Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CHADEMA yailiza CCM Igunga • Rais Mkapa, Dk. Magufuli, Wasira waelezwa kumponza Dr Kafumu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimepata pigo jingine baada ya Mahakama Kuu ya Kanda ya Tabora kumvua ubunge, Dk. Peter Kafumu, aliyekuwa Mbunge wa Igunga.

Kafumu ambaye anakuwa mbunge wa kwanza kukaa muda mfupi madarakani, alivuliwa ubunge jana baada ya mahakama kuthibitisha masipo shaka kwamba taratibu za uchaguzi mdogo uliomwingiza madarakani zilikiukwa.

Mlalamikaji katika kesi hiyo alikuwa Joseph Kashindye ambaye alikuwa mgombea wa kiti hicho kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kashinde alifungua kesi dhidi ya Kafumu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo.

Akisoma hukumu ya kesi hiyo katika Mahakama ya Wilaya mjini Nzega jana, Jaji wa Mahakama Kuu, Marry Shangali alitaja vipengele sita alivyotumia kutengua matokeo ya ubunge wa Dk. Kafumu.

Vipengele hivyo ni pamoja na matukio yaliyojitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi huo ambapo ni kutolewa kwa ahadi ya kutojengwa daraja kama hatachaguliwa Kafumu.

Jaji Shangali alisema ahadi hiyo ilikiuka mwenendo wa kampeni za uchaguzi.

Aidha, Jaji Shangali alisema pia kitendo kilichofanywa na upande wa walalamikiwa cha kwenda kutembelea hospitali na kutoa misaada mbalimbali kilikiuka taratibu na hivyo kuathiri zoezi zima la uchaguzi huo.

Kipengele kingine alichokitaja kukiuka taratibu za uchaguzi ni pamoja na kitendo cha ugawaji mahindi ya msaada siku chache kabla ya upigaji kura katika jimbo hilo la Igunga na hivyo kuwafanya wananchi kupiga kura kutokana na ushawishi wa misaada hiyo.

Pia kupanda katika majukwaa ya kampeni kwa Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM) akiwa amening’iniza silaha kiunoni nako kuliathiri mwenendo mzima wa uchaguzi huo.

Kutokana na sababu hizo na maelezo mbalimbali ya upande wa mashahidi wa pande zote mbili, mahakama imeridhia na kuamua kutengua matokeo ya ubunge wa jimbo hilo na kuwataka washtakiwa kulipa gharama zote za kesi hiyo.

CHADEMA katika kesi hiyo iliwakilishwa na mwanasheria Profesa Abdallah Safari.

Wakati wa utetezi wake, Profesa Safari aliwasilisha hoja 15 za kupinga ushindi wa Dk. Kafumu ikiwemo ya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kufanya mkutano wa kampeni katika Kata ya Igulubi wilayani Igunga akitumia madaraka yake kuahidi ujenzi wa Daraja la Mbutu kama wananchi hao watampigia kura Dk. Kafumu.

Pia Safari alidai kuwa waziri huyo aliwatisha wananchi wa kata hiyo kwamba wasipoichagua CCM daraja hilo halitajengwa na kwamba pia watashughulikiwa.

Profesa Safari alidai Baraza la Waislamu (BAKWATA) Wilaya ya Igunga liliwakataza waumini wasiipigie kura CHADEMA na kwamba naye Rais mstaafu, Benjamini Mkapa alitoa ahadi ya kugawa mahindi kwa wananchi wa Igunga siku moja kabla uchaguzi ili waichague CCM.Hukumu hiyo iliamsha shangwe na nderemo kutoka kwa mashabiki wa CHADEMA ambao walifurika mahakamani hapo kusikiliza hukumu hiyo.

Akitoa maoni yake kuhusiana na kuanguka kwake, Dk Kafumu alisema jaji hakuwasikiliza vizuri na alionesha kushangazwa na jinsi alivyokubaliana na hoja za CHADEMA alizodai kuwa zilikuwa za kusadikika.

“Sijapenda sana jambo lilivyotokea huku… wakati wa kampeni tulikuwa tunanadi sera na Ilani ya CCM. Nakubali kwamba kwa sasa mimi sio mbunge, nitaendelea kuwa mtaalamu wa madini kama ilivyokuwa, usiniulize sijaridhika na siwezi kusema sasa hivi, nitachukua hatua gani kiulize Chama Cha Mapinduzi,” alisema Dk. Kafumu.

Hata hivyo alisema hajaridhika na uamuzi huo kwani alishawahi kulalamika kwamba hana imani na jaji tangu mapema kwa sababu alikuwa anaegemea upande mmoja na suala la rufaa alitaka kiulizwe chama chake.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa msimamo wa chama kuhusu hukumu hiyo, alikuwa mbogo na kusema hana taarifa rasmi za CCM kupoteza ubunge katika jimbo hilo.

“Nimesema hivi, taarifa ikishafika tutazungumzia, chama kina mtandao wa kupokea taarifa zake, kama wewe hujanielewa Watanzania wamenielewa, usinilazimishe kusema,” alifoka Nape.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alisema kuwa chama chao kimeweka historia nyingine katika siasa za Tanzania.

Alisema CHADEMA imekuwa ikiwaonya CCM kuacha kutumia mawaziri kutoa ahadi kama za kugawa mahindi na mambo mengine kwani kufanya hivyo ni kinyume na kanuni za uchaguzi.

Alitamba kuwa CHADEMA ina uhakika wa kutwaa jimbo hilo kwani mara ya kwanza CCM walitumia hila kama hizo zilizowaangusha mahakamani.

Katika uchaguzi mdogo uliofanyika katika jimbo hilo, Dk. Kafumu alishinda kwa kupata kura 26,000 dhidi ya mgombea wa CHADEMA aliyepata kura 23,000.

Chanzo: Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO