Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Nani “CCM–B” CHADEMA au CUF? – Juma Duni Haji

MADHUMUNI ya Chama cha wananchi (CUF) kama yalivyo katika Katiba yake ni, “Kuwaunganisha Watanzania wakatae uonevu, kudhalilishwa, kunyanyaswa, kubaguliwa au maovu mengine yanayoweza kufanywa dhidi ya heshima ya utu wa binadamu, yawe yanayotendwa na serikali, kikundi cha watu walio na uwezo kwa ajili ya mabavu yao au kwa ajili ya kujinufaisha kwao kiuchumi au kisiasa na kiitikadi au kwa kujali dini, kabila jinsia au rangi zao”. (Kifungu cha, 6[1] Katiba ya CUF uk.12)

Kwa kiasi miaka miwili sasa ndugu zetu wa CHADEMA wamekuwa wakifanikiwa wakisambaza na kufanya siasa nyepesi nyepepi za maji taka kwa Watanzania Bara kwamba eti CUF ni “CCM-B” kwa sababu ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (Government of National Unity Zanzibar).
Dhamiri yangu leo ni kufanya uchambuzi na kuweka wazi kwamba hoja ni “U-CCM-B” au choyo na kuchukizwa kwa CHADEMA kwa Wazanzibari kusikilizana? au ni ukosefu wa dira na agenda sahihi ya kisiasa?

Hoja hii ya “U-CCM–B” imerejewa tena na viongozi wa CHADEMA pale Mheshimiwa, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia alipokubali uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa kumteua kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Watanzania wanapaswa kufahamu kwamba kilichopo pale Zanzibar ni Serikali ya umoja wa kitaifa si vyama vya umoja wa kitaifa.

Hakuna Chama cha CUF wala CCM ambacho kimeungana na kufanya viwili hivyo kufanya umoja unaoitwa CCM-CUF Taifa au vinginevyo.

Serikali ya umoja wa kitaifa ilipatikana baada ya kura ya maoni ya tarehe 31 Julai, 2010 kupigwa na asilimia 66.3 ya Wazanzibari bila kujali ni chama gani walikubali kuundwa Serikali hiyo ya (GNU).

Ni wananchi wa Zanzibar si wanachama wa vyama waliopiga kura ya maoni. Tunapokutana katika Baraza la Mawaziri hatukutani viongozi wa vyama, bali ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (si Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi) wanaokutana na kujadili masuala ya maendeleo ya nchi yao na wala si maendeleo ya vyama vyao.

Wakati wowote chama cha Mapinduzi wanapokutana huwa wanazungumza masuala ya chama chao na CUF huzungumza chama chao. Kwenye baraza la mawaziri tunazungumza nyaraka za wizara za Serikali siyo za idara ya chama chochote kati ya hivyo viwili. Sasa huu “U-CCM-B au A” unatoka wapi.

Hebu tuone “UCCM-B” upo wapi?
Madhumuni ya Chama cha wananchi CUF kama yalivyo katika Katiba yake kifungu cha, 6 (8) Katiba ya CUF uk.13) ni “kushika hatamu za dola ili dola au serikali itekeleze vizuri itikadi na sera za chama na ustawi wa taifa letu”.

Chama cha siasa ambacho hakina malengo ya kuunda serikali na au kuingia serikalini kuweza kusimamia utekelezaji mzuri wa sera na itikadi na badala yake inajielekeza katika kazi ya kulipua “MABOMU” na kung’ang’ania kupiga kelele za ufisadi hali chama chenyewe na watendaji wake wakiamini kuwa ufisadi ni sehemu ya njia ya kupata manufaa ya kisiasa na kiuchumi, tunavishukuru vyombo vya habari kwa kutujulisha kuhusu hali hii.

Hebu tujikumbushe tuone “UCCM-B” upo wapi? Mwaka 1991 Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi Rais wa CCM alimteua Mabere Marando (NCCR) kuwa mjumbe wa Tume ya kuratibu maoni ya wananchi juu kuanzishwa mfumo wa chama kimoja au vyama vingi chini ya Mwenyekiti Jaji Nyalali, Mwaka 2001.

Mabere Marando huyu huyu alichaguliwa na bunge kuwa Mbunge wa Bunge la EAC akiwa NCCR Mageuzi na kumshida marehemu Bob Makani aliyesimamishwa na CHADEMA, CHADEMA wakarudia, lugha hii wanayowaambia Wazanzibari kwamba NCCR Mageuzi ni CCM-B.

Leo Marando ni CHADEMA, U-CCM–B wake umeyayuka maana kaingia katika chama kitakatifu kinachopokea maono kutoka kwa Mungu?
Mwaka 2008, Rais Jakaya Kikwete alimteua Zitto Kabwe kuwa mjumbe wa Kamati ya Madini chini ya mzee Jaji Mark Bomani. Iliandikwa kuwa Mbowe amekatisha masomo yake kutoka nchini Ujerumani kuja kwenye kikao kuthibitisha uteuzi huo.

Si Zitto Kabwe wala chama cha CHADEMA kilichojitangaza kuwa wao ni CCM-B ! , Mwaka huu Rais Kikwete amemteua Profesa Mwesiga Baregu kuwa mjumbe wa Kamati ya kuratibu maoni ya uandikwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Viongozi wa CHadema, Dk. Wilbroad Slaa na Mbunge wa Singida Vijijini, Tundu Lissu, wakampongeza Rais Kikwete na Profesa Baregu, lakini muasisi wa CHADEMA akasema uteuzi huo wa Rais Kikwete una “UDINI” akimaanisha WAISLAMU WAMO KATIKA HUO UTEUZI WA KIKWETE!. Hata hivyo CHADEMA haijawa CCM-B.

John Mnyika na Tundu Lissu walikuwa na kesi za uchaguzi dhidi ya CCM kule Singida na pale Ubungo. Kesi hizi wameshinda zote chini ya utetezi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya CCM.

Hawasemwi kwamba wametetewa na mwanasheria wa serikali ya CCM na hivyo ni CCM-B!, Aprili 17, 2012 umefanyika uchaguzi mwingine wa EAC pale bungeni na CHADEMA walikuwa na wabunge 43 kati ya 48 wa chama hicho wakati kura zikipigwa.

Anthony Komu mgombea wa CHADEMA alipata kura 93, kura 50 kati ya hizo zilikua za wabunge wa CCM. CHADEMA wakaenda mahakamani ili uchaguzi urudiwe ili wapate nafasi ya kuwapata wabunge zaidi kumchagua Komu. Hapa UCCM-B. Haukuwepo?

Tarehe 22/08/2012 Mahakama Kuu Kanda ya Tabora ilitengua matokeo ya Uchaguzi Jimbo la Igunga na kuwapa ushindi wa kesi hiyo CHADEMA. Uchaguzi utarudiwa. Je, CHADEMA wamesaidiwa na Jaji wa Serikali ya CCM na hivyo na wao ni CCM-B?

James Mbatia alikuwa na kesi ya uchaguzi ya Jimbo la Kawe lakini akashindwa na Halima Mdee (CHADEMA). Mbatia akaenda Mahakamani kisheria. Viongozi wa CHADEMA wakatafuta njia za kiungwana kumaliza tatizo hilo nje ya Mahakama.

Februari 6 2012, makatibu wakuu wa NCCR-Mageuzi Samwel Ruhuza na Dk. Slaa walikubaliana kufuta kesi hiyo No.101/2010 na kumuacha Halima Mdee abaki kuwa Mbunge. Je, Halima naye ni NCCR-B au Mbatia ni CHADEMA -B?

Mwaka 2001 Rais Benjamin Mkapa, alimteua Hamad Rashid kuwa Mbunge wa Wawi (CUF), wakati huo siasa za ushabiki na mapambano zilikuwa kubwa mno na CHADEMA kilikuwepo, hoja ya CCM-B hawakuisema.

Mwaka 2009 Rais Kikwete alimteuwa Ismail Jusa kuwa mbunge, hoja za “UCCM-B” haikuwepo! Mwalimu Nyerere aliwahi kumpigia kura James Ndobho wa NCCR-Mageuzi Jimbo la Musoma Mjini na Ndobho akashinda, je, Nyerere alikuwa NCCR?

Kuna lugha ya kiswahili ya kuonewa kwa Bata kwa sababu tu ya umbo na sifa zake. Bata akitembea huambiwa anakata viuno kama mrembo wa Tanzania. Hivyo ndivyo alivyoumbwa, hakuchagua kukata viuno anapotembea na wala hajui kwamba anafanya hivyo. Bata huyu huyu anapotafuta chakula kwenye tope huambiwa anakula uchafu.

Sina hakika kwamba CHADEMA wanapokubali uteuzi wa rais huyu huyu ikawa ni sahihi chakula chao safi, lakini wengine wanapoteuliwa na rais, kwa CHADEMA huwa sawa na kula tope za choo.

Kwa CHADEMA kuku anapokwenda haja kubwa huwa anakunya, lakini bata huambiwa kaharisha, hakunya. Ukweli ni kwamba wote wamekunya, mmoja amekunya kutu ngumu mwingine kanya kutu laini, wote wamekunya mavi ya kuku na yote yananuka.

Vipi CHADEMA wao wajione watakatifu wanapopata uteuzi kwa rais wengine wawe wamekufuru, huu ni unafiki na uzandiki wa viongozi wanaotaka eti wapewe dhamana ya kuongoza nchi kwa akili kama za Panzi.

Kule Kigoma CCM na CHADEMA walikubaliana na CCM kuunda serikali ya Halmashauri ya Kigoma nusu kwa nusu ya madiwani kwa miaka mitano. Hoja ya CCM kuiona CHADEMA CCM-B haikutajwa, yaani yale kwa CHADEMA yalikuwa na mavi ya kuku CUF na CCM Zanzibar ni uharo wa bata.

Kule Arusha kulikuwa na serikali ya aina hiyo, mpaka yalipotokea malumbano na upuuzi wa wawakilishi wa wananchi madiwani walipozuiliwa na chama chao CHADEMA kuwawakilisha barazani.

Wengi tumezoeshwa kwamba siasa ni uongo na mchezo mchafu. Hapana. Moja ya suala ambalo CUF na viongozi wake tunalisimamia na kutaka watanzania waamini kuwa siasa si uongo wala si mchezo mchafu bali baadhi ya wanasiasa ndio waongo na wachafu.

Kama viongozi wanaweza kusema uongo wa kiwango cha uharo wa bata wakiwa nje ya Ikulu watakunya nini hawa wakiingia Ikulu? Kama kuna viongozi wanaweza kuiba wake za watu na kuja jukwaani kujisifu kwamba wao ni wezi wa wake za watu, je, wakiwa Ikulu watafanyaje hawa? Watawapanga foleni wanawake wote waliopo pale kwa uwezo wa madaraka yao ya urais na kuwalazimisha kufanya nao ngono.

Hivyo tunategemea hawa wakajenge nyumba ya umalaya pale Ikulu. Je, nyie ndiyo mnashangilia hayo? Eti kunja ngumi, ngumi gani ya wizi wa wake za watu? Eti kunja ngumi, ngumi ya kutengeneza vifo vya Watanzania wenzetu?

Watanzania mna kila sababu za kutafakari na kuchukua maamuzi sahihi juu ya hatima na mustakbali wa maisha yenu ya sasa na kizazi kijacho, wapi pa kuunganisha nguvu zenu ili mabadiliko ya kweli kiuchumi na kisiasa yaweze kupatikana. Siasa za milipuko na mihemuko za leo linasemwa hili na kesho linasemwa vinginevyo jambo hilo hilo hazina nafasi kwa CUF ya DIRA YA MABADILIKO.

Suala la U-A na U-B, unatoka wapi na unakujaje katika mahusiano ya chama kimoja na kingine wakati kilichojenga umoja ni ridhaa ya Wazanzibari?
Mwaka 2005 hadi 2010, wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) kiliunda kambi ya upinzani na wabunge wa CHADEMA bungeni kwa miaka mitano, na Dk. Slaa akawa Naibu Kiongozi wa kambi hiyo kwa muda wote wa miaka mitano.

Mheshimiwa Zitto na wabunge wengine wa chama hiki wakishika nyadhifa za uwaziri kivuli wa kambi hiyo. Ilikuwa ni Serikali kamili nje ya Serikali ya Muungano. Vyama viwili hivi viliendelea kubaki na shughuli zake ndani na nje ya Bunge.

Mbona hoja ya CHADEMA kujiita CUF-B haikuja wala hawakujigamba hivyo kuwa wao ni CUF-B? Chama cha wananchi CUF kilifanya hivyo kwa sababu madhumuni yake ni: “Kuwaunganisha Watanzania wakatae uonevu, kudhalilishwa, kunyanyaswa, kubaguliwa au maovu mengine yanayoweza kufanywa dhidi ya heshima ya utu wa binaadama, yawe yanayotendwa na Serikali, kikundi cha watu walio na uwezo kwa ajili ya mabavu yao au kwa ajili ya kujinufaish kwao kiuchumi au kisiasa na kiitikadi au kwa kujali dini, kabila jinsia su rangi zao”.

Muda wote huu vyama vya upinzani tumeshindwa kuungana na kukiondoa chama cha CCM kwa sababu ya udhaifu huu wa CHADEMA kujikubalisha kujigawa mafungu huku CCM ikichekelea na kutuona wajinga. Ujinga na upumbavu huu umezidi tulipogundua kwamba viongozi wa CHADEMA wanaonesha udhaifu wao kwa kukosa furaha kuwaona Wazanzibari wanasikilizana na nyinyi wananchi mnafurahia hilo kwamba tuaachwe Wazanzibari tuuane na kwamba eti hicho ndiyo chama mnachokitaka eti kiingie Ikulu.

Msimamo huu wa CHADEMA ni kuthibitisha kwamba Wazanzibari kugombana ndiyo furaha ya viongozi wa chama hicho, maana furaha na agenda ya muda mrefu ya baadhi ya viongozi watanganyika wawe wa CCM au CHADEMA ni kuhakikisha Wazanzibari tunawagawa ili tuwatawale.

Kama hivyo ndivyo wazanzibari hatuna sababu ya kushanga ya jinsi viongozi wenzetu wa Tanganyika mnavyotuona, maana sisi wazanzibari ambao wazee wetu kina mzee Karume na Mzee Thabit Kombo walimuamini Mwalimu Nyerere kwa kuunganisha nchi mbili hizi kwa faida ya pande mbili.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mara kadhaa kwamba Tanzania ipo kwa sababu ya Zanzibar. Msimamo wetu ni kuwa wazanzibari hawako tayari tena kufanywa koloni la Tanganyika. Kinachohitajika sasa ni kurekebisha makosa yaliyofanywa miaka 50 iliyopita yaliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1964.

Ninachotaka kuwakumbusha Watanzania ni kwamba Mimi binafsi na wenzangu wengi ni wahanga wakubwa wa siasa mbovu za zamani za Zanzibar, tuliathirika sana kwa kubambikiwa kesi za uhaini na kesi za mauaji.

Leo ni waziri wa serikali ya umoja wa kitaifa siyo umoja wa vyama vya CCM na CUF. Wazanzibar tumemaliza matatizo yetu ya ndani wenyewe, tumeamua kujenga nchi yetu, wakati nyinyi yenu mnaitayarisha ibomoke, sisi huko tumeshatoka.

Fursa ya kujenga siasa za kistaarabu, siasa za heshima, siasa zenye lengo la kuwasaidia watu wetu kuondokana na lindi la umaskini, maradhi na ujinga ipo, Hatujachelewa!

Tuutumie vema mchakato wa uratibu wa ukusanyaji maoni ya katiba, ipendekezwe uwepo wa uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa, CUF katika manifesto yetu ya mwaka 2010 tulilieleza hili. CUF chini ya dira ya mabadiliko inaamini katika mazungumzo.

Namaliza kwa kuwaambia Zanzibar kuna Serikali ya umoja wa kitaifa. Hakuna muungano wa vyama vya kitaifa, wala hakuna CCM-B wala CUF –G. Kilichopo ni serikali si vyama kuunganisha nguvu kujenga taifa letu.

Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Zanzibar!

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO