Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

YOUNG SCIENTISTS TANZANIA (YST) YAENDESHA MAONYESHO YA 5 YA SAYANSI DIAMOND JUBILEE DAR

Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza wa taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST), Dk. Gosbert Kamugisha, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo hii wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya siku tatu ya miradi na ubunifu wa kisayansi uliofanywa na wanafunzi kutoka shule 120 nchini. Maonyesho hayo yatafikia kilele Ijumaa Agosti 7, 2015. (Picha zote na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com).

Mwanzilishi Mwenza wa YST, Joseph Clowry, akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo hii. 
Makamu wa Rais wa kampuni ya kuchakata mafuta na gesi ya BG Tanzania, John Ulanga, akizungumzia udhamini wao katika maonyesho hayo ya YST. Kampuni hiyo imetoa kiasi cha Dola 200,000 kudhamini maonyesho ya mwaka huu. 
Naibu Balozi wa Ireland nchini, Brian Noran, akizungumzia maendeleo ya tafiti za kisayansi kwa taifa lolote duniani. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza wa YST, Dk. Gosbert Kamugisha.
Mkutano ukiwaunaendelea. 
Wanahabari wakiwa kazini. 
Wanahabari wakifuatilia kwa makini. 
Mwalimu Geofrey Ndunguru (kulia) na mwanafunzi Yussuph Mwenda kutoka Shule ya Sekonari ya Wavulana Songea nao wanashiriki maonyesho hayo kuzungumzia Uchambuzi wa Mtazamo wa Wanafunzi Wasioona kuhusiana na Sayansi. 
Mwanafunzi Gladness Mpelemba (kulia) wa kidato cha tatu kutoka Shule ya Sekondari Sumaye mjini Morogoro akielezea kuhusu utafiti wao wa 'Kutumia Njia za Asili za Kupanga Uzazi Kupunguza Madhara kwa Wanawake'. Kushoto ni mwenzake Glory Crispine. 
Wanafunzi wakiendelea kuonyesha tafiti zao. 
Mojawapo ya utafiti uliofanywa na wanafunzi Saada Abeid na Zaina Maliki wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara. 
Majaji wakiwa kazini leo hii ili kuwapata washindi watakaotunukiwa zawadi mbalimbali hapo kesho ambapo Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, ndiye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Na Daniel Mbega
MAONYESHO ya Tano ya Sayansi kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini yamfunguliwa rasmi jijini Dar es Salaam leo yakiwa yanaendeshwa na kuratibiwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST).Maonyesho hayo ambayo yanafanyika kwenye Ukumbi wa iamond Jubilee yanashirikisha jumla ya wanafunzi 240na walimu 120 kutoka shule 120 nchini yanatarajiwa kufikia kilele keshokutwa Ijumaa ingawa kesho Alhamisi zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi zikiwemo fedha taslimu, medali, vikombe, vifaa vya maabara pamoja na maktaba.
Dk. Gosbert Kamugisha, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza wa YST, amesema mgeni rasmi atakayetoa zawadi kwa washindi hapo kesho atakuwa Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
“Maonyesho haya ni kwa ajili ya kuonyesha ubunifu na utafiti wa kisayansi uliofanywa na wanafunzi wa sekondari na katika kipindi cha siku tatu kuanzia leo wanafunzi hao wataonyesha miradi mbalimbali katika maeneo tofauti ya kisayansi kama kemikali, fizikia na sayansi ya hisabati, sayansi ya kibaolojia na kiikolojia, sayansi ya kijamii na kitabia, na teknolojia,” alisema Dk. Kamugisha.
Aliongeza kwamba, kama njia ya kutambua kazi iliyofanywa na wanafunzi hao, ndiyo maana wameandaa zawadi mbalimbali kuwamotisha ambapo mbali ya zawadi zilizotajwa, pia wanafunzi sita wanaweza kupata udhamini (scholarship) kwa ajili ya masomo ya chuo kikuu kwa fani mbalimbali za sayansi na teknolojia, udhamini ambao hutolewa na taasisi binafsi ya Karimjee Jivanjee Foundation ya jijini Dar es Salaam.
“Maonyesho ya mwaka 2015 ya YST yanalenga kuonyesha vipaji na ubunifu wa wanafunzi wa sekondari, lakini pia ushuhuda wa umahiri wa mbinu za ufundishaji kwa walimu ambao ndio wanaowaongoza wanafunzi hao yakiwa ni matunda ya mafunzo yanayotolewa na YST kwa walimu wa sayansi katika kipindi cha miaka minne iliyopita,” aliongeza Dk. Kamugisha.
Amewataja wadhamini wakubwa wa maonyesho ya mwaka huu kuwa ni kampuni ya BG Tanzania inayojihusisha na masuala ya utafiti wa mafuta na gesi asilia pamojana Shirika la Kimataifa la Misaada la Ireland (Irish Aid).
Akizungumzia mafanikio ya maonyesho hayo, Dk. Kamugisha alisema mwitikio umekuwa mkubwa zaidi tofauti na walipoanza maonyesho hayo mwaka 2011.
“Wakati tulipoanza mwaka 2011 walishiriki wanafunzi nane tu, mwaka 2012 wakawa 300 kwani zilikuwepo shule 100, mwaka 2013 walishiriki wanafunzi 200, mwaka 2014 pia walikuwepo wanafunzi 200 lakini mwaka huu wamekuwa 240 kwani hata shule zimeongezeka kutoka 100 hadi 120.
“Tulipokea maombi ya shule 400 nchi nzima, lakini tukaamua kuzichagua hizi 120. Tulizitembelea shule zote 400 mara tatu kwa mwaka, ndipo hatimaye tukaziteua hizi zinazoshiriki ingawa tunaamini kwamba shule nyingi sasa zimehamasika na watoto wanapenda sayansi,” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mwanzilishi Mwenza wa YST Joseph Clowry, alisema kwamba kuna dalili za mafanikio tangu walipopata wazo la kuanzisha taasisi hiyo mwaka 2009, kwani mwitikio umeonekana kuwa mkubwa kadiri miaka inavyokwenda.
Alisema, ili taifa lolote liendelee, ni vyema kuwekeza zaidi katika tafiti za kisayansi kwa kuanzia kwenye ngazi za chini kabisa kama wao wananvyofanya.
“Ireland ilikuwa nyuma kimaendeleo kama zilivyokuwa nchi nyingi ulimwenguni, lakini walipoamua kuwekeza kwenye sayansi hali imebailika hivi sasa ambapo wapo wanasayansi mahiri kabisa na vijana nao wanapenda kujifunza masomo ya sayansi,” alisema Clowry.
Kwa upande wake, Makamu Rais wa BG Tanzania anayeshughulikia Sera na Masuala ya Uhusiano, John Ulanga, alisema wameamua kujitolea kudhamini YST kwa sababu wanatambua kwamba Tanzania inahitaji kuwa na wanasayansi wengi hasa tunapozungumzia suala la mafuta na gesi ambayo yakitafitiwa yakapatikana na kuchakatwa yanaweza kuinua uchumi wa taifa kwa kiwango kikubwa.
“Tunahitaji wanasayansi wa kutosha katika sekta hii adhimu ya mafuta na gesi, tukiwa nao wazalendo itakuwa ni bora zaidi, hivyo ni lazima tuwadhamini watu kama YST ambao wanajenga msingi imara katika kuwapata wataalamu wa kesho,” alisema Ulanga.
Ulanga alisema kwamba, kwa mwaka huu kampuni yake imetoa Dola 200,000 (takriban Shs. 450 milioni) kwa ajili ya udhamini wa maonyesho hayo na akaahidi kwamba wataendelea kudhamini kwa kadiri ya mahitaji na hali itakavyoruhusu.
Naye Brian Noran, Naibu Balozi wa Ireland nchini, amesema ni jambo la busara kwa serikali na jamii kuwekeza katika utafiti wa kisayansi kama kweli taifa linataka maendeleo, lakini akaahidi kwamba serikali yake itaendelea kusaidia kwani inatambua umuhimu wa kuwa na wanasayansi wabunifu.
Aliwapongeza YST kwa hatua waliyoifikia mwaka huu na kuwahamasisha waongeze bidii zaidi ili kujenga taifa la wanasayansi kwa kuanzia ngazi ya chini.
“Sayansi ndiyo inayoweza kuleta mabadiliko na maendeleo, hivyo ni muhimu kuendelea kuwazalisha wanasayansi ambao watakuja kuwa wabunifu wazuri hasa katika karne hii ya sayansi na teknolojia,” alisema Noran.
(IMEANDALIWA NA www.brotherdanny.com. Simu 0656-331974)


Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO