Baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaomnadi mgombea wa chama hicho katika uchaguzi wa udiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 20, 2012 katika Kata ya Daraja Mbili Jijini Arusha wametuhumiwa kuendesha kampeni za ukabila dhidi ya vyama vingine.
Inadaiwa kwamba katika mkutano wa CCM eneo la kwa Alli Nyanya Kata ya Daraja Mbili jana, yalitolewa maneno ya ubaguzi yenye kuhisiwa kuchochea ubaguzi wa kikabila kwa lengo la kutafuta kura za makabila fulani. Mtoa taarifa ambaye alihudhuria mkutano huo anasema CCM waliwaambia watu wachache waliojitokeza katika mkutano huo kuwa wasiichague CHADEMA kwasababu ni chama cha Wachaga na kuwaomba Warangi, Wasambaa na Waarusha wasiipigie kura Chadema bali CCM.
Taarifa inaeleza zaidi kuwa na baada ya kumaliza kuzungumza hivyo, watu walikuwa wakihoji hivi mgombea wa CCM Bw Mushi ni kabila gani? Baada ya kufahamu mgombea wa CCM ni mchaga wananchi hao wachache wakahoji kama Chadema ni ya wachaga kwanini yuko CCM??
Viongozi wa nchi wanapaswa kuwa makini sana na tabia kama hizi za kuchochea wananchi ili wafarakane kwa makabila ama dini zao. Blog hii inaamini amani iliyopo Tanzania (japo kumeonekana dalili za kuanza kutoweka) lazima ilindwe na kuenziwa kwa kila hali. Viongozi wasiruhusu matamshi kama haya ya kuwagawa watanzania yakaendelea kuwa sehemu ya utamaduni mpya kwasababu hatma yake inaweza isiwe nzuri.
Pichani ni tafrani iliyozuka katika mkutano wa CCM Kata ya daraja Mbili uliofanyika mwishoni mwa wiki baada ya kijana ambaye hakufahamika jina lake mara moja kushushiwa kipigo alipotaka kuharibu shughuli nzima ya kampeni. Picha na Jamii Blog
0 maoni:
Post a Comment