Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Waziri Nchimbi akutana na Ujumbe wa EU

untitled2 a91e4

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Simu: +255-22-2112035/40 S.L.P. 9223
Nukushi: +255-2122617/2120486
Barua Pepe: ps@moha.go.tz Dar es Salaam

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali ya Tanzania imesema itahakikisha inaendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kwa watanzania na raia wa kigeni waliopo na wanaoendelea kutembelea hapa nchini kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za binafsi na kimaendeleo ili watu wote waweze kutekeleza majukumu yao na kuishi kwa amani na usalama hapa nchini.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema hayo leo wakati akizungumza katika kikao baina yake na Ujumbe wa Wawakilishi wa nchi za Umoja wa Ulaya na mabalozi wa nchi hizo hapa nchini kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa wizara hiyo.

Mabalozi hao ni Dk. Ad Koekkoek wa Uholanzi, Marcel Escure wa Ufaransa, Diana Melrose wa Uingereza, Koenaad Adam wa Belgium na Luis Cuesta wa Spain.

Kikao hicho kilichowakutanisha Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil, Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP) Said Mwema , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela , Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam Suleiman Kova na Ujumbe wa Wawakilishi wa Jumuia ya Ulaya ikiongozwa na Balozi Filberto Cerani Sebregondi kimejadili hali ya usalama katika Jiji la Dar es Salaam.

Waziri Nchimbi amesema kwa sasa serikali kupitia Jeshi la Polisi imejiwekea mikakati mbalimbali ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika Jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla ikiwemo kufanya kila jitihada kuhakikisha kuwa hali ya ulinzi na usalama inaimarishwa na kwamba takwimu zinaonyesha kupungua kwa vitendo vya uhalifu.

" Jeshi la Polisi tayari limeanzisha Dawati Maalumu litakalowahudumia raia wa kigeni ili kuwawezesha kufungua kesi zao kwa urahisi, kuwepo kwa wepesi wa majadiliano na ziweze kushughulikiwa kwa haraka na hatimaye kupatiwa ufumbuzi". Amefafanua Waziri Nchimbi.

Waziri Nchimbi amesema pia katika kusimamia suala la Ulinzi na Usalama wa raia na mali zao kwa sasa wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itafanya ukaguzi wa Kampuni Binafsi ya Ulinzi ili kuangalia na kujiridhisha kama yanakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa.

Kwa upande wake Kiongozi wa Ujumbe wa Wawakilishi wa nchi za Umoja wa Ulaya hapa nchini Balozi Filberto Cerani Sebregondi amesema Umoja huo utaendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambapo pia ameishukuru Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa jitihada inayoendelea kuchukua kuhakikisha ulinzi na usalama kwa wageni na raia wa nchini Tanzania.

Kwa upande wao Mabalozi waliohudhuria kikao hicho wameitaka Serikali na Watanzania kuhakikisha usalama unadumishwa ili kutoathiri taswira ya Tanzania Kimataifa na hivyo kuhatarisha uwezekaji na utalii.

Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI,
28 Mei, 2013

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO