Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

ZOEZI LA SENSA 2012 UTATA MTUPU

Published by Pamella Mollel on August 27, 2012

RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE AKIWA NA MKEWE MAMA SALMA KIKWETE NA FAMILIA YAKE AKIJIBU MASWALI TOKA KWA KARANI WA  SENSA YA WATU NA MAKAZI BW. CLEMENT NGALABA JUMAPILI 8, 26, 2012

  • WATU WENGI HAWAKO TAYARI KUHESABIWA.
  • UHABA WA VIFAA NA UDHAIFU WA MAKARANI WA KUHESABU WATU WACHANGIA
  • TISHIO LA SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA LAPUUZWA NA WATU WENGI
  • IMANI YA KUFA BAADA YA KUHESABIWA  YATAWALA SEHEMU NYINGI ZA VIJIJINI.
  • WENGINE WASEMA HII NI JANJA YA WAZUNGU KUTUUA KWA VILE CCM WANAHONGEKA.
  • KITENDO CHA BAADHI YA WAJUMBE WA MITAA KUTOLIPWA IMEFANYA KAZI HIYO KUKOSA MSISIMKO, INGAWA BAADHI YA SEHEMU KILA MJUMBE ALILIPWA SH.20,000  NA WENYEVITI SH. 100,000.
  • BAADHI YA WANANCHI WAMELALAMIKA KUPOTEZA MUDA WAO MWINGI KUWASUBIRIA MAKARANI BILA MAFANIKIO.

SENSA ya watu na makazi iliyoanza usiku wa kuamkia Jumapili Agosti 26 2012 nchini kote, imegubikwa na kasoro kadhaa katika maeneo mbalimbali, huku suala la uhaba wa vifaa kwa makarani likionekana kuwa kubwa.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na M2S katika zaidi ya miji mitatu imegundua kuwa watu wengi walikuwa hawajatayarishwa kwa Sensa.

Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal akiangalia ramani ya Tanzania inayoonyesha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya sensa ya watu na makazi huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo ambalo litaendeshwa kwa usiri na kuongeza kuwa takwimu zitakazopatikana zitatumika katika shughuli za maendeleo na si vinginevyo.Picha na Aron Msigwa -MAELEZO

Mapungufu hayo hayakuwa kwa waislamu ambao awali walisikika wakipaza sauti zao waziwazi zikipinga zoezi hilo. Ingawa ni kweli kuna idadi kubwa ya waislamu waliojiandaa kutofanikisha zoezi hilo ila kumejitokeza kundi jingine la watu kutoelewa umuhimu wa zoezi hili ikichanganywa na watu ambao hawakuwa na nia ya kuhesabiwa

Baadhi ya watu waliohojiwa walionyesha kutokujali tishio la serikali la sheria kufuata mkondo wake. Wengi walisikika wakihoji kuwa watawekwa magereza yapi, na watashikwa na askari au hata migambo wangapi? Na watasafirishwa na magari yapi? M2S imegundua kuwa idadi ya watu watakao hesabiwa inaweza kuwa chini ya idadi ya watu walioandikishwa katika kupiga kura katika uchaguzi uliopita, kama watazidi basi watazidi kwa idadi ya watoto wadogo na si watu wazima.

Mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi, akihesabiwa na karani wa sensa Fatuma Kidashari Picha na Nathaniel Limu

Uchunguzi uliofanywa kwa pamoja kati ya blog ya Media2solution na Jamii uligundua kuwa kuna kundi kubwa la watu waliodanganyana kwa kuambiwa kuwa mafisadi wanataka watumie majina kujipatia hela toka kwa wafadhili.Wapo wengine walihoji kama zoezi ni la siku saba kwanini ianze usiku? wengine wakafika mbali kwa kusema kuwa na wezi watatumia njia hiyo hiyo kuwagongea wakijifanya kuwa ni makarani wa sensa.

Wapo watu mjini kabisa wenye imani zao toka vijijini wanaamini kuhesabiwa ni vibaya kwani watakufa.Na kuna wengi wanalalamika kuwa kuhesabu pamoja na mifugo ni dharau, kwamba nao ni wanyama.Wengine wanasema kuwa mifugo yao inahesabiwa ili ije kuchukuliwa na serikali ya mafisadi…

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na mkewe Mama Salma Kikwete na familia yake akijibu maswali toka kwa karani wa sensa ya watu na makazi Bw Clement Ngalaba Jumapili Agosti 26, 2012

Wawakilishi wetu waligundua kuwa vikundi vyenye ushawishi wa kupinga zoezi hili vilikuwa madhubuti na vyenye mbinu mbalimbali kuzidi vile vya serikali.

Igawa watu hao wenye ushawishi na kuaminika katika makundi yao madogo madogo kwenye jamii ya watanzania haikuweza kujulikana mara moja dhamira yao au ni kutokuelewa kwao tu.

Na katika makundi hayo yote kulikuwa na watu ambao waliwaamini hawa watu kama waelewa na kukubalina nao kwani sehemu nyingine walisikika wakichangia kwa kauli kama “mbona zamani hatukuhesabiwa na tuliishi”, wengine wanasema “hii ni janja ya wazungu kutuua kwa vile CCM wanahongeka” na mengine mengi sana.

Hatua hii inatufanya kuamini kuwa serikali haikufanya vizuri sana katika kujihakikishia hadi siku moja kabla watu zaidi  99% wapo tayari na wanafikika, hakuna kiongozi aliyetanguliza mbele uzalendo wake na kujaribu kufuata utaratibu wa zamani ambapo hesabu zote zilifanyika kupitia mabalozi wa nyumba kumi. Nini ilikuwa kasoro ya utaratibu huu? Au ni mbinu za kulipana posho.

DK. BILALI AKIMPOKEA KARANI WA SENSA NYUMBANI KWAKE SIKU YA JUMAPILI AGOSTI 26 2012

Katika maeneo kadhaa, vilionekana vipeperushi kwenye baadhi ya nyumba vyenye ujumbe wa kuwakataza Waislamu wasishiriki shughuli hiyo, jambo lililowalazimu polisi kusambaa mitaani na kuwatia mbaroni baadhi ya watu waliodaiwa kuvisambaza.

Pia, uelewa mdogo wa baadhi ya makarani nao ulilalamikiwa na wananchi wengi, kwani walitumia muda mrefu kuandikisha taarifa zao na huku wakidai kuwa maswali mengine yanayoulizwa kwenye dodoso hizo hayana maana yoyote.

Baadhi ya maandishi yaliyo onekana kwenye nyumba zilizodaiwa kuwa za waislamu

TAARIFA KUTOKA DAR ES SALAAM

Jijini Dar es Salaam, makarani katika baadhi ya maeneo walikwama kupata takwimu za baadhi ya wakazi kutokana na kushikilia msimamo wa viongozi wao wa kiroho wa kususia sensa hiyo.

Moja ya sehemu iliyoathirika ni pamoja na Mtaa wa Kibondemaji wilayani Temeke ambapo baadhi ya waumini wa Kiislamu walipinga waziwazi kuhesabiwa.

Mwenyekiti wa Mtaa huo, Rashidi Mrisho, alisema hadi sasa kumekuwa na upinzani kutoka dhehebu hilo ambapo katika mtaa huo, nyumba zaidi ya 13 zimepinga kuhesabiwa.

Alisema waumini hao, wamedai kuwa shughuli hiyo imekiuka kipengele namba 2.109 hadi 2.111 cha Umoja wa Mataifa, kinachosema takwimu ni lazima ioneshe kila dhehebu kama sehemu inayounda jamii nzima kwa ujumla wake, maelezo mafupi ya waumini wa dini au dhehebu.

DK. BILALI AKIHOJIWA NA MMOJA WA MAKARANI WA KUHESABU SENSA

Aliongeza kuwa, kitendo cha kutowalipa wajumbe wa mitaa, pia ni moja ya changamoto ambayo imeifanya kazi hiyo kukosa msisimko wa kutosha.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Miembeni wilayani Ilala, Saburi Saburi, alisema pamoja na watu wengi kutoa ushirikiano, bado baadhi ya Waislamu wameendeleza msimamo wao wa kupinga kwa madai kuwa wanatii maelekezo ya viongozi wao.

Alisema kuwa, katika mtaa huo inaonesha nyumba zipatazo 30 wakazi wake walipinga mpango huo wa sensa, kwa kutotoa ushirikiano kwa makarani.

Akizungumzia kuhusu malipo ya wajumbe wa mtaa, Saburi alisema tatizo hilo kwake halikuwapo kwa kuwa kila mjumbe alilipwa sh 20,000 ambapo mwenyekiti alilipwa sh 100,000.

Taarifa ambazo hazikuthibitishwa zilesema kuwa majira ya jana jioni kituo cha polisi wilayani Temeke kilivamiwa na baadhi ya wananchi waliokuwa wakidai kupinga kitendo cha wenzao kukamatwa baada ya kugomea sensa.

Tulipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Davis Misime licha ya kukanusha taarifa hizo, alikiri kuwa watu 17 walikamatwa kwa ajili ya mahojiano kwa kugoma kuhesabiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Alisema watu hao ni kutoka maeneo ya Kindungulile kata ya Mianzini, Yombo Kilakala-Barabara ya Mwinyi, Kiburugwa, Kigamboni na Kibada.

HABARI YA ZOEZI LA SENSA YA WATU NA MAKAZI KUTOKA KAGERA

Kutoka mkoani Kagera katika Wilaya ya Biharamulo, makarani 1,999 wameilalamikia kamati ya sensa kwa kuchelewa kuwagawia vifaa vya kazi katika vituo vyao.

Taarifa zinasema, kamati ya sensa wilayani humo, ilishindwa kutoa ushirikiano hali inayoweza kuchangia kutofanikiwa kwa shughuli hiyo licha ya kukaa kwenye vituo vyao kwa muda wa siku tatu kama walivyoagizwa na wasimamizi wao wakisubiri vifaa.

Mmoja wa makarani hao, Paulo Kamihanda kutoka Kata ya Nyarubungo, alisema kuwa vifaa vya kazi zikiwemo sare, kofia pamoja na malipo ya siku ya kwanza na nauli bado hawajapewa.

“Kulingana na jiografia ya Biharamulo ilivyo, mpaka kufikia muda huu hatujakabidhiwa vifaa, unategemea nini? Kama si kukwamisha sensa ni nini?” alihoji.

Aidha, aliyataja baadhi ya maeneo ambayo yamecheleweshewa vifaa hivyo ni pamoja na kata za Nyarubungo, Nemba, Nyantakala na Kalenge.

Mratibu wa sensa wilayani humo, Richard Kalulu alikiri kuwepo kwa ucheleweshaji wa vifaa, akisema vilipokelewa saa 6 usiku wa kuamkia siku ya sensa kutoka Bukoba, hivyo kusababisha uchelewaji huo.

TAARIFA KUTOKA ARUSHA

Mkoani Arusha, baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu waliamua kukesha msikitini kutimiza azma yao ya kutokuhesabiwa kama walivyohamasishwa na viongozi wao.

Wanaodaiwa kukesha msikitini, ni baadhi ya waumini wa Msikiti Mkuu wa Bondeni.

Hata hivyo, Katibu wa Baraza la Waislamu (BAKWATA) mkoani Arusha, Abudulkareem Jonjo, alikiri kupata taarifa za baadhi ya waumini kulala msikitini hapo, hivyo kuwahimiza kuacha msimamo wa kutohesabiwa.

Mratibu wa sensa wa Arusha, Magreth Martin, alisema kuwa mpaka Jumapili Agosti  26 2012 saa kumi jioni, shughuli hiyo ilikuwa ikiendelea vizuri licha ya kuwepo kwa kasoro za upungufu wa vifaa kama vizibao vinavyopaswa kuvaliwa na makarani wa sensa.

Uchuguzi ulifanyika ulibaini kuwa baadhi ya wananchi waligoma kuhesabiwa, hivyo kuwafanya makarani wa sensa kuwa katika wakati mgumu kupata takwimu zao. Hali hiyo ililazimu mratibu wa sensa kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa sensa, Mkuu wa Wilaya, John Mongela na kuitisha kikao cha dharura kushughulikia tatizo hilo haraka.

Mratibu wa sensa, Palangyo, alisema maeneo yaliyokutwa na changamoto hiyo ya mgomo ni kata za Elerai, Ngarenaro, Oysterbay, Engutoto, Sombetini na Unga Limited ambapo wahusika walikataa kuandikishwa bila kutoa sababu zozote.

HABARI YA ZOEZI LA SENSA YA WATU NA MAKAZI KUTOKA GEITA

Mkoani Geita, sensa ya watu na makazi imekumbwa na kadhia mkubwa baada ya vifaa kuchelewa kukabidhiwa kwa makarani, baadhi ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji kususia kushiriki na kucheleweshwa kwa malipo ya makarani.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Elimu, Khasan Mwibara na Khamisi Jagi ambaye ni mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyantorontoro, Kata ya Kalangalala, walisema wameshindwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa makarani hao kutokana na wao kutoshirikishwa katika mchakato mzima tangu awali.

Walidai kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakiwapigia simu tangu kuanza kwa sensa asubuhi baada ya kuwafananisha makarani na vibaka kutokana na kutokuwa na sare, vitambulisho wala kutembezwa na kiongozi yeyote wa kijiji au kitongoji.

Mratibu wa Sensa Mkoa wa Geita, Erasmus Lugarabamu, alikiri shughuli hiyo kukumbwa na changamoto mbalimbali na kudai kuwa hali hiyo ilitokana na serikali kuchelewesha vifaa vilivyohitajika kutoka jijini Dar es Salaam.

Mbali ya changamoto hizo, alisema tayari baadhi ya vifaa vimewasili japo kwa kuchelewa, na kwamba vimegawiwa na kazi inatarajiwa kuendelea vizuri

SOURCE: JAMII BLOG (Pamella Mollel)

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO