Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

MATUKIO KATIKA ULIMWENGU WA KISIASA WA JUMA DUNI HAJI

 

Mwanasiasa machachari wa upinzani kutoka Zanzibar, Juma Duni Haji aliteuliwa kuwa mgombea mwenza wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Lowassa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA); Uteuzi uliofanyika mara tu baada ya mwanasiasa huyo kukihama Chama cha Wananchi (CUF) ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA - vyama vingine vilivyomo kwenye Ukawa ni NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD)).
Viongozi wa UKAWAwalipokutana kupitia majina ya wanasiasa wenye sifa ya kuwa wagombea wenza, walikubaliana kumteua mwanasiasa huyo ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inayofanya kazi chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Mwanasiasa huyo amekuwa na historia ndefu na mara tatu amewahi kuteuliwa na CUF kuwa mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano, akiwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba. Amekuwa mgombea mwenza wa Profesa Lipumba katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, mwaka 2005 na mwaka 2010. Duni amewahi kunukuliwa akieleza kuwa yeye ni mtumishi wa watu na kila mara alikotumwa alikwenda. Hivyo, hata leo akiteuliwa kwenda kuongoza kijiji au kitongoji ilimradi Watanzania wametaka hivyo, ataitikia wito.
Juma Duni alianza safari ya kisiasa kwa “kulazimishwa” mwaka 1984, baada ya Serikali ya Muungano kutoa Waraka wa Serikali (White Paper) na kutakiwa wananchi watoe maoni yao juu ya hali na matatizo ya Muungano.
Wakati huo, makatibu wakuu wa Serikali ya Zanzibar akiwamo yeye walitoa maoni dhidi ya muungano. Uhuru huo wa kitaalamu uligeuzwa kuwa mchungu kwani walisingiziwa kwamba wamefanya kinyume na walivyoagizwa na baadhi yao wakapewa onyo kali na wengine wakateremshwa vyeo.
Juma Duni aliteremshwa cheo kutoka wadhifa wa Katibu Mkuu hadi mwalimu wa kawaida kwa Tangazo la Rais. Huko nako pia hakubaki salama kwani alituhumiwa kuwajaza wanafunzi kasumba, hivyo alirudishwa Wizara ya Elimu kama Ofisa Mipango ambako pia alituhumiwa kujihusisha na siasa za upinzani. Duni alipoona amechoka kuhamishwahamishwa na kushutumiwa, aliomba likizo ya bila malipo kwenda kusoma, ombi ambalo pia lilikataliwa.
Hapo ndipo alipoamua mwenyewe kuondoka na kwenda kujisomesha kwa fedha zake Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza na kuhitimu stashahada ya Juu ya Biashara kati ya mwaka 1993-1994. Alipofika Uingereza, akatumiwa barua ya kuachishwa kazi na kupoteza haki zake zote za miaka 18 ya utumishi serikalini.
Mwaka 1994 akiwa bado nchini Uingereza, akaunganisha masomo na kusomea Shahada ya Uzamili akibobea kwenye usimamizi wa Rasilimali Watu na kabla hajahitimu akarejea nchini ili kusaidia upinzani kujipanga kiuchaguzi. Moja kwa moja akajiunga na vuguvugu la uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi akajiunga na CUF na akateuliwa kuwa mgombea mwenza wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho, Profesa Lipumba wakati bado hajakamilisha shahada yake ya pili ya uongozi na utawala.
Tangu ajiunge CUF, Juma Duni ameshika nyadhifa mbalimbali kwa nyakati tofauti. Amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha, pia amekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi. Amekuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF nafasi aliyoishika hadi wiki hii alipojiuzulu kimkakati na kujiunga na Chadema.
Juma Duni si mgeni katika masuala ya kibunge au ya kiuwakilishi. Mwaka 1997 aligombea nafasi ya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Jimbo la Mkunazini, akashinda na kuwa mwakilishi kuanzia mwaka 1997-2000.
Mwaka 2009 aliteuliwa na Rais Amani Abeid Karume kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa mara ya pili, akakaa katika wadhifa huo hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ulipofanyika na kuundwa kwa SUK.
Katika SUK, Juma Duni aliteuliwa na Rais wa Zanzibar kuwa mwakilishi na kisha akateuliwa kuwa Waziri wa Afya wa Zanzibar, wadhifa ambao ameushikilia hadi Rais Dk Mohamed Shein alipovunja Baraza la Wawakilishi.
Sifa kubwa ya Duni ni ucheshi na kuchangamana na watu, ni rafiki wa wakubwa na wadogo kiasi cha kwamba kwa wengi wanaomfahamu humwita ‘Babu Duni.

Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO