Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Polisi wavamia msafara wa Lowassa

 

JESHI la Polisi Dar es Salaam leo limevamia na kuuzuia msafara wa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa kuingia sokoni Kariakoo.
Polisi hao walikuwa kwenye magari aina ya Land Rover huku wakiwa na silaha za moto tayari kukabiliana na hali yoyote, walimzuia Lowassa ambaye alikusudia kwenda Kariakoo shimoni.
Lowassa alifika Mtaa wa Swahili saa 6:09 mchana ikiwa ni mtaa mmoja kabla ya kuingia sokoni shimoni ambapo alikusudia kusalimia wafanyabiashara hao kama alivyofanya Tandale na Tandika.
Kabla ya kufika Mtaa wa Swahili, msafara wa Lowassa ulianzia katika Soko la Tandale na baadaye alikwenda Tandika kusalimia wafanyabiashara na wakazi wa maeneo hayo.
Polisi walimvamia na kuamuru msafara wake kuishia Mtaa wa Swahili kwa kile walichoeleza kutokuwepo kwa taarifa ya ujio wake pamoja na kuepusha msongamano ambao tayari ulianza kutokea.
Msafara wa Lowassa ulisindikizwa na wafanyabiashara wa Kariakoo waliojitokeza kumpoke huku wakiimba nyimbo za kumsifu, ambao pia walinyimwa fursa ya kumuona.
Waliimba “si si si… si mnaona, mziki wa Lowassa kuutuliza hamuwezi,” maneno waliyoyarudia mara kwa mara.
Polisi wamesema, Lowassa ambaye alikuwa ameongozana na kundi kubwa la vijana hakutoa taarifa mapema ili waimarishe ulinzi. Hata hivyo kulikuwa na majadiliano kati ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Lucas Mkondya na maofisa wa Chadema.
Makubaliano yalihitimishwa kwa Lowassa na maofisa wake kukubali kutofika sokoni mahala alipotarajia kukutana na kuzungumza na wafanyabiashara hao.
Alipokuwa Tandale
Lowassa alitoka nyumbani nyumbani kwake Masaki saa 2:35 asubui na kuelekea katika Soko la Tandale.
Kabla ya kufika sokoni Tandale, wananchi waliomwona kwenye gari walianza kumfuata, hata hivyo alikwenda mpaka sokoni ambapo alifika saa 3:20 ambapo alizungumza na wafanyabiashara wa hapo.
Said Omary ambaye ni mfanyabiashara wa nafaka alimwomba Lowassa kuwa, akifanikiwa kutwaa nchi awaboreshee miundombinu ya barabara ili kurahisisha kuingiza bidhaa zao.
“Soko halina ubora wowote maana CCM wanachangisha ushuru lakini hawalihudumii. Ni bora tuachiwe wenyewe tuliendeshe maana tunalipa ushuru wa bure.”
Omary alisema hayo baada ya kuulizwa na Lowassa kwamba, endapo ataingia madarakan, angependa amfanyie nini?
Kabla ya kuondoka Lowassa alinunua maharage kwa Sh. 30,000 kutoka kwa mfanyabiashara huyo. Baadaye alikwenda kwa mfanyabiashara wa miwa aliyejitambulisha kwa jina la Gerard.
Gerard amemwambia Lowassa “tunaomba ukiingia madarakani utukumbuke sisi vijana wako kwa kutupatia ajira ya kutosha maana hii biashara haina faida.” Alipofika kwa muuza maziwa Lowassa alinunua kikombe kimoja na kunywa fundo moja.
Alimaliza sokoni hapo saa 3:50 gari lake likisindikizwa na mamia ya watu pia akisindikizwa na vijana wa bodaboda.
Kwenda Tandika
Msafara uliingia katika Barabara ya Morogoro saa 4:01 asubuhi na kufuatiwa na pikipiki huku zikiwa zimebeba watu ambao walikuwa wakiimba nyimbo za kumsifu.
Msafara uliingia Barabara ya Mandela na kukuta wananchi wakiwa wamejipanga kumsalimia kwa kumpungia mikono huku na yeye akifanya hivyo.
Alifika Soko la Tandika saa 4:33 asubuhi ambapo shughuli zilisimama kwa muda huku mamia ya watu waliojaa sokoni hapo wakitaka kumuona.
Lowassa bila ya kujali hali ya soko kuwa chafu, aliingia ndani na kuangalia bidhaa mbalimbali na bei zake.
Lowassa akiwa ndani ya soko hilo alipata fursa ya kuzungumza na muuza maji ya kufunga maarufu kama ‘kandoro’ ambaye hakutaja jina lake.
Alimuuliza kijana huyo kiasi gani anapata kutokana na biashara hiyo? alimjibu “hakuna faida yoyote, tunaganga njaa tu ilimradi mkono uende kinywani.”
Aidha, wananchi wengine waliokuwa wamefurika sokoni hapo walisikika wakisema “Baba tunakuomba uingiapo madarakani, utujengee soko letu maana halina hadhi, ni chafu na linanuka. CCM wameshindwa kazi, wanakula pesa zetu tu.”
Hata hivyo, wananchi wengi wa sokoni hapo walipoulizwa ni kwanini wameacha shughuli zao na kumsikiliza Lowassa, wamejibu “huyo ndio rais tunayemuhitaji ambaye akiwa madarakani atajua aanzie wapi kutatua shida zetu. Rais anatakiwa kuwa mtu wa watu kama huyu, hapa kashapita.”

Mwanahalisi online

Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO