Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

“Sijazibwa Mdomo, Najipanga Kueleza Ukweli Wa Kilichonisibu” – Dr. Ulimboka

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, amezungumzia mustakabali wake huku akisisitiza kuwa kamwe hajafungwa mdomo bali anajipanga kuanika ukweli wa kile kilichomsibu.

Dk. Ulimboka pia amewataka wanataaluma wenzake kutulia hasa kwa wakati huu ambao bado ameweka kipaumbele katika tiba yake ambayo ameielezea kuendelea kuimarika na kwamba madai yao bado ni ya msingi na kamwe hayawezi kuishia hapo yaliposimamia.

Dk. Ulimboka ambaye alitekwa, kuteswa, kuumizwa vibaya na kisha kutelekezwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaamu usiku wa kuamkia Juni 27 mwaka huu, amekuwa kimya baada ya kurejea nchini akitokea Afrika Kusini alikokwenda kwa matibabu zaidi.

Tangu kurejea nchini mapema Agosti, Dk. Ulimboka amekuwa kimya kutokana na kilichoelezwa ni kutotaka wabaya wake wajue alipo ili wasije wakamdhuru na kupoteza ushahidi hasa ikizingatiwa kuwa amekuwa akiwataja hadharani baadhi ya maofisa wa Usalama wa Taifa akidai walishiriki kumteka.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana baada ya ukimya huo, Dk. Ulimboka alisema kamwe hawezi kuzibwa mdomo kama ambavyo taarifa za uvumi zilivyozagaa. Alisema kamwe hajanunuliwa na kwamba ukimya wake wa muda mrefu umetokana na kufuatilia kwa karibu masharti ya matibabu yake na si vinginevyo. Alisema kuwa muda ukifika atazungumzia masuala yote yanayohusiana na kutekwa kwake na hatua gani zitakazofuata, “Siwezi kuzibwa mdomo na yeyote, hata walionichagua kuwa mwenyekiti wao, wanafahamu hivyo, suala ni wakati tu, utakapofika hasa baada ya kukamilisha masuala ya kisheria, nitazungumza hivi karibuni ili kuondoa hofu hiyo…” “Sijanunuliwa, sijawaogopa watesi wangu, wala sijanyamazishwa kwa lolote lile. Hata hao wanaoeneza taarifa kuwa nimenunuliwa, wanajua kuwa hawana ubavu wa kuninunua,” alisema Dkt. Ulimboka.

Ukimya wake umeibua mjadala kiasi cha watu wengine kuanza kudhani kuwa amenyamazishwa asisema chochote juu ya tukio hilo ambalo limelighubika taifa kutokana na mkanganyiko uliyopo.

Dk. Ulimboka amekiri kuwa amewahi kusikia taarifa za yeye kununuliwa na kusema amekuwa akijisikia vibaya kuona kundi la watu fulani likihaha kutaka kupotosha ukweli na kuchafua jina lake.

“Huo ni uzushi mtupu. Hata walionitesa wanajua kuwa hawawezi kuninyamazisha au kuninunua. Wanajua sina bei katika kutetea masilahi ya umma. Ndiyo maana wakaamua kutumia njia ile ya kinyama kutaka kunitoa roho yangu. Siwaogopi wanaodhuru mwili, bali yule awezaye kutoa roho. Nakuhakikishia, muda si mrefu nitaanika kila kitu juu ya kutekwa kwangu, kuteswa na kutupwa kwenye Msitu wa Pande,” alisema.

Daktari huyo ambaye bado hajahojiwa na polisi juu ya aliowataja kuhusika na utekaji na utesaji huo, amesisitiza kuwa alipokamatwa alikuwa na akili timamu na kwamba anawafahamu wote waliopanga mkakati wa kumteka, “Watanzania na wapendahaki duniani kote, wana haki ya kujua kwa kina yale yaliyonisibu pamoja na watu waliohusika katika kutekwa kwangu. Hivyo ninao wajibu mkubwa wa kueleza ukweli huo na bila kuuma maneno.”

Haya ni mahoajino ya kwanza ya ana kwa ana tangu Dk Ulimboka aliporejea nchini kutoka katika matibabu Afrika Kusini miezi miwili iliyopita, “Huo ndiyo msimamo wangu na katika hili siwezi kutafuna maneno, mimi kama kiongozi ninao wajibu mkubwa wa kulieleza hili kwa Watanzania wenzangu.”

Tofauti na aliporejea, Agosti 12 mwaka huu, Dk Ulimboka ameonekana akiwa mwenye siha nzuri huku akisema mapambano ya kudai haki za madaktari bado hayajafikia tamati.

Alisema mapambano hayo ni muhimu kuendelezwa kwa kuwa ndiyo njia pekee itakayoifanya Serikali kuboresha huduma za afya nchini. Alisema ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa mamia ya wananchi wanakufa kutokana na kukosa huduma bora za afya.

Aliwataka madaktari kote nchini, kuzidisha mshikamano na kuendelea kupigania haki zao akisema wanachokidai ni haki yao.

Source: wavuti

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO