Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Tamko Maalum Kutoka Chama Cha Wananchi(CUF)Juu ya Vurugu Zilizotokea Mtwara

THE CIVIC UNITED FRONT- (CUF – Chama Cha Wananchi)


GHASIA ZA MTWARA


The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kimesikitishwa sana na vurugu zilizotokea Mtwara tarehe 22 Mei 2013 na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na polisi tarehe 23 Mei 2013. Chimbuko la mgogoro wa gesi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ni kushindwa kwa serikali ya CCM kutekeleza ahadi zaka za miradi ya kutumia gesi ya Msimbati na Mnazi Bay mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa MW 300 na kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi ya taifa.

CUF inalaani vikali vitendo vya kihalifu vya kuchomea nyumba ya mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kassim Mikongolo, na nyumba za baadhi ya viongozi wa CCM. Vile vile tunalaani vikali vitendo vya kuhujumu miundombinu muhimu likiwemo daraja la Mikindani linalounganisha Mkoa Mtwara na Mikoa ya Lindi, Pwani na Dar es Salaam.

CUF imesikitishwa sana na taarifa za vifo vya askari wanne wa JWTZ kwa ajali ya gari iliyotokea Kilimahewa wakati askari hao wakisafirishwa toka Nachingwea kwenda Mtwara kusaidia kudhibiti vurugu.Tumepeleka salamu za pole kwa CDF Jenerali Mwamunyange na kupitia kwake kwa familia za marehemu. Tunawapa pole askari wote waliojeruhiwa na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na waweze kurejea katika ulinzi wa taifa letu.

Vilevile tumesikitishwa na kifo cha raia wawili kwa kupigwa risasi akiwemo mama mjamzito na raia wengi kujeruhiwa. Tunawapa pole familia za marehemu na kuwaombea wote waloumia wapone haraka na waendelee na shughuli zao.

Taarifa za vyombo vya habari vinaeleza kuwa ghasia hizi zilianza baada ya hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nishati na Madini iliyosomwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi toka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Taarifa tulizozipata toka Mtwara zinaeleza kuwa jana kuanzia asubuhi, wakati Waziri Nchimbi akisoma tamko la serikali bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu kuwa hali ya Mtwara sasa ni shwari askari wa Jeshi la Polisi walifanya vitendo vya kinyama kwa raia wasio na hatia. Polisi walipita katika nyumba za wananchi na kuwachomoa vijana, kuwapiga na kuwachukua kuwapeleka kituo cha Polisi. Mabomu ya machozi na risasi za moto zilipigwa hovyo hovyo. Aidha katika maeneo ambayo vijana hawakuwepo waliwapiga wake zao, watoto wadogo na hata wazee kwa madai kwamba vijana wao wanasumbua. Binti mjamzito aitwae Fatuma alipigwa risasi na kufariki. Katika eneo la Mkana Read, Polisi walichoma moto soko la wananchi, nyumba nyingi za raia zimechomwa moto na polisi wamepora mali za watu zikiwemo za maduka ya wafanyabiashara. Wananchi wengi wakiwemo wanawake wamelazimika kukimbia nyumba zao. Taarifa tulizopata zinaeleza vitendo vya kinyama vya polisi vilisita baada ya maafisa wa juu wa Jeshi la Polisi kufika Mtwara.

Vurugu zilizotokea Mtwara tarehe 22 Mei hazihalalishi Jeshi la Polisi kupiga watu, kuua, kuchoma moto nyumba na vibanda vya biashara na kupora mali za watu wasio na hatia. Vitendo hivi vya polisi kupora mali na kuchoma vibanda vilitokea Tandahimba mwaka jana. Weledi ndani ya Jeshi la Polisi uko chini sana. Tunalaani vikali vitendo vya Jeshi la Polisi la kupiga watu, kuchoma nyumba na kupora. Uongozi wa Jeshi la Polisi uchukue hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya polisi waliohusika na vitendo hivyo. Tunatoa wito kwa asasi za haki za binadamu na wanaotoa misaada ya kisheria kuwasaidia wahanga wa Mtwara kudai haki zao.

Pamoja na kulaani vitendo hivi vya kihalifu na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale waliohusika na vitendo hivyo, Serikali itafanya makosa makubwa na kuingiza nchi katika mgogoro wa muda mrefu na wananchi wa mikoa ya kusini ikiwa itafumbia macho chimbuko la mgogoro huu na kushikilia hoja nyepesi kuwa mgogoro huu ni matokeo ya uchochezi wa wanasiasa wachache wanaojitafutia umaarufu. Narudia Chimbuko la mgogoro wa gesi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ni kushindwa kwa serikali ya CCM kutekeleza ahadi za miradi ya kutumia gesi ya Msimbati na Mnazi Bay mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa MW 300 na kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi ya taifa. Mradi mwingine ni kuanzisha kiwanda cha mbolea kitakachotumia gesi kama malighafi kama ilivyopendekezwa na Wentworth resources wanaomiliki visima vya gesi ya Mnazi Bay na Msimbati. Kama miradi hii ingeanza kutekelezwa nina uhakika wananchi wengi wa mikoa ya kusini hawatapinga gesi ya ziada kusafirishwa Dar es Salaam.

Kauli ya Waziri Nchimbi Bungeni kuwa serikali itawasaka waasisi wa vurugu hizi ndani na nje ya Mtwara ni juhudi za kutafuta mchawi badala ya kutathmini kwa nini wananchi wa Mtwara hawaiamini kabisa serikali ya CCM. Tumepata taarifa kuwa pana mpango kabambe wa kuwakamata viongozi mbalimbali wa CUF na kuuaminisha umma kuwa wanaohusika na kuchochea, kupanga na kutekeleza vurugu za Mtwara ni viongozi na wafuasi wa CUF. Serikali ya CCM imekubuu katika kubambikia kesi nzito watu wasiokuwa na hatia. CUF inafanya siasa kwa kujenga hoja. Katika suala la gesi tumejenga hoja za kiuchumi na maendeleo na uwajibikaji wa kisiasa kuhusu utekelezaji wa miradi ambayo CCM na serikali yake iliahidi kuitekeleza. Viongozi wa CUF hawajachochea vurugu wametumia majukwaa ya mikutano ya hadhara na maandamano ya amani kujenga hoja za kimsingi.

Mimi binafsi nilienda Mtwara mwaka jana nikazuwiwa kufanya mkutano wa hadhara Mtwara mjini kwa madai kuwa hali siyo shwari wilaya ya Tandahimba. Wananchi wa Mtwara walitaka nifanye mkutano huo pamoja na kuwa umezuwiwa na polisi, nikawasihi tusifanye hivyo na wakakubali. Tarehe 14 Aprili 2013 nilikuwa Mtwara nikazuwiwa kufanya mkutano wa hadhara sikukaidi nikafanya mkutano wa ndani. Maalim Seif, Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alitaka kufanya ziara ya mkoa wa Mtwara akaambiwa hana ruhusa ya kufanya mikutano ya hadhara mkoa wa Mtwara na hivyo akasitisha ziara yake.

Kuwakamata viongozi wa CUF wa wilaya za Mtwara na Lindi na wa kitaifa hakutamaliza mgogoro kati ya serikali na wananchi wa Mtwara ikiwa serikali itaendelea kuwabeza, kuwadharau na kutowasikiliza. Badala yake itaongeza chuki dhidi ya serikali.

Wakati wananchi wa Mtwara wamepoteza imani kwa uongozi wa CCM na serikali yake, Serikali imezuia vyama vingine vya siasa na asasi za kiraia kufanya shughuli za kuwasiliana na wananchi wa Mtwara na kwa hiyo kuunyima umma miongozo ya kisiasa za demokrasia. Umma uliokata tamaa na unaoamini unabezwa, kudharauliwa na kudanganywa na watawala unaweza kuchukua hatua zenye madhara hata kwa maslahi yao wenyewe.

Serikali imekuwa inapotosha kwa makusudi madai ya msingi ya wananchi wa Mtwara ambayo ni kuwa serikali itekeleze miradi ya gesi iliyoahidi wananchi wa Mtwara. Badala yake wananchi wa mikoa mingine wanalishwa sumu kuwa Wananchi wa Mtwara hawataki raslimali ya gesi iwanufaishe Watanzania wengine. Umeme ukifuliwa Mtwara na kuunganishwa katika gridi ya taifa utatumiwa na wote waliounganishwa na gridi ya taifa. Kiwanda cha mbolea cha Mtwara kitazalisha mbolea itakayotumiwa nchi nzima. Wananchi wa Mtwara hawajasema Watanzania wengine hawana haki ya kwenda Mtwara kupata ajira au kufanya shughuli za kibiashara. Wanaobomoa umoja na mshikamano wa kitaifa ni wale wanaowabeza, kuwadharau na kuendelea kuwadanganya wananchi wa Mtwara na kupandikiza sumu kwa Watanzania wengine kwa kupotosha madai ya msingi ya wananchi wa Mtwara na kushindwa kwa serikali kuwajibika kisiasa kwa ahadi ambazo viongozi akiwemo Rais alizitoa kwa wananchi wa Mtwara.

Wananchi wa Mtwara zaidi ya elfu 24 wameweka sahihi na kupeleka ombi (petition) kupitia Mhe. Habibu Mnyaa, Mbunge wa Mkanyageni kujadili kutekelezwa kwa miradi ya gesi ya Mtwara. Spika Anna Makinda kazuwia ombi hilo kujadiliwa.

Bunge limeshindwa kuisimamia serikali na kuhoji kwa nini mradi wa kufua umeme MW 300 ambao katika mwaka wa bajeti wa 2011/12 ulitengewa na kutumia shilingi 540 milioni umesitishwa. Mpaka hivi sasa hakuna kamati ya Bunge iliyoenda kusikiliza kilio cha Wananchi wa Mtwara badala yake Spika amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono vitendo vya serikali badala ya kuhakikisha kuwa Bunge linaisisimamia serikali.

Katika hotuba ya bajeti ya mwaka huu, Waziri kaeleza serikali kupitia TANESCO kwa kwa kushirikiana na kampuni ya Symbion itajenga kituo cha kufua umeme cha MW 400 na kuunganisha Mtwara na gridi ya taifa kupitia Songea. Hata hivyo bajeti ya maendeleo haijautaja mradi huu wala kutenga hata shilingi 1 kwenye mradi. Wananchi wa Mtwara wanaona wanaendelea kudanganywa na serikali ya CCM. Mikogo, majigambo na kauli za kejeli za Waziri wa Nishati kuhusu uelewa mdogo wa wananchi wa Mtwara katika masuala ya gesi zinazidi kuongeza chuki na jazba za wananchi. Mpaka hivi sasa serikali imekataa kuweka wazi mkataba wa ujenzi wa bomba na upembuzi yakinifu wa mradi huu. Hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nishati haielezi kama Wentworth Resources wanaoendesha visima vya gesi wataweza kuzalisha gesi kukidhi ukubwa wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na ahadi mpya za miradi ya kutumia gesi mkoani Mtwara.

Linalonistusha na kunitisha ni kwa nini viongozi wa juu wa serikali hawataki kuwa wawazi kuhusu mradi huu na wako tayari kupotosha, kuwagawa wananchi na kudanganya alimuradi mradi huu utekelezwe na usihojiwe?

Gesi ya Mnazi Bay, Mtwara iligunduliwa toka mwaka 1982 lakini mpaka hivi sasa haijatumiwa kikamilifu. Kampuni ya Artumas ilianza utaratibu wa kuichimba gesi mwaka 2006 na kuitumia kufua umeme wa Megawati 18. Tarehe 17 Oktoba 2007 kampuni ya Artumas ilitoa taarifa ya mpango wake wa kujenga kituo cha kufua umeme wa MW 300. Mpango huu ulitarajiwa kugharamiwa toka Mfuko wa Maendeleo wa Uholanzi - Netherlands Development Finance Company. Gharama za mradi wa kufua umeme zilikadiriwa kuwa dola za Marekani 225. Kampuni maalum ya kuendesha mradi huu ya Tanzania Generation Company Ltd (TANGEN) ilisajiliwa ili kujenga na kuendesha mradi huu. Kampuni hii ingekopa dola milioni 160 na dola milioni 65 zingechangiwa kama hisa na kampuni nyingine zikiwemo mifuko ya pensheni ya Tanzania na kampuni ya madini ya Barrick International.

Kampuni nyingine maalum ilitarajiwa kuanzishwa ili ijenge msongo wa umeme (nguzo za nyaya za kusambaza umeme) na kuunganisha umeme wa Mnazi Bay kwenye gridi ya taifa. Mradi huu ungegharimu dola milioni 400. Mradi huu ulitarajiwa kugharamiwa na mifuko ya pensheni ya Tanzania na wawekezaji kutoka Mashariki ya Kati. Mpango huu ulikubaliwa na serikali na ukaingizwa katika Mpango Kabambe wa Taifa wa kufua na kusambaza umeme (National Power Development Master Plan). Mradi huu wa kufua umeme MW 300 Mtwara ulipangwa uwe umekamilika mwaka wa 2012. Tovuti ya Tanesco inaueleza mpango huu kuwa ni wa muda wa kati. Bila shaka serikali iliukabali mradi huu baada ya kuufanyia utafiti na upembuzi yakinifu.

Mtikisiko wa sekta ya fedha na uchumi wa dunia wa mwaka 2008 uliathiri kampuni ya Artumas. Thamani ya hisa moja ya Artumas iliporomoka toka dola za Marekani 10.80 mwezi wa Aprili 2008 na kufikia dola 0.12 mwezi wa Machi 2009. Kampuni ilipata matatizo makubwa ya ukata na ilibidi serikali iisaidie dola milioni 7 ili iweze kuendelea na ufuaji wa umeme wa MW 18 Mtwara. Barrick International ilijitoa katika mradi wa TANGEN. Katika kujiunda upya Kampuni ya Artumas Group Inc. iliamua kubadilisha jina lake na kuwa Wentworth Resources Limited na kuteua menejimenti mpya.

Tarehe 10 Juni 2009 Rais Kikwete alipokuwa anawahutubia Wabunge na Wananchi katika Ukumbi wa Kilimani Dodoma kuhusu athari za mtikisiko wa uchumi duniani alieleza “Kwa sababu ya matatizo ya uchumi uwekezaji wa vitega uchumi kutoka nje umepungua. Wawekezaji wamekuwa wanakosa fedha kutoka mabenki na masoko ya mitaji. Matokeo yake ni kuchelewa au kukosa kabisa au kuahirishwa miradi mikubwa ambayo ingetoa mchango muhimu kwa ukuaji wa uchumi wetu na ajira. Kwa mfano: Mradi wa umeme wa MW 300 kule Mtwara kwa sababu ya Barrick Gold Ltd. kujitoa na Artumas peke yake haina uwezo wa kifedha; mradi wa nickel Kabanga, mradi wa aluminium smelter, Mtwara; mradi wa usambazaji umeme mkoani Mtwara, miradi ya viwanda vya saruji na mbolea Mtwara.” Kwa kauli ya Rais ambayo wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla waliisikia kwani hotuba hii ilirushwa live na Shirika la Utangazaji la Tanzania – Radio na Televisheni na vyombo vingine vya habari. Miradi ya kutumia gesi ni pamoja na kufua umeme MW 300, kutengeneza mbolea inayotumia gesi kama malighafi, aluminium smelter inayohitaji umeme mwingi, na kiwanda cha saruji ambacho kinatumia umeme na kinu chake kinaweza kutumia gesi. Wananchi wakamuamini Rais wetu na wakaelewa kuwa miradi hii imekwama kwa sababu ya mtikisiko wa uchumi na kwamba serikali inajitahidi kutafuta njia mbadala ya kujikwamua ili miradi hiyo iendelee.

Wakati wa kampeni ya uchaguzi wa 2010, Rais Kikwete aliwaeleza wananchi wa Mtwara akichaguliwa ataendeleza miradi ya Mtwara itakayotumia gesi ya Mnazi Bay. Maelezo ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi wa 2010, ibara ya 63 kifungu (j) Kuzalisha umeme (300MW) kutokana na gesi asili ya Mnazi Bay (k) Kupanua mitambo ya kusafisha gesi na bomba la kusafirisha gesi kutoka Songo Songo hadi Dar es Salaam. Mitambo ya kufua umeme ya Dar es Salaam ilitegemewa itumie gesi ya Songosongo kwani bomba la kutoka Songosongo hadi Somanga mpaka Dar es Salaam lingepanuliwa. Toka mwaka 2010 kampuni ya Globeleq- Songas ilijiandaa kutekeleza mradi wa kuongeza uwezo wa bomba la gesi kutoka Songosongo – Somanga – Dar es Salaam ili likidhi mahitaji ya gesi ya vituo vya kufua umeme Dar es Salaam kikiwemo kituo cha Kinyerezi. Serikali iliisitisha kampuni hiyo isiendelee na mradi huo ambao hivi sasa ungekuwa umekamilika na kuongeza uwezo wa kufua umeme kwa kutumia gesi kwa alau MW 200.

Rais Kikwete alipoenda Mtwara kuhudhuria sherehe ya Mashujaa tarehe 25 Julai 2011 alizungumza na wananchi wa Mtwara na kueleza miradi ya maendeleo itakayotekelezwa kwa kutumia gesi ya Mnazi Bay ikiwemo ufuaji wa umeme wa MW 300 na kupanua bandari ya Mtwara.

Tarehe 12 Oktoba 2011, Ikulu ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Oktoba 12, 2011, amepokea ripoti kutoka makampuni mawili ya kimataifa kuhusu Mpango Kabambe ya mradi mkubwa wa umeme ambao utaunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa yote sita ambayo kwa sasa haiko kwenye gridi hiyo. Rais Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka makampuni ya China National Machinery&Equipment Import&Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani ambayo kwa pamoja yanatarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida. Mradi huo mkubwa wa umeme wa megawati 300 utakaogharimu karibu dola za Marekani milioni 684 na utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na wenye nguvu kubwa ya 300 kV (300 kV High Voltage Direct Current – HVDC) utagharimiwa kwa pamoja na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China na Serikali ya Tanzania.”

Mikoa sita ambayo bado haijaunganishwa na gridi ya taifa ni Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera. Mradi huu pamoja na kufua umeme wa MW 300 Mtwara ungekamilisha kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye gridi ya taifa. Taarifa iliendelea kueleza “Kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye Gridi ya Taifa ilikuwa moja ya ahadi kubwa zilizotolewa na Serikali ya Rais Kikwete wakati anaingia maradakani na kwa kuuunganisha mikoa hiyo sita kwenye Gridi hiyo, Serikali hiyo itakuwa imetimimiza ahadi hiyo.”

Maelezo haya yametolewa na Ikulu na vyombo vya habari vikayatangaza na wananchi wa Mtwara wakasikia. Kutekeleza mradi wa kufua umeme kutaifanya Mtwara iwe na umeme wa kutosha kushawishi kampuni kuanzisha viwanda hasa ukizingatia ahadi ya Rais Kikwete ya kupanua bandari ya Mtwara. Mwaka wa fedha wa 2011/12 serikali ilitenga na kutumia shilingi 540 milioni fedha za maendeleo za mradi wa Mnazi Bay 300MW Development Project. Baada ya hapo mradi huu haukutengewa fedha tena. Badala ya mradi huu kuendelezwa kama Rais alivyowaahidi wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla badala yake wanasikia serikali imezindua mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi toka Mtwara kuja Dar es Salaam.

Kwa taarifa ya Ikulu gharama za mradi wa kufua umeme wa MW 300 Mtwara na kuiunganisha mikoa sita katika gridi ya taifa gharama yake ni dola milioni 684. Mradi wa kutandaza bomba la gesi unagharimiwa na mkopo wa dola milioni 1220 kutoka Benki ya Export Import Bank ya China. Ni wazi gharama za kufua umeme Mtwara na kuunganisha mikoa sita kwenye gridi ya taifa ni ndogo zaidi kuliko gharama za kutandaza bomba la gesi.

Msongo wa umeme za kV 400 unajengwa kuunganisha Iringa – Dodoma – Singida na Shinyanga. Mradi huu unatekelezwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika. Nyaraka ya mradi unaonyesha gharama za kujenga umeme za kV 400 ni dola za Marekani 600,000 kwa kilomita 1. Gharama za kujenga bomba la gesi lenye kipenyo (upana wa nchi 36) ni dola 1,309,636 kwa kilomita 1. Kwa madhumuni ya kufua umeme, gharama ya kujenga bomba la gesi ni zaidi ya mara mbili ya gharama za kunganisha Mtwara na Dar es Salaam. Isitoshe unaweza kuongeza ufuaji wa umeme Mtwara na kusambaza kwa msongo huo huo.

Ujenzi wa bomba la Dar es Salaam Mtwara umeanza bila kuwa na mipango ya kuhakikisha kuwa kutakuwepo na gesi ya kutosha kuisafirisha hadi Dar es Salaam. Bomba hili litakuwa na uwezo wa kusafirisha futi za ujazo bilioni 200. Uwezo wa gesi ya Mnazi Bay na Msimbati kwa hivi sasa ni futi za ujazo bilioni 80. Hakuna mpango unaoeleweka wa kupata futi za ujazo bilioni 120 ili bomba la gesi liweze kutumiwa kikamilifu.

Mpaka hivi sasa gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 33.7 imegunduliwa katika bahari yenye kina kirefu. Uchimbaji wa gesi hii bado haujaanza. Inaweza kuchukukua miaka 7 – 10 kabla ya shughuli ya uchimbaji wa gesi kukamilika. Kampuni zilizogundua gesi bahari kuu bado hazijafanya uamuzi wa utaratibu wa kuichimba na kuisafirisha gesi hadi nchi kavu. Kwa kuwa gharama za kujenga bomba la gesi chini ya bahari ni za juu sana, kampuni hizi zitapendelea kutandaza bomba kwenda nchi kavu kwenye eneo lililo fupi kuliko yote. Statoil imegundua gesi nyingi eneo la Zafarani bahari kuu eneo la mkoa wa Lindi. Hivi sasa wanatazama maeneo ya Kilwa kuweza kuweka kituo cha nchi kavu. Bandari ya Lushungu kata ya Limalyao, wilaya ya Kilwa ambayo ina kina kirefu cha bahari yaelekea kuwavutia. Kwa hivi sasa hakuna uhakika gesi iliyogunduliwa bahari kuu itapelekwa Mtwara. Uamuzi wa kujenga bomba kubwa umefanywa haraka haraka bila kutathmini kikamilifu faida zake kiuchumi. Jambo la kujiuliza kwa nini uamuzi huu umechukuliwa na kuacha kutekeleza mradi wa kufua umeme Mtwara wenye mantiki kiuchumi, kijamii na uwajibikaji wa kisiasa?

Wentworth Resources wamefanya upembuzi yakinifu (feasibility study) na kubaini kwamba njia nzuri ya kibiashara na kiuchumi ya kutumia gas wanayoweza kuzalisha Mnazi bay hivi sasa ni kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mbolea na kemikali nyingine Mtwara. Kiwanda cha mbolea chenye faida kubwa kinaweza kuanzishwa na kuendeshwa hata kama akiba ya gesi iliyogunduliwa siyo kubwa sana kama ilivyo Mnazi Bay. Mradi wa kujenga kiwanda unaweza kukamilishwa kwa muda mfupi. Pamoja na mbolea kiwanda kitazalisha methanol yenye soko kubwa duniani. Kiwanda kitatumia hewa ukaa (carbondioxide) na kwa hiyo kuweza kupata fidia ya kuboresha mazingira. Uongozi wa Wentworth Resources una uzoefu wa miaka mingi katika miradi ya kutumia gesi. Wanajua wanalolieleza. Hata hivyo serikali imewamrisha kupeleka gesi watakayozalisha kwenye bomba la gesi la kwenda Dar es Salaam.

Serikali imeanzisha mgogoro wa gesi kwa kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa kutandaza bomba la mafuta na kuacha miradi yenye manufaa makubwa kiuchumi na kijamii kwa taifa letu. Uchunguzi huru na wa kina ufanyike kubaini sababu za serikali kuacha miradi ya kutumia gesi Mtwara na kukumbatia mradi wa kutandaza bomba. Ripoti aliyopewa Rais ya mradi wa kufua umeme Mtwara na kuunganisha mikoa 6 katika gridi ya taifa itolewe ili Watanzania waweze kuelewa mantiki ya mradi huu. Mkataba wa mkopo na utekelezaji wa mradi wa kutandaza bomba la gesi uwekwe wazi. Serikali iruhusu kampuni ya Wentworth resources kuendelea na mradi wa kiwanda cha mbolea. Rais aende Mtwara kuwaeleza wananchi kuwa ahadi alizoeleza za kutumia gesi Mtwara zitatekelezwa.

Vyama vya siasa na asasi za kiraia viruhusiwe kufanya mikutano ya hadhara kueleza njia za kidemokrasia za kudai haki za kiuchumi za wananchi wa Mtwara. Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza kwa nini Mradi wa Kufua umeme MW 300 umesitishwa na serikali, upembuzi yakinifu wa mradi wa bomba la gesi na mikataba yote inayohusiana na mradi huu.

Sakata hili la gesi ya Mtwara linaonyesha wazi kuwa hatuna sera muafaka na mkakati wa kuendeleza sekta ya gesi kwa manufaa ya taifa letu na Wananchi wa kawaida. Badala ya gesi kuwa neema inaelekea kuwa itakuwa balaa na laana. Sera ya gesi inapaswa kuweka taratibu zitakazohakikisha kuwepo kwa uwekezaji wa kutosha katika sekta hii na utakaolinufaisha taifa letu bila kuathiri motisha kwa wawekezaji wenye teknolojia ya kutafuta na kuchimba gesi. Wananchi wa Mtwara wanahitaji kushirikishwa. Serikali iwe wazi na kutoa taarifa sahihi kuhusu miradi ya gesi.

Prof. Ibrahim Haruna Lipumba,

Mwenyekiti wa Taifa, Mei 24 2013.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO