Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

MTUHUMIWA WA UGAIDI ARUSHA AFIKISHWA KIZIMBANI CHINI YA ULINZI MKALI, WANNE RAIA WA KIGENI WAACHIWA

Mtuhumiwa wa kurusha Bomu kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph,Parokia ya Olasiti ,Jimbo Kuu la Arusha,Victor Ambrose Calist (pichani) dereva wa Bodaboda na mkazi wa eneo la Kwa Mromboo, Arusha amefikishwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la Polisi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ,mbele ya Hakimu Mkazi,Devota Kamuzora leo.


Ambrose amesomewa mashtaka 21 ya kuua na kujaribu kuua wakati wa uzinduzi wa kanisa hilo ambao mgeni rasmi alikua Balozi wa Vatican nchini,Askofu Mkuu,Fransisco Padilla ambaye alikuwa na mwenyeji wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha,Josephat Lebulu.

Wakisoma kwa kupokezana hati ya mashtaka, Mawakili wa Serikali, Zachariah Elisaria na Haruna Matagane walidai Calist pia anatuhumiwa kwa makosa 18 ya kujaribu kuua.

Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kimyakimya akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa polisi na hakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mashtaka yanayomkabili yanapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 27, mwaka huu itakapotajwa tena na mtuhumiwa amerudishwa mahabusu.

Saa moja kabla ya Ambroce kupandishwa kizimbani saa nne asubuhi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas aliitisha mkutano na waandishi wa habari kitendo ambacho kiliwafanya baadhi yao kushindwa kufuatilia vyema tukio hilo.

Katika hatua nyingine Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha,Liberatus Sabas amesema kuwa watuhumiwa watatu raia wa  United Arab Emirates(UAE) walioshikiliwa na kuachiwa wamegundulika kuwa ni watumishi wa Serikali.

Kamanda Sabas aliwataja kuwa ni Abdul Azziz Mubarak (30), (Mamlaka ya Mapato), Fouad Saleem Ahmed Al Hareez Al Mahri (29), (Zimamoto) na Daeed Abdulla Saad (28), ambaye ni Askari wa Usalama Barabarani.

Raia hao pamoja na mwenzao, Al-Mahri Saeed Mohseen (29) kutoka Saudi Arabia, walikabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji kuchunguzwa iwapo waliingia nchini kihalali.

Abdul Aziz Mubrak(30)ambaye ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato ,Fouad Saleem Ahmed Hareez Al Mahri(29)Saeed Abdulla Saad(28)ambaye ni askari Polisi na raia mmoja wa Saudia Arabia,Al Mahri Saeed Mohseens(29)

Sabas amesema watuhumiwa wengine bado wanahojiwa kuona namna gani wanahusika na kitendo hicho cha kigaidi.

Na mwandishi maalum kupitia Rweyemamu Info Blog, Picha na Woinde Shizza


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSIANA NA MAENDELEO YA UPELELEZI WA TUKIO LA MLIPUKO WA BOMU KATIKA KANISA LA MT. JOSEPH – OLASITI JIJINI ARUSHA LILILOTOKEA TAREHE 05/05/2013

Ndugu wanahabari, mtakumbuka kwamba mara ya mwisho nilipokutana nanyi niliwaahidi kwamba nitaendelea kuwapa mara kwa mara taarifa juu ta maendeleo ya upelelezi wa tukio la mlipuko wa bomu lililotokea katika kanisa katoliki la mtakatifu joseph mfanyakazi parokia ya olasiti tarehe 05/05/2013 na kusababisha vifo vya watu watatu(3) na wengine kudhaa kujeruhiwa.

Kama nilivyowaeleza hapo awali, baada ya tukio hilo jumla ya watuhumiwa tisa(9) walikamatwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo la mlipuko wa bomu kanisani. Watuhumiwa haoa ni victor Ambros Kalist, (20), dereva wa bodaboda na mkazi wa kwa Morombo; Yusuph Lomayani Josee (18) mwendesha bodaboda mkazi wa kwa Morombo na George Bathlomeo Silayo (23) mfanyabiashara na mkazi wa Olasiti.

Watuhumiwa wengine waliokamatwa ni raia watatu toka nchi za falme za kiaruabu (UAE) Abdul Aziz Mubrak (30) mfanyakazi wa mamlaka ya mapato katika falme za kiarabu, Fouad Saleem Ahmed Al Hareez Al Mahri (29) mfanyakazi wa kikosi cha zimamoto katika Falme za Kiarabu, Saeed Abdulla Saad (28) askali polisikitengo cha traffic katika falme za Kiarabu, pamoja na raia mmoja wa Saudi Arabia Al-Mahri Saeed Mohseens (29)

Rai hao wa kigeni walikamatwa pamoja na wenyeji wao wawili ambao ni raia wa tanzania wenye asili ya Yemen.  Majina ya watanzania hao ni Mohamed Suleiman Saad, (38) mkazi wa ilala jijini Dar es Salaam na Jasm Mubarak (29) mkaazi wa mtaa wa Bondeni jijini Arusha.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na timu ya upelelezi ukihusisha taaasis nyingine za upelelezi FBI pamoja na INTERPOL kuhusiana na tukio hilo la mlipuko wa bomu kanisani umebaini kuwa raia hao wanne wa kigeni hawakuhusika katika shambulio hilo.

Baada ya jalada la tukio hilo kufikishwa ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali Arusha – divisheni ya mashtaka imeelekeza kuwa watuhumiwa hao wakabidhiwe ofisi za idara ya uhamiaji mkoa wa arusha ili kuona kama kuna taratibu zozote za kiuhamiaji ziikiukwa na wageni hao wakati walipoingia nchini ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa dhidi yao. 

Pia ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali imeandaa mashitaka dhidi ya victor S/O Ambros kalisti na amefikishwa mahakamani leo kwa tuhuma za mauaji na kujaribu kuua. Uchunguzi dhidi ya watuhumiwa waliosalia unaendelea kwa sasa tunao wataalamu kutoka kenya na Uganda ambao tunashirikiana nao katika upelelezi wa shauri hilo.

Aidha, hadi sasa idadi ya majeruhi wa tukio hilo la mlipuko wa bomu wanaoendelea kupata matatibabu katika hospitali mbalimbali ni 31 ambao kati yao 19 wanaendelea na matibabu katika hospitali ya mkoa mount Meru arusha, 4 katika hospitali ya St. Elizabeth arusha na wengine 8 katika hospitali ya taifa muhimbili jijini dar es salaam na taarifa zinaonyesha hali zao zinaendelea kuimarika.

Hata hivyo jeshi la polisi linaendelea kufuatilia taarifa za watuhumiwa wengine wanaohusishwa na tukio hilo ili waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani pia jeshi la polisi linaendelea kuwaomba wananchi au raiayeyote mwenye taarifa zitakazowezesha kubaini mtandao wa kigaidi nawatuhumiwa wengine wanaohusika na tukio hilo wajitokeze na kuwasilisha taarifa hizo; tayari mkuu wa jeshi la polisi (IGP) amekwishaahidi zawadi nono ya Tshs. 50,000,000/= kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa hizo za siri kwa kukamatwa kwa watu hao.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA.

IMETOLEWA NA KAMANDA WA POLISI MKOA WA ARUSHA

LIBERATUSI SABAS – ACP

TAREHE 13/05/2013.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO