SIRI za hila na hujuma katika uchaguzi wa CCM zimeendelea kufichuka, ambapo inadaiwa kuwa Sh milioni 300, zilitumika kumwangusha Makongoro Nyerere, katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mara.
Makongoro ambaye alikuwa anatetea nafasi ya Mwenyekiti katika mkoa huo, aliangushwa na kada mwingine wa chama hicho, Christopher Sanya.
Katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo, Sanya alipata kura 501, Makongoro kura 370 na Enock Chambiri, alipata kura 470 idadi ambayo ilidaiwa kuwa ni kubwa kuliko idadi ya wajumbe waliotangazwa.
Hata hivyo katika uchaguzi wa marudio, idadi ya wajumbe ilitajwa kuwa ni zaidi ya 900, ambapo Makongoro alipata kura 422, huku Sanya akipata kura 481.
Hivyo kutokana na matokeo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi huo, Nazir Karamagi alimtangaza Sanya kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM Mkoa wa Mara.
Makongoro alitajwa katika uchaguzi hou uliofanyika Jumamosi, katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Songe Musoma mjini.
Baadhi ya wajumbe walioshiriki mkutano huo na ambao hawakutaka majina yao yatajwe, walithibitisha kuwapo kwa matumizi makubwa katika uchaguzi huo.
Mmoja wa wapambe wa Sanya, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alikiri kuwa ushindi wa mgombea wao, ulichangiwa na matumizi makubwa ya fedha.
Chanzo hicho kilianika wazi kuwa, fedha hizo zilichangwa na wafanyabiashara wa Musoma, Mwanza na Arusha, ambao wapo katika mtandao wa mtu mmoja anayetajwa kuwania urais mwaka 2015.
Mbali ya matumizi ya fedha, sababu nyingine inayodaiwa kumwangusha Makongoro, ni kwamba mwaka 2010 alichangia CCM kupoteza kiti cha ubunge wa Jimbo la Musoma Mjini.
Katika hoja hiyo, Makongoro anadaiwa kuponzwa na msimamo wake wa kukataa kumkana Mbunge wa Musoma Mjini Vicent Nyerere (CHADEMA), wakati wa uchaguzi mkuu 2010.
Wakati wa kampeni hizo za uchaguzi, Makongoro alitakiwa kumkana hadharani Vicent kwamba, si ndugu yake, jambo ambalo alilipinga kwa nguvu zake zote.
“Makongoro anadaiwa kuwa, mwaka 2010 hakwenda Musoma Mjini na alipotakiwa kumkana mgombea wa Chadema kwamba si ndugu yake alikataa.
“Makongoro alisema, Vicent ni mdogo wake mtoto wa baba yake mdogo mzee Kiboko, hivyo hayuko tayari kumkana ndugu, kwa sababu za kisiasa, kilisema chanzo hicho.
Mjumbe huyo ambaye alishiriki kukusanya fedha hizo, alianika wazi akisema kuwa, siku moja kabla ya uchaguzi wanamtandao hao walikutana katika hoteli mbili tofauti Musoma Mjini na kuweka mikakati ya ushindi.
Katika mkakati huo, watu hao walipanga kununua kura 300 kwa kila kura moja Sh 300, 000. Pia walipanga kura 150 zinunuliwe kwa Sh 150, 000 na kura 100 zinunuliwe kwa Sh 20, 000 hadi 50, 000.
“Kwa kweli Makongoro ni mtu mwenye jina kubwa na ni mtu anayependwa, kwani mkakati wetu na fedha tulizotumia, tulitegemea awamu ya kwanza tu ya uchaguzi tungeshinda, lakini tulishangaa uchaguzi ukarudiwa.
“Sasa hapo tulifikia hatua kununua baadhi ya kura moja kwa Sh 500, 000. Hapo kama mambo yalikuwa magumu, bila kufanya hivyo mgombea wetu alikuwa anaangukia pua.
“Uchaguzi ulikuwa ni mgumu na hii ilikuwa ni bahati yetu, tuligawa makundi ya kwenda kukutana na wajumbe kabla ya kufika ukumbini.
“Tungengojea kutoa pesa pale ingekuwa ngumu, kwani kulikuwa na ulinzi mkali sana, lakini ile awamu ya pili tuligawa fedha kwa viongozi wa wajumbe ukumbini hatukuruhusiwa hata kunyanyuka kwenda katika wilaya nyingine,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema kuwa, baadhi ya wajumbe walipiga kura za chuki dhidi ya Makongoro, kwani majina ya ndugu zao yalikatwa na mgombea huyo wakati wa uchaguzi wa halmashauri.
Akizungumza na Mtanzania, Makongoro alisema uchaguzi wa mkoa huo, ulitawaliwa na mizengwe na kusema kuwa, kushindwa kwake kumechangiwa na matumizi makubwa ya fedha.
Hata hivyo Makongoro alisema, hawezi kuendelea kukaa kimya wakati akijua rafu zilizotendeka na badala yake anajipanga kuchukua hatua zaidi, ikiwa ni pamoja na kukata rufaa.
Kwa upande wake Sanya wakati akizungumza na vyombo vya habari alisema kuwa, anachofahamu ni kuwa ameshinda na kwamba hajui kama fedha zilitumika kufanikisha ushindi wake.
Source: Mtanzania
0 maoni:
Post a Comment