WATOTO wa kaka yake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu, Steven Wassira (pichani) wametangaza kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwa mujibu wa watoto hao, uamuzi wao wa kujiunga CHADEMA unatokana na kuona nuru ya mabadiliko kupitia chama hicho.
Vijana hao, Esther Wassira na Lilian Wassira ambao ni watoto wa George Wassira, walijiunga na chama hicho jana.
Walipokewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Dar es Salaam.
Vijana hao ambao ni wanasheria, wamaliki Kampuni ya Uwakili ya Armicus Atorneys.
“Tuna haki ya kuchagua chama cha kujiunga nacho,Wassira ni baba yetu mdogo na atabaki kuwa hivyo lakini sisi tuna hiari ya kufanya kile tunachokiamini,”alisema Esther.
Esther ambaye ni mdogo wa Lilian, alisema hivi sasa Tanzania inahitaji mabadiliko ya dhati kwa kuunga mkono Vuguvugu la Mabadiliko (M4C kuondoa kero zinazokwamisha maendeleo nchini kwa zaidi ya miaka 50 sasa.
“Kwa mara ya kwanza nimeamua kujiunga na M4C, naiona CHADEMA ni chachu ya mabadiliko. Ni wakati mpya kukiweka chama hiki kwenye uso mwingine wa siasa.
“...huu ni mfumo wa vyama vingi, hatuwezi kuendelea na CCM ambayo siku zote inacheza ‘muziki’ na kufuata nyayo za Chadema. Bila shaka ni chama chenye sera nzuri.
“Sisi kama vijana tunaona bado tunayo nafasi ya kufanya kitu kupitia Chadema, lazima nifanye kitu kwa ajili ya nchi yangu naamini wanaweza kutufikisha pale tunapotaka,” alisema Esther.
Naye Lilian alitoa wito kwa Watanzania kuamini mabadiliko ya maendeleo yanawezekana kupitia chama hicho.
“Naamini hatujapotea, tuko sahihi na tumeingia chama sahihi, tunaona wanavyopambana, tumeamua kuwa sehemu ya mabadiliko… sifuati ukongwe wa chama bali sera zenye matumaini ya dhati kwa ajili ya kizazi chetu Watanzania.
“Tukiunganisha nguvu Tanzania mpya inakuja, bila madadiliko hakuna ushindani. Tunataka maendeleo, tumechoshwa na sera za CCM, naamini kwa msaada wa Mungu inawezekana,” alisema Lilian.
Akizungumza baada ya kuwapokea, Dk. Slaa alisema hatua yao hiyo ni kielelezo tosha kwamba yale yanayozungumzwa na CCM kupitia kwa Wassira kuwa Chadema ni chama cha vurugu na fujo ni propaganda zilizopitwa na wakati.
“Siamini watu wenye akili timamu kama vijana hawa wanaweza kujiunga na chama ambacho ni cha fujo na vurugu kama ambavyo imekuwa ikisema kwa nguvu kubwa na kupitia kwa Wassira,”alisema Dk.Slaa.
Kuhusu chama hicho kudaiwa kuwafanyia vurugu wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) mkoani Arusha, Dk.Slaa alisema si haki kukihusisha chama hicho na vurugu hizo kwa sababu hakina hatimiliki na Arusha.
Alisema si kila mfanyabiashara ndogo ndogo (machinga) ni mwana Chadema.
“Kumezuka na upotoshaji kujenga dhana kwamba kila machinga wa Arusha ni mfuasi wa CHADEMA. Sisi hatuna hatimiliki Arusha, kila chama kinayo haki ya kufika kila kona ya nchi hii kufanya siasa bila kuingiliwa, lakini wasituhusishe na vurugu za CUF,” alisema Dk.Slaa.
Imechapishwa na Mtanzania, Jumapili Septemba 30, 2012
0 maoni:
Post a Comment