Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Msigwa awalipua vigogo CCM, serikali • Waziri Nchimbi ajitosa kumsafisha Kinana

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulahman Kinana

**********************************************

MSEMAJI Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, amewalipua vigogo wa serikali na makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akidai kuwa wana maslahi yanayotilia shaka katika sekta ya uwindaji wa kitalii na kusababisha kuwapo kwa ujangili.

Kama alivyofanya mwaka jana na hata kwenye mikutano yake mingi ya hadhara, Msigwa alimtaja tena Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na mkewe, kwamba anamiliki kampuni ya Sharaf Shipping Co, Ltd ambayo meli yake inadaiwa kunaswa na kontena la shehena ya meno ya tembo.

Hata hivyo, hotuba ya Msigwa ilikatizwa kwa mwongozo wa mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM), akihoji kitendo cha mbunge mwenzake kudai ofisi ya Spika ni kaburi la kuzika haki. Hata hivyo Spika Anna Makinda aliwataka wawe wavumilivu kwani yako maneno mengine mengi kama hayo.

Hata hivyo Msigwa aliendelea kusoma maoni ya kambi ya upinzani kuhusu makadirio ya matumizi na mapato ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.

Huku wabunge wa CCM wakimwangalia kwa makini na wengine kutikisa vichwa kumpinga, Msigwa alimtaja mfanyabiashara na kada wa CCM, Mohsin Abdallah.

Msigwa ambaye alikuwa akikariri taarifa ya kamati ya waziri wa zamani wa wizara hiyo, Antony Diallo, aliwataja  makada waandamizi wengine wa CCM wenye maslahi ya aina hii kuwa ni kampuni ya Coastal Wilderness (Tz) Ltd., ambayo wakurugenzi wake wanatajwa kuwa ni Napono Edward Moringe Sokoine na Namelok Edward Moringe Sokoine; Enzagi Safaris (Tz) Ltd., yenye wakurugenzi Makongoro Nyerere, Muhamed Seif Khatib na Saidi Kawawa; na Hunting Safaris yenye wakurugenzi, Chande Kawawa na Hassan Kawawa.

Kampuni zingine ni M.S.K. Tours & Hunting Safari Co. ya Muhamed Seif Khatib.

Msigwa alisema mengi ya makampuni haya yalipewa vitalu vya uwindaji wakati hayana uzoefu wala mtaji wa kuendesha biashara ya uwindaji wa kitalii katika vitalu hivyo.

Alisema matokeo yake ni kwamba makampuni hayo yalishindwa kusimamia uhifadhi wa wanyamapori katika vitalu vyao na kusababisha tatizo la ujangili kushamiri katika vitalu hivyo.

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa kauli mbele ya Bunge lako tukufu ni kwa nini serikali hii ya CCM imekuwa ikitoa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa makada waandamizi wa CCM ambao wanajulikana kuwa hawana weledi wala uwezo wa kibiashara wa kuendesha biashara ya uwindaji wa kitalii na hivyo kusababisha tatizo la ujangili kuwa kubwa zaidi na kuleta hasara kwa taifa letu!” alisema.

Akiwa amerejea bungeni baada ya adhabu ya siku tano, Msingwa alisema serikali imeanza kufedheheshwa katika mikutano ya kimataifa ya uhifadhi kwa sababu CCM imeamua kukumbatia makada wake waandamizi aliodai wanajihusisha na ujangili.

Alitolea mfano Mkutano wa 16 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya Wanyama Walio Hatarini Kutoweka (CITES) uliofanyika Bangkok, nchini Thailand mwezi uliopita.

Msigwa alisema kuwa Mohsin Abdallah alitajwa na Shirika la Upelelezi wa Masuala ya Mazingira (Environmental Investigations Agency, EIA) kuwa ni mmoja wa majangili wakubwa wanaojihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo lakini serikali imeshindwa kumchukulia hatua za kisheria kwa sababu ya ushawishi wake mkubwa katika siasa za ndani ya chama tawala na serikali.

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni fedheha ya aina gani kimataifa itakayoiamsha serikali hii ya CCM katika usingizi wake wa pono ili iweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya makada wa CCM wa aina hii?”alihoji Msigwa.

Kuhusu Kinana, Msigwa alisema kampuni yake ya wakala wa meli ya Sharaf Shipping Co. Ltd, si tu kwamba imehusishwa na usafirishaji haramu wa pembe za ndovu kutoka Tanzania bali pia inadaiwa kutoa ajira haramu kwa wageni.

Alisema wakati shehena ya meno hayo ya tembo inakamatwa nchini Vietnam, nyaraka zilizoambatana na shehena hiyo zilionyesha kwamba kibali cha kusafirisha shehena hiyo kilisainiwa na raia wa India anayeitwa Samir Hemani mnamo Novemba 13, 2008.

Alisema wakati raia huyo wa kigeni anasaini kibali cha kusafirisha shehena ya meno ya tembo kwa niaba ya wateja wa Kinana na mkewe, kibali chake cha kuishi Tanzania kilikuwa kimeisha tangu Mei 7, 2008.

Msigwa alimshambulia Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, na kumtaka ajiuzulu kwa madai kuwa ameshindwa kulinda rasilimali za nchi na kusababisha wanyamapori kutoweka kwa kuuawa na majangili.

Alimshambulia pia Spika Anna Makinda kuwa Bunge lake limekuwa kaburi la kuzikia  utekelezaji wa maazimio mengi kuhusu kashfa mbalimbali zilizogubika utendaji wa Ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii na utekelezaji wa majukumu yake kisheria. 

Nchimbi ajibu mapigo

Hoja za Msigwa zilimlazimu Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuomba nafasi ya kwanza kuchangia hotuba ya Waziri Kagaeshiki na hivyo kutumia muda huo kurusha makombora mazito kwa CHADEMA kwa kuwaita kuwa ni genge la uongo ndani ya Bunge.

“Kabla sijaendelea, nitumie nafasi hii kuipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri na katika hotuba hii ya Waziri Kagasheki imejidhihirisha wazi kwa kipindi hiki kifupi kuwa wamekamata watuhumiwa wa ujangili 354 na zipo mahakamani kesi 283, bunduki 435 zimekamatwa.

“Ukiona mtu anasimama na kusema serikali haijafanya kazi, basi upeo wake wa kufikiri ni mdogo,” alisema Nchimbi.

Waziri huyo alijielekeza kwenye baadhi ya hoja zilizolengwa dhidi ya Kinana ambapo alisema Msigwa ameamua kusema uongo ili kulipotosha Bunge na Watanzania kwa ujumla kwamba katibu huyo alikamatwa na meno ya tembo nje.

“Nimejaribu kufuatilia kwa umakini kujua kwamba kifungu hicho alikimaanisha, alikielewa, alikitafakari au aliandikiwa tu kisha akaenda kukisoma.

“Baada ya kutafakari kwa kina nimegundua kwamba hakuwa na nia mbaya bali alikuwa ameandikiwa tu na kuisoma,” alisema.

Nchimbi alitumia muda huo kufafanua majumu ya kati ya Shipping Agency na Clearing and Fowarding.

“Kampuni ya shipping agency duniani kote ni kumwakilisha mwenye meli, agenti hawezi kuwa mwenye meli ila anamwakilisha mwenye meli, kuna shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye meli.

“Kuna mambo ya kuhudumia watumishi kwenye meli, kuwapelekea chakula watumishi, kufanya usafi, kupelekea mahitaji muhimu lakini wapo watu wanaofanya ‘clearing and fowarding’ na  Kiswahili chake ni kupeleka na kutoa.

“Hawa ndio wanaopeleka mizigo bandarini na kule ndiko kuna utaratibu wa upekuzi kwa hiyo huko hahusiki mtu wa shipping agency, sina mashaka hata kidogo kuwa Mchungaji Msigwa analijua hili ila amelifumbia macho kwa makusudi na kwa maslahi yasiyokubalika kwa taifa,” alisema.

Wakati akiendelea kuchangia, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), aliomba mwongozo wa Spika kutaka kutoa ufafanuzi, lakini Spika alikataa.

“Mliposema ninyi, wenzenu walinyamaza, mtulie hivyo hivyo, naomba uendelee hakuna cha taarifa, endelea Mheshimiwa Nchimbi na nyie mnanyamaza kama walivyonyamaza wenzenu,” alisema Makinda.

Nchimbi aliendelea kusema kumekuwepo uvumi ambao unafanywa kwa  Kinana kwamba anamiliki meli iliyotumika  kusafirisha pembe za ndovu.

Alisema baada ya uchunguzi wa kutosha kuhusu kesi hii, ikabainika na watuhumiwa wakashtakiwa kwa uhujumu uchumi kwa kufunguliwa kesi namba 3 na 4 ya mwaka 2006.

Nchimbi aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Eradius Tesha, Shaban Abura, Eric, Issa Abubakar na Omar Hussein.

“Mh Spika, hawa ndiyo waliopelekwa mahakamani na uchunguzi ulijidhihirisha kuwa hawa ndiyo watuhumiwa wa kesi hiyo na kambi ya upinzani inalijua hili,” alisema.

Alisema wakati kesi iko Kisutu, ulihitajika ushahidi kutoka nchi ya Vietnam na nchi hiyo imesema haina ushirikiano na Tanzania katika mambo ya jinai.

“Hivi sasa tunazungumza na ubalozi wa China watupe kibali cha kufanya upelelezi ili kesi hiyo iweze kuendelea na kwa msingi huo Mahakama ya Kisutu inataka ushahidi huo ili kesi iendelee na hili wapinzani wanalijua,” alisema.

Chanzo: Tanzania Daima, 1 May 2013

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO