Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

JK Atuma Salamu Za Rambirambi Msiba Wa Askofu Kikoti

 

-- -----

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kufuatia kifo cha Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Baba Askofu William Pascal Kikoti.

Kifo cha Askofu Kikoti kilitokea jana Jumanne tarehe 28 Agosti, 2012 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mkoani Mwanza alikokuwa amelazwa kwa matibabu kutokana na ugonjwa wa Shinikizo la Damu.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Baba Askofu William Pascal Kikoti wa Jimbo Katoliki la Mpanda akiwa bado na umri mdogo wa miaka 55 wakati ndiyo kwanza utumishi wake ulikuwa ukihitajika zaidi”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake na kuongeza,

“Ni dhahiri kwamba kifo cha Baba Askofu Kikoti kimeacha pengo kubwa la kiuongozi siyo tu kwa Kanisa Katoliki hapa nchini, bali pia Jumuiya ya Waamini wa Kanisa hilo kote duniani”.

Rais Kikwete amesema anatambua jitihada kubwa za Marehemu Baba Askofu William Pascal Kikoti enzi za uhai wake katika kuwatumikia Waumini wa Kanisa lake, na hususan wa Jimbo Katoliki la Mpanda, tangu alipopata Daraja la Upadre mwaka 1988, kuteuliwa kwake kuwa Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Mpanda mwaka 2000, na hatimaye alipowekwa Wakfu na Kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo hilo mwaka 2001.

“Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia wewe Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Salamu zangu za Rambirambi, na kupitia kwako kwa Kanisa Katoliki na kwa Waumini wote wa Kanisa hilo hapa nchini hususan wa Jimbo Katoliki la Mpanda, kwa kumpoteza mmoja wa Viongozi muhimu na wa ngazi ya juu wa kiroho, Marehemu Baba Askofu William Pascal Kikoti”, ameongeza kusema Rais Kikwete.

Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipumzishe mahala pema peponi Roho ya Marehemu. Amewahakikishia wote waliofikwa na msiba huo kuwa yuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo kwa kutambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu.

Dar es Salaam.

29 Agosti, 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO