Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Matonya ombaomba amefariki dunia

 

OMBAOMBA maarufu katika miji ya Dar es Salaam na Morogoro, Matonya. ambaye alikuwa na staili ya aina yake katika uombaji kwa kulala chali huku akishikilia kopo, amefariki dunia jana kijijini kwake Mpamantwa, wilayani Bahi, mkoani Dodoma.

Matonya alianza kuugua kikohozi mwezi Mei mwaka huu na kwa wakati wote hakuwa na msaada wa aina yoyote wa kumfikisha hospitali kutokana na ukata.

Akizungumza na Tanzania Daima mtoto wa nne wa Matonya, David Paulo, alisema kuwa familia haikuwa na uwezo wa kumpeleka baba yao hospitalini kutokana na kukabiliwa na ukosefu wa nauli na fedha za matibabu.

“Hatukuweza kumpeleka kupata vipimo kwani hatukuwa na uwezo wa kwenda mjini Dodoma kutokana na kukosa hata nauli ya kufanya hivyo, ndiyo maana tumekuwa kimya hadi Mungu alipomchukua,’’ alisema Paulo.

Naye Mtoto mkubwa wa marehemu, Elizabeth Paulo, alisema kuwa baba yake hakuacha chochote huku akikanusha uvumi ulioenea kuwa mzee huyo alikuwa na mali nyingi.

Taarifa za kifo cha Matonya zilisambaa jana majira ya asubuhi ambapo ilielezwa kuwa alifia nyumbani kwake Kijiji cha Mpamantwa mahali yalipofanyikia maziko yake.

Umaarufu wa Matonya ulitokana na kupingana na serikali kwa nyakati tofauti ambapo alipinga kurudishwa kijijini kwao na mara kadhaa alimweleza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusufu Makamba, kuwa yeye ni mtoto wa mjini hivyo asingeweza kuondoka.

Matonya ambaye kwa jina la ubatizo anaitwa Paulo Mawezi, alizikwa hatua chache kutoka katika nyumba aliyokuwa akiishi yeye na mkewe wa tatu Paulina Yohana.

Hata hivyo familia ya marehemu Matonya ililazimika kupunguza siku za matanga kutokana na hali duni ya kiuchumi inayoikabili familia hiyo.

Matonya aliingia jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza Desemba 7, mwaka 1961, ambapo alikuwa gumzo kwa serikali na viongozi huku akipachikwa jina la ‘Kiboko ya Makamba.’

Mkoani Morogoro Matonya aliweka kambi katika eneo la Darajani, mahali aliposema kuwa ilikuwa ni makazi mapya yake katika utafutaji wa maisha, na hapo ndipo alipobuni staili yake ya kuomba akiwa amelala chali kwa muda mrefu bila kuchoka.

Mke wa marehemu ambaye alikuwa na mzee huyo hadi kifo chake, Paulina Matonya, alisema kuwa walitengana na Matonya zaidi ya miaka 37 iliyopita na wakati huo alikuwa na mali nyingi (ng’ombe).

“Tulipotengana tu, mimi nilirudi kwetu na watoto wangu walikuwa bado wadogo na bahati mbaya mdogo wake aliyekuwa akiwatunza ng’ombe wa Matonya alifariki duania na huo ukawa ndio mwanzo wa kumaliza mifugo yote kwani watu waliiba yote,’’ alisema Paulina.

Kwa mara ya mwisho, Matonya alirudi kijijini kwake Novemba 2010 akitokea mkoani Morogoro ambapo alikuwa amerudi kwa ajili ya mapumziko ya mwishoni mwa mwaka na Sikukuu ya Krismasi na hiyo ilikuwa ni kawaida yake.

Matonya ambaye hadi jana umri wake ulikuwa ni wa kukisiwa, ameacha mjane na watoto watano, wakiwamo wajukuu tisa huku nyumba yake ndogo ya tembe ikikosa hata kuku wa kufugwa.

Habari na Tanzania Daima, 25 August 2012. Picha za maktaba vyanzo tofauti

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO