboni humo kutokana na wagombea wawili wenye ushindani mkubwa, Mbunge anayemaliza muda wake Godbless Lema (Chadema) na Phillemon Mollel (CCM).
BUNDA MJINI
Mpambano katika jimbo hilo ulianza ndani ya CCM baada aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Vijana, Esther Bulaya kulitaka na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira ambaye anamaliza muda wake.
Hivi sasa Bulaya, anagombea jimbo hilo kwa kusimamishwa na Ukawa kupitia Chadema baada ya kujiunga na chama hicho hivi karibuni.
MOSHI MJINI
Ni ngome ya Chadema iliyokuwa inaongozwa na Philemon Ndesamburo maarufu kama `Ndesa Pesa’, lakini kwa sasa amestaafu na kumwachia Meya wa Manispaa hiyo, Jaffar Michael.
CCM kimeamua kulikomboa jimbo hilo kwa kumsimamisha mfanyabiashara maarufu, Davis Mosha.
BARIADI MASHARIKI
Aliyekuwa anashikilia jimbo hilo, Andrew Chenge (CCM), aliyepachikwa majina lukuki ya utani yakiwamo ‘Mzee wa rada’ ‘Mzee wa vijisenti’ ‘Nyoka wa makengeza’ atapambana na Godwin Simba ( Chadema).
NYAMAGANA
Ni jimbo lenye ushindani mkubwa kutokana na historia yake ya kutoongozwa na mbunge kwa vipindi viwili tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
KilaMbunge anayeshinda jimbo hilo huongoza kwa kipindi cha miaka mitano na kisha kuondoka. Hivi sasa linaongozwa na Ezekiel Wenje (Chadema). Uchaguzi huu atakuwa na wakati mgumu wa kupamba na mgombea wa CCM, Stanslaus Mabula
ILEMELA
Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na Highness Kiwia (Chadema) ni mojawapo ya ngome ya Chadema kwa muda mrefu, CCM kimejipanga kulichukua jimbo hili kwa kumsimamisha Angelina Lubala.
SIMANJIRO
Ni mchuano kati ya mgombea wa CCM, Christopher Ole Sendeka na James Millya (Chadema).
Wagombea wote hawa wanapendwa na wananchi wa Simanjiro pia wana uwiano sawa wa umaarufu, kwa kuwa wote ni wazoefu katika siasa.
CHANZO: NIPASHE
0 maoni:
Post a Comment