Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

SERIKALI YAPEWA SIKU 7 KULIFUNGULIA MwanaHalisi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 22 Agosti 2012

YAH: KUFUNGIWA KWA GAZETI LA MWANAHALISI

KWA mara nyingine tena, tumewaiteni hapa kuwaomba mtufikishie ujumbe wetu huu kwa watawala. Ujumbe wenyewe unahusu kufungiwa kwa gazeti la kila wiki la MwanaHALISI na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda aliyoitoa bungeni, Alhamisi tarehe 16 Agosti 2012. Kama mnakumbuka vema, wakati akijibu swali bungeni siku hiyo, Waziri Mkuu Pinda alisema, “Serikali imechukua wajibu wake kulifungia gazeti hilo, na kwamba kama wahusika hawakuridhika na hatua iliyochukuliwa na serikali wana haki ya kukata rufaa kwa mamlaka za juu.”

Awali ya yote, tuseme wazi, kuwa hatukuridhika na majibu ya Waziri Mkuu kuhusu kufungiwa kwa MwanaHALISI. Majibu ya Waziri mkuu Pinda yamelenga kuahirisha tatizo, siyo kutatua. Kwanza, Waziri Mkuu anatetea uamuzi huo uliofanywa na sheria katili na kandamizi ya magazeti. Sheria inayonyang’anya uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kuwasiliana. Pili, Mheshimiwa Pinda anatumia sheria hiyo kutaka kuliangamiza gazeti hili ambalo limesifiwa kwenye ripoti mbalimbali za ndani na nje ya nchi ikiwamo ile iliyotolewa majuzi na Baraza la Habari Tanzania (MCT) inayochambua Mwenendo wa vyombo vya Habari nchini kwa mwaka 2011 inayosema katika ukurasa wa tisa:

“Pamoja na kusakamwa na serikali, MwanaHALISI limesimamia uandishi wake wa kuikosoa serikali.”

Serikali imelituhumu gazeti hili kwa kuchapisha habari ambazo inasema “zinakiuka” vifungu 32(1) (a), (c) – (d); 32(1)(c) na 36(1) vya Sheria ya Magazeti Na. 3 ya 1976. Habari hiyo inahusu kutekwa, kuteswa kinyama na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande kwa kiongozi wa madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka. Hii ndiyo habari ambayo serikali inaita ya “uchochezi.” Yaani badala ya serikali inayojigamba ina mkono mrefu wa kumfikia yeyote kuutumia mkono huo kutafuta watuhumiwa waliotajwa na gazeti kuwa walifanikisha kutekwa kwa Dk. Ulimboka, imeamua kutumia mabavu kulifungia MwanaHALISI huku wakiacha maisha ya Dk. Ulimboka na wanaharakati wengine njia panda.

Serikali imechukua hatua hiyo, huku wakijua kuwa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Mabadiliko ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (2005), ilipanua haki ya kutoa, kutafuta, kupokea, na kusambaza habari. Mabadiliko hayo yaliondoa kivizo cha “kwa mujibu wa sheria” Kila mtu- anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi; anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.

Aidha, mabadiliko hayo yanatoa haki kwa kila raia ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio muhimu mbalimbali kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii. Hivyo basi haki na uhuru wa kujieleza, kupokea na kutoa habari haina vipingamizi ambavyo serikali inadai kuwamo katika Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976.

Vilevile, kuwekwa kwa Vipengele vya Haki za Msingi na Wajibu wa Mwanadamu (Bill of Rights) katika Katiba ya nchi yetu kulibadilisha sheria zote ambazo zinakiuka haki za binadamu. Vifungu vyote tulivyovitaja hapo juu viliguswa moja kwa moja na Vipengele vya Haki za Msingi na Wajibu wa Mwanadamu. Ibara ya 14 ya Katiba inalinda haki ya kuishi na inaitaka jamii kutoa hifadhi ya maisha kwa kila mtu. Kana kwamba hiyo haitoshi, Ibara ya 26(1) na (2) zinataka kila mtu na serikali kutii Katiba ya nchi na vilevile kuchukua hatua za kuheshimiwa haki na sheria za nchi.

Waziri mkuu anayajua haya vizuri. Anafahamu kuwa sheria iliyotumiwa kufungia gazeti, ni sheria katili na imepitwa na wakati. Kuitumia sheria hii kunaendeleza dhana ya kuwa serikali hii inatumia udhaifu wa Katiba na baadhi ya sheria kukandamiza Haki za Binadamu na Uhuru wa Habari! Mambo haya hayakubaliki.

Kutokana na hali hiyo, sisi watetezi wa haki za binadamu na asasi nyingine za kiraia:

1. Tunarejea wito wetu wa kuitaka serikali kulifungulia mara moja na bila masharti, gazeti hili ambalo limekuwa kipenzi cha wananchi. Tunaitaka serikali ndani ya siku saba (7) kutekeleza hilo kwa kuangalia maslahi mapana ya jamii badala ya kuangalia maslahi ya baadhi ya viongozi wenye maslahi fulani katika kutimiza malengo yao binafsi.

Serikali itekeleze takwa hili haraka iwezekanavyo, na kwamba asasi za kijamii hazikubaliani na kauli ya Waziri Mkuu ya kutaka wahusika waende kwenye vyombo vya juu kwa sababu tatu zifuatazo:

Kwanza, sheria ya magazeti hairuhusu ukataji wa rufaa kwa waziri wa Habari ambaye ndiye aliyetuhumu na kuhukumu gazeti bila kutoa nafasi kwa wahusika kusikilizwa. Pili, Waziri Mkuu Pinda pamoja na sheria hiyo kutomtaja, hakueleza kuwa yuko tayari kupokea malalamiko ya MwanaHALISI. Hivyo kutoelekeza kwake tunakuchukulia kama njia ya kukwepa wajibu wake.

Tatu, hatukubaliani na kauli ya Waziri Mkuu na wengine wanaoitaka MwanaHALISI waende mahakamani kutafuta haki yao kwa kuwa serikali yenyewe haikutumia njia ya mahakama kufungia gazeti. Serikali inataka kuitumia mahakama ili kuchelewesha MwanaHALISI kupata haki yake. Nyote mnajua jinsi mahakama zetu zinavyokabiliwa na gonjwa kubwa la ucheleweshaji wa kesi.

2. Serikali, baadala ya kushughulika na watetezi wa haki na wanahabari wanaofichua uovu, ishughulike na wahalifu waliomteka, kumtesa na hatimaye kumtelekeza Dk. Ulimboka. Ushahidi uliobainishwa na gazeti hili haukuacha shaka yeyote juu ya waliohusika na sakata hili, na kama serikali au watendaji wake waliotajwa (na waliohusishwa) wana mashaka wangetumia ushahidi na taarifa zile kutafuta haki zao: kwanini wasiende mahakamani au wajitokeze na ushahidi wa kukanusha yaliyobainishwa?

3. Serikali iachane kabisa na ukandamizaji huu wa haki na uhuru wa habari. Matendo aliyofanyiwa Ulimboka, habari zilizobainishwa na MwanaHALISI juu ya sakata hili na kufungiwa kwa gazeti hili kunaonesha mtiririko wa matukio ya serikali kuminya uhuru na haki.

Ikumbukwe pia kuwa, Kesi Na. 34/2009 iliyofunguliwa tangu 2009 kupinga sheria ya magazeti ya mwaka 1976 iliyotumika kuwafungia MwanaHALISI haijasikilizwa mpaka sasa. Hii inaenda sambamba na serikali kufumbia macho mahitaji ya sheria ya uhuru wa habari na kudharau mapendekezo ya muswada wa habari tangu 2007 bila kupeleka Bungeni.

Kwa hoja hizo, sisi watetezi wa haki za binadamu, asasi za kijamii na wadau wakuu wa habari nchini, tunaendelea kusisitiza kuwa serikali itimize wajibu wake kwa kulifungulia mara moja gazeti hili na kufanyia kazi yaliyobainishwa. Kama ikishindwa kufanya hivyo, tutaitisha maandamano ya kupinga hatua ya serikali kufungia gazeti hili, kuminya uhuru wa habari, haki za binadamu na uteswaji wa wanaharakati na watetezi wa haki na kwamba tukifika hapo tunawaomba waandishi wa habari mtuunge mkono kwa yafuatayo.

i. Msichapishe habari yoyote inayomhusu Waziri wa Habari, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, na pia Mkurugenzi wa Maelezo. Tunawasihi wahariri wasiwatume waandishi katika Ukumbi wa Habari Maelezo kwa ajili ya kuchukua habari kama ilivyo kawaida na badala yake Watanzania wote wahakikishiwe kupata habari kwa njia nyingine mbadala.

ii. Tunawasihi wadau wote wanaoweza kutuunga mkono mara tutakapohitaji msaada wao ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye maandamano na kupata mawakili ambao watasaidia katika uendeshaji wa shauri letu mahakamani.

iii. Tunawasihi wanaharakati wote wasichoke wala wasirudi nyuma katika azma hii ya kutetea haki, uhuru na ulinzi kwa haki na watetezi wake.

Marcossy Albanie

Mwenyekiti wa Kamati

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO