Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CHADEMA yafunika Igunga, Mamia wajitokeza kuiaga CCM

 

Dr Slaa Igunga 2012Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr Wilbroad Slaa akihutubia wananchi wa Igunga jana.

*****

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana kimeutikisa mji wa Igunga na vitongoji vyake katika mkutano mkubwa wa hadhara kusherehekea kushinda kesi ya uchaguzi, huku Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa akiwatakia mahasimu wao, CCM ‘wafanye kosa la heri kukata rufaa’ ya kesi hiyo.

Akihutubia maelfu ya wakazi wa mji huo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Dk. Slaa, alisema ameshangazwa na kauli ya CCM ya kutaka kukata rufaa katika kesi hiyo wakati kisheria na kwa kesi za uchaguzi chama hakina nafasi yoyote bali mgombea au mwanachama wa chama husika, ndiye anaweza kwenda mahakamani kufungua kesi na kupinga.

Alisema kuwa katika suala la wananchi wa Igunga kupata mbunge wao, CCM na serikali yake hawana chaguo la kuweza kuwaponya, akijigamba kuwa hata uchaguzi ukirudiwa chama chake kitashinda ‘saa nne asubuhi’.

“Juzi nasoma, CCM wanasema watakata rufaa, nami ninasema ninawaombea wafanye kosa hilo la heri la kukata rufaa, ingawa kauli hiyo pia imenifanya niwashangae zaidi CCM kama kweli wanajua sheria au wanazidi kudhihirisha umbumbumbu wao, katika kesi za uchaguzi chama hakina nafasi yoyote, bali mgombea au mpiga kura, chama hakina nafasi katika hili, sasa wao wanasema wanataka kukata rufaa sijui kwa sheria ipi.

“Lakini kama nilivyosema mapema, ninawaombea CCM wafanye kosa hilo la heri la kukata rufaa, kwa sababu wakikata rufaa, wanasheria wetu watafanya kitu ambacho kisheria kinaitwa cross appeal, yaani tutaiomba Mahakama ya Rufaa sasa itazame tena na kuzingatia masuala ya muhimu ambayo hayakuzingatiwa katika hukumu ya Mahakama Kuu juzi. Hapo tutawakamata CCM na makosa ya rushwa.

“Kwanza sijui kama rufaa yenyewe watafanikiwa kwani nani hajui kuwa Magufuli alitamka maneno juu ya daraja la Mbutu, nani hajui kuwa Rage alikuwa na silaha jukwaani na siku moja kabla na siku yenyewe ya uchaguzi alipita mitaani akiwatangazia wananchi kuwa mgombea wetu amejitoa, nani hajui kuwa waligawa mahindi kupitia matawi ya CCM wakisema kuwa ni msaada wa serikali, nani hajui kuwa Mkama aliwatisha wananchi kuwa CHADEMA imeingiza makomandoo?” alihoji.

“Sasa mpaka hapo hawana pa kupita, lakini wakiamua kukata sasa tutaiomba mahakama izingatie pia masuala ya rushwa waliyofanya wakati wa kampeni za uchaguzi Igunga, wataona jinsi tutakavyowang’ang’ania kooni kwa ushahidi wa rushwa waliyokuwa wakitoa wakati wa uchaguzi huo, ndiyo maana nasema ninaomba sana wafanye kosa hilo la heri.”

Dk. Slaa alisema kuwa siku ya jana ilikuwa ni kwa ajili ya wananchi wa Igunga kusherehekea na kupongezana kwa mshikamano waliouonesha wakati wote wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Suala la silaha

Akizungumzia tuhuma za CCM kuingiza silaha nchini bila kibali wala leseni, kisha kuwapatia vijana wake kwa ajili ya kuteka, kutesa na hata kuua watu, walengwa wakubwa wakiwa ni makada wa CHADEMA, Dk. Slaa alisema kuwa suala hilo si maneno matupu wala propaganda kama ambavyo polisi na chama hicho wanataka kuligeuza.

Alisisitiza kuwa CCM waliingiza silaha ndani ya nchi, na kuwapatia vijana wake katika makambi ya Ilemo yaliyopo Iramba mkoani Singida, katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo uliofanyika mwaka jana.

Alibainisha kuwa vijana hao walikuwa wakipewa mafunzo ya kijeshi na jambo hilo linamhusu Mwenyekiti wa chama hicho na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete hivyo si sahihi mtu mwingine kulitolea majibu au ufafanuzi.

Alisema kuwa wakati wa uchaguzi wa Igunga walitoa taarifa polisi kuwa CCM kimeweka vijana wake katika makambi, ikiwemo kambi ya Ilemo, wilayani Iramba, Singida ambapo walikuwa wakipewa mafunzo ya kijeshi.

“Suala hili si suala la propaganda, maana juzi nimemsikia vuvuzela wao ambaye mimi wala si saizi yangu, siwezi hata kumtaja wala kumjibu akiropoka, anafikiri wote tunafanya propaganda, suala hili la CCM kuingiza silaha nchini bila kibali wala leseni na kuweka vijana kwenye makambi linamhusu Kikwete kama mwenyekiti na kama Amiri Jeshi Mkuu, tunamtaka atupatie majibu.

“Upo ushahidi mpaka wa picha ukiwaonesha vijana wale wakiwa makambini, pia walipokuja hapa kumpokea Mkapa wakati wa uzinduzi wa kampeni.

“Nimekwenda mbali zaidi na kutoa mfano wa silaha iliyoingizwa bila kibali wala leseni, nimetaja namba yake kuwa ni J137, iliyotengenezwa China yenye uwezo wa kubeba risasi 8 kwenye magazine, na nimesema kuwa nitatoa nyaraka zingine katika wakati mwingine utakaofaa kadri mambo yanavyozidi kwenda. Namtaka Kikwete atuambie mambo haya yanafanyika yeye akiwa wapi kama hayana ruhusa yake?

“Na katika hili sitahojiwa mpaka Katibu Mkuu wa CCM, Mkama ahojiwe juu ya kauli zake kuwa CHADEMA kimeingiza makomandoo ndani ya nchi kutoka nje. Maana wakati ule nilimjibu tu kuwa kama kweli tumeingiza wakati serikali yao ndiyo yenye jeshi, polisi, usalama wa taifa na uhamiaji, lakini hawana uthibitisho wala hawajatukamata basi atangaze serikali yao imeshindwa watukabidhi sisi vidume,” alisema.

Kashindye

Dr Slaa Igunga 2012 2Naye aliyekuwa mgombea ubunge wa CHADEMA katika uchaguzi wa Igunga uliofanyika Oktoba 2, mwaka jana, Joseph Kashindye, aliwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa mshikamano wao waliompatia wakati wote wa kupigania haki iliyopatikana mahakamani wiki iliyopita baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kubatilisha matokeo ya uchaguzi yaliyompatia ushindi aliyekuwa Mbunge, Dalali Kafumu.

“Nawashukuru wote tulioshikamana wakati wote wa kesi, wale wote Watanzania maskini wa Igunga waliodhihirisha nguvu ya CHADEMA ni umma, waliochangia shilingi moja moja mpaka tukafikisha milioni 6 kuniwezesha mimi kukaa kule bila tatizo, fedha ambazo ndizo zilisaidia kuwasafirisha mashahidi kutoka maeneo mbalimbali ya Igunga kwenda kwenye kesi. Yote haya yaliwezekana kwa sababu ya uchungu wa wananchi kupigania haki yao.

“Wakati chama kinaniambia nifungue kesi, nilisita sana kuwa sina kitu mfukoni, lakini kikaniambia wewe fungua kesi, hii siyo kesi yako ni kesi ya wananchi wa Igunga, ni kesi ya chama. Pia nawapeni pole sana kwa kunitafuta tangu siku ya hukumu, najua hamkunipata.

“Wakati mnanitafuta kwa heri kuna wengine walikuwa wananitafuta kwa shari, kuna watu wajinga wanafikiri Kashindye akiondoka kwenda kuzimu au kuhama watachukua jimbo, nawaambia mimi ni kama nyasi moja kwenye nyumba, ukiiondoa nyumba haiwezi kuvuja,” alisema Kashindye.

Mkutano huo wa CHADEMA ulihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wa Tabora, Kansa Mbarouk na Mwenyekiti wa Mkoa wa Morogoro, Suzan Kiwanga. Wabunge waliohudhuria walikuwa ni Raaya Khamis Ibrahim na Mchungaji Israel Natse

Chanzo cha habari: Tanzania Daima, 26 Auust 2012; Picha na Chadema Blog

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO