Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Askari FFU wa Arusha wakamatwa na bangi gunia 18 •wakiisafirisha kwa gari la mkuu wa FFU

SIKU chache baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuwakamata askari 16 wakituhumiwa kujihusisha na biashara ya magendo, askari wengine wawili wa jeshi hilo wamekamatwa mkoani Kilimanjaro wakiwa na shehena kubwa ya bangi wakiisafrisha kwenda nchini Kenya.

Askari hao walikamatwa Mei 19 mwaka huu saa nne usiku eneo la Kilemapofu, Wilaya ya Moshi Vijijini wakiwa na magunia 18 ya bangi ambayo walikuwa wameyapakia kwenye gari la Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Arusha aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba PT 2025.

Akithibitisha kukamatwa kwa askari hao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema askari hao walikuwa wakipeleka bangi hiyo Wilaya ya Rombo kwa mfanyabiashra mmoja ambaye hakutaka kumtaja jina lake.

Kamanda Boaz aliwataja askari waliokamatwa na wanashikiliwa kwenye kituo kikuu cha polisi katika mji mdogo wa Himo kuwa ni F.1734 Koplo Edward (dereva) wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mkoani Arusha na G.2434 Konstebo George wa kituo cha polisi Ngarenanyuki Wilaya ya Arumeru.

Alibainisha kuwa kukamatwa kwa askari hao kunatokana na operesheni ya kukabiliana na dawa za kulevya inayofanywa na polisi katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Alisema operesheni hiyo imefanyika kikamilifu katika Mkoa wa Arusha uliokuwa ukitumika kupitishia bidhaa hiyo, na sasa wahusika wameamua kuutumia Mkoa wa Kilimanjaro.

“Baada ya kuwahoji askari wale, walidai kuwa walikodishwa na mfanyabiashara huyo kuipeleka bangi hiyo wilayani Rombo tayari kwa kusafirishwa kwenda nchini Kenya ambako inaaminika kuna soko kubwa,” alisema.

Kamanda Boaz alisema hivi sasa polisi wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na wenzao wa Arusha wanafanya uchunguzi kubaini mtandao wa askari hao unaojihusisha na vitendo haramu.

Aliongeza kuwa hatua inayofuata kwa askari hao ni kufunguliwa mashtaka ya kijeshi na iwapo watakutwa na hatia watafukuzwa kazi kisha watafikishwa katika mahakama za kiraia.

Kamanda Boaz alibainisha kuwa kwa kawaida askari wanapotoka mkoa mmoja kwenda mwingine hupatiwa kibali maalumu cha kusafiria (Movement Order).

Alisema kibali hicho husaini kila mkoa ambao askari husika hupita, lakini waliokamatwa na bangi hawakuwa nacho.

Kamanda Boaz alibanisha kuwa kwa hali ilivyo askari hao waliondoka na gari la mkuu wa FFU bila kumpa taarifa wala kupata kibali chake.

Tanzania Daima limedokezwa kuwa askari hao wamekuwa wakisafirisha bangi hiyo mara kwa mara kupitia mji huo wa Himo bila kukamatwa kutokana na gari lao kuwa na namba za kijeshi, hivyo kuwa vigumu kwa askari wenzao kuwatilia shaka.

Taarifa zaidi zimedai kuwa kukamatwa kwa askari hao kulitokana na gari lao kupata hitilafu katika eneo hilo la Kilemapofu, na ndipo askari wa doria walipofika kwa lengo la kutoa msaada kwa wenzao, lakini ghafla walisikia harufu ya bangi.

Mtoa taarifa aliyezungumza kwa sharti la kutotaka jina lake litajwe, alisema baada ya askari hao kusikia harufu ya bangi waliwaarifu viongozi wao waliowaamrisha walifanyie upekuzi gari hilo sambamba na kuwaweka chini ya ulinzi askari wote waliokuwamo.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa katika upekuzi huo walibaini uwepo wa magunia 18 ya bangi yaliyolengwa kupelekwa nchini Kenya.

Kilibainisha kuwa baada askari hao kukamatwa, mmoja wao alisikika akiongea na mtu aliyemuita bosi kumuarifu kukamatwa kwao.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa bosi aliyearifiwa tukio hilo alihoji imekuwaje wakakamatwa kizembe namna hiyo.

Kilidokeza kuwa bosi huyo alimhoji aliyempigia simu kuwa wamebaki na shilingi ngapi ili wawape rushwa polisi waliowakamata.

“Bosi aliambiwa kuna laki tano, naye akawaambia wawape fedha hizo zote, lakini kwa bahati mbaya hawakufanikiwa,” kilisema chanzo chetu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, hakukiri wala kukanusha kuwapo kwa taarifa za kukamatwa kwa askari wake.

Tanzania Daima lilitaka kujua Jeshi la Polisi mkoani Arusha limechukua hatua gani dhidi ya askari hao ambapo kamanda Sabas alisema hayupo katika nafasi nzuri ya kulizungumzia jambo hilo kwa kuwa yupo hospitalini.

Chanzo: Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO