Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kitakuwa na mahafali ya 42 tarehe 27 Oktoba 2012 na Novemba 3, 3012.
Jumla ya wahitimu 3,643 watatunukiwa shahada na stashahada wakati wahitimu 902 wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi (UCLAS) watatunukiwa shahada.
UCLAS kwa sasa ni sehemu ya UDSM.
Hayo yalisemwa na Makamu Mkuu wa wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala akitoa taarifa kwa umma kupitia waandishi wa habari.
“Tunapenda kuufahamisha umma pia kuwa, katika mahafali ya sasa wanafunzi wa UCLAS na wao watatunukiwa shahada kama wanafunzi wa UDSM, uamuzi huu umefuatia kumalizika kwa kesi Lello & Others Vs Ardhi University, University of Dar es Salaam and Attornry General, Misc.Civil Cause No. 69 of 2008, iliyofunguliwa na wanafunzi wa UCLAS wakipinga kupata shahada za UCLAS kwa madai kuwa udahili wao ulibaki wa UDSM, hivyo UDSM kinakubalina kwa dhati na uamuzi wa Mahakama Kuu,” alisema Prof Mukandala.
UDSM imekubali kuwatunuku shahada mbalimbali wahitimu hao 902 waliomaliza masomo yao UCLAS ambao awali waligoma kutunukiwa shahada zao na chuo hicho (UCLAS) katika Mahafali ya 42 kutokana na madai kuwa walipata udahili chini ya UDSM wakati UCLAS kilipopata hadhi ya kuwa chuo kikuu kinachojitegemea mwaka 2007 hivyo walistahili kutunukiwa shahada na chuo kilichowadahili. Wanafunzi hao ni wale waliohitimu masomo katika miaka ya 2007 hadi 2010.
Wanafunzi hao kwa kupinga suala hilo walifungua kesi mahakamani dhidi ya Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Sisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tumekubaliana kwa dhati na uamuzi huu wa mahakama na tumeamua kuwatunuku shahada wanafunzi hao kwa vile hakuna rufaa iliyokatwa dhidi ya uamuzi huo,” alisema Profesa Mukandala.
Kati ya watakaotunukiwa shahada mbalimbali, 28 watatunukiwa Shahada za Uzamivu, 671 Shahada ya Uzamili; 153 Stashahada za Uzamili na 2, 790 Shahada ya Kwanza.
Licha ya mahafali hayo, Profesa Mukandala alisema chuo hicho kitahitimisha maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwake kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwamo kufanya mkutano na wahitimu waliowahi kusoma chuoni hapo shughuli ambayo itafanyika Alhamisi.
Profesa Mukandala alisema wakati wa kuhitimisha sherehe hizo, shughuli zitakazofanyika ni kuweka jiwe la msingi la jengo la kituo cha wanafunzi, kuzindua Dira ya Chuo hicho (UDSM Vision 2061) na kutoa tuzo mbalimbali kwa watu na vikundi vilivyotoa mchango uliotukuka kwa chuo kikuu katika miaka 50 iliyopita.
Akizungumzia dira hiyo, alisema itakuwa ni ya nusu karne ijayo na malengo yake ni kufikia mwaka 2061 chuo kitakuwa katika nafasi za juu za viwango vya ubora vya kimataifa
Source: Habari Mpasuko
0 maoni:
Post a Comment