Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Makala ya Efracia Massawe: TanzaniteOne yachangia bil. 1.9/- Simanjiro

KITENDO cha serikali kushindwa kuwajibika isapavyo katika nyanja mbalimbali, kimekuwa kishawishi kikubwa kwa sekta binafsi kuingilia kati kupunguza adha mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Serikali ni yenye wajibu mkubwa kwa jamii katika kupanua wigo kwa wananchi kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kila sekta na nchi kwa ujumla.

Hiyo ni kauli iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya TanzaniteOne, Wessel Marias, baada ya uzinduzi wa mashine na kisima cha kusafisha maji safi katika Kata ya Naisinyai, Wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Marias anasema wananchi wanahitaji kuwekezewa miradi mbalimbali ambayo kwa namna moja ama nyingine, wanaweza kuitumia kwa ajili ya kuwaingizia kipato.

Mkurugenzi huyo anabainisha kuwa kampuni hiyo imechukua jukumu la kujenga kisima na mashine ya kusafisha maji na kukikabidhi kwa serikali ya kijiji kwa ajili ya matumizi ya kijiji.

Katika hilo, anaongeza kwamba kisima na mashine hiyo kilichogharimu zaidi ya sh milioni 60, kitakuwa msaada katika wilaya hiyo hususan katika kusafisha maji yanayotoka katika mabomba kwani kijiografia, eneo hilo ni lenye maji chumvi ambayo nayo si salama kwa matumizi.

Anafafanua kuwa kisima hicho kitatumiwa na wanakijiji wa ndani na nje ya eneo hili ambao awali walikuwa wakikabiliwa na tatizo sugu la maji chumvi.

“Nawashukuru sana uongozi wa Wilaya ya Simanjiro, Tarafa ya Moipo kwa ushirikiano wenu hususan katika kipindi chote ambacho sisi kampuni tupo eneo hili kwa idhini ya wanakijiji wenyewe, hivyo lengo letu kwa sasa ni kushikamana kama sehemu ya wadau wa maendeleo ya jamii nchini,” anasema Marias.

Anasema watoto wengi katika eneo hilo wameathirika sehemu mbalimbali za miili yao kama kuungua meno (kubadilika rangi ya asili) na kupinda au kupata matege kutokana na matumizi ya maji hayo yenye madini ‘florine’ chumvi.

“Mtambo huu unatumia teknolojia maarufu duniani ‘Reverse Osmosis’ ambao hutumika katika kutengeneza maji safi na salama yafaayo kwa matumizi ya afya ya binadamu, na una uwezo wa kutengeneza lita 30,000 za maji kwa siku,” anasema.

“Tumeshakaa na kijiji kujadili namna ya kutafuta watu wawili kwa ajili ya kupewa mafunzo ya uendeshaji na usimamizi wa mtambo, kwa sasa zoezi hili litakuwa chini ya uangalizi wa kampuni kwa takriban mwaka mmoja baada ya hapo tutaukabidhi kwa uongozi wa kijiji kwa ajili ya kuuendeleza mradi kipindi hicho tunaamini utakuwa umejipanga vizuri,” anabainisha Marias.

Mbali ya kisima hicho, anachanganua kuwa kampuni kwa kushirikiana na wanakijiji pamoja na wadau mbalimbali wamefanikiwa kujenga na kuzindua kituo cha Polisi kinachofahamika kama polisi ‘post,’ ambapo kampuni iligharamia sh mil. 55, kitakachotumika kama chachu ya kubadilisha tabia katika eneo hilo.

Anafafanua kuwa kituo hicho kiliwekwa jiwe la msingi na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Saidi Mwema miaka minne iliyopita kwa kuzingatia umuhimu na usalama wa wananchi kutokana na usumbufu pindi wanapokwenda kupata huduma katika kituo cha polisi kilichopo Mererani na wakati mwingine Machimboni.

“Kwa kuzingatia umuhimu wa kufanya marejesho kwa jamii inayotuzunguka, sisi TanzaniteOne tumeshirikiana na wananchi kuibua miradi na huduma mbalimbali kama ujenzi wa kituo jamii ‘Community Centre’ kutenga fungu la fedha kwa ajili ya ada ya wanafunzi wasiokua na uwezo shuleni, pamoja na bwawa la kunyweshea mifugo.

Changamoto katika utendaji

Mkurugenzi huyo anakwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa licha ya kampuni kuingia katika misukosuko mbalimbali baina yake na kampuni nyingine hususan katika utendaji kazi, bado inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo ya ufinyu wa fedha za kutatua mahitaji mbalimbali ya wanakijiji katika eneo husika.

Anaongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo kampuni iliingia katika upandaji wa Mlima Kilimanjaro wa hisani kwa dhumuni la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuvisadia vikundi mbalimbali vinavyojihusisha na malezi ya watoto yatima katika eneo la Mererani.

Katika hilo anatabanaisha kwamba wafanyakazi wa mgodi wa kampuni hiyo wamefanikiwa kuchangisha fedha sh milioni 76, ambazo zitakabidhiwa kwa Kituo cha New vision (TNV) kinachojishughulisha na malezi ya watoto yatima kilichpo Mererani.

“Mbali ya hilo, bado kampuni inatarajia kukamilisha zoezi la ujenzi wa madarasa mawili sanjari na chumba cha kompyuta katika shule ya msingi na kukarabati shule ya kata ya sekondari Naisinyai, mpaka sasa mchakato wa kupata makisio ya gharama (BOQ) umekamilika.

Published by tanzania Daima on 23rd October, 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO