Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Ajali ya ghorofa lililoporomoka: Simulizi ya aliyenusurika kifo kutoka ghorofa ya 15

Rais Kikwete na Mkewe, Mama Salma Kikwete wakimpa pole Yusuph Abdallah katika Hospitali ya Muhimbili walipotembelea majeruhi wa ajali ya kuporomoka jengo la ghorofa 16. Picha na Muhidin Michuzi 

*****************

Dar es Salaam.

Fundi ujenzi, Yusuph Abdallah ambaye amelazwa katika Taasisi ya Mifupa (Moi), ameeleza jinsi alivyonusurika kifo baada ya jengo la ghorofa 16 kuporomoka Ijumaa iliyopita.

Yusuph aliliambia Mwananchi akiwa wodini kwamba kilichomponya ni neema za Mungu kwani kabla jengo hilo kuporomoka yeye alikuwa ghorofa ya 15 kwenye jengo hilo katika Mtaa wa Indira Gandhi akiendelea na ujenzi.

Alieleza kuwa hakuwa anafahamu kinachoendelea, bali aliona ghafla jengo linaaanza kuporomoka, na baada ya hapo hakufahamu zaidi kilichotokea hadi alipojikuta yuko hospitalini.

“Kweli jengo lilipoanza kuporomoka sikutambua nini kinachoendelea kwani nilipoteza fahamu na kujikuta nipo hapa Muhimbili,” anasimulia Abdallah.

Alisema anahisi alipoanguka alifunikwa na kifusi kilichomponda na kuvunja miguu yote.

Fundi huyo ambaye amefungwa plasta gumu (P.O.P) miguu yote, alisema hakuweza kuona watu waliomwokoa.

Mwingine aokolewa na mkewe

Mkazi wa Ubungo, Ally Mlela ambaye ni fundi madirisha anasimulia jinsi mke wake alivyomwokoa katika ajali hiyo baada ya kumtaka asiende kufanya kazi siku hiyo.

Akisimulia jinsi ilivyokuwa Mlela anasema siku ya tukio aliwasiliana na rafiki yake ambaye amepoteza maisha katika ajali hiyo na kumtaka aende akaonane na mkandarasi wa jengo hilo, ili ampe kazi ya kuweka madirisha.

“Majira ya asubuhi kati ya saa mbili na saa tatu hivi nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu jina maarufu anajulikana kama Tafu, ambapo alinitaka niende nikaonane na mkandarasi wa jengo hilo ili anipe kazi ya kuweka madirisha,” anasema Mlela.

Anasema wakati akijiandaa kutoka mke wake alimwambia siku hiyo apumzike asiende kufanya kazi naye akakubali, lakini haikupita muda mrefu mke wake alimfuata na kumuuliza amesikia taarifa kwamba kuna jengo limedondoka?

“Niliamua kwenda katika eneo la tukio na ndipo alipogundua kwamba eneo hilo ndiyo alipotakiwa kwenda kufanya kazi. Wakati juhudi za uokoaji zikiendelea nilijaribu tena kumpigia simu rafiki yangu.Nikiwa bado kwenye eneo la tukio ghafla nikaona mguu ukitolewa kwenye mchanga na nilitambua ulikuwa mguu wa rafiki yangu baada ya kuona kiatu chake.”

JK awatembelea majeruhi

Rais Jakaya Kikwete jana aliwatembelea majeruhi wa ajali hiyo ambao wamelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwapa pole.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Tiba wa Taasisi ya Mifupa (Moi), Dk Cuthbert Mcharo alisema walipokea majeruhi sita na hadi jana walikuwa wamebakia wanne.

Miili zaidi yapatikana

Katika hatua nyingine kikosi cha uokoaji jana kilipata miili ya watu saba iliyopatikana. Mmoja kati ya miili hiyo baada ya kuuchunguza, ulikutwa na kitambulisho cha kupigia kura kinachomtambulisha kwa jina la Salumu Mwaliko kutoka Kijiji cha Kwadeboma, Handeni mkoani Tanga.

Hatua hiyo inafanya idadi ya watu waliopoteza maisha katika maafa hayo kufikia 31.

NHC kugharimia majeruhi, mazishi

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema amepokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu kwamba kuna majengo matatu ya ghorofa ambayo yanatakiwa kubomolewa kutokana na kuchakaa. Mbali na hilo, Mkuu wa Mkoa amesema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linatakiwa kulipa gharama zote za watu walioathirika na ajali ya Ijumaa iliyopita.

Alisema NHC wanapaswa kuwahudumia majeruhi wote pamoja na kugharimia mazishi ya watu waliopoteza maisha.

Chanzo: Mwananchi

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO