Katibu wa Jukwaa la Wahariri Nevil Meena (mwenyekipaza sauti) Picha ya Maktaba
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limemsimamisha uanachama kwa muda usiojulikana, Mhariri wa Mtanzania Jumatano, Charles Mulinda, kwa sababu za kukiuka maadili ya uandishi wa habari. Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Jukwaa hilo, Nevil Meena, alisema TEF imechukua uamuzi huo baada ya kupokea na kujadili kwa kina taarifa ya kamati ndogo ya wahariri watatu ambayo iliongozwa na Mhariri wa Nipashe, Jesse Kwayu, kwa ajili ya kuchunguza habari iliyochapishwa na gazeti la Mtanzania, Jumatano Aprili 17, mwaka huu ikiwa na kichwa kisemacho ‘Mtandao Hatari’.
Katika habari hiyo, Meena alidai kuwa iliwataja wahariri wawili, Ansbert Ngurumo wa Tanzania Daima na Deodatus Balile wa Jamhuri kuwa ni washirika wa Joseph Ludovick, mshitakiwa katika kesi ambayo ilikuwa ikihusishwa na ugaidi (kabla ya kubadilishwa na mahakama) lakini ikiwahusisha kwa namna moja au nyingine na tukio la kuumizwa kwa Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda.
“Yalikuwa ni maoni ya wahariri wengi katika mkutano wa Aprili 18, 2013, kwamba habari hiyo ilikuwa na upungufu mkubwa kitaaluma, hivyo kuamua kuchunguza habari hiyo na kubaini iwapo kulikuwa na ukiukwaji wa maadili na misingi ya kitaaluma ya habari. “Pamoja na mambo mengine ilipaswa kuchunguza mazingira ya kuchapishwa kwa habari hiyo na kama kulikuwa na msukumo wowote nyuma ya kuandikwa kisha kuchapishwa kwakwe,” alisema...
Meena alisema kamati hiyo ilipaswa kuchunguza ushahidi wa tuhuma zilizotolewa dhidi ya Deodatus Balile na Ansbert Ngurumo (kama Mullinda) alivyokiambia kikao cha Aprili 18 kwamba alikuwa na ushahidi wa yale aliyoyaandika. Aliongeza kuwa TEF ilibaini kulikuwa na ukiukwaji wa maadili ya kitaaluma katika mchakato mzima uliowezesha kuandikwa na kuchapwa kwa habari husika na kwamba habari hiyo haikuwa na sifa wala vigezo vya kihabari. Hata hivyo, Meena alisema Mulinda alipotakiwa kutoa ushahidi wa tuhuma dhidi ya wahariri aliowataja, alishindwa kuthibitisha usahihi wa taarifa hiyo.
Kwa kuzingatia matokeo hayo TEF inaushauri uongozi wa New Habari (2006) Ltd na vyumba vingine vya habari kuboresha mfumo wake wa usimamizi wa uhariri ili kuziba mianya kwa habari tata kama hiyo ya ‘Mtandao Hatari’ kupenya na kuwaumiza baadhi ya watu bila kuwapo kwa uthibitisho wa tuhuma husika.
TEF inaendelea kuchukua hatua nyingine za ndani kuimarisha usimamizi wa nidhamu na maadili kwa wahariri, na itaendelea kuchukua hatua dhidi ya ukiukwaji wowote ule wa kitaaluma utakaofanywa katika vyombo vya habari.
Chanzo: Tanzania Daima
3 maoni:
Wahariri hapa naona mmekosea kweli kupitia chama chenu,hivi mara ngapi ?wahariri wanaandika abari zenye utata mkubwa na za uzushi mtupu lakini hamchukii hatua yoyote ile zaidi ya kukaa kimyaa,lakini leo hii mmoja wenu kawatuhumu wenzake mara moja mmeita vikao na kunda kamati ndogo kuchunguza sasa hili hamuoni kuwa ni kutumia vibaya chama chenu??
lakini mdau (Anonymous 2:03 PM)
huoni kama labda hii ni hatua moja zaidi kuelekea kule ambako uanatamanai wangekuwa wakifanya mara kwa mara bila kuoneana aibu?
tutuombe mungu ajali huu uwe ndo mwanzo wa kwenda mbele na kutoa fursa kwa watu kupata habari za ukweli zisizokuwa na chumvi na uzushi
Post a Comment