Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CHADEMA: TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAUAJI YA MOROGORO

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapinga kauli za Serikali, Jeshi la Polisi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zenye kulipotosha taifa kuhusu mashambulizi na mauji yanayoelezwa kufanywa na askari Mkoani Morogoro na badala yake kinataka uchunguzi huru ufanyike haraka kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act).

Kauli zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani zina mwelekeo wa kulilinda Jeshi la Polisi ambalo askari na maofisa wake ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji, badala ya kuwezesha ukweli kuthibitika na hatua kuchukuliwa kwa wahusika.

Hivyo kutokana na kujirudiarudia kwa mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola CHADEMA kinatoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye kwa mujibu wa katiba ibara ya 33 ni mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu aingilie na kuwezesha uchunguzi wa kina.

Ikumbukwe kwamba tarehe 27 Agosti 2012 Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro lilifyatua risasi za moto na kupiga mabomu ya machozi wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamejikusanya kwa ajili ya kuelekea kwenye mkutano halali wa CHADEMA na wengine waliokuwa wakiendelea na shughuli zao eneo la Msamvu, hivyo kusababisha kifo cha raia mmoja asiye na hatia na kujeruhi wengine wawili.

CHADEMA kinaukumbusha umma kwamba kwa mauaji hayo na mengine katika maeneo mbalimbali nchini serikali inayoongozwa na CCM kupitia vyombo vya dola inaendelea kukiuka Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua kwamba uhai ni haki ya msingi kwa raia wote.

CHADEMA hakikubaliani na hatua zilizochukuliwa na Serikali mpaka sasa kuhusu tukio husika pamoja na maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani tarehe 28 Agosti 2012 ambayo kwa sehemu kubwa yametokana na taarifa zisizo za kweli kutoka kwa maofisa wa Jeshi la Polisi ambao ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji husika.

CHADEMA haina imani na timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi kuchunguza tuhuma za askari kufyatua risasi na mabomu ya machozi na kusababisha mauaji kwa kuwa tayari serikali na Jeshi la Polisi wametoa maelezo yenye kutofautiana kwa kiwango kikubwa na maelezo ya mashuhuda waliokuwepo na ushahidi wa picha za eneo la tukio.

Wakati Serikali na Jeshi la Polisi wakitoa maelezo kuwa marehemu alikutwa umbali wa mita 300 na kupelekwa hospitali na wasamaria wema, mashuhuda wameeleza wazi kuwa askari walifika jirani na eneo lake na ofisa mmoja akaonyesha ishara na ndipo risasi za moto na mabomu ya machozi yakafyatuliwa mojawapo kumpata marehemu na kudondoka.

Mashuhuda wote waliohojiwa wanaeleza kwamba bunduki ya polisi ndiyo ilielekezwa na kufyatuliwa kwa marehemu, maelezo pekee yanayotofautiana ni kuwa baadhi wameeleza kuwa ni bunduki ya risasi za moto na wengine wa wameeleza kuwa ni bunduki ya kufyatulia mabomu ya machozi.

Mara baada ya kudondoka gari hilo liliondoka na gari lingine la polisi lilifika likiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia cha Mkoa ambaye alitoa amri ya gari lingine kumbeba Ali Hassan Singano (Zona) na kuondoka naye, hivyo si kweli kwamba matukio hayo yalitokea mbali na eneo bali pembeni ya meza ya muuza magazeti huyo karibu na barabara ya kwenda Iringa eneo ambalo polisi ilikuwa ikifanya mashambulizi.

Kauli zilizotolewa na Serikali kuwa Jeshi la Polisi lilizuia maandamano ya CHADEMA yaliyopangwa kufanyika Mkoani Morogoro kwa sababu ya sensa ya watu na makazi si za kweli kwa kuwa sababu pekee zilizotolewa ni ufinyu wa barabara na kuwa maandamano yalipangwa siku ya kazi. Ushahidi wa suala hili ni barua ya Jeshi la Polisi lenyewe ya 23 Agosti 2012 yenye Kumb. Na. MOR/A.25/1/VOL. II/202.

CHADEMA kinaujulisha umma kwamba Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro ndilo lililoacha kuheshimu utawala wa sheria na makubaliano yaliyofikiwa baada ya mazungumzo yaliyohusisha kikosi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kikiongozwa na Kamanda wa Operesheni za Jeshi hilo Simon Siro na hivyo kuwa chanzo cha mauaji yaliyotokea na madhara mengine kwa wananchi waliokuwepo maeneo yaliyorushiwa mabomu ya machozi.

Ikumbukwe kwamba awali CHADEMA kilipanga kufanya maandamano na mikutano katika Jimbo la Morogoro Mjini tarehe 4 Agosti 2012 na kuwasilisha taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Polisi wakakataa kufanyika kwa maandamano na mikutano kwa kisingizio cha Sikukuu ya Nanenane, mgomo wa walimu na ratiba kugongana na ile ya mikutano ya CCM, sababu ambazo zilibainika kwamba hazikuwa na msingi wowote.

Baada ya mvutano na mazungumzo CHADEMA ilikubali kutii sheria na kuzingatia matakwa ya Jeshi la Polisi pamoja na kuwa yalitolewa kinyume cha Sheria kwamba maandamano na mkutano wa CHADEMA vifanyike mara baada ya siku ya kuanza kwa sensa tarehe 26 Agosti 2012 na CHADEMA ilipendekeza tarehe 27 Agosti 2012 ambayo Jeshi la Polisi liliikubali.

Polisi walifanya hivyo wakielewa ukubwa wa barabara za Morogoro na pia wakitambua kwamba ilikuwa ni siku ya kazi, hata hivyo tarehe 23 Agosti 2012 Jeshi la Polisi liliandika barua ya kueleza kwamba limetoa kibali cha mkutano (suala ambalo si mamlaka yake kisheria) na pia limekataza maandamano.

CHADEMA kikaamua kwa mara nyingine tena kurudi katika meza ya mazungumzo na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, tarehe 24 Agosti 2012 ambapo polisi ilikubali maandamano ikiwemo ya watembea kwa miguu na kupendekeza njia mbadala na tarehe 26 Agosti 2012 mazungumzo yakaendelea kwa lengo la kukagua barabara.

Hata hivyo, kufuatia shinikizo la Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile kinyume na Sheria ya Jeshi la Polisi ambayo imetoa mamlaka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya kuhusu taarifa za mikutano, polisi ikarejea katika msimamo wa kukataza mapokezi ya watembea kwa miguu na badala yake tarehe 26 Agosti 2012 bila sababu za misingi ya kisheria na zisizozingatia haki za kikatiba ikapendekeza kwamba yafanyike mapokezi kwa kutumia magari.

Maelezo ya Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa iwapo vyama vya siasa visiporidhika na mazingira kama hayo yapo mamlaka ya kukata rufaa yanapotosha kwa kuwa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa hazijaweka utaratibu wa rufaa hivyo njia pekee ya kisheria ni kutumia mahakama.

Jeshi la Polisi lingeheshimu utawala wa sheria na mazungumzo lingeruhusu CHADEMA ifanye maandamano na kutoa ulinzi mpaka eneo la mkutano kwa muda mfupi badala yake jeshi hilo likaamua kutumia nguvu kubwa na kusababisha mauaji, barabara kufungwa kwa muda mrefu na kuathiri wananchi waliokuwa wakiendelea na kazi zao.

Iwapo wanachama na wananchi waliokuwa wamekusanyika kuwapokea viongozi na kuelekea kwenye mkutano wangekuwa wamekiuka sheria Jeshi la Polisi lingeweza kuwakamata kwa mujibu wa sheria, hata hivyo hakuna kiongozi yoyote wa CHADEMA aliyefunguliwa jalada mpaka sasa katika kituo chochote cha polisi kwa kudaiwa kukiuka sheria.

Kinyume chake Jeshi la Polisi ambalo likiwa kwenye mazungumzo lilikubali kuwa mapokezi yafanyike kwa msafara wa vyombo vya moto, lakini tarehe 27 Agosti 2012 likaamua kupiga mabomu ya machozi kwa wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamekusanyika eneo la Msamvu wakiwasubiri viongozi bila hata ya kusubiri kuona iwapo yangefanyika matembezi ya miguu kuelekea eneo la mkutano au maandamano ya magari na vyombo vingine vya usafiri.

Kitendo cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa kinyume cha sheria na kusababisha mauaji na kufunga barabara kwa muda mrefu kiliwafanya wanachama wa CHADEMA na wananchi kwa ujumla kutawanyika kuelekea eneo la mkutano na wengine kuingia barabarani kutembea kuelekea eneo la mkutano na hatimaye polisi walipoona wamesababisha hali hiyo wakaamua kulinda misafara hiyo mpaka eneo la mkutano hali inayodhihirisha kuwa uamuzi kama huo ungechukuliwa kutoka mwanzo yasingetokea madhara yoyote.

Kwa kuzingatia utofauti mkubwa baina ya maelezo yanayotolewa na Serikali na Jeshi la Polisi kuhusu matukio husika na ukweli halisi ulivyotokea, CHADEMA kinasisitiza kuwauchunguzi huru ufanyike kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania.

CHADEMA kwa mara nyingine kinaitaka Serikali inayoongozwa na CCM kurejea katika kifungu cha 3 cha Sheria ya Uchunguzi wa Vifo, ambacho kinatoa mamlaka ya Waziri mwenye dhamana na masuala ya Sheria kuanzisha Mahakama ya Kuchunguza Vifo hivyo (Coroner’s Court) katika maeneo ya serikali za mitaa kwa kushirikiana na Jaji Kiongozi.

CHADEMA kinaikumbusha Serikali kuwa, kufuatia kauli ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mawaziri Vivuli husika kueleza bungeni taarifa za mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola kwa nyakati mbalimbali, Waziri Mkuu na Mawaziri wengine waliahidi bungeni kwamba sheria hiyo itaanza kutumika kuchunguza vifo vyenye utata.

Katika muktadha huo uchunguzi wa kifo cha Ali Zona haupaswi kufanywa na timu ya polisi bali sheria hiyo sasa ianze kutumika.

Kwa upande mwingine, CHADEMA imeheshimu taratibu za maziko zilizopangwa na familia ambapo mwili wa marehemu ulisafirishwa jana tarehe 28 Agosti 2012 kwenda Mkoani Tanga kwa ajili ya maziko na CHADEMA kuwasilisha rambirambi zake za awali, taarifa zaidi kuhusu ushiriki kwa CHADEMA kwenye maziko zitaelezwa baada ya majadiliano yanayoendelea na familia.

CHADEMA kwa kuheshimu mazungumzo na utawala wa sheria kwa mara nyingine tena tarehe 28 Agosti 2012 CHADEMA kimesitisha Operesheni za Maandamano na Mikutano yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa rai iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ili kupisha kukamilika kwa zoezi la sensa ambayo imetokana pia na maelezo ya mamlaka zingine za kiserikali.

CHADEMA inatambua kwamba wakati maandamano ya CHADEMA yametolewa rai kuwa yasitishwe kupisha sensa, maandamano ya wagombea wa CCM kurudisha fomu za uchaguzi wa ndani ya chama chao yameachwa yakiendelea katika barabara kadhaa nchini bila kusitishwa kwa kisingizio hicho.

Aidha, wakati CHADEMA ikiheshimu mazungumzo na kusogeza ratiba yake mbele ya tarehe 26 Agosti 2012 mpaka tarehe 27 Agosti 2012 kupisha sensa hatua ambayo ilifanywa pia na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilitangaza ratiba yake kuendelea baaada ya tarehe hiyo.

Tume hiyo inaendelea na mikutano yake ya hadhara inayokutanisha wananchi katika kata za mikoa mbalimbali wakati huo huo zoezi la sensa likiendelea lakini kwa mikutano ya CHADEMA inaonekana kufanyika kwake ni kuingilia sensa.

CHADEMA inataka Serikali na Polisi kueleza iwapo matukio haya na mengine hayana mwelekeo wa ubaguzi na uhujumu wa vuguvuvugu la mabadiliko linaloendelea nchini kwa kurejea ukweli kuwa maisha ya wachache yanaweza kuwekwa mashakani lakini si mabadiliko kwa maslahi ya wengi.

CHADEMA itaeleza hatua za ziada itakazochukua baada ya kupata ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu (post mortem) uliofanyika tarehe 28 Agosti 2012 na uamuzi wa Serikali kukubali au kukataa mwito wa kutumia Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) kuwezesha uchunguzi huru.

Imetolewa tarehe 29 Agosti 2012 na:

John Mnyika (Mb)

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO