Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

M4C yaitisha CCM; Nape akerwa na mabilioni yanayochangishwa na CHADEMA

 

 

VUGUVUGU la Mabadiliko (M4C) linaloendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limeanza kukitia kiwewe Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimesema hakiamini kwamba Watanzania ndio wanaochanga mamilioni katika mikutano na harambee za CHADEMA.

Vuguvugu hilo linaifanya CHADEMA kuwa chama kiongozi, kwa kuifanya CCM kufuatilia nyendo zake na kujaribu kufuta nyao kwa propaganda zinazoonesha hofu inayokipata chama tawala.

Baada ya vijana wa CHADEMA kuandaa hafla ya kuchangia chama hicho juzi Dar es Salaam na kupata zaidi ya Sh 500 milioni (fedha taslimu na ahadi), jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliibuka na kudai mabilioni ya CHADEMA hayachangwi na wapenzi wake bali wafadhili kutoka nje ya nchi.

Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Nape alidai kuwa CHADEMA kinaandaa harambee kama njia ya kuhalalisha mabilioni waliyopewa na wafadhili wao kutoka nje ya nchi.

Nape, ambaye katika siku za karibuni amekuwa akieneza propaganda dhidi ya CHADEMA alisema: “Umekuwa utamaduni wa CHADEMA kuwahadaa watu kwa kuitisha harambee za kisanii baada ya kupewa mabilioni na wafadhili wao, ili mradi wahalalishe kuwa fedha wanazotumia zimetokana na michango ya Watanzania wakati sikweli.”

Alisema kuwa, CCM wana ushahidi wa kutosha unaoonesha mabilioni waliyopewa CHADEMA juzi na wafadhili hao kwa lengo la kuendeleza operesheni mbalimbali nchini.

“Cha kushangaza badala ya kuwaambia wanachama wao na Watanzania ukweli wa haya mabilioni, wanaanza kuwahadaa kwa kuwachangisha na kugeuza mapato haya mtaji wa baadhi ya watu binafsi ndani ya chama,” alisema Nnauye.

Alihoji kuwa kwa nini mabilioni haya yanatolewa kwa CHADEMA sasa ambapo nchi yetu imeendelea kufanya utafiti na ugunduzi wa rasilimali mbalimbali zikiwemo gesi na mafuta?

Nape aliongeza kuwa, iwapo CHADEMA hawatawaeleza ukweli wananchi, CCM itawasidia kuwaeleza ukweli wa kiasi halisi cha mabilioni hayo, walikozitoa na mikataba waliyoingia.

Nape anasema hayo huku akijua kuwa baadhi ya wanachama waandamizi wa CCM, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, wamekuwa wakichangisha mamilioni ya shilingi katika harambee mbalimbali za kisiasa na kidini, kutoka kwa wananchi maskini na matajiri wa Kitanzania.

Hata hivyo, Mkurugenzi wake wa Habari na Uenezi, John Mnyika, alisema kauli ya CCM ni kiwewe kinachotokana na nguvu ya M4C.

“Propaganda chafu hizi ni ishara ya kwamba CCM inaumizwa na namna ambavyo Watanzania wanajitokeza kuunga mkono CHADEMA kwa hali na mali; CCM sasa inatapatapa kujaribu kudhibiti wimbi la mabadiliko kwa kutumia siasa chafu,” alisema.

Mnyika alisema CCM wanapaswa kueleza Watanzania iwapo mikakati hiyo michafu ina baraka za mwenyekiti wao na serikali yake, kwani madai kama hayo yaliyotolewa na Waziri wa Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, kuwa CHADEMA itasambaratishwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa mbinu mbalimbali.

Aliongeza kuwa, CCM imekuwa ikipata fedha za uchaguzi kwa njia za kifisadi, na sasa wanataka kuichafua CHADEMA inayopata fedha kutoka vyanzo halali kwa njia za wazi, na kwamba lengo la CCM ni kukatisha tamaa umma wa Watanzania unaochangia vuguvugu la mabadiliko.

“Ni ukweli ulio wazi kwamba CHADEMA imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati mbalimbali katika kumbi na katika mikutano ya hadhara, ikiwemo ya vijijini ambapo michango hutolewa kwa uwazi… Aidha michango kwa njia ya simu inaweza kufuatiliwa na kuthibitisha bila shaka yoyote,” alisema.

Mnyika alisisitiza kuwa, madai ya CCM kuwa CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni ya shilingi kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi, na akarudia kukitaka chama hicho kitaje majina ya serikali, taasisi ama kampuni za nje ambazo kinadai kwamba zimetoa mabilioni ya shilingi katika siku za karibuni au zinatarajia kutoa.

“Badala ya CCM kuisingizia CHADEMA, ilipaswa ieleze Watanzania orodha ya vigogo wa serikali na wanachama waandamizi wa chama hicho, ambao wanaelezwa kuwa na akaunti nchini Uswisi na nchi nyingine, wakituhumiwa kupewa fedha za kifisadi kutoka kwa makampuni ya utafutaji wa mafuta, gesi asili pamoja na uchimbaji wa madini.

“Madai haya si mapya kutolewa na CCM, yaliwahi kutolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 akidai kuwa CHADEMA imepokea fedha kutoka mataifa ya Ulaya kwa ajili ya kufanya maandamano ya kuiondoa CCM madarakani, lakini akashindwa kuthibitisha,” alisema

Chanzo: Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO