Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Chenge kumtetea Mramba kortini

ALIYEKUWA Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, ni miongoni mwa mashahidi watakaomteteta aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba (71) na wenzake wawili wanaokabiliwa na kesi ya kutumia madaraka vibaya na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 kupitia msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart ya nchini Uingereza.

Hayo yalibainika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati Mramba akitoa utetezi wake mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, John Utamwa.

Alidai jumla ya mashahidi tisa watafika mahakamani kumteteta na kwamba watatu kati ya hao watatoa ushahidi wao kwa maandishi.

Aliwataja mashahidi wengine kuwa ni Mwakilishi kutoka Kampuni ya Alex Stewart, N. Florence, Gavana wa Benki Kuu kwa wakati huo, Daudi Balali au mwakilishi wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha za Serikali, John Cheyo, mtaalamu wa ushauri wa masuala ya kodi, Flavia Busigara na mmoja ambaye alidai kutokuwa na uhakika kama atakuja au la.

Awali, akitoa utetezi wake, huku akiongozwa na wakili wake, Herbert Nyange, Mramba ambaye ni mtuhumiwa wa kwanza katika kesi hiyo, alidai chimbuko la kesi hiyo ni malalamiko ya wananchi na vyombo vya habari walipokuwa wakihoji masuala mbalimbali hasa kuhusu Tanzania kutonufaika na migodi kutokana na uuzaji wa dhahabu nje ya nchi kutofanyika sawa sawa.

Sehemu ya mahojiano kati ya Wakili Nyange na Mramba yalikuwa kama ifuatavyo:

Nyange: Tatizo la kosa hili limeanzia wapi?

Mramba: Ni kutokana na makosa yaliyofanyika pindi nilipokuwa Waziri wa Fedha, kutokana na kusamehe kodi kwa kampuni iliyoletwa nchini kufanya ukaguzi wa migodi.

Nyange: Nani alikuwa mhusika wa kuiingiza nchini kampuni hiyo kufanya kazi?

Mramba: Kazi hiyo ilifanywa na Benki Kuu, ndiyo iliyotakiwa kumchagua mkandarasi, ili kufanya kazi kwa niaba ya serikali.

Nyange: Ni nani aliyeagiza Benki Kuu kufanya kazi hiyo?

Mramba: Iliagizwa na Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa.

Nyange: Waziri wa Fedha alipewa nafasi gani ya udhibiti katika suala hilo?

Mramba: Niliagizwa na Mkapa kwamba gharama za kumlipa mwekezaji huyo zitapatikana, iwe ndani ya serikali au Benki Kuu au katika sehemu zote mbili.

Nyange: Hilo neno la kumtafuta mkaguzi kwa Kiingereza linaitwaje?

Mramba: Procurement

Nyange: Nani alikuwa na mamlaka ya kufanya procurement?

Mramba: Gavana wa Benki Kuu

Nyange: Katika zoezi hilo lililofanywa na gavana wewe ulihusika vipi?

Mramba: Sikuhusika na zoezi hilo bali kazi niliyopewa na Rais Mkapa ni kuhakikisha analipwa.

Nyange: Katika ushahidi uliowahi kutolewa hapa mahakamani ilielezwa kuwa kulikuwa na mnyororo wa kumtafuta mwekezaji, wewe ulihusika vipi?

Mramba: Sikuhusika na wala sikumwambia mtu yeyote kwenda kumtafuta mwekezaji.

Nyange: Kamati iliyomtafuta mkandarasi walitumia njia gani?

Mramba: Hilo nilikuja kufahamu baadaye kwamba walifanya ushindani, walitumia mitandao wakapata kampuni mbili na wakasainiana mkataba na kampuni moja ya Stewart.

Nyange: Hebu iambie mahakama ulikuwa na input gani?

Mramba: Mimi kama waziri kupitia katibu mkuu tulituma ofisa mmoja kutoka wizarani ambaye alikwenda kujadili mkataba na alikuwa mwanasheria.

Nyange: Unamkumbuka Soka na alikuwa na mamkala gani?

Mramba: Namkumbuka, aliombwa ashughulikie ule msamaha wa kodi naye alifanya hivyo.

Baada ya Mramba kueleza alituma mwanasheria kutoka wizarani wakati awali alikana kutuma mwakilishi, Wakili Nyange aliomba ruhusa kwa jaji kwenda kuteta na mteja wake na baada ya dakika 20 wakili Kiongozi wa Serikali, Frederick Manyanda alieleza kutokubaliana na tukio hilo.

Hata hivyo, alipotaka kusahihisha kauli hiyo, alisikika kurudia kauli kuwa alituma mwakilishi.

Nyange: Mkataba ulisainiwa na nani?

Mramba: Gavana Daudi Balali pamoja na Mkuu wa Kampuni ya Alex Stewart, Elvin Frolence.

Nyange: Balali alisaini kwa mamlaka gani?

Mramba: Kwa maagizo ya Rais Mkapa.

Pamoja na hayo, Mramba alidai aliwahi kumshauri Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo, kwa kumwandikia barua kabla hata ya kusainiwa mkataba na kuiomba mahakama kupokea barua hiyo kama kielelezo.

Hata hivyo, barua hiyo ilizua mvutano kisheria baada ya wakili wa serikali, Manyanda kupinga barua hiyo kupokewa kwa kuwa si halisi (original) na kwamba haijagongwa mhuri wa serikali ilipotoka.

Wakili Nyange alidai kuwa waliomba barua halisi muda mrefu, lakini serikali haijawapatia, hivyo kuomba mahakama kuipokea.

Kutokana na mvutano huo, Jaji Utamwa alisema leo atatoa uamuzi iwapo barua hiyo ipokewe ama la.

Katika kesi hiyo, mbali na Mramba, washitakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja

Source: Tanzania Daima, 23 August 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO