MWANAMITINDO anayetamba kwa sasa hapa nchini, Jokate Mwegelo, amefungua rasmi kampuni yake yenye Chapa ya Kidoti itakayokuwa ikijishughulisha na masuala mbalimbali ya urembo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Jokate alisema ameamua kuanzisha kampuni hiyo ambayo kwa sasa imeanza na uuzaji wa nywele na baadaye ataendelea na mambo mengine mbalimbali ya urembo, ikiwemo nguo na vitu mbalimbali vya urembo na vipodozi.
Alisema kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 2011 na kuzinduliwa rasmi jana, kwa nia ya kubadilisha mtazamo mzima wa tasnia ya mitindo na kuwa, chapa hiyo itasheheni bidhaa mbalimbali.
“Kidoti ni chapa yenye uwezo wa kubadilisha jinsi tunavyoichukulia tasnia ya mitindo hivi sasa na mimi na wenzangu katika kampuni hii yenye maskani yake Barabara ya Bibi Titi hapa jijini, tumejipanga kuhakikisha wadau wetu mbalimbali wanakuwa na mwonekano tofauti,” alisema Jokate.
Aliongeza kuwa, chapa hiyo imeundwa katika taswira yake mwenyewe na kuwa ameamua kutumia jina hilo kutokana na sifa yake ya kuwa na kidoti juu ya mdomo wake, ambako awali jina hilo lilianza kama utani na baadaye kulipokea na kulifanya kianzilishi cha biashara kwa ajili ya kuinua uchumi kwa jamii nzima na yeye binafsi.
Alisema kaulimbiu ya kampuni yake ni ‘Ainisha Uzuri Wako’ ambako chapa hiyo imekuwa ikileta hamu katika soko kupitia mitindo ya nguo, ambayo imeonekana ikivaliwa na watu maarufu na wasanii wengi nchini katika matukio mbalimbali.
Aliongeza kuwa harakati ya Kidoti inaendeshwa na timu ya vijana wabunifu, pamoja na kwamba, shughuli za kidoti zinaendeshwa kutoka Dar es Salaam, chapa hii ni ya kiulimwengu zaidi na kuwaomba wadau mbalimbali kumpa sapoti
Imeandikwa na Clezencia Tryphone wa Tanzania Daima
0 maoni:
Post a Comment