WATANZANIA 27 wakiwamo wanasiasa na wafanyabiashara, imebainika kuwa ndiyo wameficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi, huku mmoja wao akiwa anamiliki Dola za Marekani milioni 56 (sawa na Sh89.6 bilioni).
Katika uchunguzi wake, Mwananchi imebaini pia kuwa kiasi cha fedha kilichothibitishwa kumilikiwa na Watanzania hao ni jumla ya Dola za Marekani 186 milioni (Karibu Sh300 bilioni) kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1600 kwa Dola ya Marekani.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa mbali na kigogo anayemiliki Sh90 bilioni, wapo wengine wanne, ambapo anayefuatia anamiliki Dola 30 milioni (Sh48 bilioni), mwingine Dola 20 milioni (Sh32 bilioni) na wengine wawili kila mmoja anamiliki Dola 10 milioni (Sh16 bilioni).
Kwa kuangalia fedha hizo ni dhahiri kwamba vigogo watano tu kati ya kundi la Watanzania 27, wanamiliki Dola 126 milioni (Sh201.6 bilioni) sawa na asilimia 67.74 ya fedha hizo, wakati wengine 22 waliobaki wanamiliki Dola 60 milioni (Sh96 bilioni) sawa na asilimia 32.25.
Kwa hesabu za kawaida, kiasi cha Sh300 bilioni, kinaweza kugharimia ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya 33,300, ikiwa chumba kimoja kinaghirimu kiasi cha Sh9 milioni.
Read more » kupitia Chadema Blog
Published by Mwananchi on 18th August 2012
0 maoni:
Post a Comment