Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare akipelekwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, Picha na Venance Nestory
HATMA ya dhamana ya Mkurugenzi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, na Joseph Ludovick, imebaki kuwa kitendawili baada ya hakimu anayesikiliza kesi hiyo kuwa na udhuru.
Lwakatare na Ludovick Joseph, wanakabiliwa na kosa la kula njama baada ya Mahakama Kuu kuwafutia mashtaka ya ugaidi.
Kesi hiyo ilitajwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, baada ya Hakimu Mkazi Alocye Katema anayeisikiliza kesi hiyo kutokuwapo mahakamani.
Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, wakili wa utetezi, Peter Kibatara, aliomba mteja wake apatiwe dhamana kwa kuwa kosa hilo lina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Prudence Rweyongeza, aliomba ombi hilo litupwe kwa kuwa mahakama haiwezi kutoa dhamana kwa kesi isiyokuwepo.
Alidai kilichopo mahakamani ni jalada la tuhuma zinazowakabili washtakiwa ambazo ziko hatua ya uchunguzi na kwamba mwisho wa siku itafunguliwa kesi rasmi Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza.
“Shauri liko katika hatua za uchunguzi na bado DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini) hajafungua kesi rasmi Mahakama Kuu, sasa tunashangaa mawakili wa washtakiwa wanawasilisha ombi la dhamana leo,” alidai.
Hivyo aliiomba mahakama itupilie mbali maombi hayo kwa kuwa hakuna kesi rasmi iliyofunguliwa na DPP Mahakama Kuu.
Baada ya kuwasilishwa kwa hoja hizo, Hakimu Fimbo aliahirisha kesi hadi Mei 27 mwaka huu na kusema Hakimu Katemana ndiye atakayetolea uamuzi maombi hayo.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Desemba 28 mwaka jana, huko Kimara King’ong’o Stop Over, walikula njama kwa kutaka kumdhuru Denis Msaki ambaye ni mhariri wa habari wa gazeti la Mwananchi kwa kutumia sumu.
Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliwafutia mashtaka matatu washtakiwa hao likiwemo la ugaidi.
Chanzo: Happiness Katabazi, Tanzania Daima
0 maoni:
Post a Comment