VIGOGO 10 wametajwa kuhusika katika kashfa ya kuficha Sh303.7 bilioni katika benki mbalimbali nchini Uswisi. Katika orodha hiyo inadaiwa kuwa yupo kiongozi mmoja mwandamizi mstaafu, maofisa watatu wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mawaziri wastaafu ambao baadhi yao bado ni wabunge na aliyewahi kuwa kiongozi mwandamizi wa Benki Kuu Tanzania (BoT).
Juzi, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alimshukia Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah akimtuhumu kuandika barua Uswisi akisema Tanzania haina masilahi na mabilioni ya fedha yaliyofichwa katika benki zilizopo nchini humo. Hata hivyo, Dk Hoseah alikanusha madai hayo akisema hajawahi kufanya hivyo.
Akizungumza jana Zitto alisisitiza kauli yake akisema: “Sijawahi kumsema Dk Hoseah kwa lolote, kwa nini leo nimsingizie? Yeye mwenyewe anajua ushirikiano niliompa wakati wabunge wanapinga yeye asichunguze malipo ya posho mara mbili kwa wabunge.”
“Nilisimama kidete kusema Takukuru wapo sahihi na mimi nilikwenda mwenyewe kwao kuhojiwa na kuagiza wajumbe wa kamati yangu (Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma), waende kuhojiwa. Spika aliyestaafu (Samuel Sitta) akaizima kashfa ya wabunge kupokea posho mara mbilimbili. Mwulizeni amesahau? Sasa leo nimzushie ili iwe nini?.”
Alisema orodha ya Watanzania wenye fedha huko Uswisi, ipo na ameiona na nyaraka zinaweza kutolewa kwa taasisi za Serikali tu.
“Dk Hoseah kazuia nyaraka hizo. Akitaka nimwonyeshe mtu anayeweza kutoa nyaraka hizo, nipo tayari isipokuwa aahidi kuiweka wazi,” alisema Zitto.
Alisema katika orodha ambayo Waziri wa Fedha wa Ufaransa anayo, kuna Watanzania lakini akaituhumu Serikali akisema haitaki kufuata njia halali za kupata orodha hiyo kwa kuwa viongozi wengi na wafanyabiashara wakubwa wana akaunti katika benki za Uswisi.
Juni 26, mwaka huu gazeti hili lilichapisha habari kuhusu utoroshwaji wa fedha hizo na kueleza kuwa Polisi wa Kimataifa (Interpol) nchini kwa kushirikiana na Takukuru inachunguza suala hilo.
Kiasi hicho cha fedha kimedaiwa kuingizwa katika akaunti za Watanzania na kampuni moja ya uchimbaji mafuta na kampuni kadhaa za uchimbaji madini ambazo zinafanya kazi Tanzania.
Chanzo hicho kiliongeza kwamba kiasi hicho cha fedha kipo katika akaunti sita tofauti zinazomilikiwa na Watanzania wakiwamo wanasiasa wakubwa. Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa tangu akaunti hizo zifunguliwe, wamiliki wake halali hawajawahi kuingiza hata shilingi.
“Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa fedha hizo zipo katika akaunti sita tofauti ambazo zinamilikiwa na wanasiasa wakubwa nchini na wenzetu wa Uswisi wameeleza fedha hizo zimeingizwa na kampuni kadhaa ambazo zinahusika na mafuta pamoja na madini hapa nchini,” kilidokeza chanzo hicho.
Kugundulika kwa kiasi hicho cha fedha katika benki za Uswisi ni kutokana na ripoti ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB) iliyotolewa mwaka huu.
Chanzo: Mwananchi, 29 Oktoba, 2012
0 maoni:
Post a Comment