Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CCM kulia au kucheka leo

Kafumu

MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Tabora leo itawaliza au kuwafurahisha wanachama wa CCM, wakati itakapotoa hukumu ya kesi ya kupinga matokeo ya ubunge yaliyompa ushindi Mbunge wa Jimbo la Igunga, kupitia chama hicho, Dk. Peter Kafumu.

Hukumu hiyo ambayo inavuta hisia za wananchi wengi wa Igunga, inatarajiwa kutolewa leo saa tatu asubuhi na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.

Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge katika uchaguzi huo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Kashindye. Uchaguzi huo mdogo ulifanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Mbali ya Dk. Kafumu, wengine wanaolalamikiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Protace Magayane.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa rasmi mapema Machi 26 mwaka huu na jaji wa mahakama hiyo, Mery Shangali.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, Silvester Kainda, alisema, mahakama hiyo ilipanga hukumu hiyo isomwe jana, lakini haikuwezekana kutokana na siku hiyo kuangukia Iddi Pili, hivyo hukumu hiyo inasomwa leo.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, wakili wa mlalamikaji Profesa, Abdallah Safari alisema, katika kesi hiyo hoja 13 za kupinga ushindi wa Dk. Kafumu ziliwasilishwa katika mahakama hiyo.
Ushindi wa Dk. Kafumu unadaiwa kuwa na dosari kutokana na viongozi wa Serikali kutoa ahadi ya ujenzi wa Daraja la Mbuntu na ahadi za kugawa chakula cha njaa wakati wa kampeni, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Profesa safari alisema, kulingana na malalamiko hayo wanaiachia mahakama iweze kutoa uamuzi wake.
“Kutokana na hoja tulizowasilisha, tunaiachia mahakama itoe hukumu, kwani kwa kila kitu tumekiwasilisha na kila upande ulikwishatoa majumuisho,” alisema.

Katika kesi hiyo Dk. Kafumu aliwakilishwa na mawakili wawili ambao ni Antony Kanyama, pamoja na Kayaga Kamaliza.

Habari kutoka Igunga zinasema, wafuasi wa vyama vya CCM na Chadema, wanatarajiwa kufurika mahakamani kusikiliza hukumu hiyo, ambayo ni ya kwanza katika historia ya jimbo hilo.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari makundi ya vijana wa Chadema jana walionekana katika maeneo ya sokoni mjini Igunga, wakichangishana fedha kwa ajili ya kukodi usafiri kwenda mjini Nzega ilipo mahakama hiyo.

Kwa upande wa CCM ni kama hivyo, ambapo vijana wa chama hicho nao hawakuwa nyuma, wanadaiwa kuendesha harambee za muda mfupi kuhakikisha wanafika Nzega.

Uchaguzi mdogo wa Igunga ulifanyika Oktoba 2011, ambapo Dk. Kafumu alitangazwa kuwa mshindi kwa kura 26, 484 sawa na asilimia 50.56 huku Kashindye wa Chadema akipata kura 23, 260 sawa na asilimia 44.32.

Wagombea hao walifuatiwa kwa mbali na aliyekuwa mgombea wa CUF, Leopald Mahona, ambaye aliambulia kura 2,104. Mahona kwa sasa si mwanachama wa CUF.
Wapigakura walioandikishwa katika jimbo la Igunga ni 171,019, lakini waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo walikuwa 53,692 sawa na asilimia 31.3

Imechapishwa na Mtanzania, Jumanne, Agosti 21, 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO