Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Makala: Ujio wa FBI, Usalama wa Taifa Utakuwaje salama?

 

UJIO wa wapelelezi kutoka Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kusaidia uchunguzi au upelelezi katika tukio la shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Olasiti, jijini Arusha, pamoja na matukio ya kigaidi Zanzibar, kwa upande wangu, ni wa kutafakari upya mwelekeo wetu kiusalama nchini.

Msaada wa kiusalama ni muhimu, lakini hata hivyo suala muhimu zaidi ni kwa namna gani unadhibiti nafasi yako ndani ya msaada husika. Kwa lugha nyingine, unachukua hadhari gani wakati wa operesheni za msaada husika wa kiusalama?

Historia ya FBI ni ndefu, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1908 (miaka 105 sasa) kwa wakati huo kikiitwa kitengo cha uchunguzi (Bureau of Investigation - BOI) na baadaye mwaka 1935 kubadilishwa jina na kuitwa FBI – Federal Bureau of Investigation.

Hata hivyo, ingawa historia ndefu na uwezo ni mambo mawili tofauti lakini ukweli ni kwamba, uwezo wa FBI katika kazi za kipelelezi ni mkubwa na wakati wote unatanguliza maslahi ya taifa lao na kwa hiyo, ingawa si vibaya kwa FBI kusaidiana na vikosi vya usalama nchini katika upelelezi wa matukio ya kihalifu, hasa yenye sura za kigaidi lakini suala la hadhari dhidi yao ni muhimu pia.

Tatizo hapa si msaada wa FBI nchini bali ni kwa namna gani, vikosi vyetu vya upelelezi na usalama vimejipanga (wakati wote wa msaada wa ki-operesheni kutoka FBI) kuhakikisha hawajianiki moja kwa moja au kujisalimisha mikononi mwa FBI katika mazingira ambayo yanathibitisha viashiria vya udhaifu katika maeneo kadhaa kwa upande wetu.

Eneo la kwanza lenye viashiria vya udhaifu kwa upande wa vikosi vyetu hivyo nadhani ni uwezo binafsi wa kutathmini vitisho dhidi ya nchi (threats assessment).

Katika eneo hili (threats assessment) mazingira yanadhihirisha kwamba kuna wakati vikosi vyetu vimepata kuonyesha udhaifu. Kama ambavyo wamekuwa wakilalamika viongozi mbalimbali wa dini kwamba kumekuwa na uenezaji wa wazi wa chuki za kidini, kuanzia uuzaji wa kanda za video na machapisho mbalimbali, hali hiyo haikufanyiwa uchambuzi wa kina na kwa sasa chuki imeenea nchini wakati ingeweza kudhibitiwa kama kungefanyika tathmini ya kina ya vitisho hivyo na namna ya kuvikabili mapema.

Eneo jingine la pili ni dalili za udhaifu wa vikosi vyetu hivyo katika kukusanya na kutumia (kwa wakati) taarifa za kijasusi kutoka sekta na taasisi mbalimbali nchini au hata nje ya nchi (counterintelligence) ili kudhibiti viashiria vyote vya hatari dhidi ya usalama wa nchi.

Katika eneo hili la pili, nadhani kuna uwezo mkubwa wa kukusanya taarifa lakini pia nina shaka kama taarifa hizo zinazokusanywa zinatumika ipasavyo na kwa wakati. Inawezekana pengine wakubwa wenye kuamua taarifa gani zitumike au la na kwa wakati gani, ndiyo wenye matatizo.

Kwamba inawezekana kuna maofisa waandamizi wasiomudu majukumu yao, wameshikilia madaraka wasioyamudu. Inawezekana katika vikosi vyetu wapo maofisa wabobezi katika masuala ya counterintelligence lakini si waamuzi wa mwisho katika eneo hili.

Mambo kadhaa yamekuwa yakithibitisha kuwapo kwa tatizo hili na kati ya hayo, vurugu za hivi karibuni, miezi kadhaa iliyopita katika mikoa ya kusini, hususan mkoani Mtwara, wakati wa kelele kuhusu gesi asilia ziliposikika na kusababisha vurugu kubwa za uvunjifu wa amani, upotevu wa mali na tishio dhidi ya uhai wa raia.

Kwamba mambo yalifikia hatua ya kulipuka na kusababisha madhara, pengine kutokana na udhaifu wa ama maofisa wa ngazi za chini au viongozi waandamizi ambao inawezekana, licha ya kuwa na taarifa, hawakuwa wepesi kufanya uamuzi katika maeneo mawili niliyoyabainisha hapo awali, yaani tathmini ya vitisho vya hatari dhidi ya nchi (threat assessment) na counterintelligence.

Na hapa ni lazima tuwakane wazi, Tanzania itachafuliwa kimataifa kama mchezo huu wa kushindwa kutumia taarifa za kiintelinjensia kwa wakati utaendelezwa (kwa kuzingatia mifano ya uenezaji chuki za kidini).

Matukio ya vurugu yatakuwa yakitokea na kusababisha vifo na maafa mengine, licha ya ukweli kwamba matukio hayo yanaweza kudhibitiwa baada ya maafa hayo kutokea na kisha eti kuendeleza upelelezi kwa kuwashirikisha FBI.

Jambo la msingi ni kufanyia kazi taarifa muhimu kwa wakati na si kutafakari namna ya kudhibiti fujo. Ingawa matukio ya maafa yanayotokana na vurugu wakati mwingine hutokea popote duniani licha ya uimara wa vyombo vya ulinzi na upelelezi (rejea shambulio la jijini Boston – Marekani wanakotoka FBI) lakini ni busara zaidi kwa vikosi vyetu kujielekeza katika kuwekeza zaidi kwenye kuzuia (prevention) na si kukabili (combating), na hasa kuzuia matukio ambayo msingi wake ni vitisho vya wazi.

Ni hatari kuwa na vikosi vya upelelezi na usalama vyenye kutenda kazi yake katika mwelekeo wa kukabili matukio hatari badala ya kuyazuia.

Tutafakari, kama vikosi vyetu vya usalama na upelelezi mara kwa mara vinayumba katika kujiendesha kwenye mazingira ya hapa nchini, hasa katika kuzima matukio mabaya ya ndani (domestic counterintelligence) hali inakuwaje pale vikosi hivyo vinaposhirikiana na vikosi vya mataifa makubwa, kama FBI? Je, mianya ya FBI kunufaika na ulegevu wowote wa vikosi vyetu imezibwa?

Tanzania inao watalaamu wa usalama wenye mafunzo kutoka nchi mbalimbali duniani lakini swali la msingi; je, utaalamu wao unatumika katika misingi ya weledi? Nahoji hivyo kwa sababu, inawezekana nchi inao watalaamu wa kutosha na makini, tena waliofuzu vizuri zaidi katika mafunzo yao lakini kuwa na utaalamu ni jambo moja na fursa ya kutumia utaalamu husika, kwa weledi, ni jambo jingine.

Ni kweli katika ushirikiano huo na vyombo vya kimataifa vya nchi nyingine kama FBI, mafanikio yanaweza kujitokeza kwa mfano kuwakamata wahusika wa matukio ya uhalifu, lakini hata hivyo, bado tatizo ni lile lie ni kwamba, ni kwa namna gani FBI na vikosi vyetu wataheshimu mipaka yao kikazi, na kwa namna gani hali ya kutazamana kwa ‘jicho’ la kufanyiana ujasusi wa kujihami (defensive counterintelligence) itakuwa ya kujiridhisha kwa upande wa Tanzania?

Binafsi nadhani, ushirikiano wetu na FBI ni muhimu lakini nafasi yetu katika ushirikiano huo kwenye matukio haya inaweza kuwanufaisha zaidi wao kuliko angalau kupata manufaa nusu kwa nusu kati yetu na wao hasa katika zama hizi za uwekezaji wa mashirika makubwa ya kimataifa hapa nchini, kuanzia kampuni za uchimbaji gesi hadi uzalishaji umeme bila kusahau kile kinachoitwa mashirika au taasisi za kimataifa za misaada na maendeleo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika


Na Godfrey Dilunga, Raia Mwema

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO