Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Mbunge wa Iringa Mjini Mh Peter Msigwa Akamatwa na Polisi Kufuatia Vurugu za Machinga

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) amekamatwa na polisi leo hii kwa tuhuma kuwa ndiye chanzo cha kuhamasisha wafanya biashara wadogo wadogo (wamachinga) kufanya vurugu huko Iringa.Askari polisi wa kutuliza ghasia (FFU) katika Manispaa ya mji wa Iringa pia imewakamata zaidi ya watu hamsini, akiwemoo aliyekuwa mgombea udiwani katika kata ya Mvinjini, Abuu Majeck.

Biashara zilisimama wakati wa sekeseke hilo, moshi ulitanda kutokana na matairi kuchomwa moto katika barabara za kuu ya Iringa-Dodoma na ile ya Mashine Tatu.Leo hii pia, Mbunge huyo alikuwa katika eneo la chuo cha Tumaini kwenye harambee iliyokuwa imehudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye kama inavyoonekana kwenye pichaa chini


Gazeti Mwananchi linasimulia zaidi…

Mji wa Iringa uligeuka kuwa uwanja wa vita kati ya polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wafanyabiashara jana asubuhi. Watu 50 walikamatwa kutokana na tukio hilo akiwamo Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

Katika vurugu hizo, gari la zimamoto lilivunjwa kioo na gari lingine dogo liliharibiwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda alisema Mchungaji Msigwa alikamatwa saa saba mchana kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo na kwamba watu wapatao 50 walikuwa wamekamatwa katika fujo hizo zilizochukua karibu saa tatu.

“Mchungaji Msigwa amekamatwa kwa makosa ya uchochezi, kufanya maandamano bila kibali na kuhamasisha watu kufanya biashara kwenye eneo ambalo limekatazwa kisheria.

Tumemkamata na hatutamwachia hadi uchunguzi wa suala hili utakapokamilika. Pia na hao watu wengine,” alisema Kamanda Kamhanda.

Alisema waliamua kufanya doria katika eneo hilo baada ya kupata taarifa za kiitelijensia kuwa wafanyabiashara walikuwa na mpango wa kuwashambulia mgambo wa Iringa kama wangekwenda kuwazuia.

Vurugu hizo zilichangiwa na mvutano uliokuwa unafukuta kwa muda mrefu kati ya Uongozi wa Manispaa na Mbunge huyo kuhusu amri ya kuzuia watu kufanya biashara kwenye Barabara ya Mashine Tatu, Iringa.

Uongozi wa Manispaa ya Iringa ulitoa tangazo Aprili 28, mwaka huu ukipiga marufuku kufanya biashara katika eneo hilo jambo ambalo lilipingwa na Mchungaji Msigwa na wafanyabiashara hao.

Alfajiri

FFU walianza kuimarisha ulinzi katika Barabara ya Mashine Tatu tangu alfajiri jana na wafanyabiashara hao walipofika kwenye eneo hilo walikuta limezingirwa na polisi.

Kusambaa kwa taarifa hizo kulimfikia Mchungaji Msigwa ambaye alifika hapo saa mbili asubuhi na kuanza kuzungumza na wafanyabiashara hao.

Watu walipomwona ndipo wakamzunguka na kuanza kuimba nyimbo za kumsifu na kumshangilia: “Rais wetu... Rais wetu... Rais wetu.”

Maofisa wa Polisi walimfuata Mchungaji Msigwa na kumwomba aondoke lakini aligoma akidai ni mwakilishi halali wa wananchi kwa hiyo hawezi kuondoka.

Badala yake alipanda kwenye gari lake na kuanza kuzunguka eneo hilo huku akifuatwa na umati wa watu. Polisi nao walikuwa wakimfuatilia kwa magari yao.

Baada ya idadi ya watu kuongezeka kwa wingi barabarani na kuanza kufanya kitu kama maandamano wakiwa nyuma ya gari ya Msigwa, polisi waliwataka kutawanyika lakini waligoma huku wakizidi kuimba nyimbo za kumsifia mbunge huyo.

Mabomu ya machozi

Ilipotimu saa tatu na nusu asubuhi, polisi walianza kutumia magari ya kumwaga maji ya kuwasha na kutumia mabomu ya machozi na kusababisha watu kukimbia ovyo, huku wengine wakikusanya mbao, matairi na mawe na kuwasha moto ili kuwazuia polisi wasiwafikie.

Moto huo ulisababisha nyumba moja kuwaka moto ndipo gari la zimamoto lilipokwenda kuzima lakini nalo likashambuliwa.

Msigwa kukamatwa

Mchungaji Msigwa alikamatwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Kabla ya kukamatwa, aliwaambia waandishi kuwa polisi walikuwa wanawaonea wafanyabiashara hao na kwamba manispaa haikuwa na mamlaka ya kisheria ya kuwazuia wafanyabiashara hao.

Mei 15 na 16, mwaka huu Msigwa alifanya mikutano ya hadhara kwenye Viwanja vya Mwembetogwa na Magorofani na kuwataka wafanyabiashara kutokuogopa kufanya shughuli zao kwenye eneo la Mashine Tatu.  


Msigwa katika harambee kabla ya kukamatwa

Mbunge Msigwa akisalimia katika harambee  iliyoendeshwa na  Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye(wa tatu Kushoto leo (jana) katika  chuo  cha Tumaini Iringa

Mbunge wa iringa Mjini-Chadema Mchn Msigwa (kulia)akizungumza na msaidizi  wa askofu  wa KKKT dayosisi ya Iringa muda mfupi kabla ya kukamatwa na polisi leo (jana)

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO