Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Lema apinga kuvuliwa ubunge kwa hoja 42

na Peter Saramba, Arusha

MAJAJI watatu wa Mahakama ya Rufaa, Natalia Kimaro, Mbarouk Salim Mbarouk na Salum Masati Septemba 20,mwaka huu watapitia kurasa 990 zenye hoja 42 zilizowasilishwa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema kupinga kuvuliwa ubunge.

Awali katika rufaa yake iliyowasilishwa mahakamani kupinga hukumu ya kumvua ubunge iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibarila Aprili 5, mwaka huu, Lema kupitia kwa wakili wake, Method Kimomogoro aliwasilisha kitabu cha rufaa chenye kurasa 985 na hoja 18 zinazoeleza kwanini anapinga hukumu hiyo, kabla ya kuongeza kitabu kingine cha kurasa tano na hoja za ziada 24 Julai 3, mwaka huu.

Pamoja na kubeba kumbukumbu zote za mwenendo wa shauri namba 13/2010 na vielelezo vyote vilivyowasilishwa mahakamani na pande zote mbili za wadai na wadaiwa, kitabu hicho cha kurasa 990 pia kimebeba maelezo ya kina na hoja za kuishawishi mahakama ya rufaa kumpa nafuu Lema kwa kutengua hukumu hiyo.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za kimahakama, tayari walalamikaji Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo wamejibu hoja zote za rufaa kupitia kwa mawakili wao Alute Mughwai na Modest Akida.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Wakili Kimomogoro alithibitisha kukamilisha taratibu zote za kisheria kuhusu rufaa ya mteja wake na kilichosalia ni kusubiri tarehe ya kusikilizwa na uamuzi.

Kwa mujibu wa hati ya rufaa hiyo, hoja ya kwanza hadi nne zinapinga uamuzi wa Jaji Aloyce Mjulizi aliyesikiliza shauri hilo katika hatua za awali kwa kutupa pingamizi za awali zilizowasilishwa na upande wa utetezi kwenye kesi ya madai namba 13 iliyofunguliwa na wapiga kura watatu waliopinga ushindi wa Lema.

Miongoni mwahoja hizo ni kuwa wadai, Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo hawakuwa na haki kisheria kufungua shauri hilo kwa sababu hakuna haki yao iliyovunjwa kisheria kama wapiga kura.

Lema anadai aliyekuwa na haki kisheria kulalamikia kauli na maneno ya kashfa na udhalilishaji anazotuhumiwa kutoa kwenye mikutano yake ya kampeni ni aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Batilda Burian ambaye pamoja na kutajwa na mashahidi wote wa wadai, hakufika mahakamani kuthibitisha madai hayo licha ya umuhimu wa ushahidi wake.

Serikali katika shauri hilo liliwakilishwa na wakili wa serikali, Timon Vitalis na Juma Masanja waliodai aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Batilda Burian ndiye alikuwa na haki kisheria kulalamikia ushindi na maneno ya kashfa yanayodaiwa kutolewa dhidi yake na Lema hoja ambayo Jaji Rwakibarila alitupilia mbali katika hukumu yake iliyozua mjadala baada ya kudaiwa kuvuja kabla ya kusomwa.

Hoja ya tano hadi 18 zinapinga hukumu ya Jaji Rwakibarila ambapo katika suala la hukumu yake kukosa hadhi kisheria, wakili Kimomogoro anadai hakutolea maamuzi athari za wadai kushindwa kuwasilisha mahakamani CD zinazomwonyesha Lema akitoa maneno ya kashfa na udhalilishaji walizodai kuwa nazo katika hati yao ya madai.

Kimomogoro anadai Jaji alikosea kwa kutotumia hata kesi moja kama rejea kati ya kesi kadhaa zilizotajwa na mawakili wa pande zote mbili za wadai na wadaiwa.

Jaji Rwakibarila ambaye ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga pia anadaiwa kukosea kisheria kwa kukubali na kuegemea ushahidi wa mdomo pekee katika hukumu yake bila kuwepo ushahidi wa mazingira, Video wala maandishi kuunga mkono ushahidi wa mdomo.

Mrufani pia anadai Jaji alikosea kwa kutumia viwango na vigezo tofauti kwa mashahidi wa upande wa wadai na utetezi kwa kukataa ushahidi wa Lema na mashahidi wake kwa madai kuwa walikuwa na maslahi kwa sababu ni wanachama na viongozi wa Chadema lakini akaukubali ushahidi wa wadai na mashahidiwao waliothibitika kuwa ni wanachama na viongozi wa CCM kutengua matokea.

Lakini kwa mujibu wa wakili Kimomogoro, Lema na  viongozi wa juu wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, hoja ya msingi iliyofanya wakate rufaa ni kitendo cha Jaji Rwakibarila kutumia kifungu cha 114 cha sheria za uchaguzi kwa kuagiza taarifa za hukumu hiyo kupelekwa kwa Mkurugenzi wa uchaguzi ikimaanisha Lema hataruhusiwa kupiga wala kupigiwa kura kwa kipindi kisichopungua miaka mitano kinyume na makosa aliyoshtakiwa nayo.

Published by Mwananchi on Monday, 20 August 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO