MBUNGE wa Jimbo la Hai, Mheshimiwa Freeman Mbowe (pembeni mlangoni kulia) akishuhudia kile alichokiita ni 'maajabu ya elimu ya Tanzania' pale alipokuta wanafunzi wa darasa la tatu (kushoto) na darasa la nne (kulia) katika Shule ya Msingi Mlima Shabaha, wakifundishwa ndani ya chumba kimoja cha darasa kwa wakati mmoja, wakisoma masomo tofauti, wakisimamiwa na walimu wawili tofauti. Wakati wanafunzi wa darasa la tatu walikuwa wanafundishwa somo la hesabu, wale wa darasa la nne walikuwa wakisoma somo la lugha ya Kiingereza. Katikati ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Stephano Ndosi, kushoto ni Mwalimu Anameni Kimaro na kulia ni Mwalimu Love Hoza. Picha na Tumaini Makene, Afisa Habari, Chadema
Mbowe aliwaambia walimu na wazazi wa watoto wanaosoma shule hiyo kuwa hali hiyo haikubaliki na akawaahidi kuwa atashirikiana nao kuhakikisha kuwa ndani ya wiki moja watoto hao wanaondokana nayo ili wasome katika mazingira sahihi waweze kujifunza, kupata maarifa, taarifa, kuelewa na kufaulu.
Wazazi wa watoto wanaosoma katika shule hiyo walimwambia mbunge huyo namna ambavyo wamehangaika kwenda sehemu mbalimbali, ikiwemo kumuona Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya ya Hai, kwa ajili ya kutatuliwa tatizo katika shule yao, lakini waliambulia patupu.
Walihoji juu ya utaratibu wa kusimamia elimu nchini, hasa ngazi ya msingi hadi sekondari, ambapo kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kutokana na kuwekwa chini ya wizara mbili tofauti, huku wakienda mbali na kuhoji zaidi kwa nini mgao wa bajeti unaohusika na kuwasaidia wananchi katika ujenzi wa madarasa na masuala mengine, umekuwa ukichelewa kufika katika halmashauri za wilaya, kupitia TAMISEMI.
Baada ya ziara ndogo kuzungukia maeneo ya shule hiyo iliyofuatiwa na kikao kifupi kilichofanyika shuleni hapo, ambapo Mwalimu Mkuu, Ndosi, Mwenyekiti wa Kamati ya Wazazi wa shule hiyo, Noeli Elia, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kilima Shabaha, Emmanuel Leiza kutoa taarifa juu ya hali ya shule hiyo, Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, aliomba kuondoka na Mwenyekiti wa Kamati ya Wazazi na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, kwa ajili ya kikao ofisini kwa mbunge, ambako aliidhinisha wapate milioni 6.5 kwa ajili ya kukamilisha mahitaji ya vifaa/mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa ajilinya wanafunzi na waalimu katika shule hiyo.
0 maoni:
Post a Comment